Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio: Matumaini na furaha ya kweli kwa kukesha na kungojea ujio wa Kristo Yesu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio: Matumaini na furaha ya kweli kwa kukesha na kungojea ujio wa Kristo Yesu. 

Jumapili ya Kwanza Kipindi cha Majilio: Matumaini na Furaha Ya Kweli

Dominika ya kwanza ya Majilio ndio mwanzo wa mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa; Ni wakati wa kungojea ujio wa kuzaliwa kwake Yesu Kristo kwa imani iliyojaa matumaini makubwa. Ni kipindi cha neema, matumaini na furaha kwa ujio wake Mwana pekee wa Mungu, anayekuja na kukaa nasi, kusafiri na kutembea pamoja na Kanisa lake siku zote mpaka mwisho wa dahari. Ujio wa Yesu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Dominika ya kwanza ya Majilio ndio mwanzo wa mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa; Ni wakati wa kungojea ujio wa kuzaliwa kwake Bwana na Mkombozi wetu, Yesu Kristo kwa imani iliyojaa matumaini makubwa. Ni kipindi cha neema, kwani tunaalikwa kuwa na matumaini na furaha kwa ujio wake Mwana pekee wa Mungu, anayekuja na kukaa nasi, kusafiri na kutembea pamoja na Kanisa lake siku zote mpaka mwisho wa dahari. Sehemu ya Injili ya leo, Lk 21: 25-28, 34-36 tunapoisoma tunabaki na mashaka na hata hofu kubwa, maana mara nyingi wengi wanaitafsiri kama kuonesha jinsi hali itakavyokuwa itakapofika mwisho wa ulimwengu.  Kama ndivyo basi tunabaki na hofu na woga mkubwa ndani mwetu, badala ya matumaini na faraja tunapongojea ujio wake Bwana na Mkombozi wetu, Yesu Kristo. Kama lengo na shabaha ya Yesu Kristo ni hilo la kutuachia hofu na mashaka, basi nia yake ya kuja ulimwenguni haitakuwa imetimia. Yesu Kristo haji ili sisi tubaki na wasiwasi na woga na mashaka, badala yake kutuweka huru kutoka mashaka yote, na kutujaza furaha ya kweli na matumaini. Ni Habari njema inayokuja kati ya wanadamu na sio habari ya kutuangamiza na kututeketeza, anayekuja ni Bwana na Mwokozi wetu, ni Upendo na Huruma ya Mungu mwenyewe kati yetu na si kinyume chake. Ni Mungu Mwokozi na Mkombozi anayekuja ulimwenguni na si kinyume chake.

Na ndio maana nawaalika tutafakari vema na kwa utulivu sehemu hii ya Injili ya Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio.  Lugha inayotumika katika sehemu hii ya Injili ya leo ndio ile ya Kiapokaliptiko. Ni lugha ya mficho na mafumbo, hivyo kuupata ujumbe kusudiwa, hatuna budi kuondoa kilemba kilichoficha kilicho ndani, na ndio lazima kufungua, kuiweka bayana ili kuuona ujumbe kusudiwa. Ni lugha ngumu ya Kiapokaliptiko, na hivyo inahitaji kufafanuliwa vizuri, la sivyo tutabaki na mashaka na wasiwasi na uoga usiokuwa na sababu za msingi na wala sio lengo lake Bwana wetu Yesu Kristo kuja kwake ulimwenguni. Kipindi cha Majilio ni kipindi cha neema, yaani Kairos na matumaini yenye furaha kwani Mkombozi wetu anakuja na kukaa kati yetu. Kwa mara nyingine tena leo ishara zinazotumika ni zile za Kiapokaliptiko tulizozisikia Dominika mbili zilizopita, yaani ile ya 33 mwaka B, ni ishara zinazoashiria kitu kingine na hivyo hatuna budi kuelewa maana ya hizo ishara. Lugha ya Kiapokaliptiko daima inatutaka kuondoa kilemba kilichoficha siri iliyomo ndani, ili tuweze kuupata na kuuweka bayana ujumbe kusudiwa. Aina ya uandishi wa Kiapokaliptiko unatutaka kila mara kuelewa maana ya lugha za ishara zinazotumika, kwani sio lugha ya moja kwa moja ya kuweza kupata ujumbe kirahisi.

Ishara zinazotajwa leo ni zile zile ambazo zinatajwa wakati wa uumbwaji wa ulimwengu katika Kitabu cha Mwanzo. (Jua, mwezi, nyota, bahari na ishara za angani) Mwanzo 1:2 Pale mwanzo kabla ya kuwepo ulimwengu tunaona kulikuwa na ile fujo kubwa (tohuhabohu kwa Kiebrania); fujo kubwa hapa ikimaanisha kutokuwepo na chochote kabla ya uumbwaji wa ulimwengu, ila ni kwa njia ya Neno la Mwenyezi basi ulimwengu ukafanyika na vyote vilivyomo ndani yake, iwe ni ishara za angani, ardhi na hata bahari na wanyama na viumbe vyote. Na mwisho tunaona vyote alivyofinya Mwenyezi Mungu vilikuwa ni vema na vizuri. Kinyume chake ni Injili ya leo kwani inageuza vyote vizuri vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu na kuturudisha katika fujo ile ya awali kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu. Lugha ya Kiapokaliptiko anayotumia Yesu Kristo haimaanishi kamwe kuwa kutakuwa na ile fujo iliyokuwepo kabla ya kuumbwa ulimwengu; badala yake anazungumzia hali halisi iliyopo sasa katikati yetu. Ni ulimwengu wetu ambao haukisi tena ule uzuri na utukufu na utakatifu wa Mungu ambao ulikuwepo baada ya kuumbwa kwa ulimwengu. 

Ni ulimwengu wa kukosa haki, wa chuki na fitina, majungu, wa vita na mafarakano, tabia kinyume na asili yetu ya ubinadamu, hata uharibifu wa mazingira yetu, na kadhalika na kadhalika na yote mabaya ambayo chanzo chake ni sisi wanadamu kwenda kinyume na mpango wa Muumba wetu, iwe tabia zetu kati yetu sisi wanadamu au kuelekea viumbe na uumbaji mzima kwa ujumla. Leo duniani tunalia sote kwa mabadiliko ya tabia nchi, na chanzo cha yote haya ni ukaidi na kiburi cha mwanadamu, yaani cha mimi na wewe. Ni ukaidi wetu wa kutokuthamini na kutunza ulimwengu wetu, ulio ni nyumba yetu sisi sote. Na ndio tunabaki na hofu na mashaka makubwa juu ya hatima na kesho yetu na ya vizazi vijavyo baada yetu.  Tabia zetu kinyume na maadili yanayoakisi asili yetu kama wanadamu wenye akili na utashi, kudharau kwetu kwa tunu za kibinadamu na kiutu. Leo hii tuna mifano mingi ya kuweza kuiweka hapa. Mwanadamu hataki tena kumuona Mungu ndiye asili ya maisha yetu na maadili yetu. Ni mwanadamu anataka kuwa mungu mtu na kujiweka kuwa kipimo cha maadili yake mwenyewe. Mwanadamu hataki tena kuwa chini ya kanuni za asili za uumbaji, hata kufikia kudai kuwa ni haki ya mtu mume kuoana na mtu mume, au mtu mke kuoana na mtu mke, na mengi mengineyo yafananayo, ni kiburi cha mwanadamu kwa Muumba wake, ni kugeuza uumbaji mzuri unaoakisi utukufu na mwanga wa Kimungu na kukaribisha giza ulimwenguni.

Ni mwanadamu anayerudi kuishi katika ile fujo ya awali, ile fujo ya kutokuwepo na chochote kwani nasi tunapojitenga na Muumba wetu hapo tunabaki kuwa watupu, tunabaki bila chochote, tunarudi katika giza na fujo ile ya kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu. Pamoja na yote haya mabaya tunayoweza kuyazungumzia kadiri ya kanuni asili za uumbaji, bado Bwana wetu Yesu Kristo anatualika kungojea ujio wake kwa matumaini, kwani anakuja Masiha mwenye nguvu na shauri mabegani mwake. Tusiogope kwani anakuja kugeuza ulimwengu wetu na kumshinda yule mwovu, hivyo uovu hautashinda bali daima nguvu ya KRISTO MFUFUKA itageuza na kufanya yote mapya. Hata katika nyakati hizi tunapotishwa na mambo mengi mabaya na hata ya kukatisha tamaa, ila kila mfuasi anaalikwa kunyanyua kichwa chake juu kwa matumaini. Kuweka kichwa chini ni kukubali kutawaliwa na uoga na hofu; bali tunyanyue vichwa vyetu juu kwani anayekuja ni Bwana mwenye nguvu na kwa Neno lake vyote vitafanyika upya na nchi itageuka. Ni Utawala wa Mungu pekee utakaoshinda na kuutawala ulimwengu wote na kufanya yote kuwa mapya.

Watu wengi bado wanatembea wamepinda, hawana nguvu ya kunyanyua vichwa vyao na kutembea kwa matumaini kuelekea ulimwengu mpya. Ni watu mathalani, mwanamama aliyetelekezwa na mume wake, wazazi waliojeruhiwa na maisha ya watoto wao, wenye misongo mbalimbali ya maisha iwe kazini, katika familia au jumuiya zetu, wahanga wa chuki na ukatili wa kila aina, wahanga wa hisia za kimwili na kiakili; wote hawa wanaalikwa kunyanyua vichwa vyao. Hakuna fujo au ubaya ambao Mwenyezi Mungu hataumaliza ulimwenguni. Ni ulimwengu mpya utakaoanza mara tu tutakapokubali Yesu Kristo atujie na kuyabadili maisha yetu. Yesu Kristo aje na awe Bwana na Mtawala wa maisha yetu, hapo nasi tutakuwa na mwanzo mpya na maisha mapya yanayoakisi nuru na utukufu ule wa Kimungu. Majilio ni kipindi cha kubadili vichwa, kuwa na namna mpya ya kufikiri na kutenda, ndio ile ya kuongozwa na Neno wa Mungu, yaani Logos. Majilio ni wakati wa kufanya mapinduzi ya kweli ya maisha yetu, yaani, metanoia au meta-nous, ndio ile ninayowaalika mara nyingi kabisa ya kubadili vichwa vyetu, kuwa na namna mpya na ndio ile ya kadiri ya mantiki ya Mungu mwenyewe katika maisha yetu. Kuwa na vichwa tofauti kabisa na vile tulivyonavyo sasa.

Tunaalikwa kama Kanisa kutoka katika mantiki ile ya ulimwengu na kuivaa ile ya Kristo Mfufuka. Kanisa kama Ekklesia (Ek kalein – kutoka katika malimwengu na ulimwengu), linaalikwa wakati wa Majilio kuyapyaisha tena mahusiano yake na Mwenyezi Mungu. Na huu ni mwaliko wa kila mmoja wetu kama Kanisa tunalosafiri pamoja, Kanisa la Kisinodi. Majilio ni kipindi cha kusafiri pamoja, ndio kushikana mikono na kusaidiana katika kufanya mabadiliko ya ndani na ya kweli. Mwinjili Luka anaorodhesha kila aina ya ubaya ambao tunaweza kujikuta nao ikiwa tutapoteza matumaini kwa ujio wake Mwokozi wetu na kukutahadharisha na hayo maovu. Ni kututaka tuwe na kichwa kipya yaani kinachokubali maongozi ya Neno la Mungu. Tusilewe na kukosa maamuzi sahihi, tusibaki katika maongozi kadiri ya ulimwengu huu na badala yake kubadili yote na kuongozwa na Nuru ya kweli itokayo kwa Mungu mwenyewe. Kanisa la kweli ni lile linalokuwa tayari kujitenga na mantiki ya ulimwengu na kuongozwa na ile ya Mungu mwenyewe kwa njia ya Neno lake.

Anatualika kukesha kwa maana ya kuwa macho katika namna zetu za maisha.  Na ili tuweze kweli kuenenda katika njia iliyo sahihi, mwinjili Luka anatualika kukesha katika kusali. Sala inatusaidia kuwa macho katika kusubiri ujio wake Mwokozi wetu Yesu Kristo. Ni sala inatusaidia nasi kujua nini ni mapenzi ya Mungu katika maisha yetu na kuifuata njia ile inayotupeleka kwake na si kwa yule muovu. Anayesali anakubali kuingia katika shule ya mahusiano na Mungu mwenyewe, ni yule anayekubali kwa imani yenye matumaini na mapendo katika kuishi mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Anayesali ni yule anayetambua hawezi kitu bila neema na msaada wa Mungu katika maisha yake. Sala na kusali ni shule ya Mungu mwenyewe kwetu wanadamu. Wapendwa majilio daima ni kipindi cha kungojea kwa matumaini ujio wake Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, anayeleta nuru ya kweli ulimwenguni, ni Neno anayekaa katikakati yetu ili awe taa na nuru ya kutuongoza katika kweli yote. Ni kipindi cha matumaini kwa kila mmoja wetu anayetambua kuwa bila Mungu kusafiri pamoja nasi, basi hapo hatuwezi kitu chochote. Ni Mungu anayetwaa mwili wetu na kutaka kukaa na kusafiri na kila mmoja wetu katika kumwelekea Yeye. Ni Mungu anakuja na kukaa nasi ili atawale na kuongoza maisha yetu ya siku kwa siku, ili sote tuweze kukua katika utakatifu na utu wema.

Nawatakia Dominika njema na majilio yenye kila neema na baraka zake Mwenyezi Mungu. Majilio ni kipindi cha neema, ni kairos, ni wakati uliokubaliwa, ni wakati wa Mungu mwenyewe na mwanadamu ili kuujenga ufalme wake wa Upendo, Haki na Amani kwa watu wote hapa duniani. Safari njema ya Majilio ya kuelekea sherehe za fumbo lile la Umwilisho wake Bwana wetu Yesu Kristo.

25 November 2021, 11:45