Tafuta

Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu! Huu ni Ufalme wa: Kweli, uzima, utakatifu, neema, haki, amani na mapendo. Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu! Huu ni Ufalme wa: Kweli, uzima, utakatifu, neema, haki, amani na mapendo. 

Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme: Ukweli, Haki, Amani na Mapendo!

Kristo Yesu ni sadaka safi iletayo amani na utulivu moyoni ili kukamilisha kazi nzima ya ukombozi kwa kuviweka vitu vyote chini ya utawala wa Ufalme wa Kristo Yesu. Huu ni Ufalme wa: Kweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki, Amani na Mapendo. Sherehe hii ilianzishwa rasmi na Papa Pius XI, kunako tarehe 11 Novemba 1925 na kutangazwa katika Waraka wake wa kitume “Quas Primas”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu inayoadhimishwa Jumapili ya 34 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Siku ya Wavuvi Duniani huadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Novemba. Kwa mara ya kwanza Siku hii iliadhimishwa kunako mwaka 1998. Lengo ni kuwaenzi wavuvi wanaotekeleza wajibu wao katika mazingira magumu na hatarishi na kwamba, wanachangamotishwa kuwa makini katika matumizi ya rasilimali iliyoko majini, ili iweze kuwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Leo pia tunaadhimisha Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya kijimbo au kwenye Makanisa mahalia. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Mwaka 2021 unanogeshwa na kauli mbiu “Inuka. Nimekuteua uwe Shahidi wa mambo haya uliyoyaona.” Mdo 26: 16.

Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anagusia changamoto ambazo zimejitokeza kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na umuhimu wa kuinuka na kuendelea na safari ya maisha kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ngazi ya Kijimbo kwa Mwaka 2021 yanaongozwa na ushuhuda wa Mtakatifu Paulo Mtume mbele ya Mfalme Agripa, baada ya kukutana na Kristo Yesu Mfufuka na kujitambulisha kwake akisema kuwa ni Yesu Mnazareti, kweli mang’amuzi haya yana umiza. Baba Mtakatifu anawataka vijana kutambua upofu wa maisha yao, kuwa tayari kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, na hatimaye kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ni muda muafaka kwa vijana kuinuka na kuanza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Huu ni wakati wa kuinuka na kuanza kusherehekea Siku ya Vijana Ngazi ya Kijimbo!

Kristo Yesu ndiye Masiha na Mpakwa wa Bwana, aliyejisadaka Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, na hivyo kumshikirisha maisha ya uzima wa milele. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba,  Kristo Yesu ni sadaka safi iletayo amani na utulivu moyoni ili kukamilisha kazi nzima ya ukombozi kwa kuviweka vitu vyote chini ya utawala wa Ufalme wa Kristo Yesu.  Huu ni Ufalme wa: Kweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki, Amani na Mapendo. Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu ilianzishwa rasmi na Papa Pius XI, kunako tarehe 11 Novemba 1925 na kutangazwa katika Waraka wake wa kitume “Quas Primas”. Sherehe hii ni kilele cha kazi nzima ya ukombozi wa mwanadamu ambayo Kanisa limeadhimisha katika Mafumbo na Liturujia na kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mfalme wa ulimwengu pamoja na kuualika ulimwengu mzima kutambua kuwa hija ya maisha ya hapa duniani inahitimishwa katika ufalme wa Kristo Yesu aliye “Jana na Leo, Alfa na Omega”, mwanzo na mwisho, nyakati zote ni zake!

Papa Pius XI katika maadhimisho haya anawaalika waamini kuwa ni mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hii ni fursa ya kuendelea kujifunza na kumwilisha tunu msingi zinazofumbatwa katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa ulimwenguni, kwa kujikita katika Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Maadhimisho haya ni katekesi endelevu na fungamani katika masuala ya: haki, amani, ukweli na upendo.

Ni Sherehe inayoadhimishwa Dominika ili kutoa nafasi kwa waamini kushiriki kikamilifu kama sehemu ya ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na kwa njia ya Liturujia waweze kutakatifuzwa na hatimaye, waweze kufika mbinguni. Itakumbukwa kwamba, hii ni Sherehe ambayo imeanzishwa mara tu baada ya Vita kuu ya Kwanza ya Dunia. Kumbe, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanapaswa kusimama kidete ili kulinda uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; haki na utakatifu wa maisha. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Yeye ni Bwana wa historia na viumbe vyote na hatima ya yote haya ni ufalme wa Kristo Yesu aliyedhalilishwa kwa kukamatwa, kuteswa na hatimaye kufa Msalabani kana kwamba, alikua anawania madaraka ya kisiasa, yaani, kuwa ni mfalme wa Wayahudi!

Ni katika muktadha huu, Pilato alimuuliza Yesu mara mbili, ikiwa kama kweli Yeye ni Mfalme! Leo hii waamini wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda wa imani kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo; ili kupandikiza mbegu ya upendo kati ya watu wa Mataifa; kwa kuondokana na ubinafsi, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kupata furaha ya kweli katika maisha. Ufalme wa Mungu haufumbatwi kamwe katika chuki, hasira,vurugu, fujo na vita na ndiyo maana wafuasi wake, hawakupigana vita ili kumlinda! Yesu anakaza kusema, ikiwa kama ufalme wake ungekuwa ni wa ulimwengu huu, watumishi wake wangelimpigania, ili asitiwe mikononi mwa Wayahudi. Hapa Yesu alitaka kuonesha kwamba, Mwenyezi Mungu ni mkuu na ana nguvu zaidi kuliko viongozi wa kisiasa na kwamba, ufalme wake haujengwi kwa nguvu za kibinadamu! Kristo Yesu amezaliwa kwa ajili ya hayo, ili kuonesha nguvu ya upendo wa Mungu unaoganga na kuokoa ili kushuhudia kushuhudia kweli.

Huu ndio ukweli wa Kimungu na kiini cha Injili, kwamba, Mungu ni upendo na anataka kuanzisha na kujenga ufalme wa: upendo, haki na amani utakaodumu hadi mwisho wa nyakati! Historia inaonesha kwamba, falme ambazo zimejengwa kwa nguvu ya “mtutu wa bunduki na ncha za upanga zimedumu kwa kitambo na mwishowe, zitaporomoka na kutoweka katika uso wa dunia! Ufalme wa Mungu unafumbatwa katika misingi ya ukweli, uzima, utakatifu, neema, haki, upendo na amani na kujikita katika sakafu ya nyoyo za watu na hivyo kuwakirimia wote wanaoupokea amani, uhuru wa kweli na utimilifu wa maisha. Binadamu wataweza kupata: amani, uhuru na utimilifu wa maisha ikiwa kama watatoa nafasi kwa upendo na ufalme wa Mungu uweze kukita mizizi katika nyoyo zao; ikiwa kama ufalme wa Kristo utazamisha mizizi yake katika nyoyo za watu, watafanikiwa kupata amani, uhuru na utimilifu wa maisha!

Changamoto kubwa ni kumwachia nafasi ili Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu aweze kutawala katika nyoyo zao! Huyu ndiye ambaye kwa njia ya maisha, maneno na matendo yake ametundikwa Msalabani, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Fumbo la Msalaba linaonesha dira na mwongozo wa maisha kwa watu waliopoteza dira na kuanza kutembea katika hofu na mashaka yanayowaandama mwanadamu kila kukicha. Ufalme wa Kristo Yesu si wa ulimwengu huu, kwani ana uwezo wa kutoa mwelekeo mpya wa maisha, hata katika majaribu na mashaka, jambo la msingi ni kufuata katiba ya maisha yake yaani upendo kwa Mungu na jirani. Tunatafakari mambo ya nyakati kwa kuwa macho dhidi ya manabii wa uwongo; majanga asilia, vita na kinzani; dhuluma na mauaji; matunda ya dhambi za wanadamu. Katika muktadha kama huu waamini wanahimizwa kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, haki na amani; tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hatima na mustakabali wa maisha ya mwanadamu uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma ya Baba wa milele mwaliko kwa waamini ni kuendelea kuwa ni mashuhuda wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: Ukweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki, Mapendo na Amani.

Kristo Mfalme
19 November 2021, 15:04