Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Majilio. Bikira Maria anamtembelea Elizabeti, tuombe mapendo kwa Mungu na jirani. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Majilio. Bikira Maria anamtembelea Elizabeti, tuombe mapendo kwa Mungu na jirani.  

Bikira Maria Anamtembelea Elizabeti: Tuombe Mapendo Kwa Mungu na Jirani

Maneno ya Elisabeti kwa Maria: Umebarikiwa kati ya wanawake wote, yanatutafakarisha pia na kuona hata katika Agano la Kale katika Kitabu ya (Yudithi 13:18). Ni kupitia Maria pia Mwenyezi Mungu anapenda kutekeleza kazi yake ya kuukomboa ulimwengu. Maria anatumika kama chombo na hivyo kuwa ni Mama wa Mungu na Ulimwemngu Aliyembarikiwa kuliko wanawake wote!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Wapendwa, sehemu ya Injili ya leo Rej. Lk 1:39-45 mara zote inatupa wazo juu ya ukarimu na upendo kwa jirani hasa kwa kitendo cha Mama Bikira Maria anapotoka nyumbani kwake na kwenda kumtembelea ndugu yake Elisabeti. Lakini tunaposoma kwa makini sehemu hii ya Injili na kuangalia matukio yote tunabaki na maswali mengi yasiyokuwa na majibu ya wazi. Hivyo naomba tuchukue muda pia kusoma na kutafakari ili kuweza kupata ujumbe mahususi wa Mwinjili Luka. Sisemi kuwa kitendo cha Maria kwenda kumtembea ndugu yake Elisabeti kuwa sio cha upendo na ukarimu ila nitatumia muda zaidi kuelezea aina ya lugha inayotumika ili kupata ujumbe kusudiwa wa Mwinjili Luka. Labda itachosha kidogo ila nitajitahidi kutumia lugha rahisi ili tuweze kuelewa vema. Maria aliyekuwa bado ni binti mdogo mwenye umri wa takribani miaka kumi na nne, anatoka katika kijiji chake cha Nazareti na kwenda katika mji wa milimani wa mzee Zakaria na Elizabeti, tunabaki na mengi ya kutushangaza kuliko kutupa uhalisia wa mambo. Elisabeti aliyekuwa kwanza mama mtu mzima na aliishi katika kijiji kile cha Ain Karim katika mkoa wa Yuda, na kwa hakika alizungukwa na wanawake wengi wa umri na rika lake ambao kwa hakika wangeweza kumsaidia, na hasa ukizingatia mume wake alikuwa kuhani, hivyo ni familia iliyofahamika kwa majirani zao. Ikumbukwe kwa Wayahudi ukarimu ni tunu ya msingi kama ilivyo katika jamii zetu nyingi za kiafrika.

Hata umbali wa kutoka Nazareti mpaka mji wa Yuda ni mkubwa na ni njia yenye hatari nyingi, hivi kwa nini Mwinjili Luka anamtaja tu Maria binti mdogo anayefanya safari hii hatarishi bila kusema alikuwa na nani wengine alioambatana nao. Hakika hatutegemei kuwa Maria alifanya safari ile ndefu na hatarishi peke yake. Na bado tunaona Maria anarejea kwake mara baada ya kujifungua kwake Elisabeti, pia ni jambo la kushangaza kwani tunajua mama aliyejifungua anahitaji msaada zaidi wakati huo labda hata kabla ya kujifungua kwake. Maria anabaki na Elisabeti kwa miezi mitatu tu na kurejea kwake. Kwa nini miezi mitatu tena ya wakati wa mimba na si baada ya kujifungua ili amsaidie mama mzazi. Wanapokutana Maria na ndugu yake Elisabeti tunasoma kuwa kitoto kikaruka kwa shangwe tumboni mwake kwa furaha, bado inatafakarisha ni kwa jinsi gani mtikisiko wa mtoto tumboni mwa mama yake tunaweza kusema bila mashaka kuwa ulikuwa ni wa furaha. Mwinjili anafikaje kusema kwa hakika kuwa kuruka kwa mtoto ndani ya tumbo la mama yake ilikuwa ni kwa furaha. Ni swali linalotutafakarisha.

Na hata salamu na mazungumzo kati ya Maria na Elisabeti tunaona ni maneno yanayochukuliwa kutoka katika Maandiko Matakatifu, yaani Agano la kale. Siyo salamu au mazungumzo ya ndugu wawili tena walio watu wa kawaida kabisa, na badala yake tunaona wanatumia maneno yasioakisi mazungumzo ya kawaida ya akina mama, bali ni kama mazungumzo kati ya wataalamu au wabobezi wawili wa Maandiko Matakatifu na Teolojia. Hivyo ni vema tangu awali naomba kuwaalika tukumbuke kuwa, Biblia kimsingi ni kitabu cha imani na sio kitabu cha historia kama historia au cha elimu ya sayansi, na lengo na shabaha yake ni kutoa katekesi ili kukuza imani yetu. Daima tunaposoma Biblia Takatifu yafaa kuona kila taarifa tunayokutana nayo au kuisoma nyuma yake kuna ujumbe wa kiimani. Hivyo Mwinjili Luka anatupa taarifa zile zinazokuwa muhimu na lazima kwa imani yetu na si vinginevyo. Na ndio maana huwa mara nyingi nawaalika kuelewa aina ya uandishi na lugha na hata mazingira ya uandishi ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa. Tuepuke kusoma Biblia kama Riwaya tu ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa kwa ajili ya imani yetu. Biblia ni kitabu cha imani!

Sehemu ya Injili ya leo inaanza kwa kusema Maria alienda kwa haraka; Baba Mtakatifu Francisko anatumia kitendo hiki cha kwenda kwa haraka kuwa ni mwaliko kwangu na kwako tunapoitwa kutimiza utume wake Mwenyezi Mungu, ni wito na mwaliko wa kimisionari kuishi kweli za Injili bila kukawia au kupoteza muda. Kama Maria tunapopokea ujumbe wa Mungu tunaalikwa mara moja kuuweka katika maisha yetu, tunaalikwa kupenda leo na sasa na si kusema nitapenda kesho au keshokutwa au nitasali kesho au keshokutwa. Ni kuamka mara moja na kuweka katika maisha ulio ujumbe wa Mungu kwetu. Mwinjili Luka anatuonesha kuwa Maria anafika nyumbani kwa Zakaria na kumsalimia Elisabeti. Hapa pia tunabaki na mshangao kwani mkuu wa nyumba ni mzee Zakaria ila hatusikii juu ya salamu kwake kutoka kwa Maria. Salamu anayoitaja hapa sio salamu ya kawaida kama kusema shikamoo au habari za hapa, na ndio maana Mwinjili anakazia tena na kusema hata mtoto Yohane aliyekuwa bado tumboni mwa mama yake alisikia salamu ile. Mimi sio mtaalamu wa elimu ya viumbe au Baiyolojia ila inaleta mashaka mengi kwa mtoto aliye tumboni kuanza kusikia salamu ya mtu anayekuwa nje ya tumbo lile la uzazi. Ni simulizi linalochochea hisia za kutafakari kiundani zaidi.

Wayahudi wa nyakati zile kama vile wa leo wanapokutana wanasalimiana, “Shalom” neno la Kiebrania lenye maana ya amani. Amani au Shalom ni sawa na kusema mema yote ambayo Mwenyezi Mungu amewaahidia babu zao yaweze kuwafikia na ukamilifu wake ni wakati wa ujio wa Masiha. Hivyo ni kumtakia mwingine mema yale ya kimasiha, mema yatokayo kwa Mungu mwenyewe na yakushikie katika ukamilifu wake kwa ujio wa Masiha. (Rejea Zaburi 72:7 na Isaya 9:5). Hivyo neno Shalom kutoka kinywani mwa Maria ni tangazo rasmi la Injili, tangazo la Habari Njema, ni Mbiu rasmi ya ujio wa Masiya aliye ukamilifu wa mema yote na amani ya kweli, kwani ndiye mfalme wa amani. Ni Mbiu ya Kimasiha! Hivyo Maria ndiye anambeba tumboni mwake, huyu aliye ukamilifu wa amani yote, ukamilifu wa mema yote, mfalme wa amani. Hivyo kama Maria katika milima ile ya Uyahudi, na malaika Betlehemu wanaimba, amani duniani kwa wale wote waliopendwa na Bwana Mungu. (Luka 2:14) Na ndio mwaliko wa Yesu Kristo kwa wafuasi wake kila nyumba mnayoingia semeni amani katika nyumba hii na wote waishio ndani mwake. (Luka 10:5)

Mtaona nami pia natumia kila ninapoanza tafakuri zetu natumia salamu ile ya Kifranciskani ya Pax et Bonum, Peace and Good, Amani na Salama. Sio lengo langu leo kuingia ndani na kuielezea salamu hii ila nia na shabaha yake ni kumtakia mwingine kila mema yatokayo kwa Mungu mwenyewe. Ni sawa na salamu ya Kiongozi wa Ibada ya Misa anaposema Bwana awe nanyi, amani yetu na salama yetu ni kuwa na Mungu mwenyewe. Shalom ni kumtakia mwingine awe na Mungu ndani mwake anayekuja na mema yote na kutujalia furaha ya kweli. Na ndio salama na amani waliyoipata Elisabeti na mtoto mchanga tumboni mwake maana wamefikiwa na Mungu mwenyewe nyumbani mwao. Ni ujio wa Masiha katika familia na nyumba yao, ni Mungu katikati yao. Maneno ya Elisabeti kwa Maria: Umebarikiwa kati ya wanawake wote, yanatutafakarisha pia na kuona hata katika Agano la Kale katika Kitabu ya (Yudithi 13:18), yanatumika maneno ya aina hii. Ni kupitia Maria pia Mwenyezi Mungu anapenda kutekeleza kazi yake ya kuukomboa ulimwengu. Maria anatumika kama chombo na hivyo kupata upendeleo maalumu wa kuwa Mama wa Mungu na Mama wa ulimwengu mzima. Aliyembarikiwa ni yule aliye na Mungu ndani mwake kama Mama yetu Bikira Maria, na pia kila mmoja wetu tunaporuhusu uwepo wa Mungu ndani mwetu hapo nasi tunakuwa pia wabarikiwa, tunaojaliwa kushiriki maisha ya Mungu mwenyewe, maisha ya neema, ndio yale ya utakatifu.

Elisabeti anatamka kama Mfalme Daudi kuwa yeye ni nani hata mama wa Bwana wake amjilie nyumbani mwake. Elisabeti akiwa ni mama mtu mzima inashangaza kutamka maneno haya kwa binti mdogo wa miaka 14 lakini maneno haya yanadhihirisha ukweli mwingine wa imani. (Rejea 2 Samueli 6:9) Mfalme Daudi anapopokea Sanduku la Agano Jerusalemu naye anatamka maneno kama haya kuonesha kuwa yeye hastahili kulipokea Sanduku lile la Agano, kwani Sanduku la Agano lilibeba pia Amri za Mungu, ni ishara ya uwepo wa Mungu kati ya watu wake, ni ishara ya watu wa Agano waliokubali kuwa watiifu kwa Mungu na kumwabudu Yeye peke yake. Sanduku la Agano kama vile Maria bado kuna mengi yanayofanana hapa. Sanduku lile lilipokelewa kwa furaha kubwa, shangwe na kucheza na kubaki katika Nyumba ya Yuda kwa miezi mitatu. Sanduku la Agano ni chanzo cha kila baraka kwa familia ile iliyofikiwa nalo. (2 Samueli 6: 10-11) Mtoto Yohane Mbatizaji ni ishara ya watu wa Agano la Kale wanaopokea kwa furaha ujio wa Masiha waliyeahidiwa na kumsubiri kwa hamu kubwa kwa miaka mingi.

Hivi tunaona lengo na shabaha ya Mwinjili Luka ni kutuonesha kuwa Maria ni Sanduku la Agano Jipya.  Tangu Mungu anapokubali kufanyika mtu habaki tena katika umbo lile lililotengenezwa kwa mawe au hekaluni au sehemu fulani bali katika tumbo la huyu binti aliye Bikira yaani Maria. Maria ni tabernakulo ya kwanza! Hivyo kila sehemu na mahali anapofika Maria aliye Sanduku la Agano Jipya basi hapo kunajaa na kulipuka kwa furaha; na ndio kitoto kinaruka kwa shangwe na furaha, na mama yake Elisabeti pia anajawa na furaha kutembelewa na Bwana, na maskini wanaruka kwa furaha kwani imefika saa ya wokovu wao, yaani, Kairos, saa ya neema. Ujio wa Masiha ni wakati wa furaha na ndio Mzee Zakaria naye ataimba kwa kumtukuza Mungu kwani amewakomboa watu wake. (Luka 1:68) Pia Malaika watatangaza katika kesha lile la Noeli, ninawatangazia habari njema ya furaha kwa watu wote. (Luka 2:10) Na hata Mzee Simeoni atajawa na furaha atakapomshika mtoto Yesu mikononi mwake na kuuona Wokovu wa Mungu kwa watu wake na mwanga wa Mataifa yote. (Luka 2:29-32). Noeli ni sherehe ya furaha, hivyo tufungue milango ya mioyo yetu kumpokea Mtoto Yesu, ili nasi nafsi zetu zibubujikwe na kujawa na furaha ya kweli. Mara nyingi tunaishia kuona Noeli ni kula vizuri au kunywa vizuri au kuvaa vizuri au kupamba nyumba zetu au makanisa au majengo yetu mbali mbali kwa mapambo mengi mazuri, na kusahau kuwa ni mwaliko wa kufungua nafsi zetu ili Mungu mwenyewe aingie na kutupatia furaha ya kweli.

Maria ni mbarikiwa kwa vile ameamini alichoambiwa na Bwana. Tofauti na wale wanaoona kuwa ahadi za Mungu zinakawia au zinakuwa kinyume na mapenzi yao, Maria anapokea ujumbe wa Mungu na kuamini, tena katika umri wake mdogo alijikabidhi mzimamzima katika mpango wa Mungu, hakika hata mengine bila kuelewa sana, na ndio maana yeye ni mbarikiwa. Heri yake aaminiye, ndio heri ya kwanza katika Injili ya Luka. Si tu Maria ni mbarikiwa ila kila mmoja wetu anayeamini, anayekubali mpango wa Mungu katika maisha yake, anayeacha nafasi ili Mungu aongoze na kutawala maisha yake. Ni yeyote anayejikabidhi mzimamzima kwa Mungu mwenyewe.  Katika Injili ya Yohane pia tunaona kule mwishoni, Yesu Kristo Mfufuka anasema heri yake asiyeona na akaamini. (Yohane 20:29) Imani ya kweli ni kama hii ya Maria, siyo ile inayosubiri kuelezewa kwa vielelezo vya kisayansi au vitu vinavyoweza kuthibitishwa pasi na mashaka yeyote. Imani ya kweli inatokana na kusikiliza Neno la Mungu na kulishika kwani tuna hakika kuwa Mungu wetu ni mwema na mwaminifu. Imani ni tukio la kukutana na kukiri ukuu wa Mungu kwetu. Maria anatambua tangu mwanzo kuwa Mwenyezi Mungu haangalii kama mwanadamu, na anatumia watu wa kawaida na hata kudharaurika ili kudhihirisha ukuu na enzi yake. Na ndio mwaliko wa Mungu kwetu katika maandalizi yetu ya Noeli kukubali udogo na udhaifu wetu ili tuweze kumruhusu Yeye mwenye uwezo wote aongoze na kuyabadili maisha yetu ili kuweza kuwa na furaha ya kweli. Nawatakia tafakari njema na maandalizi mema ya sherehe hii ya furaha kuu ya Mungu kuwa mwanadamu na kukaa pamoja nasi. Ni Neno anafanyika Mwili na kukaa kwetu, anachukua nyama na kuwa sawa nasi. Verbum Caro factum est!

14 December 2021, 11:46