Tafakari ya Neno la Mungu Domenika ya IV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Fumbo la Umwilisho: Emanueli yaani Mungu pamoja nasi. Tafakari ya Neno la Mungu Domenika ya IV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Fumbo la Umwilisho: Emanueli yaani Mungu pamoja nasi.  

Dominika ya 4 Ya Kipindi cha Majilio: Mungu Pamoja Nasi

Kwanza, Elizabeti alitamka maneno mazito yanayomtambulisha B. Maria “Umebrikiwa wewe katika wanawake wote, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa”. Haya ni maneno tunayosali daima katika sala ya Salamu Maria ambayo Elizabeti alikuwa wa kwanza kuyatamka akiangaziwa na Roho Mtakatifu na hivyo kukiri hadhi hii kubwa aliyopewa Bikira Maria ya kuwa ni Mama wa Mungu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya nne ya majilio mwaka C wa Kanisa. Hii ni Dominika ya mwisho ya kipindi cha majilio inayotualika kusherehekea kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Emanueli, Mungu pamoja nasi, siku ya Krismasi, Noeli kwa maneno ya wimbo wa mwanzo tukiimba: “Dondokeni, enyi mbingu toka juu, mawingu na yammwage mwenye haki; nchi ifunuke, na kumtoa Mwokozi” (Isa. 45:8). Ni maneno ya faraja na matumaini makubwa sana kwetu sisi wanadamu kwani yanatuonesha kuwa Mwokozi yu-karibu kuzaliwa. Kumbe masomo ya dominika ya nne ya majilio yanatuandaa na kutuweka katika mkao wa kusheherekea kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Nabii Mika (Mik. 5:2-4). Ili kulielewa vizuri somo hili yatupasa kuifahamu japo kwa kifupi historia yake. Jina Mika linatokana na neno la Kiebrania “Mikayah” likimaanisha; “Ni nani aliye kama Bwana?” Mika alizaliwa huko Moresheth-Gathi (1:14), kusini magharibi mwa Yerusalemu, katika ufalme wa Yuda, upande wa kusini wakati wa utawala wa Yothamu (751-736 K.K.), akaaishi mpaka kipindi cha utawala wa Ahazi (736-716K.K.) na Hezekia (716-687K.K).

Kumbe tunaona Mika aliishi wakati mmoja na Isaya na Hosea. Hivyo aliona na kushuhudia kuanguka kwa ufalme wa Israeli na kuwa jimbo la Ashuru (722-721 K.K). Kama Nabii Amosi alivyotabiri kuangamizwa kwa miji ya Samaria na Yerusalemu kwa sababu ya watawala, manabii na makuhani wake kuwa waongo na waovu, wafanya biashara kutokuwa waaminifu na mahakimu wao kupokea rushwa na kushindwa kuonyesha hali ya uchaji na hofu ya Mungu katika wajibu wao na hivyo kukakosekana kwa haki katika jamii, maskini kuonewa, maisha ya watu kukosa uadilifu na kukosekana kwa utakatifu katika maisha ya kila siku; ndivyo Mika navyo alivyowaonya watu juu ya dhambi zao za udhalimu, uroho, uchoyo, ufisadi na ibada za sanamu akiwaambia kuwa hali hii itapelekea hukumu iwapo hawatatubu na kuziacha njia zao mbaya. Hali halisi ya kisiasa ilivyokuwa inaelezwa vizuri katika 2Wafalme 15-20 na 2Nyakati 26-30. Kitabu hiki cha Mika kimegawanyika katika sehemu kuu nne; sehemu ya kwanza inahusu hukumu dhidi ya miji ya Samaria na Yerusalemu (1:1-16), ambapo Mika anaonya juu ya hukumu ya Mungu dhidi ya ufalme wa Yuda ambao mji wake mkuu ulikuwa Yerusalemu na Ufalme wa Israeli ambao mji wake mkuu ulikuwa Samaria.

Sehemu ya pili inaongelea uonevu wa viongozi wake (2:1-3:12); sehemu ya tatu inahusu utabiri wa marejesho ya kiMungu (4:1-5:15) na sehemu ya mwisho inahusu hukumu na huruma ya Mungu (6:1-7:20). Sehemu tunayosomwa katika domenika hii ya nne ya majilio ni sehemu ya tatu ya marejesho ya kiMungu. Sehemu hii inatujulisha ahadi ya Mungu ya kumleta Mkombozi wa pekee kutoka Bethlehemu mji wa mfalme Daudi. Ni ahadi ya kufanywa upya kwa Sayuni na kurejeshwa kwa utawala wa amani kwa wale wanaomwamini na kumtumaini Mungu. Sayuni itakayofanywa upya itakuwa ndiyo kitovu cha utawala wa ulimwengu wote, mahali ambapo amani halisi na haki vitatawala. “Mtawala katika Israeli,” ambaye atazaliwa Bethlehemu, atasimamisha utawala ambao utadumu milele. Huyu mtawala ndiye Yesu Kristo, mfalme wa amani na haki tunayemsubiri azaliwe upya ndani ya mioyo yetu ili kurejesha upya utawala wa Mungu katika maisha yetu.

Somo la Pili la Waraka kwa Waebrania (Ebr. 10:5-10); ni mhutasari wa lengo la la fumbo la umwilisho: “Tazama nimekuja kuyafanya mpenzi yako Ee Mungu”; ndivyo anavyoshuhudia Yesu Kristo nafsi ya pili ya Mungu (Ebr 10:5). Na mapenzi ya Mungu ni wote wapate uzima wa milele kwa njia yake. Kwa sababu ya kazi hiyo, Mungu Baba alimpa Mwana mwili ili ajitoe sadaka kwa ajili ya utakaso wa dhambi zetu. Somo hili la waraka kwa Waebrania, latueleza kuwa Yesu mwenyewe aliutoa mwili wake kwa hiari kama sadaka pekee na kamilifu akitimiza matakwa ya Mungu Mwenyezi. Somo hili latufundisha pia kuwa Sadaka ya Yesu Msalabani ni sadaka kamili na timilifu iliyofunga Agano jipya na la milele na kukomesha lile la zamani ambalo halikuwa timilifu maana lilifanywa kwa dhabihu, matoleo na sadaka za kuteketeza wanyama ambazo Mungu hakupendezwa nazo sababu hazikuwa timilifu sababu ya dhambi.

Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk. 1:39-45); ni simulizi la kukutana kwa Mariamu (Bikira Maria) na Elisabeti; wanawake maarufu katika mpango wa Mungu wa kutukomboa sisi wanadamu kutoka utumwa wa dhambi na mauti, ambapo Yohane Mbatizaji akiwa tumbani mwa mama yake anashangilia kwa kufuraha kukuta na mkombozi wetu Yesu Kristo naye akiwa tumboni mwa mamaye Bikira Maria. Hivyo, kabla ya kuzaliwa kwake, Yohane anaanza kazi ya kumdokeza Mkombozi anayekaribia. Elisabeti anatambua kwanza ishara inayodokezwa na mwanawe, na kwa furaha na uchaji anampokea Mariamu. Mwinjili Luka anasimulia kwa ustadi mkubwa mno yaliyotokea na kutamkwa na Elizabeti baada ya Bikira Maria kuingia kwake na kumsalimu. Kwanza, Elizabeti alitamka maneno mazito yanayomtambulisha Maria kuwa ni Chombo kiteule cha Mungu cha kumleta Mkombozi ulimwenguni akisema; “Umebrikiwa wewe katika wanawake wote, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa”. Haya ni maneno tunayosali daima katika sala ya Salamu Maria ambayo Elizabeti alikuwa wa kwanza kuyatamka akiangaziwa na Roho Mtakatifu na hivyo kukiri hadhi hii kubwa aliyopewa Bikira Maria ya kuupokea na kuufunua kwetu mpango wa Mungu wa ukombozi wa mwanadamu.

Elizabeti akaendelea kusema; “Limenitokeaje neno hili, hata Mama wa Bwana wangu anijie mimi?” Kwa maneno haya Elizabeti anatutangazia kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu-Theotokos kwani kwake nafsi yake ya pili – Mungu-Mwana kwa fumbo la umwilisho alizaliwa Mwokozi Yesu Kristo naye Bikira Maria ni mama ya Kristo-Christokos. Kisha Elizabethi akaendelea kusema: “Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kiliruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu”. Mtoto huyu ni Yohane Mbatizaji, mtangulizi wa Yesu Kristo ambaye angali bado tumboni mwa mama yake Elizabeti alimtambua Maria kuwa ni Mama wa Mungu na akamshangilia kwa furaha yeye na Masiya aliyemchukua. Nao Mababa wa Kanisa wanasema kuwa kwa nafasi hii ya Yohane Mbatizaji kumtambua na kumtambulisha Kristo kwa watu angali bado tumboni, alipata bahati ya kuondolewa dhambi ya asili kabla ya kuzaliwa kwake. Tukio hili la Bikira Maria kumtembelea Elizabeti linaweka wazi kuwa Bikira Maria ni Mama wa furaha na amani, ni mama aliyejaa fadhila ya unyenyekevu na uvumilivu, aliyeshiriki fumbo la ukombozi wetu na hivyo kustahili kupalizwa Mbinguni mwili na roho anakoendelea kutuombea nasi tufike mbinguni aliko yeye.

Kwa unyenyekevu na upendo kwa mwanadamu, Mungu nafsi ya pili, Yesu Kristo alijishusha na kutwaa ubinadamu wetu katika fumbo la Umwilisho ili apate kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Basi tunaposubiri ujio wa Masiha, tuweke nia sahihi ya kubadili mienendo yetu ambayo inapingana na maisha yetu ya kikrito. Bikira Maria awe kimbilio letu, awe kiongozi wetu awe mwombezi wetu kwa mwanae ili nasi tupate neema na baraka za kuufikia uzima wa milele. Tuitumie vyema nafasi hii ya pekee ya siku zilizobaki katika kipindi hiki cha majilio tujipatanishe na Mungu Baba katika nafsi zetu, ili Kristo ajapo atukute tupo katika hali ya neema ya utakaso aweze kuzaliwa upya katika mioyo yetu atujaze neema na baraka zake za amani na upendo nasi tuweze kuendelea kuisha kwa furaha.

Majilio J4
14 December 2021, 15:10