Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 32 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Ukarimu na sadaka kwa Mungu huvuta neema na baraka katika maisha ya mwamini! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 32 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Ukarimu na sadaka kwa Mungu huvuta neema na baraka katika maisha ya mwamini! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 32: Ukarimu Huvuta Neema na Baraka

Ujumbe tunaoupata katika masomo ya domenika ya 32 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa ni huu: Neema na baraka za Mungu haziishi kamwe kwa walio na moyo wa ukarimu kwa wengine. Somo la kwanza la kitabu cha kwanza cha Wafalme (17:10-16); linatufundisha kwamba daima Mungu ni mfadhili wa wale wanaomtumainia! Ukarimu na sadaka huvuta neema na baraka ya Mungu

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 32 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe tunaoupata katika masomo ya domenika hii ni huu: Neema na baraka za Mungu haziishi kamwe kwa walio na moyo wa ukarimu kwa wengine. Somo la kwanza la kitabu cha kwanza cha Wafalme (17:10-16); linatufundisha kwamba daima Mungu ni mfadhili wa wale wanaomtumainia. Usemi huu ni wa kweli. Kwa mwujiza, Mungu alimlisha mjane wa Serepta wakati wa njaa kwa maana aliyaweka matumaini yake yote kwake hata akatoa kilichokuwa chakula chake yeye na mwanae akampa mtumishi wa Mungu Eliya. Eliya alimwambia mjane wa Sarepta; “Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa na kipande cha mkate mkononi mwako.” Huyu mama mjane alimjibu Elia mtumishi wa Mungu; “Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe.” Eliya akamwambia, “Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema; “Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haikauka, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.”

Naye kwa kuamini maneno ya Eliya akaenda, akafanya kama alivyoagizwa nao wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.” Kumbe nasi tukiweka matumaini yetu kwa Mungu, tukawahudumia wengine kwa moyo wa ukarimu hatutapungukiwa na kitu kwani Bwana Mungu yeye ndiye mchungaji wetu (Zab. 23). Somo la pili la Waraka kwa Waebrania (9:24-28); linatueleza jinsi Yesu alivyojitoa sadaka kwa ajili yetu “mara moja tu katika utimilifu wa nyakati, amefunuliwa, azitengue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake” tofauti na “vile kuhani mkuu alivyoingia katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake.” Na kwamba Kristo kuhani wetu Mkuu atakapofika mara ya pili atatimiza utukufu wa wale wanaoitikia mwito wake, na atawaadhibu wale wanaomkana. “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.” Kwa maana yeye hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono ya wanadamu, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekani sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu.”

Huu ni ujumbe wa matumaini na faraja kwetu, kwamba tukimtumaini Yesu Kristo kuhani wetu mkuu tutaokolewa kutoka utumwa wa dhambi na kushirikishwa uzima wa milele, na tusipomtumaini hukumu ya milele inatuhusu. Injili ilivyoandikwa na Marko (12:38-44); inatupa fundisho la moyo wa ukarimu kupitia kwa mama mjane kama mama mjane wa sarepta alivyokuwa mkarimu kwa Eliya katika somo la kwanza. Mara nyingi wajane wanachukuliwa kuwa ni watu wasio na msaada na kutokana na hali yao Mungu hawadai makubwa. Tendo la mama mjane maskini aliyetoa senti mbili, kiasi cha nusu pesa kama sadaka ni fundisho kuwa ukarimu hautegemee wingi wa vitu tunavyotoa bali utayari wa moyo kutoa kile tulichonacho kwa upendo kwa ajili ya wengine ndiyo maana Yesu anasema; “Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndivyo riziki yake yote lakini wengine wametoa katika ziada yao.”

Kumbe, ukarimu unahitaji moyo wa sadaka na kuwa tayari kujiachia kwa ajili ya wengine. Ndiyo maana kila mara Mama Kanisa anatufundisha umuhimu wa kutoa sadaka kwa kuwa hili ni tendo la kiliturjia. Na kwa kuwa liturjia ni kazi ya Ukombozi, kila anayetoa sadaka anashiriki kazi ya ukombozi. Ndiyo maana moyo wa sadaka na ukarimu unahitaji moyo wa Imani na Matumaini. Kwa imani utatambua kuwa unafanya kazi hiyo kwa niaba ya Mungu maana wimbo wa katikati unatuambia; “Bwana huwapa wenye njaa chakula; naye huwafungua waliofungwa; huwategemeza yatima na mjane”. Imani na matumaini yanatuwezesha kutambua kuwa Mungu anapenda kazi ya ukombozi iendelee kwa njia ya majitolee yetu, kwa nguvu na ujuzi anaotujalia. Imani na matumaini kwa Mungu yanatusaidia kushinda kishawishi cha woga kuwa nikitoa nitabakia na nini? Mjane wa kwenye Injili; “Katika umaskini wake alitia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia”. Tukumbuke kuwa; “Mbegu ikianguka ardhini na kufa huzaa matunda mengi” (Yoh 12:24). Mjane wa Sarepta kwa kumpatia Eliya mkate, “pipa la unga halikupungua wala chupa ya mafuta haikuisha”. Maandiko Matakatifu yanatufundisha kuwa; “Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi na Mungu ampaye mkulima mbegu na mkate kwa chakula, atawapa ninyi pia mbegu mnazohitaji, na atazifanya ziote, zikue na kuwapa mavuno mengi ya ukarimu wenu. Yeye atawatajirisha ninyi daima kwa kila kitu” (2 Kor 9:6, 12).

Waswahili husema; Mkono utoao ndio upokeao. Kamwe katika kutoa usijilinganishe na wengine. Hivyo, aliye na vichache asiogope kutoa alichonacho akijilinganisha na wenye vingi. Waliojaliwa vingi wasitoe vichache wakijilinganisha na wengine ambao wanatoa kidogo au hawatoa kabisa. Usitoe sadaka yako kwa kulalamika. Mama wa Serepta hakumpa mkate Eliya huku akilalamika au kunung’unika. Mama mjane hakulazimishwa kutoa riziki yake yote. Paulo anatufundisha kuwa; “Kila mmoja na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha” (2Kor 9:7).  Maandiko matakatifu yanaendelea kusisitiza; “Usicheleweshe sadaka yako kwa maskini mwombaji. Usikatae kumsaidia mwombaji aliye na taabu, wala usimpe kisogo masikini. Usiepe kumwangalia mtu fukara, usimpe nafasi ya kukulaani. Maana akikulaani katika uchungu alionao, Muumba wake ataisikia sala yake” (Sira 4: 3-6). Basi tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atujalie moyo wa ukarimu ili utusaidie kujipatia neema na baraka zitakazotustahilisha kuingia katika ufalme wa Mungu Mbinguni.

Tafakari J32
03 November 2021, 15:55