Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 33 ya Mwaka B wa Kanisa: Siku ya Hukumu ya Mwisho! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 33 ya Mwaka B wa Kanisa: Siku ya Hukumu ya Mwisho! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 33 ya Mwaka: Hukumu ya Mwisho

Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, toka huko, Kristo Yesu atakuja kuwahukumu wazima na wafu na Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Yeye ni Bwana wa ulimwengu na wa historia. Ndani yake historia ya mwanadamu na pia kazi nzima ya uumbaji hujumlishwa na kutimilizwa kwa namna iliyo bora kabisa. Ukombozi ni chemchemi ya mamlaka ya Kristo Yesu katika Roho Mt.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Leo tunaadhimisha pia Siku ya Maskini Duniani ambayo kimsingi ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, na kwa mara ya kwanza iliadhimishwa kunako mwaka 2017.  Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni kumbukumbu endelevu na fungamani ya upendo na huruma ya Mungu inayopaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa waamini katika ujumla wao. Siku hii ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki wa kijamii, umoja na udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali kuta za utengano na maamuzi mbele! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya V ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2021 unanogeshwa na kauli mbiu: “Maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi” Mk 14:7. Baba Mtakatifu kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya V ya Maskini Duniani, Ijumaa tarehe 12 Novemba ametembelea mjini Assisi, akakutana na kusali na maskini kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amegusia wasifu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi katika huduma kwa maskini; umuhimu wa sala, ukarimu na utamaduni wa watu wa Mungu kukutana. Ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kwa watu kukutana na kujadiliana katika ukweli na ujasiri, tayari kuwatangazia watu Injili ya imani na matumaini ili kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu! Imani yetu katika Kristo Yesu ambaye alijifanya maskini, na daima alikuwa karibu na maskini kwa ajili ya maskini na wale wote waliotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii ndiyo msingi wa kujihusisha kwa Kanisa na ustawi, maendeleo na mafao ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Maadhimisho haya yatuwezeshe kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi. Rej. EG 186-192.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa inachota utajiri wake kutoka katika Kitabu cha Nabii Danieli 12: 1-3, Ebr. 10: 11-14, 18 na Injili ya Marko 13: 24-32. Wazo kuu ni Hukumu ya Siku ya Mwisho. Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, toka huko, Kristo Yesu atakuja kuwahukumu wazima na wafu na Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Yeye ni Bwana wa ulimwengu na wa historia. Ndani yake historia ya mwanadamu na pia kazi nzima ya uumbaji hujumlishwa na kutimilizwa kwa namna iliyo bora kabisa. Ukombozi ni chemchemi ya mamlaka ya Kristo Yesu ambayo anayatekeleza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu juu ya Kanisa. Manabii na hatimaye, Yohane Mbatizaji alitangaza katika mafundisho yake kuhusu hukumu ya siku ya mwisho. Hapo matendo ya kila mmoja yatafunuliwa pamoja na siri za nyoyo za watu. Kumbe, huu ni wakati muafaka wa kutumia vyema neema ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo!

Kristo Yesu ni Bwana wa uzima wa milele na anayo haki kamili ya kutoa hukumu thabiti juu ya matendo na nyoyo za watu kwa sababu Yeye ni mkombozi wa ulimwengu. Kristo Yesu amejipatia haki hii kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Na Baba naye amempa mwana hukumu yote. Tunakumbushwa kwamba, hata hivyo Mwana hakuja ili kuhukumu, bali ili kuokoa na kutoa uzima kwa yule aliye ndani yake. Na kwa kukataa neema ya uzima huo, ambako kila mmoja hujihukumu tayari yeye mwenyewe, hupokea kadiri ya matendo yake na anaweza pia kujilaani mwenyewe kwa milele kwa kumkataa Roho wa upendo. Rej. KKK 668-682. Mama Kanisa anafundisha kwamba, ufufuko wa wafu wote wenye haki na wasio na haki pia utatangulia hukumu ya mwisho, kwa wale waliotenda mema watapata maisha na uzima wa milele na wale waliotenda mabaya watapata ufufuo wa hukumu na watakwenda kuingia kwenye adhabu ya milele, bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele. Hukumu ya mwisho itakuja Kristo Yesu atakaporudi kwa utukufu. Lakini hakuna mtu anayejua saa wala wakati, huu ni muda muafaka wa kukesha.

Hukumu ya mwisho itaifunua haki ya Mungu ambayo imeshinda maonevu yote yaliyotendwa na viumbe vyake, na kwamba, upendo wake una nguvu kuliko mauti. Ujumbe wa Hukumu ya Mwisho ni wito na mwaliko wa toba na wongofu wa ndani. Huu ndio ule muda uliokubalika, yaani Siku ya Wokovu. Hiki ni kipindi cha kuchochea hofu takatifu ya Mungu na kutangaza tumaini lenye heri na baraka la kurudi kwa Bwana atakayekuja ili kutukuzwa katika watakatifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki.  Rej. KKK 1038-1060. Kristo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “lakini siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hatautoa mwanga wake. Na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu. Mk 13: 24-27. Mwisho wa nyakati ni mwisho wa maisha ya kila mwanadamu. Hiki ni kipindi cha neema na baraka ya kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema hii itakuwa ni Siku ya furaha, huruma na raha tele kwani huu ni mwisho wa kazi ya uumbaji na huo ndio mwisho wa maisha. Huu ndio wakati wa kufanya tafakari kuhusu mambo ya Siku ya Hukumu ya Mwisho ambayo inatisha na kuogofya kama tulivyosikia kwenye somo la kwanza na kwenye Injili. Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani! Ndugu yangu, tumwombe Roho Mtakatifu ili aweze kutusaidia kujiandaa vyema kukutana na Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Kristo Yesu ndiye Hakimu mwenye: huruma na mapendo, kiini cha imani ya Kikristo! Tumwombe atujalie hekima ili tuweze kuwa ni mwanga angavu katika kutenda haki, ili tung’ae milele! Tukimbilie huruma na upendo wa Mungu katika maisha yetu na tujiandae kwa imani, matumaini na furaha tele ili kukutana na Kristo Yesu atakapokuja kwa mara ya pili. Ninawatakieni maadhimisho mema ya Siku ya V ya Maskini Duniani kwa mwaka 2021.

Liturujia J33
13 November 2021, 15:21