Tafuta

Mwinjili Yohane katika Injili ya leo anato kwa muhtasari kuhusu Fumbo la Umwilisho. Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya waja wake. Mwinjili Yohane katika Injili ya leo anato kwa muhtasari kuhusu Fumbo la Umwilisho. Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya waja wake.  

Dominika ya Pili ya Noeli: Neno Alitwaa Mwili Na Kukaa Kwetu

Logos ni Mungu mwenyewe wa milele yote katika Nafsi ile ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Noeli ni sherehe ya Neno kuutwaa mwili na hivyo kufanyika mwanadamu na kukaa kwetu. Ni Mungu anayetwaa ubinadamu wetu na kubaki Mungu kweli na mtu kweli kati yetu kama tunavyokiri katika sala ya Imani yetu, yaani, Nasadiki ile ya Nicea katika Misa za kila Dominika na Sherehe.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Somo la Injili ya Yohane 1:1-18 ni ufupisho wa nini maana ya maadhimisho haya ya Noeli, na hasa utambulisho wa huyu Mtoto aliyezaliwa, kuwa ni Mtu kweli na Mungu kweli. Ni somo juu ya Fumbo la Noeli, yaani, Umwilisho wa Neno wa Mungu, anayekuja na kukaa kati yetu. Ni Neno wa Mungu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu yaani Mungu Mwana, anayeutwaa ubinadamu wetu na huku akibaki kuwa Mungu kweli na wakati huo huo Mtu kweli kama tunavyokiri katika Kanuni ya Imani ya Nicea. Yohane Mwinjili anaanza na Injili yake kwa wimbo huu mzuri wa fumbo hili la Umwilisho wa Neno wa Mungu, yaani, Λογος (Logos) kwa Lugha ya Kigiriki cha Agano Jipya (Koine). Yesu ni Logos, Neno wa Mungu, aliyekuwepo na Mungu milele yote ambaye kwa njia yake ulimwengu ukapata kuwepo. Na ndio anatuonesha pia Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Wakolosai (1:15-20), ni kwa njia ya Kristo vitu vyote vinapata kuwepo, au vimeumbwa kwa njia yake.

Neno wa Mungu, Logos, sio logos yenye herufi ndogo yenye maana ya neno lolote linaloweza kutamkwa na kuwa katika ukizanzani na mtanziko na maneno mengine au kwa Kigiriki logoi(maneno). Ni Logos yenye maana ya Hekima ya Mungu mwenyewe ya milele yote, na kwayo ulimwengu wote ukapata kuwepo. Logos ni Mungu mwenyewe wa milele yote katika Nafsi ile ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani mwenye asili moja na Baba pamoja na Mungu Roho Mtakatifu. Noeli ni sherehe ya Neno kuutwaa mwili na hivyo kufanyika mwanadamu na kukaa kwetu. Ni sherehe ya umwilisho wa Neno wa Mungu. Ni Mungu anayetwaa ubinadamu wetu na kubaki Mungu kweli; ni mtu kweli na Mungu kweli kati yetu kama tunavyokiri na kusali katika sala ya Imani yetu, yaani, Nasadiki ile ya Nicea katika Misa za kila Dominika na zile za sherehe za amri ya Kanisa. Ni Mungu anautwaa ubinadamu wetu ili mwanadamu apate kushiriki maisha ya Kimungu kama walivyopenda kufundisha mababa wa Kanisa. Ni kwa njia hiyo Mungu anajishusha na kuja kati yetu tulio duni na wadhambi ili tupate kukombolewa kutoka katika giza nene la dhambi na maovu. Ni Mungu anayeshuka na kutushika mkono ili atutoe katika dimbwi lile la matope na uchafu wa kila uovu na dhambi, ni upendo wa namna gani huu!

Neno wa Mungu ni zawadi ya upendo na huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Ndio zawadi kwa maana halisi, zawadi inapata umaana wake pale inapokuwa sio kitu cha kuweza kurejesha kwa mtoaji, inakuwa zawadi kwa mpokeaji kwani anachoona mbele yake sio deni bali ni upendo mtupu usiokuwa na hila wala makandokando yeyote yale. Mtakatifu Tomaso wa Akwino anajaribu kutuonesha nini maana ya zawadi kwa maneno haya: “Donum proprie est datio irredibilis”, zawadi ni kile ambacho mpokeaji hawezi kurejesha kwa mtoaji. Hivyo, Noeli ni mwanadamu na uumbaji kwa ujumla wake tunapokea zawadi hii ambayo hatuna uwezo wa kuirejesha kwa mtoaji, kwani ni Mungu mwenyewe anayejitoa na kuja na kukaa kati yetu kama nuru na mwanga wa ukweli wote, kama Bwana wa uzima wetu sio tu ule wa kimwili (Bios) bali sana wa Kiroho (Zeos). Injili ya Yohane inaanza na wimbo wa ushairi juu ya Neno wa Mungu au kwa Kigiriki Λογος (Logos) na Kilatini Verbum. Mwinjili Yohana anamtambulisha Yesu Kristo kuwa ni NENO wa MUNGU ametumwa kutoka kwa Baba, ni asili ya maisha, mwanga wa ulimwengu, aliyejaa neema na kweli, Mwana pekee wa Mungu, anayeufunua kwetu utukufu wa Mungu Baba na ni sura halisi ya Mungu Baba. Nasi tumeuona utukufu wake, ni Utukufu wa Mungu kati yetu wanadamu.

Neno, kwa lugha rahisi, ni mojawapo ya nyenzo ya mawasiliano kwani kwa neno au maneno tunaweza kuwasiliana. Mtoto aliyezaliwa bado ni mtoto mchanga na hivyo bado hawezi kuongea au kutumia maneno kama njia ya mawasiliano. Lakini bado mtoto huyu anaongea nasi kwa nafsi yake kama zawadi ya upendo wa Mungu kwa wanadamu wote. Huyu mtoto ndiye NENO WA MUNGU (Λογος). Ni Upendo wa Mungu kwetu wanadamu na ulimwengu mzima. Neno (Logos) wa Mungu ndio Hekima ya milele ya Mungu, ambayo kwayo Mungu ameumba ulimwengu. Neno halikuumbwa bali lilikuwepo pamoja na Mungu, na kwalo Mungu akauumba ulimwengu. Ni kwa njia ya Neno, Mungu anaumba ulimwengu. Ni Neno linaleta nuru duniani na kututoa katika maisha ya dhambi na giza. Hivyo ni nuru kwetu wanadamu. Yohane Mbatizaji sio ile nuru, bali ametumwa na Mungu kuja kushuhudia hiyo nuru ya kweli.  Amekuja ili kutuelekeza wanadamu nuru yenyewe. Alikuja ulimwenguni ile nuru yenyewe, ila watu hatukuitambua ile nuru, ila wale walioitambua na kuipokea wakafanyika wana wa Mungu. Ni kwa njia ya Neno nasi tunafanyika kuwa wana wa Mungu. Neno ni Mungu, hivyo anatunyanyua na kututoa katika uduni na udogo wetu ili nasi tuweze kushiriki maisha ya neema, yaani, ya urafiki na Mungu.

Neno alifanyika mwili na kukaa kwetu. Noeli ni sherehe ya umwilisho. Mwili katika lugha ya Kibiblia ni ishara ya uduni na unyonge wetu kama wanadamu, tunaweza kurejea nabii (Isaya 40: 6-8). Huyu Neno anafanyika mwili sawa na sisi katika yote isipokuwa hakuwa na dhambi. Ni upendo wa Mungu kutaka kufanana na mwanadamu ili mwanadamu aliye mnyonge na dhaifu aweze kushirika utukufu na utakatifu wa Kimungu. Mwanadamu anayekufa na kupotea katika uso wa nchi apate kuishi milele pamoja na Mungu, ndio upendo wa Mungu kwetu wanadamu na ulimwengu mzima. Nasi tutaona utukufu wake. Katika Biblia, mwanadamu hawezi kumuona Mungu kwa macho ya kibinadamu au macho ya nyama. Mwanadamu anaweza tu kuutafakari utukufu wa Mungu, yaani ishara za uwepo wa Mungu, na ukuu wa kazi zake kama alivyoonesha ukuu na uweza wake kwa Wamisri na Farao na jeshi lake. (Kutoka 14:17) Ila katika nafsi ya Yesu Kristo tunamwona Mungu. Anayemwona Yesu Kristo anamwona Mungu Baba kama alivyosema Yesu kwa Filipo. (Yohane 14:9)

Ni Mungu kwa mara ya kwanza anajifunua na kujidhihirisha kwa mwanadamu katika nafsi ya Mwana pekee wa Mungu na hivyo huyu mtoto aliyezaliwa amejaa neema na kweli.  Neema na kweli katika Maandiko Matakatifu ni sawa na upendo wa kiaminifu wa Mungu kwa watu wake. Ni uwepo wa Mungu mwenyewe kati yetu. Katika nafsi ya Yesu Kristo kuna ukamilifu wa upendo wa Kimungu kwa watu wake. Mtoto aliyezaliwa ni zawadi isiyo kifani ya Mungu mwenyewe kwa watu wake. Ni Mungu mwenyewe anajitoa zawadi kwetu. Yohane mwinjili mara nyingi anatueleza kuwa hakuna aliyemwona Mungu (Yoh. 5:37; 6:46; 1 Yoh. 4:12,20) na pia (Kutoka 33:20) ila hapa anatueleza kuwa aliyemwona Yesu, amemwona Mungu. Yatosha kumtafakari Yesu Kristo, kuangalia yale anayoyafanya, anayofundisha na kutuelekeza kuweza kukutana na Mungu mwenyewe. Nuru ya kweli inayotupelekea kuuona utukufu wa Mungu Baba ni nafsi ya huyu mtoto aliyezaliwa. (Yoh 14) Fumbo la umwilisho linatuacha na mshangao mkubwa juu ya Upendo wa Mungu kwetu wanadamu.

Mungu aliye wa milele anakubali kuchukua ubinadamu wetu wenye kuharibika, Mungu asiyeonekana anajifunua kwetu katika nafsi ya Mtoto Yesu. Ni rahisi labda kueleweka kwa Mungu anayebaki juu mbinguni na kutoa hukumu zake kali kwa wadhambi na wakosefu. Ila ni upendo wa namna gani aliye Muumba wetu anashuka na kukaa kati yetu, na ndio mwaliko wa Noeli kumkaribisha Masiha na kuishi naye katika maisha yetu ya siku kwa siku. Mtoto amezaliwa kwa ajili yetu, tumepewa mtoto mwanamume. Mtoto aliyezaliwa ni nuru ya kweli ili sote tuweze kutembea katika mwanga wa kweli, kuishi maisha adilifu kadiri ya mpango wa milele wa Mungu na sio kadiri tutakavyo sisi au inavyotupendeza sisi. Leo duniani tunaona kila aina ya uovu katika maisha yetu binafsi na kwa ulimwengu mzima kwa ujumla, kwa sababu tunakataa kumpokea na kumkaribisha huyu aliye nuru ya kweli katika maisha yetu, tunakataa kutembea katika nuru ya kweli na badala yake tunabaki tukitembea gizani, katika giza nene la dhambi na maovu.

Noeli ni mwaliko wapendwa wa kuanza maisha mapya, ya kutembea katika mwanga na nuru ya kweli, kuanza kuishi maisha ya neema, ndio maisha ya kuunganika na Mungu. Mwanga wa kweli ni Yesu Kristo, Logos, yaani, Neno wa Mungu aliyeutwaa mwili wetu wa kibinadamu na kukaa kati yetu. Noeli njema kwenu nyote na Mtoto Yesu azidi kuzaliwa katika maisha yetu, afanyike mwili na kukaa nasi. Na kila lenye heri na baraka kwa Mwaka mpya 2022! Kila mmoja wetu awe kweli baraka na zawadi kwa wale wote wanaotuzunguka katika mwaka huu mpya! Puer natus est nobis, et filius datus est nobis:Cuis imperium super humerum eius: et vocabitur nomen eius magni consilii angelus. Cantate Domino canticum novum, quia mirabilia fecit.

30 December 2021, 11:01