Jumapili ya Kwanza ya Kipindi Cha Majilio: Hukumu na Fumbo la Umwilisho
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
UTANGULIZI: Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio. Hii ni dominika inayoashiria mwanzo wa mwaka mpya wa kiliturujia. Kama tunavyofahamu, mwaka wa kiliturujia wa Kanisa huanza na kipindi cha Majilio na huitimishwa kwa Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Kumbe tunauanza mwaka wa kiliturijia tukifuatisha jinsi ilivyoanza historia ya ukombozi wetu. Historia hiyo ilianzaje? Ilianza na ahadi ya Mungu kumkomboa mwanadamu baada ya anguko lake katika bustani ya Edeni. Baada ya ahadi hiyo, mwanadamu akikaa kipindi kirefu akingojea ujio wa huo ukombozi. Na hiyo ndiyo ilikuwa Majilio ya kwanza. Sisi nasi kila unapoanza mwaka mpya wa Kanisa, tunairudia Majilio hiyo kwa kipindi cha majuma manne. Lakini hii Majilio yetu sisi nakuwa na sura mbili: sura ya kwanza ni ile ya kujiandaa kuadhimisha kuzaliwa kwa Mkombozi wetu Yesu Kristo na sura ya pili ni ile ya kujiandaa kwa ujio wake wa pili atakapokuja kwa utukufu kuwahukumu walio hai na wafu.
MASOMO KWA UFUPI: Katika sura hizo mbili za Majilio tunayoiadhimisha, Dominika hii ya kwanza na hata ile ya pili inakuwa ni ya kutualika kujiandaa kwa ule ujio wa pili wa Kristo atakapokuja katika ile tunayoiita siku ya mwisho. Wakati sisi sasa tunazungumza kuhusu ujiio wa pili wa Kristo, hali haikuwa hivyo katika Agano la Kale. Kristo alikuwa anasubiriwa aje kwa ujio wake wa kwanza na hali haikuwa wazi kama tunavyofikiri. Wao walikuwa na matumaini kuwa siku inakuja ambapo Mungu atayamaliza matatizo yote ambayo wanayapitia katika maisha na watu wataanza kuishi katika haki, amani na ustawi. Katika somo la kwanza, Yer 33:14-16, utabiri tunaousikia unadokeza pia hali hiyo: taifa lilikuwa limesambaratishwa kwa uvamizi wa jeshi la Babeli, Yerusalemu umeangamizwa, hekalu limebomolewa na watu wamechukuliwa mateka wakapelekwa utumwani. Unabii wa ukombozi unapokelewa kama kitendo cha Mungu kuingilia kati hali hiyo isiyofaa. Anaingilia kati kwa kumwinua mfalme mahiri kama Daudi, mfame atakayerejesha haki kwa watu wake. Ni baadaye sana walikuja kutambua kuwa ukombozi aliowaahidia Mungu, sawa, ni ukombozi unaogusa uhalisia wa kijamii na kisiasa lakini hauanzii hapo. Unaanza kwa kuikomboa mioyo kutoka utumwa wa dhambi, na mioyo ikishakombolewa basi ukombozi huo utafika tu katika maeneo mengine ya maisha ya mwanadamu.
Somo la pili linakuja katika mazingira tofauti na yale ya somo la kwanza. Ni kipindi cha mwanzo cha ukristo na mitume wanaendelea kuyaweka hai mafundisho ya Kristo kwa watu wake. Tunasoma kutoka waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Watesalonike (1Thes 3:12-4:2) na tunachokiona ni kuwa kwa wakristo hao wa mwanzo, ile dhana kwamba Kristo atarudi tena waliichukulia kwa uzito mkubwa. Siku hiyo waliingoja kwa hamu sana. Kutoka katika matumaini ya ukombozi wa kimwili katika Agano la Kale, hapa matumaini yalikuwa ni ya ukombozi wa kiroho. Mtume Paulo anapowaandikia kuhusu fundisho hili anawakumbusha umuhimu wa kudumu katika upendo na kuishi kwa kumpendeza Bwana ili waifikie siku hiyo bila hatia machoni pa Bwana. Katika somo la Injili (Lk. 21, 25-28. 34-36) ni Yesu mwenyewe anayezungumza kuhusu siku ya ujio wake wa pili. Anataja matukio ya kustaajabisha yatakayoambatana na siku hiyo na anatoa himizo la kukesha. Anasema “kesheni kila wakati mkiomba ili mpatate kuokoka.” Ukombozi ule ulioanza kusubiriwa tangu mwanzo kama kitu kinachotoka moja kwa moja kwa Mungu kuja kwa mwanadamu, sasa unawekwa mikononi mwa mwanadamu mwenyewe kama kitu kinachotegemea jitihada zake. Kwa maana anayekesha na kuomba ndiye atakayeokoka.
TAFAKARI YA JUMAPILI: Ndugu zangu, kuna haja wakati fulani kufikiria juu ya kesho ili kujipanga kuiishi vizuri leo. Ukijua jambo unalolifanya sasa hivi litakuletea matokeo gani siku za usoni itakusaidia sana. Kama matokeo ni mazuri na ndicho unachokitarajia hakuna shaka kwamba bidii na utayari wa kulifanya jambo hilo utaongezeka. Na kama matokeo yajayo si mazuri na siyo unayotarajia, kwa kawaida uzito wa kufanya jambo lenyewe unaweza kuanza kujitokeza. Kipindi hiki cha majilio, na hasa katika dominika hizi mbili za mwanzo, kinakuja katika mfumo unaofanana na huo. Ni kipindi kinachotualika tuyatupie macho mambo ya mbele, mambo ya mwisho yahusuyo maisha yetu na kwa namna hiyo tutaweza kujipanga na kuishi vema sasa ili tuweze kuufikia mwisho huo. Kuna haja ya kupambanua jambo hili: tunapozungumzia mambo ya mwisho tunaamanisha nini hasa? Zipo maana mbili zinazokaribiana. Maana ya kwanza ni ile inayohusu hatima ya maisha ya mwanadamu hapa duniani. Kwamba maisha ya hapa duniani yana mwisho na hivi mwanadamu anaalikwa kuishi akilizingati hilo.
Maana ya pili ni ile inayohusu lengo la maisha yenyewe ya mwanadamu. Kwamba lengo la maisha ya mwanadamu ni kuifikia hali ile aliyoikusudia Mungu wakati anamuumba mwanadamu. Sasa kuzungumza juu ya mambo ya mwisho kunakuwa ni kumualika mwanadamu ayaishi maisha yake akiyaelekeza kulifikia lengo la kuumbwa kwake na lengo la kukombolewa kwake. Kila anachokizungumza Yesu katika Injli ya leo, kinaelekea zaidi katika maana hii ya pili. Anazungumza juu ya ishara zitakazotokea: kutatokea hiki, kutatokea kile…ishara katika jua, mwezi na nyota; mataifa kupata dhiki na ulimwengu kuvurugika vyote vitu vinavyoonekana kutisha na kuleta hofu. Yesu lakini hahitaji kumtia hofu mtu yeyote. Yeye ni mkombozi, sio nabii wa hofu. Yeye anakuja kumnasua mwanadamu kutoka hali zinazomzuia kuishi kadiri ya lengo la kuumbwa kwake. Vitu anavyovitaja ni vile vilivyoonekana kuwa na nguvu juu ya maisha ya mwanadamu, ni vitu vilivyotawala maisha yake: Jua, mwezi na nyota viliabudiwa kama miungu na wapo waliokuwa wakitabiri maisha ya mwanadamu kwa kuangalia mwenendo wa jua, mwandamo wa mwezi au muundo wa nyota.
Anauzungumzia ukombozi kama kuumbwa upya kwa ulimwengu. Ulimwengu wa mwanzo na mfumo wake wote hautamfaa tena mwanadamu. Ili sasa mwanadamu aweze kuufikia mwisho wake, yaani lengo la kuumbwa na kukombolewa kwake, anapaswa kuongozwa na mfumo mpya wa ulimwengu na mfumo huo ni Kristo mwana wa Adamu. Majilio inakuja kutualika kuwa wokovu wetu u karibu. Haya anayoyatangaza leo Kristo ni mambo ambayo Kristo anaendelea kuyatenda kote ulimwenguni na anayatenda ndani yetu siku kwa siku. Kwa maana kila tunapoendelea kudumu katika sala, katika sakramenti na katika ushuhuda wa maisha ya ukristo, kazi ya Kristo ya ukombozi inaendelea kutendeka ndani yetu. Nawatakia Majilio njema.