Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu inafunga kipindi cha Mwaka wa Kanisa, kwa kuweka matumaini kwa Kristo Yesu Mfalme wa Haki, amani, upendo na mshikamano. Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu inafunga kipindi cha Mwaka wa Kanisa, kwa kuweka matumaini kwa Kristo Yesu Mfalme wa Haki, amani, upendo na mshikamano. 

Tafakari Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu: Haki na Amani!

Sherehe ya ya KRISTO MFALME WA ULIMWENGU ndio kilele cha Mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa. Sherehe hii iliwekwa katika kalenda ya Liturujia ya Kanisa na Papa Pio XI, mwaka 1925, miaka michache baada ya kumalizika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Ilikazia kwa namna pekee, matumaini kwa Kristo Yesu, Mfalme wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli na watu wote!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Sherehe ya Dominika ya KRISTO MFALME wa ulimwengu, ndio kilele cha Mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa. Sherehe hii iliwekwa katika kalenda ya Kiliturujia na Papa Pio XI, mwaka 1925, miaka michache baada ya kumalizika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Ni katika mazingira ya ubabe wa kisiasa na ukosefu wa amani, maisha ya mashaka kulikosababishwa na watawala wa nyakati zile, na hasa ila hali ya kutoelewana kwa mataifa makubwa yenye nguvu duniani; Baba Mtakatifu anasukumwa na hali hiyo na kutualika kwa kumwangalia daima Yesu Kristo aliye Mfalme wa kweli. Ni nyakati zilizojaa kila aina ya hofu iliyopelekea hata Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Hivyo ni katika mazingira magumu na mashaka mengi ya amani duniani, Baba Mtakatifu anaiweka rasmi katika kalenda ya kiliturjia ya mwaka wa Kanisa, Sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu. Ni yeye anapaswa kuwa mtawala na kiongozi wetu, ni yeye anapaswa kuongoza mataifa yote ya ulimwengu na hata maisha ya siku kwa siku ya kila mmoja wetu.

Mwinjili Yohane katika masimulizi ya mateso yake Bwana wetu Yesu Kristo, anarudiarudia juu ya ufalme wake Yesu mara kumi na mbili. Na katika sehemu ya Injili ya leo, tunasikia neno mfalme na ufalme karibia mara sita. Pamoja na kwamba inatushangaza kwani ni katika muktadha ule wa mateso na mashitaka, Mwinjili Yohane anatuonesha juu ya ufalme wake Yesu Kristo. Kiti chake cha enzi si kingine bali ni Msalaba wake alioubeba na hata kufa juu yake, Msalaba unaoneshwa na Mwinjili kuwa ni kiti cha utukufu, kiti cha ukuu na upendo na huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu na ulimwengu mzima. Yesu anaingizwa kwenye Praitorio ya Pilato, iliyokuwa imejengwa juu kabisa katika mji ule wa Yerusalemu. Mayahudi wanamleta mbele ya Pilato kwa mashitaka ya Kisiasa na Kidini kwa wakati mmoja, ya kuwa Yesu anajifanya kuwa mfalme wa Wayahudi, ndio kusema anakwenda kinyume na kupinga utawala wa Kirumi. Na ndio tunaona swali la kwanza la Pilato; “Je, Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”.

Swali hilo ni la msingi ambalo Pilato anamuuliza Yesu Kristo wakati wa kusikiliza mashtaka yake kutoka kwa wakuu wa dini ya Kiyahudi, ni juu ya ufalme wake.’’ Je, wewe ni mfalme wa wayahudi?’’. Yesu Kristo hapingi kuwa yeye si mfalme bali anajaribu kumuonesha Pilato kuwa ufalme wake hautokani na ulimwengu huu bali watoka juu, ni tofauti na jinsi watawala wengine wanavyotawala kwa nguvu na mabavu. Mantiki ya ufalme wake ni tofauti na ile tuliyonayo kwa watawala wa ulimwengu huu, utawala wa mabavu na nguvu na hata vita. Hivyo, tunaona aina mbili zinazokinzana juu ya Ufalme, moja ni ile ya mantiki ya mbinguni na nyingine kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu. Majibizano ya Pilato na Yesu Kristo yanatusaidia nasi kuweza kuuelewa ni aina gani ya ufalme na hasa asili ya ufalme huo wa Yesu Kristo. Swali la Pilato linaakisi pande mbili za ukweli; Yaani kama Yesu Kristo ni mfalme wa Wayahudi au masiha au mpakwa mafuta wa Bwana, basi ni kiongozi wa kidini wa watu wake na hivyo yeye Pilato hahusiki katika shitaka hilo lenye sura ya kidini au imani, la sivyo kama ufalme wake ni wa kisiasa basi anapingana na utawala na kirumi. Na ndio Yesu Kristo anamuuliza Pilato kama haya anayasema yeye nwenyewe au ni wengine walimwambia juu ya hayo?

Wayahudi walijua fika kuwa kama watamshtaki kuwa Yesu Kristo ni Masiha wao au mkuu wao wa kidini, basi Pilato hahusiki katika shauri hilo, na hivyo shitaka lao kukosa mashiko na hivyo ilibidi watunge mashtaka ya uongo, kuwa mtu huyu ni mtenda mabaya, ni mfitini wa Kaisari ni mtu muovu kama wale wawili waliosulubiwa na Yesu Kristo pale juu msalabani. Pamoja na kujaribu kila njia za kumshtaki Yesu Kristo kwa Pilato, tunaona Pilato bado haoni kosa kwake. Pilato anatimiza wajibu wake wa kisiasa wa kuwasikiliza na kila mara kutoka nje kuwahoji washitaki wake maana walibaki nje kwa hofu ya kunajisika ikiwa wangeingia katika jumba lile la watawala wa kirumi, watu wapagani, lakini zaidi sana ilikuwa ni tayari maandalizi ya Pasaka ya Kiyahudi. Ni wakuu wa Makuhani ndio wanaomtoa Yesu kwa Pilato ili ahukumiwe na hata ikibidi afe kwa mashtaka yasiyokuwa ya kweli. Yesu Kristo anaweka wazi kuwa asili na namna ya ufalme wake ni tofauti na ule wa Kaisari wa Kirumi au watawala wengine wa ulimwengu. Na ndio maana hata Petro alipotoa upanga wake Yesu Kristo anamzuia na kumwalika kuurudisha upanga ule alani mwake. Ufalme wake sio wa mabavu na vita, sio wa kutumia silaha. Ni ufalme wa haki, amani na mapendo thabiti.

Utanguli wa Ibada ya Misa Takatifu unatusaidia zaidi kuona ni aina gani ya ufalme wake Yesu Kristo; Kinyume na watawala wa ulimwengu wetu ambao hata mara nyingine kujipa au kupenda majina yanayoonesha nguvu zao za kiutawala ili kuwaogopesha wanaowatawala; yeye anajitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wetu, ufalme wake ni wa milele na wa ulimwengu mzima, ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utaua na neema, ufalme wa haki, upendo na amani. Ni kwa sababu hiyo amezaliwa na kuja ulimwenguni ili nasi tuongozwe katika kweli. Kweli katika mazingira ya kiyahudi ndio kusema mfanano na uhalisia wenyewe, isiyo na mawaa kwani ni mfanano kamilifu. Ni ufalme wa kweli sio kama ule wa mantiki za kiulimwengu, watawala wa mabavu bali wake ni kutaka kuongoza maisha yetu ili tuishi katika kweli. Ukweli ni Mungu mwenyewe anayetualika nasi kufanana naye, kumpenda Mungu na jirani katika kweli na si kwa maneno tu bali kama alivyofanya Yesu Kristo hata kutoa maisha yake kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu mzima.

Kwa Wanafalsafa wa Kigiriki, ukweli ni katika kujua na uwelewa wa mambo jinsi yalivyo, ni kung’amua siri inayojificha katika vitu mbali mbali. Katika Maandiko Matakatifu, Ukweli ni uaminifu katika Neno la Mungu, ni Mungu mwenyewe aliye Ukweli wote katika ukamilifu wake. (Kutoka 34:6) Kwa Muyahudi, ukweli sio kitu cha kufikirika, au chakula cha ubongo bali ni katika maisha halisi, ni kile kinachojiri katika historia ya mwanadamu. Ukweli ndio mipango ya upendo ya Mungu kwa watu wake, ni safari ya siku kwa siku ya mwanadamu akihusiana na Mungu. Yesu Kristo amekuja ulimwenguni ili kuishuhudia hiyo kweli, kwani ni kwa njia yake tunapata kukutana na Mungu, kama anavyojitambulisha Yeye mwenyewe, kuwa ni Njia, Ukweli na Uzima. (Yohane 14:6) Kwa maisha yake tumepata kukutana na sura halisi ya Mungu, upendo na huruma ya Mungu kwa watu na viumbe vyake vyote. Kuishi kweli na kutembea katika kweli, ni mwaliko kwetu sisi kuwa waaminifu kwa kweli za Injili, kwa kulishika na kuliishi Neno lake siku zote za maisha yetu, ni kuwa waaminifu kwa maagano ya Ubatizo wetu. (Yohane 3:21 na Waraka wa pili wa Yohane 4).

Daima kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu (Yohane 14:17; 15:26; 16:13), ndio uwepo wa Mungu ndani mwetu, nasi tunaweza kuwa mashahidi wa ile kweli sio tu kwa maneno yetu bali zaidi sana kwa maisha yetu. Ni kwa kuishi ukweli huo nasi tunakuwa huru, kwani ni mmoja anayeishi kadiri ya kweli za Injili ni huyo anayetembea katika uhuru wa wana wa Mungu. (Yohane 8:32) Kinyume chake ni kubaki kuwa mtumwa wa shetani na uovu. “Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu”, ndio hitimisho la sehemu ya Injili ya leo. Ni maneno yenye kutualika kila mmoja wetu kutambua umuhimu wa kuongozwa na Injili, Neno la Mungu katika maisha yetu. Kufikiri na kuenenda kadiri ya kweli za Injili, na ndio hapo tunaweza kwa pamoja kuujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani. Dominika hii ya kilele cha kalenda ya mwaka wa Kanisa ni mwaliko pia kutafakari juu ya kilele cha maisha ya kila mmoja wetu. Kilele chetu kama vile kilivyo chanzo chetu hakina budi kuwa Yesu Kristo mwenyewe, awe mfalme wetu, kwa maana kiongozi wa maisha yetu, Neno lake liwe taa ya miguu yetu, maisha yetu yaakisi Neno lake la uzima na kweli, linalotufikisha katika ile Kweli yaani Mungu mwenyewe. Tafakari na sherehe njema ya Kristo Mfalme na maandalizi mema ya Majilio na Noeli.

16 November 2021, 16:01