Uongozi Mintarafu Dhana ya Sinodi Katika Maisha na Utume wa Kanisa
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Mpasuko na mgawinyiko wa kwanza wa Kanisa ulitokea mbele ya macho ya Yesu: wafuasi wawili dhidi ya kumi na wale kumi dhidi ya wawili. (Marko 10:35-41). Mpasuko ule wa kwanza kabisa haukutokana na kupishana katika mafundisho ya kitaalimungu bali nafasi na madaraka, nani awe nani, nani awe na nafasi gani. Ndio dhambi ya uchu wa madaraka, ndio dhambi inayoleta migawinyiko mingi katika maisha ya Kanisa si tu nyakati za Yesu Kristo bali hata leo katika nyakati zetu. Sehemu ya Injili ya leo, Yesu bado yupo njiani pamoja na wafuasi wake wakielekea Yerusalemu; wakiwa njiani Yesu anatumia fursa hii kuwafunulia na kuwafundisha wanafunzi wake wa karibu juu ya hatima yake akiwa Yerusalemu, ndio ile ya kukataliwa na kukusanywa ili apitie njia ile ya mateso, kifo na siku ya tatu kufufuka. Ni fundisho gumu kupokeleka na hata kueleweka na wanafunzi wake. Mwinjili Marko katika aya chache zinazotangulia somo la Injili ya leo, anatuonesha tena Yesu kwa mara ya tatu anawafundisha wanafunzi wake juu ya kukataliwa, kutukanwa, kuhukumiwa kifo, kupigwa mijeledi na kuuawa kifo cha aibu pale juu Msalabani. (aya 32-34).
Hata baada ya kufundishwa mara tatu juu ya mateso, kifo na ufufuko, wanafunzi wale wa Yesu bado hawakuwa tayari kubadili vichwa vyao, namna zao za kufikiri, na hivyo walibaki katika kutegemea na kusubiria utawala wa kidunia mara Yesu atakapofika Yerusalemu, ndio utawala wa dunia hii, utawala wa mabavu na nguvu, utawala wa kisiasa na kiitikadi. Na ndio tunaona katika somo la Injili ya leo, wanafunzi wake wakiwa na mawazo ya kuwa na nafasi za heshima, nafasi za kwanza, nafasi za kuweza kunufaika na matajamala binafsi. Mitume Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba.” Yesu akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” Wakamjibu, “Uturuhusu kuketi mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.” Hii ndio kiu na hitaji lao kwa Yesu, kwani bado walibaki katika kumtazama Yesu kama Masiha anayekuja kwa sababu za kisiasa na kijamii tu. Na ndio maana hawalileti mbele ya Yesu kama ombi, bali kama haki yao kwani wanataka wafanyiwe, wapewe nafasi hizo za kulia na kushoto kwa Yesu, za kushiriki kwa karibu kabisa na nafasi za heshima katika utawala wake.
Mwinjili Marko, wakati anaandika Injili, tayari Yakobo na Yohane walikuwa wameelewa fundisho lile la Yesu, kwani ni baada ya mateso, kifo na ufufuko, Kanisa lile la mwanzo likaanza kuelewa maana ya mafundisho ya Yesu. Yakobo tayari alikufa shahidi pale Yerusalemu. (Matendo 12:2) na Yohane alikuwa ameyatoa maisha yake akihubiri Injili. Na ni hapo tunaweza kuona waliyaelewa mafundisho yale ya Yesu sio wakiwa njiani kuelekea Yerusalemu walipotamani nafasi za kwanza na za heshima, bali pale tu baada ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Na ndio tunaona Mwinjili Luka hataji wala kutuonesha juu ya tukio hili na pia Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa hitaji na kiu ile haikuwa ya mitume wale wawili bali ya mama yao. (Mathayo 20:20-24). Mitume hawa wawili, kadiri ya Mwinjili Marko anatuonesha kabla hawakuelewa fundisho la Yesu, juu ya ufalme na utawala wake, lakini si tu hawa wawili bali kundi zima la wanafunzi wale wa mwanzo kabisa wa Yesu. Ni kundi zima la mitume kumi na wawili walikuwa bado kuelewa fundisho lile mama la mafundisho yote, fundisho juu ya hatima ya Yesu, fundisho juu ya ukombozi wa mwanadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko. Mwinjili Marko si tu anawaalika Waamini Wakristo wa jumuiya yake bali hata nasi leo, juu ya hatari ya ulevi wa madaraka, kishawishi cha kutaka kutawala wengine, cha kutaka kutumikiwa, kishawishi cha kuwa wa kwanza na nafasi za heshima.
Baba Mtakatifu Francisko anatualika Waamini Wakatoliki na hasa katika Dominika ya uzinduzi wa Sinodi ya Maaskofu majimboni pote ulimwenguni, kutafakari kwa pamoja nini maana ya Kanisa la Kisinodi. Ndilo Kanisa lile anatualika Kristo mwenyewe, kila mbatizwa na kila mwamini kuwa ni kiungo hai katika Mwili fumbo wake, yaani, Kanisa. Kila mbatizwa anaalikwa kuwa mshirika hai, anayeshiriki kikamilifu na pia anayekuwa na moyo wa kimisionari. Kanisa ni jumuiya waamini walio hai wa Kristo, kila mbatizwa anaalikwa kuwa jiwe lililo hai katika umoja na pamoja katika kushiriki umisionari au utume wa Kanisa. Kamwe kusitokee kikundi cha watu au kishawishi cha wanaohodhi au kumiliki Kanisa, kwani Kanisa ni la Kristo. Kanisa linatualika kusafiri na kutembea kwa pamoja, kamwe asibaki hata mmoja nyuma, anayekuwa mtazamaji wa mbali, asiyekuwa na shirika wala ushiriki katika umisionari wa kutangaza na kuwa mashahidi wa Injili katika nyakati zetu za leo. Kanisa la Kisinodi ndilo Kanisa linalotembea kwa pamoja, kwa kushirikishana yote kwa uwazi na upendo mkubwa, linalokubali kujishusha na kutambua kila mmoja wetu anaalikwa kuwa mtumishi wa wengine, kuwa mdogo na mwenye kutumikia kila mmoja kwa nafasi yake mintarafu hiarakia ya Kanisa. Kusiwepo hata mmoja wetu anakuwa ni mmiliki wa Kanisa na badala yake sisi sote ni mabawabu wa Kanisa la Kristo, ni walinzi na watumishi wa mafumbo ya Kristo Yesu.
Ni wito wa Kristo tunapotembea kwa pamoja kama Kanisa la Kisinodi, kutambua hatari na kishawishi cha kuwa wa kwanza, kuwa na nafasi ya heshima katika jumuiya zetu, kishawishi ni kujiona mkubwa na mtawala, cha kujiona wa maana kuliko wengine, na ndio maana Baba Mtakatifu anatualika kwa namna ya pekee kujitafakari sisi sote kuanzia familia zetu, jumuiya zetu, vigango, parokia na majimbo yetu, kama tunasafiri kwa pamoja na kwa kushirikiana na kushirikishana katika utume wetu wa kimisionari. Yesu anatualika kuwa macho na kishawishi cha ulevi wa madaraka au kutaka kutawala wengine. (Marko 8:33; 9:33-36). Yesu anawakumbusha Yakobo na Yohane kuwa hawajui waliombalo na ndipo hapo anatumia lugha ya picha ile ya kikombe na ubatizo. Kikombe katika muktadha wa Wayahudi kilikuwa na maana ya baba wa familia, ambaye mezani alikuwa na kikombe chake maalumu na ambacho angeweza kuwashirikisha wale tu wanaompendeza. Hata hivyo katika Maandiko Matakatifu picha ya kikombe inatumika mara kadhaa ikiwa na maana chanya(Zaburi 16:5) na mara kadhaa ikiwa na maana hasi(Isaya 51:17) “Amka ewe Yerusalemu!Amka usimame wima!Mwenyezi-Mungu amekunywesha kikombe cha ghadhabu yake,nawe umeinywa mpaka tone la mwisho,mpaka ukayumbayumba.”
Kikombe ndio hatima, hivyo inaweza kuwa chanya au hasi. Yesu anatambua kuwa kikombe chake ndio kile cha kukataliwa, mateso na kifo. Kikombe ambacho anamuomba Mungu Baba kama ni mapenzi yake apende kumuepusha nacho, lakini yatimizwe mapenzi ya Mungu Baba. (Marko 14:36). Ubatizo pia una maana ile ile ya kupitia njia ya maji ya kifo. Ndio maji ya kukubali kuyatoa maisha yake, kwa ajili ya Wokovu wa ulimwengu mzima. Yesu leo anatufundisha nasi nini maana ya kuwa wafuasi wake, nini maana ya kuwa Wakristo, ndio kuwa tayari kushiriki kikombe na ubatizo wake, yaani njia ile ya mateso na kifo ili mwishowe tuweze nasi kushiriki utukufu wake wa mbinguni milele yote. Utukufu wake, yaani, wokovu wetu ni zawadi ya Mungu kwa kila mmoja wetu, hivyo sio taji tunaloweza kulipata kwa nguvu na jitihada zetu pekee, bali ni kwa msaada wa neema za Mungu. Ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa kila mmoja anayekuwa tayari kuipokea zawadi hiyo, ambayo, ndio uzima wa milele. Ndio furaha ya milele, yaani, kuunganika na Mungu milele na milele. Na ndio Yesu anachukua nafasi hii kutufundisha sisi wafuasi wake kutukuwa watawala kwa maana ile ya ulimwengu huu na badala yake kufanyika watumwa, kufanyika watumwa wa Injili na kweli zake, kuwa watumwa wa Kristo katika maisha ya kila mmoja wetu.
Ni mwaliko wa kuwa watumishi, kwenda kuwatumikia wengine kwa upendo. Kamwe tusiingie katika kishawishi hatari kabisa cha kupenda kuwatala na kuwatumikisha wengine bali daima kuwa wadogo na kutumikia wengine, na ndio ile namna ya kuishi Kisinodi, tukishikimana na kushirikiana na kutembea kwa pamoja, ni safari ya kushikana mikono, na kamwe tusimwache hata mmoja wetu nyumba na pia asitokee mmoa wa kuwa mbele ya wengine. Ndio Baba Mtakatifu anatualika kujitafakari kama Kanisa, kuona ushirika wetu, ushiriki wetu na pia umisionari wetu katika maisha ya kila mmoja wetu. Kama vile Kristo mwenyewe hakuja ili kutumikiwa bali kutumikia basi nasi tunaalikuwa kuwa watumwa na watumishi. Ni Yesu mwenyewe anayeinama na kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuwaalika nao kutenda vivyo hivyo, ndio maisha ya kutumikia wengine kwa unyenyekevu na upendo mkuu. Na ndio wito tunauopokea kutoka kwa Mungu Roho Mtakatifu hususani kwa njia ya Sakramenti za Ubatizo na Kipaimara. Nawatakia Dominika njema ya mwanzo wa Kanisa la Kisinodi na tafakari njema ya Neno la Mungu.