Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio: Mungu ni Mwaminifu Kweli!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio mwaka C wa Kanisa. Tumemaliza mwaka B katika Liturujia ya Kanisa na tunaanza mwaka mpya C wa Kiliturujia kwa kipindi cha majilio. Katika Kalenda ya Liturujia, Kanisa limetenga kipindi hiki kwa ajili ya maandalizi ya kumpokea Mungu anayekuja kwetu katika Nafsi yake ya Pili Mungu Mwana, Bwana wetu Yesu Kristo, akiwa katika umbo na hali ya kibinadamu kwa njia ya umwilisho mwilini mwa Mama Bikira Maria. Kipindi hiki kinaitwa majilio. Neno majilio lilivyotumika tangu zamani lina maana mbili: Kwanza lilitumiwa na wapagani kumaanisha ujio wa miungu yao, katika siku maalumu ambapo walionesha sanamu za miungu yao ili kuzisujudia na kuziabudu, ziwapatie baraka na fanaka. Pili neno majilio lilimaanisha mda wa maandalizi kwa “ziara rasmi ya mfalme”. Wakristo wa mwanzo walichukua maana hizo kumaanisha ujio wa Mungu wetu wa kweli hapa duniani ambaye amejifunua na kujidhihirisha mwenyewe katika nafsi ya Mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo na pili kumaanisha kipindi cha maandalizi ya ziara ya Mungu kwetu sisi wanadamu.
Kumbe, majilio kwetu ni kipindi cha kuandaa mazingira ya kiroho ili kumpokea Yesu Kristo, Emanueli; Mungu pamoja nasi. Kipindi hiki cha majilio kimegawanywa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza huanza na Dominika ya kwanza ya Majilio na huishia tarehe 16 Desemba. Katika sehemu hii, Kanisa linatualika kutafakari juu ya ujio wa pili wa Kristo katika utukufu wake. Sehemu ya pili huanza tarehe 17 hadi 24 Desemba. Masomo ya sehemu hii yanatuongoza kutafakari juu ya ujio wa kwanza wa Yesu Kristo. Liturujia na masomo ya sehemu hii yatukumbusha zile siku Waisraeli walipokuwa wakimsubiri mkombozi. Ni wakati wa matayarisho ya sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo katika historia ya maisha ya mwanadamu. Kumbe katika jumapili ya kwanza ya majilio tunaanza tafakari ya sehemu ya kwanza kama masomo yanavyotuongoza na kutuelekeza kuhusu habari za ujio wa pili wa Yesu katika utukufu. Lakini kabla ya kuzama katika tafakari ya masomo haya ni vyema kuchukua tahadhari. Kuna uwezekano wa kufikiri na kudhani kuwa hakuna jipya katika kipindi hiki na kipindi kilichopita cha mwaka wa kiliturujia.
Tukumbuke kuwa kila adhimisho la tukio lolote la kiliturujia katika historia ya wokovu wa mwanadamu linapoadhimishwa katika mzunguko wa mwaka wa Liturujia wa Kanisa lina hali mbili; kwanza kutukumbusha yaliyotokea katika historia ya ukombozi wetu na pili kuhuisha na kupyaisha maisha yetu ya kiroho katika kumfusa Kristo. Kumbe kila mwaka wa kiliturujia ni mpya na wa pekee na hakuna unaofanana na mwingine, maana kila mwaka unapyaisha na kuhuisha maisha yetu ya kiroho na hivyo kutuleta karibu zaidi kwa Mungu. Daima tukumbuke kuwa matukio yote ya kiliturujia tunayoadhimisha zaidi ya kutukumbusha yaliyotokea zamani, pia yanafanya sehemu ya maisha yetu na yanatufanya tuonje upendo wa Mungu katika mafumbo yanayoadhimishwa katika kila hatua ya maisha yetu hapa duniani tupoelekea maisha ya umilele huko mbinguni. Kumbe tusikianze kipindi hiki kwa mazoea kana kwamba hakuna jipya lolote bali kwa moyo wa usikivu tufungue macho na masikio ya mioyo yetu tuweze kujichotea neema na baraka zitokanazo na kipindi hiki kwa njia ya Yesu Kristo Bwana na Mwokozi wa maisha yetu.
Nabii Yeremia katika somo la kwanza (Yer. 33:14-16); anatukumbusha uaminifu wa Mungu katika ahadi zake. Ahadi kuu ya Mungu ni kutuletea Mkombozi atakayeleta amani na haki. Nabii Yeremia ambaye aliteuliwa na Mungu kwa utume wa kinabii akiwa na umri mdogo kabisa (miaka 22), ni mmoja miongoni mwa manabii wakumbwa katika Agano la Kale. Yeremia alitumwa kupeleka ujumbe wa Mungu kwa wafalme na watu wa Israeli waliojikita zaidi katika mambo ya siasa na ustawi wao kiasi cha kumsahau na kumuasi Mungu. Ujumbe wa Mungu kwa kinywa cha Yeremia ni kuwaita watu wake wamrudie wawe watakatifu. Kutokana na ugumu wa mioyo yao, watu hawa hawakumsikiliza na mapato yake walikumbwa na madhulumu na kupelekwa utumwani. Sehemu ya Maandiko Matakatifu tunayoyasoma domenika ya kwanza ya majilio ni ya wakati ule mji wa Yerusalemu unateketezwa na watu kuchukuliwa mateka huko Babiloni mnamo mwaka 587 K.K. Tafrani hiyo ilitabiriwa kama hawatamrudia Mungu. Ujumbe wa Yeremia kwa waisreaeli u-wazi; Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake licha ya maasi yao na kukengeuka kiasi cha kukosa uaminifu kwake. Uaminifu wa Mungu kwa ahadi zake unatimia kwa ujio wa Mkombozi wetu Yesu Kristo, katika historia na kila tunapofungua mioyo yetu kumpokea katika maadhimisho ya kisakramenti nyakati zetu.
Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake wa Kwanza kwa Wathesalonike (1Tes. 3:12-13; 4:1-2); anawapongeza Wathesalonike kwa bidii yao ya imani na upendo wao kwa Yesu Kristo. Mtume Paulo anaiandikia jumuiya hii ya waamini katika mji wa Thesalonike aliyoianzisha wakati wa safari yake ya pili ya kimisionari mnamo mwaka 50 BK (Mdo 17:1-11). Kihistoria, mji wa Thesalonike ulioko kaskazini-mashariki mwa nchi ya Ugiriki, ulikuwa chini ya utawala wa Warumi kuanzia mwaka 140KK. Umaarufu wa Thesalonike ulitokana na kuwa kwake makao makuu ya mkoa wa Makedonia. Mji huo ulibahatika kuwa na bandari nzuri pamoja na barabara nzuri iliyounganisha nchi za Magharibi na Mashariki. Wakazi wa Thesalonike walijumuisha Wagiriki, Warumi na Wayahudi. Mataifa haya yote yaliingiza imani na madhehebu ya dini zao. Mtume Paulo alipoingia Thesalonike alihubiri katika Sinagogi la Wayahudi. Watu wengi walipokea ujumbe wa Mungu kwa kinywa cha Paulo. Lakini viongozi Wayahudi katika Sinagogi waliona wivu na kufanya ghasia za kumwondoa Paulo katika mji wao. Paulo na wasaidizi wake waliondoka Thesalonike wakaendelea na safari ya kutangaza habari njema ya wokovu, wakapitia mji wa Bera hadi mji wa Athene. Toka mjini Athene Paulo alimtuma Timotheo aende Thesalonike ili akaone na kutathimini maendeleo ya mbegu ya imani aliyoipanda.
Wakati Timotheo anaelekea Thesasonike, Paulo aliendelea na safari mpaka mji wa Korintho na kumsubiri mjumbe wake Timotheo arudi toka Thesalonike. Baada ya kujionea hali halisi ya mbegu ya imani huko Thesalonike, Timotheo alienda Korintho alikokuwa Paulo na kumpa ripoti kuwa waamini waliendelea kushika imani aliyoipanda licha ya mateso walinayopata. Lakini pia baadhi ya waamini walipata huzuni kuona wenzao wanakufa kabla ya kushuhudia ujio wa pili wa Yesu Kristo. Hali hii ilimsukuma Paulo aandike barua kwa Kanisa la Thesalonike: Kwanza, kuwashukuru na kuwapongeza kwa kuipokea na kuendelea kuizingatia imani hata katika mazingira magumu. Pili, kuwatuliza na kuwafariji waliofiwa na ndugu zao akiwaeleza habari za ujio wa pili wa Yesu Kristo ambapo waamini wote wazima na wafu, watakavyoshiriki katika tukio hilo. Tatu, kuwaasa waamini waepukane na utovu wa maadili. Kumbe basi, Mtume Paulo anatuhimiza tuendelee kuishi katika pendo la Kristo katika kipindi hiki cha majilio ili Kristo ahuishwe ndani mwetu.
Himizo la Mtume Paulo ni sala ya kutuombea akisema; “Bwana na awaongoze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote.” Kipindi hiki cha majilio ni kipindi cha kuongeza bidii katika sala na kujitahidi kuuishi upendo wa kikristo na kudumisha zaidi amani na kuishi kwa pamoja na umoja. Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk.21:25-28,34-36); inatueleza mambo ya kutisha na kuogofya yatakayotokea wakati wa ujio wa pili wa Yesu Kristo kama mshindi wa ulimwengu baada ya ule wa kwanza iliposherehekewa Noeli ya kwanza kule Betlehemu ya Uyahudi. Mambo yanayoambatana na kuonekana kwa Mwana wa Adamu ni pamoja na dhiki, uvumi wa bahari na msukosuko wake, kuvunjika mioyo kwa hofu ya kuona mambo yanayoupata ulimwengu. Ni wazi kuwa kunapokuwa na tafrani watu hukimbia kujificha. Lakini mwinjili Luka anatuambia kuwa mambo hayo yaanzapo kutokea, tuchangamke, tuviinue vichwa vyetu.
Kwanini? Kwa sababu ukombozi wetu umekaribia. Lakini kuna masharti; kujiangalia mioyo yetu isilemewe na ulafi, ulevi, na masumbufu ya maisha haya kwasababu “siku ile itakuja ghafula. Hivyo basi, tunapaswa kukesha, kuwa tayari wakati wote. Kumbe unabii wa Nabii Yeremia unatuaminisha kuwa haya yote ni kweli na yatatokea kweli maana Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake. Paulo katika somo la pili na Luka katika Injili wanatualika kutathimini matendo yetu ili siku ya kiyama itakapowadia katu tusiiogope kwani siku hiyo ndio mwanzo wa maisha mapya ya huko mbinguni. Hivyo basi, tunapaswa kuuangalia vizuri mwenendo wetu wa maisha hapa duniani katika kipindi hiki cha majilio, tukijiweka daima tayari kumpokea Emanueli Mungu pamoja nasi siku ya Noeli. Lakini tukumbuke kuwa maisha yote ya mkristo ni kipindi cha majilio, yaani mwendelezo wa kumsubiri Kristo hadi atakapokuja tena kutuita kwa njia ya kifo. Nawatakia mwanzo mwema wa mwaka mpya wa kiliturujia na majilio mema tujiandae vyema kiroho ili Kristo aje azaliwe ndani ya mioyo yetu na kutuhuisha katika maisha ya kiroho kwa kutuweka karibu zaidi na Mungu Baba yetu.