Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 32 ya Mwaka B wa Kanisa: Sadaka na ukarimu wa wanawake wajane na maskini: Ibada ya kweli inasimikwa katika: imani, haki, utu na heshima ya binadamu! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 32 ya Mwaka B wa Kanisa: Sadaka na ukarimu wa wanawake wajane na maskini: Ibada ya kweli inasimikwa katika: imani, haki, utu na heshima ya binadamu! 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili 32: Sadaka na Ukarimu wa Wajane!

Ibada na Sala ya kweli inafumbatwa katika misingi ya haki, amani, utu, heshima, imani na unyenyekevu; mambo msingi yanayofafanuliwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 32 ya Mwaka B wa Kanisa! Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza, Inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake! AMECEA inazindua mchakato wa maadhimisho yake kwa Mwaka 2022!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 32 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Upendo na ukarimu kwa maskini kwa ajili ya maskini wenzao ni ushuhuda wa hali ya juu kabisa wa imani. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza moyo wa upendo, ukarimu, unyenyekevu na imani thabiti, ili kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kama alivyofanya yule mwanamke mjane wa Sarepta na mjane na maskini anayesimuliwa katika Injili ya Marko. Ibada na Sala ya kweli inafumbatwa katika misingi ya haki, amani, utu, heshima, imani na unyenyekevu; mambo msingi yanayofafanuliwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 32 ya Mwaka B wa Kanisa! Kristo Yesu mwanzoni kabisa mwa Injili Mk 12: 38-44 anatoa onyo akisema: “Jihadharini!” kwa lugha ya Kigiriki ni “βλέπετε” “blepete” hii ni amri inayowataka wafuasi wa Kristo Yesu kujihadhari, kuwaogopa, kuwa macho, ili wasitumbukie katika mtego wa Waandishi na Mafarisayo kwani hawa “wanapenda kutembea wamevaa mavazi marefu.” Hayo ni mavazi ya pekee yanayowatofautisha na watu wengine.

Alama ya pili inayowatofautisha na wengine ni “Kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu,” yaani wanapenda heshima ya pekee anayostahili kupewa Mwenyezi Mungu peke yake aliye Muumba na Mkombozi. Kristo Yesu anawataka  wanafunzi wake wawe ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma ya upendo, huruma na ukarimu unaofumbatwa katika unyenyekevu. Alama ya tatu ni kuwa “Hula nyumba za wajane.” Hawa wajane walikuwa ni maskini na wanyonge, ni watu waliokuwa wanaishi kwa kudra ya Mwenyezi Mungu. Waandishi walikuwa wanawanyonya kwa kupokea ufadhili toka kwao. Alama ya nne, “kwa unafiki husali sala ndefu.” Huo ni unafiki mbele ya Mungu mwenyewe, kwa kusali sala ndefu halafu unadhulumu maskini. Yesu kwa mara ya kwanza anatamka hukumu kwa watu wa aina hiyo kwamba “hao watapata hukumu iliyo kubwa.” Kwa sababu hawa ni watu wanaojihesabia haki na utakatifu wa maisha. Rej. 18:9. Tumekumbushwa kwenye Wimbo wa Kati kati Zab 146: 6-10: Bwana hushika kweli milele huwafanyia hukumu walioonewa huwapa wenye njaa chakula, Naye huwafungua waliofungwa. Bwana huwategemeza yatima na mjane, Bali njia ya wasio haki huipotosha!

Fundisho kuu katika Injili ya leo ni usiri katika kutoa sadaka. Rej. Mt 6:1ff. Kristo Yesu katika hili si kwamba anazuia maisha ya sala, ibada na liturujia, bali kile anacho dai kutoka kwa waamini ni ile njia na moyo safi, mweupe pe “kama tui la nazi”. Mwinjili Marko anatoa kipaumbele cha pekee kwa wanawake kama kielelezo cha imani, sadaka na upendo thabiti. Kuna mkwe wa Petro Mtume, Mwanamke aliyetokwa damu kwa muda wa miaka 12, Msirofoinike, Mwanamke wa Bethania aliyeonesha upendo usiokuwa na mipaka kwa kumpaka marashi Kristo Yesu. Na mwanamke mjane na maskini anayesimuliwa katika Injili ya leo! Darasa linalotolewa na Kristo Yesu kwa wafuasi wake ni kwamba, wajane na maskini wameendelea kuteseka hata katika ulimwengu mamboleo. Jambo la msingi ni kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza kwa kuzingatia utu, heshima na haki zao msingi. Wajane na maskini ni watu wanaojiaminisha kwa urahisi sana katika ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu. Mwanamke mjane maskini akatia pesa mbili kiasi cha nusu pesa. Hii ilikuwa ni siri kubwa kati ya mwanamke mjane na maskini na Mwenyezi Mungu anayeona sirini. Huyu ndiye yule anayewakirimia waja wake: furaha, amani na utulivu wa roho.

Waandishi na Mafarisayo kwa mambo mengi si watu wa kuigwa kwani wanakosa fadhila ya unyenyekevu! Usiogope! Rejea. 1 Fal. 17: 10-16. Mwanamke mjane wa Sarepta aliogopa kutenda ukarimu akihofia maisha yake na yale ya mwanaye. Lakini, alipopiga moyo konde na kutekeleza ombi la Nabii Eliya lile pipa la unga halikupungua wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawa sawa na neno la Bwana alilonena kwa kinywa cha Nabii Eliya. Hapa tunakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu ni mfadhili mkubwa kwa wale wote wanaomtumainia na kujiaminisha kwake kama ilivyokuwa kwa Mwanamke mjane wa Sarepta. Sadaka ya Kristo Yesu, Kuhani Mkuu na wa milele! Ebr. 9:24-28. Kristo Yesu kwa mateso na sadaka yake ya Msalaba, amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Ataraudi tena kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima. Kristo Yesu amejisadaka mwenyewe kwa ajili ya dhambi za binadamu ili kutimiza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni na hivyo sadaka yake inakuwa ni chanzo cha ukombozi.

Hiki ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha mapendo yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huu ni upendo wa ukombozi. Kristo Yesu ndiye yule Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Hiki ni kielelezo cha upendo usiokuwa na kifani. Mateso na hatimaye, kifo cha Kristo Yesu Msalabani ni sadaka ya pekee na halisi. Hii ni sadaka ya Agano Jipya na la milele. Hiki ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utii kwa Baba yake wa mbinguni. Ni sadaka inayopata hitimisho lake Mlimani Kalvari! Na kwa njia hii Kristo Yesu amekuwa ni mpatanishi kati ya Mwenyezi Mungu na mwanadamu. Mababa wa Kanisa wanasema, Msalaba ni ngazi ya kuwafikisha waamini mbinguni. Rej. KKK 599 hadi 618.

Itakumbukwa kwamba, Tarehe 23 Juni kila mwaka ni Siku ya Wajane Kimataifa, ni siku ambayo mataifa duniani kote yanatambua vurugu, ubaguzi na unyanyapaaji unaofanywa dhidi ya wajane na kusherehekea mchango muhimu wa wajane. Ni siku ambayo serikali zote zinatakiwa kuchukua hatua za makusudi kulinda, utu, heshima na haki za wajane. Radio Vatican inapenda kuungana na familia ya Mungu nchini Tanzania kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa Bugando iliyoko Jijini Mwanza, Tanzania. Hospitali hii ilifunguliwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tarehe 3 Novemba 1971. Tunaungana pia na Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania katika uzinduzi wa maadhimisho ya Mkutano wa AMECEA kwa Mwaka 2022 utakaofanyika nchini Tanzania.

Liturujia J32
05 November 2021, 14:19