Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 33 ya Mwaka B wa Kanisa: Jiandaeni vyema kwa ajili ya kukutana na Kristo Yesu hakimu mwenye haki siku ya mwisho! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 33 ya Mwaka B wa Kanisa: Jiandaeni vyema kwa ajili ya kukutana na Kristo Yesu hakimu mwenye haki siku ya mwisho! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 33: Jiandaeni Kwa Hukumu ya Mwisho

Mama Kanisa anatualika kutafakari juu ya siku ya mwisho wa dunia. Ni wakati wa kujichunguza mienendo, mahusiano yetu kwanza na nafsi zetu, pamoja na ndugu zetu na hivi kujiandaa vema kwa ujio wa pili wa Yesu ambapo injili inatudokeza namna siku hiyo itakavyokuja na nini kitaitangulia hiyo siku nasi tujipange vizuri ili siku hiyo itakapokuja tustahili kuingia mbinguni. Yaani!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 33 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Tupo ukingoni mwa mwaka B wa Kanisa. Jumapili ijayo tutaadhimisha Jumapili ya Kristo Mfalme na ndiyo Jumapili ya mwisho ya Mwaka B inayotupa fursa ya kuanza Liturujia ya mwaka C., kwa Jumapili ya kwanza ya Majilio. Ndiyo maana Mama Kanisa anatualika kutafakari juu ya siku ya mwisho wa dunia, yaani mwisho wa maisha yetu hapa duniani. Ni wakati wa kujichunguza mienendo yetu, mahusiano yetu kwanza na nafsi zetu, pamoja na ndugu na jamaa zetu na hivi kujiandaa vema kwa ujio wa pili wa Yesu Kristo ambapo injili ya dominika hii inatudokeza namna siku hiyo itakavyokuja na nini kitaitangulia hiyo siku nasi tujipange vizuri ili siku hiyo itakapokuja tustahili kuingia mbinguni. Kumbe basi, masomo ya domenika hii yanatukumbusha jukumu letu la kuyafanya maisha yetu yafae muda wote kwa kukutana na Mfalme wa haki, Bwana wetu Yesu Kristo katika hukumu ya mwisho.

Somo la kwanza la Kitabu cha Nabii Danieli (12:1-3); ni ufunuo wa Mungu kwa njia ya Nabii Danieli unaotujulisha kuwa baada ya kufa kuna ufufuko wa miili na katika ufufuko huo kila mmoja atahukumiwa ambapo walioishi vema watapata uzima wa milele na walioishi vibaya watapata aibu na madharau yao milele kama anavyosema Danieli; “Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele.” Ni mwaliko kwetu sote wa kujichunguza na kujitafakari namna tunavyoishi; kama maneno na matendo yetu yana kibali machoni pa Mungu ili siku hii ikifika itukute tuko tayari ili tustahilishwe kuingia katika uzima wa milele.

Somo pili la Waraka kwa Waebrania (10:11-14, 18); ni mwendelezo wa mafundisho yanayohusu ukuhani na sadaka za Agano la kale kuwa vimekamilishwa katika ukuhani wa Yesu kwa Sadaka yake msalabani. Somo hili linatueleza kuwa kurudiarudia kwa sadaka za makuhani wa Agano la kale kila mwaka ni kwasababu sadaka hizo zilikuwa hafifu na hazikuweza kuondoa dhambi za watu wote. Lakini Sadaka ya Yesu ilitolewa mara moja tu na iliwatakasa watu wote kwa nyakati zote. Misa Takatifu ni Sadaka ile ile ya Yesu Kristo ambapo kila inapoadhimishwa kama inavyopaswa watu huondolewa dhambi na kutakaswa kama wakitimiza masharti na maagano ya sadaka hii ya Misa Takatifu.

Katika Injili kama ilivyoandikwa na Marko (13:24-32); ni utabiri wa Yesu juu ya uangamizi wa Yerusalemu ambao ni mfano wa mwisho wa dunia. Siku hiyo Yesu Kristo atawahukumu watu wote. Atawakusanya wateule wake na kuwaingiza katika uzima wa milele na wabaya atawaadhibu. Yesu pia anatueleza namna siku hiyo itakavyokuwa na matukio yatakayotokea kabla (Mk 13:24–27). Matukio hayo ya ajabu ni kama vile; jua kutiwa giza, mwezi kutotoa mwanga wake na nyota kuanguka chini. Katika hali hiyo, Yesu anawaambia wanafunzi wake kuwa watamwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. Mahali pengine Kristo anafafanua zaidi kuwa siku hiyo itakapotokea watu watakuwa katika shughuli zao za kila siku (Mt 24:36). Ili tukio hilo lisije kuwa la ghafla kwao Yesu aliwaambia wanafunzi wake; wajiweke tayari, kwa kuwa katika saa wasiyoidhania Mwana wa Adamu yuaja” (Mt 24:44). Kumbe sote tunaalikwa kujiweka tayari mda wote kukikabili kifo na adhabu ya mwisho kwa kutenda mema kila siku. Na huko ndiko kukesha kama watu wanaomngojea Bwana wao atakaporudi (Lk 12:35-36).

Sehemu hii ya injili inatukumbusha mafundisho ya Maandiko Matakatifu yanayohusu hukumu ya mwisho kuwa sisi binadamu tunakabiliwa na hukumu mbili baada ya maisha yetu hapa duniani. Kuna hukumu ya kwanza ambayo ni hukumu binafsi na hukumu ya pili au ya mwisho inayowahusu watu wote. Hukumu ya kwanza ni tendo la Mungu kumpa mtu haki yake kulingana na matendo yake na imani yake mara baada ya kifo chake (Lk 23:43; KKK: 1022): Katika hukumu hii roho ya mtu peke yake ndiyo inayohukumiwa. Hukumu ya mwisho itatanguliwa na ufufuko wa watu wote wenye haki na wasio na haki pia (Mdo 24:15). Siku hiyo roho zitaungana na miili yake halisi, kisha walio wema watatengwa kwa uzima wa milele, na waovu kwa hukumu ya milele (Yn 5:28–29). Maandiko Matakatifu yanatuelekeza kuwa, katika hukumu ya mwisho ufalme wa Mungu utapata utimilifu wake; wenye haki watatawala daima pamoja na Kristo, wakiwa wametukuzwa mwili na roho. Suala hili la hukumu ya mwisho halikuwa jambo geni kwa Waisraeli. Tangu manabii wa kale hata Yohane Mbatizaji, wote walihubiri juu ya uwepo wa hukumu hii hata kabla ya Kristo kuja (Dan 7:10, Mal 4:1–3, Mt 3:7–12), kama nabii Danieli anavyotueleza katika somo la kwanza juu ya ufufuko wa miili ili ipate kuhukumiwa pamoja na roho zake (Dan 12:1-3).

Yawezekana wakawepo wenye mashaka juu ya ukweli wa fundisho hili la hukumu ya mwisho kwa kuangalia jinsi wadhambi wanavyostawi na kunawiri. Tukumbuke maneno ya Yesu kuhusu hukumu ya mwisho; “Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno, na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao; Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome moto; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu” (Mt 13:30). Katika mfano huu; ngano ni watu wema na magugu ni watu waovu. Na kawaida magugu ndiyo yanayokua haraka kuliko mimea iliyopandwa. Basi tujitahidi kuishi vyema huku tukijua ya kuwa ujio wa pili wa Kristo hautafuta tena dhambi zetu, bali utaleta hukumu (1Kor 1:8; Rum 2:6). Hii ina maana kuwa hakutakuwa na nafasi tena ya kutubu wala kuomba msamaha. Basi tumwombe Bwana wetu Yesu Kristo atusaidie katika juhudi zetu za kujiandaa kwa hukumu ya mwisho kwa kutenda mema na kuacha dhambi.

Tafakari J33
11 November 2021, 16:34