Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 33 Mwaka B: Yesu Kristo Jua la Haki!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Mwinjili Marko wakati anaandika sehemu ya Injili ya leo, himaya ya Kirumi ilikuwa imetoka katika vita na mabalaa mengi, mfano magonjwa ya milipuko na uvamizi wa wadudu katika mashamba yao. Si tu himaya ya Kirumi bali hata Jumuiya ya Wakristo katika himaya ile walikuwa wametoka kupitia kipindi kigumu cha mateso na madhurumu ya Mfalme Nero, aliyewatesa na kuwaua Wakristo wale wa kwanza. Hivyo katika mazingira ya namna hii magumu na yenye mateso mengi waamini walikuwa wanajiuliza nini maana ya haya yote na kwa nini wanapitia hayo yote. Hata nasi leo dunia nzima tunajiuliza maswali mengi mintarafu janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kwa nini Mungu anaruhusu tujaribiwe, tupatwe na kupitia kipindi kigumu namna hii? Nini hasa maana na lengo lake? Mwinjili Marko ni katika mazingira ya namna hii anaandika sehemu ya Injili hii ya leo yenye aina ya uandishi ya kiapokaliptiko. Apokaliptiko ni neno lenye asili ya Kigiriki litokanalo na maneno mawili ambayo ni apo likimaanisha kuweka mbali au tenganisha, pamoja na kaliptiko likimaanisha weka bayana. Hivyo aina ya uandishi ya kiapoliptiko ni ile inayotumia lugha isiyo kuwa wazi sana, au lugha ya mficho hivyo kupata ujumbe wake ni lazima kufunua au kufumbua mafumbo na lugha ile ya mficho.
Na huo ndio mwaliko wa Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya leo anapotuonya tusidanganyike tunapoona mambo hayo yakitokea katika ulimwengu wetu. Hata katika nyakati zetu kuna mengi yanayotokea na hata mara kadhaa kushawishika kusema mwisho wa dunia umekaribia. Hiyo pia ilikuwa ni hofu ya Wakristo wale wa mwanzo, hivyo mwinjili anaona hitaji la kuwaandikia ujumbe huu wa kiapokaliptiko. Marko mwinjili anatumia lugha ya picha ya kiapokaliptiko kama jua na mwezi na ishara nyingine za angani. Kwa watu wa Mashariki ya kati walikuwa wanaabudu ishara za angani kama jua na mwezi kama miungu yao, na hivyo hata kutolea sadaka pale wanapoona kuwa mambo yao yanakwenda kinyume na matarajio yao. Rejea Kumbukumbu la Torati 4:19 ambapo Musa anawaalika Wanawaisraeli kumwabudu Mungu wa kweli na sio nyota au jua au mwezi wa angani. Hata Nabii Isaya 13:10; 34:4 pia anaawalika kumwabudu Mungu wa kweli na si nyota wala jua wala mwezi. “Nyota na vilimia vyake angani hazitaangaza; jua linapochomoza litakuwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake” (Isaya 13:10) Ujumbe huu haukuwa kwa ajili ya kuwatisha na kuwaogofya kuwa jua na mwezi na nyota zitaacha kutoa mwanga wake wa asili, bali kuwatia matumaini kuwa nuru na mwanga wa kweli unatoka kwa Mungu mwenyewe na si katika vitu vya angani. Hivyo ni ujumbe wa furaha na matumaini. Mwanga na nuru ya kweli ni Yesu Kristo mwenyewe katika maisha ya kila mfuasi wake.
Na ndio mwinjili Marko anaandika sehemu hii ya Injili yake ambapo Yesu Kristo anatumia pia lugha hii ya kiapokaliptiko kwa lengo la kuwafariji waamini wanaopitia kipindi kigumu cha mateso na madhurumu. Na hata kwetu leo ni neno la faraja na matumaini hata kama tunakuwa katika kipindi chenye magumu na changamoto nyingi katika maisha ya kila mmoja wetu. Ni kawaida kujiuliza maswali nini maana ya magumu na mateso katika maisha yetu, na hata tunapojibidisha kusali na kuwa waaminifu katika imani yetu, bado tunakutwa na mahangaiko katika maisha ya siku kwa siku. Nini maana ya mateso, kwa nini mateso katika maisha ya ufuasi? Tunaalikwa kunyanyua vichwa juu kwani wokovu wetu unakaribia, ulimwengu mpya wa ufalme wake Mungu. Mwanzo mpya ambapo mtawala mpya ni Mungu mwenyewe anayetaka kukaa na kuwaongoza watu wake. Ni mwanzo wa ufalme wa Upendo, Amani na Haki. Dhiki, jua kutiwa giza, mwezi kukoma kutoa mwanga wake, nyota zikianguka na nguvu za mbinguni kutikisika, zote hizi ni ishara ya yule muovu na uovu ulimwenguni. Ni kwa ujio wa Yesu Kristo ulimwenguni basi yule muovu na uovu hauna nguvu tena, hauna nafasi tena kwani tunaalikwa kuunda ulimwengu mpya, ndio ufalme wa Mungu kati yetu, katika maisha yetu.
Ni ujumbe wa faraja kuwa Mungu mwenyewe atamtuma malaika wake, hapa malaika pia ni lugha ya kiapokaliptiko likimaanisha mjumbe wa Mungu ambaye ujio wake sio kuja kuhukumu ulimwengu bali kuwaunganisha wana wake kutoka pande zote za dunia baada ya kutawanywa na yule mwovu. Mwana wa mtu hataruhusu wapotee bali atawakusanya wote. Ni mjumbe wa Habari Njema ya wokovu kwa watu wote bila ubaguzi wa aina yeyote, mjumbe huyu ndio kila mmoja wetu anaposhiriki katika kueeneza Ufalme wa Mungu hapa duniani, kuwa wajumbe wa kweli za Injili kwa maneno na matendo yetu. Pia neno malaika katika Maandiko Matakatifu si tu linamaanisha viumbe wale wenye roho tupu bali kila mmoja anayekuwa mjumbe au mpelekaji wa Habari Njema ya Mungu. Ni yule anayekubali kutumika katika mpango wake Mwenyezi Mungu. Musa aliyewaongoza wanawaisraeli kutoka nchi ile ya utumwa anatambulishwa kama malaika (Kutoka 23:20,23) na hata mwanzoni wa Injili ya Marko, tunaona Yohane Mbatizaji anatambulishwa kama malaika. (Marko 1:2) Hivyo malaika inamaanisha kila mmoja wetu anayekubali kutumika kama mjumbe wa Habari Njema ya Mungu iwe kwa maneno au kwa maisha ya ushahidi.
Ni katika muktadha huo kama nilivyotangulia kusema hapo juu, Mwinjili Marko anawaandikia Wakristo wale waliokuwa wanapitia mateso na madhulumu mengi, na hata baadhi yao kufa kifodini kama mashahidi wa imani yao, na hata kati yao kuwa na migawanyiko na magomvi kiasi hata cha kupelekani kwenye mahakama za Wapagani. Ni jumuiya ile inayokuwa mbali na ile ya mwanzo kabisa waliyodumu katika roho na moyo mmoja. (Matendo ya Mitume 4:32) Ni jumuiya inayoona bado inazungukwa na uovu mwingi, na hivi wanahitaji neno la matumaini na kuwaimarisha tena katika safari yao ya imani. Na ndio Mwinjili Marko anawakikishia kuwa Mungu atamtuma malaika wake, mjumbe wake ili kuweza kuwaleta pamoja kutoka pande zote nne za dunia. Na Yesu Kristo pia anatumia mfano wa mtini uliokuwa unaeleweka vizuri kwa wasikilizaji wake waliokuwa na majira mbalimbali ya hali ya hewa katika mwaka. Miti upukutisha majani yake wakati wa majira ya baridi kali na inaanza tena kuchipua mara pale kipindi cha baridi kinapokwisha, na ndio huwa wakati wa mavuno. Hivyo na Yesu Kristo katika sehemu ya pili ya Injili ya leo anatumia lugha hiyo ya mtini kama ujumbe wa matumaini, ni pale mtini unapoanza kuchipua majani basi mkulima anakuwa na matumaini ya kupata mavuno.
Kuchipua kwa mtini ni dalili ya majira na mwanzo mpya wa matumaini na furaha, ndio kipindi cha neema na kipindi cha baraka. Daima hatuna budi kunyanyua sura zetu kwa matumaini na imani kuu hata kama kwa sasa tunapaswa kupitia nyakati ngumu na zenye changamoto mintarafu imani yetu. Wapendwa ni vema kutambua kuwa hata katika nyakati ngumu daima tunaalikwa kumwangalia Yesu Kristo Mwenyewe aliye nuru na mwanga wetu wa kweli. Ujumbe wa Injili ya leo sio ujumbe wa kutuogopesha bali kutujaza matumaini na faraja kuwa Yeye daima yupo pamoja nasi. Uwepo wake ni mwanzo wa majira mapya, majira ya mavuno, ni majira ya kuukaribisha ufalme wake utawale na kuongoza maisha yetu ya siku kwa siku. Ni wakati wa neema na baraka. Nawatakia Dominika njema.