Dominika ya Tatu Ya Majilio: Yesu Ni Chimbuko la Furaha ya Kweli
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
UTANGULIZI: Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Majilio. Dominika hii inajulikana kama dominika ya furaha. Inachukua jina hili kutokana na mwaliko wa furaha ambao inautangaza; inatuambia “Furahini katika Bwana sikuzote, nasema tena furahini. Bwana yu karibu.” Kumbe tangu mwanzo kabisa dominika hii inatualika kutambua kuwa kama katika maisha yetu tunayemtazamia na ambaye kwake tumeweka tumaini letu ni Kristo, basi hatuna haja ya kuogopa. Tunahitaji kuwa na furaha. La, endapo katika maisha yetu tunamtazamia mwingin na tumeweka tumaini letu katika vitu vingine au mwingine nje ya Kristo, hapo hofu lazima iendelee kututawala. MASOMO KWA UFUPI: Ujumbe anaoutoa nabii Zefania katika somo la kwanza (Zef. 3:14-17) tunaweza kuulinganisha na mtu anayekwenda kumsalimu mgonjwa aliye taabani au aliye na majonzi mazito halafu anamwambia “simama, rukaruka na uchangamke”! Inaonekana si kawaida kabisa, lakini ndicho alichokifanya Zefania. Ujumbe wake uliwaendea waisraeli wakiwa utumwani, katikati kabisa ya mahangaiko, akawaambia “imba ee binti Sayuni, piga kelele ee Israeli…Bwana ameziondoa hukumu zako. Ni nini anachomaanisha nabii huyu? Zefania anatualika kuwa na furaha hata katika nyakati ngumu za kiimani na kimaisha. Kuna tofauti kati ya raha na furaha. Katika nyakati ngumu, ni wazi huwezi kuwa na raha; unaweza lakini kuwa na furaha; furaha inayotokana na imani na tumaini katika nguvu ya Mungu ya kuokoa.
Mtume Paulo katika Somo la Pili (Fil. 4:4-7), anaipeleka mbali zaidi dhana hii ya furaha. Anapowaandikia wafilipi anawasihi kuwa watu wa furaha daima katika Bwana. Kwa mwaliko huu tunatambua kuwa furaha ni tabia ya ndani kabisa tunayopaswa kuwa nayo mkristo. Kufurahi katika Bwana ni kuyaishi maisha ya kikristo sio kama mzigo au adhabu bali kama utashi kamili tunaoupokea kwa furaha pamoja na yote yaliyonayo. Tunapotoa huduma, tuitoe kwa furaha; tunapomtumikia Bwana, tumtumikie kwa furaha; ndoa zetu tuziishi kwa furaha, nadhiri zetu tuziishi kwa furaha, upadre wetu tuuishi kwa furaha. Tufurahi katika Bwana siku zote. Somo la Injili lenyewe linaendeleza mafundisho na ushuhuda wa Yohana Mbatizaji kutoka dominika iliyopita. Leo anatualika kuchukua maamuzi sahihi katika maisha. Wanamuuliza Yohane “tufanye nini basi” na yeye anawajibu kila mmoja kadiri ya hali yake. Umati anawaambia “mwenye nguo mbili ampe asiye naye”; watoza ushuru anawaambia “msitoze zaidi ya kilichoamriwa”; maaskari anawaambia “msidhulumu mtu wala kumshtaki kwa uongo na tena mtosheke na mishahara yenu”.
TAFAKARI YA Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio: Dominika ya leo inadokeza jambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Jambo hilo ni furaha katika maisha. Na kimsingi furaha ni mojawapo kati ya mahitaji makubwa ya mwanadamu. Mambo mengi tunayafanya, pamoja na malengo mengine, ili kupata furaha katika maisha. Yesu pia aliwahi kukutana na kijana aliyemuuliza, mwalimu mwema nifanye nini ili niurithi ufalme wa mbinguni? Nifanye nini ili niifikie furaha katika ukamilifu wake? Yesu alikuwa na la kumjibu na akamjibu. Awali tumedokeza juu ya kutokuchanganya mambo haya mawili: raha na furaha. Kuna utofauti kwa sababu si vyote vinavyompa mwanadamu raha vinamletea furaha katika maisha yake. Uzoefu wenyewe wa maisha unaonesha kuwa unaweza kuwa na vitu vyote vinavyokupa raha ila ukakosa furaha katika maisha. Na sababu yake ni moja tu kuwa raha inagusa vionjo vya nje vya maisha ya mwanadamu. Ni jambo la kimwili. Furaha yenyewe inagusa undani wa maisha yake. Inaugusa moyo.
Sasa, ni nini ambacho mwanadamu anatakiwa afanye ili afikie kuwa na furaha katika maisha yake? Ni nini kitamsaidia kufikia hali ile iliyodokezwa na masomo ya leo, hali ya kuwa na furaha hata katika mateso na mahangaiko kama ulivyo ujumbe wa nabii Zefania; hali ya kuwa na furaha kama tabia ya kila siku ya maisha ya mkristo kama ulivyo ujumbe wa Mtume Paulo? Jibu la swali hili sio rahisi, ni mchakato. Sio rahisi kama kusema kumeza kidonge fulani kinachoitwa furaha na kidonge hicho kikaenda kutibu mara moja ukosefu wa furaha moyoni. Ni mchakato unaohitaji siku kwa siku kuujaza moyo na yale yaliyo matamanio yake ya kweli. Sasa, kipindi hiki cha majilio kinapokuja na kutuamshia tumaini letu la kumngoja Kristo, kinatuambia pia kuwa Kristo ndio tumaini letu. Ni yeye tunayemtazamia na ni yeye anayeweza kuijaza mioyo yetu na furaha akatujalia furaha maishani. Mwaliko wenyewe wa dominika hii ni huo huo. Unasema “furahini katika Bwana”. Ndiyo kusema yeye atafutaye furaha katika maisha yake, na aitafute katika Bwana wetu Yesu Kristo. Nje ya Kristo hatuwezi kuipata kwa maana ni Kristo pekee anayejua mahitaji halisi ya mioyo yetu na ni yeye atujaliaye.
Tuhitimishe tafakari yetu kwa kunukuu sehemu ya maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa alipoualika ulimwengu mzima akisema; “msiogope, fungueni milango ya mioyo yenu kwa Kristo. Fungueni mioyo yenu kwa nguvu yake ya kuokoa. Fungueni mipaka ya nchi, fungueni mifumo ya kiuchumi, fungueni tamaduni zenu na harakati zote za maendeleo kwa Kristo, msiogope! Kristo anajua kilicho ndani ya moyo wa mwanadamu. Ni yeye pekee anayejua. Fungueni mioyo yenu kwa Kristo.”