Dominika ya Pili Baada ya Sherehe ya Noeli Mwaka C wa Kanisa: Hekima
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
UTANGULIZI: Dominika ya II baada ya Sherehe za Noeli. Tunaendelea kutakiana Heri na Baraka kwa mwaka mpya 2022 ili mwaka huu uendelee kuleta Neema ya Mungu katika maisha yetu. Tupo bado katika kipindi cha Noeli na dominika hii tunaadhimisha dominika ya II ya Noeli, dominika ambayo inazidi kutufunulia Fumbo la Neno wa Mungu kutwaa mwili na kuja kufanya makao yake kati yetu. Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza linatoka katika Kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira (Sir 24,1-4.12-16). Kwa utangulizi mfupi tu, hiki ni mojawapo ya vitabu saba katika Agano la Kale ambavyo vipo katika Biblia yetu ya kikatoliki lakini havipo katika Biblia ya kiprotestanti. Pamoja na kuwa vitabu hivi viliandikwa kwa lugha ya Kiyunani (Kigiriki) tofauti na lugha ya Kiyahudi (Kiebrania) kama vitabu vingine vya Agano la Kale, Kanisa Katoliki limevipokea kwa sababu tangu mwanzo, Wakristo wa Kanisa la mwanzo kabisa walivipokea kama vitabu vilivyo na ufunuo wa kimungu na vimethibitika kuwa hivyo. Katika somo la leo, Kitabu hiki kinatuletea Utenzi wa Hekima. Katika utenzi huu, Hekima inahuishwa na ni yenyewe inaanza kuimba sifa zake.
Hekima hii ni kitu gani? Katika Uyahudi, hekima ilimaanisha maarifa yanayomfanya mtu kuishi vizuri na katika uhusiano mwema na Mungu wake. Hii ilikuwa ni tofauti na jinsi mataifa mengine yalivyoielewa hekima. Kwao hekima ilikuwa ni maarifa yaliyomwezesha mtu kufanikiwa na kuishi kwa raha. Kwa Wayahudi hakukuwa na mafanikio katika Maisha kama mtu haishi katika mahusiano mem ana Mungu. Ni kwa sababu hii, hekima waliifananisha na Torati – sheria ya Musa. Wakristo wa mwanzo walienda mbele zaidi. Hawakuiona hekima kama Torati peke yake yake. Ndani ya hekima walimwona Kristo. Kristo ndiye hekima ya Mungu, yeye ndiye ampaye mtu maarifa ya kuishi Maisha mema na yanayompendeza Mungu Maneno ya utenzi wa hekima tunayoyasikia katika somo la kwanza yanahusishwa moja kwa moja na fumbo la Kristo kutwaa mwili. Hekima anasema “mimi nilitoka kinywani mwake Aliye juu… nikatia shina katika taifa lililo tukufu, naam katika sehemu ya urithi wa Bwana.” Maneno haya yanatimia katika Kristo aliyetoka kwa Mungu Baba akashuka, akazaliwa katika taifa la watu wa Mungu. Mtume Paulo katika somo la pili (Ef 1,3-6.15-18) anahitimisha utenzi wa sifa kwa Mungu akimwomba kwa ajili ya Wakristo wa Efeso ili Mungu awape roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua Yeye. Roho ya hekima ni roho ya Kristo; ni Kristo mwenyewe aliyetwaa mwili akazaliwa kwetu.
Somo la Injili linatoka katika Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn 1:1-18). Ni mwanzo wa Injili ya Yohane na ni mwanzo ambao unatupeleka mwanzo. Inatuonesha kuwa hapo mwanzo kulikuwa na Neno naye Neno alikuwa kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu. Kisha huyo Neno akatwaa mwili akakaa kwetu, nasi tukauona utukufu wake. Injili hii inamzungumzia Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwanadamu. Na inatuonesha kuwa huyu Neno wa Mungu alikuwapo kabla hata ya kuwapo vitu vingine vyovyote. Mwanzo unaozungumziwa hapa sio mwanzo kwa maana ya muda, ni mwanzo ule wa uumbaji. Ndiyo maana ukiangalia vizuri namna injili hii inavyoanza, inatumia maneno yaleyale kama ya kitabu cha Mwanzo katika Agano la Kale, Kitabu kinachoelezea uumbaji wa ulimwengu na vyote vilivyomo. Jambo la pili linaloelezwa na Injili ya leo ni kuwa Neno huyo ni Mungu. Na la tatu ni kuwa huyo Mungu, kwa njia ya Neno ameshuka duniani akafanyika mwili. Naye amekuwa mwanga na uzima kwa wote wanaompokea.
Tafakari fupi: Mpendwa msomaji na msikilizaji wa Vatican News, Dominika hii ya pili ya Kipindi cha Sherehe za Noeli na inaendelea kutufafanulia Fumbo la Noeli tunaloliadhimisha. Tumeona katika masomo, Kristo anafananishwa na Hekima, na pia anafananishwa na Neno. Anaelezewa katika lugha ya ufahamu na ya kimapokeo ambayo ilieleweka vizuri sana kwa watu wakati huo Maandiko haya Matakatifu yalipoandikwa. Katika tafakari yetu ya leo, tuliangalie hilo fundisho linazidi kurudiwa rudiwa katika masomo haya ya Noeli, fundisho kuwa Hekima hiyo na Neno hilo ambalo ni Kristo, limetwaa mwili na likaweka makao yake kati yetu. Ni fundisho linalotuambia tena na tena kuwa katika Kristo, Mungu mwenyewe ameshuka duniani. Mungu ameamua kuondoa umbali uliopo kati yake na mwanadamu, ameamua kuja kuishi naye ili amkomboe. Mara nyingi sana mwanadamu amekuwa anajiuliza: Mungu yuko wapi? Wakati wa mauaji ya kimbari Rwanda na Burundi, wakati wa vita ambapo watu wasio na hatia kabisa wanauawa kinyama na wengine kuachwa na vilema vya maisha Mungu huwa yuko wapi? Sasa hivi dunia nzima inateseka kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na watu maelfu kwa maelfu wanazidi kupoteza maisha, hivi Mungu haoni? Yuko wapi? Wakati familia zinasambaratika kwa magomvi, wakati ndoa zinavunjika, wakati maovu yanaongezeka na watu wanazidi kuteseka Mungu yuko wapi?
Fumbo la Noeli tunaloliadhimisha linazidi kutuambia kuwa Mungu wetu sio Mungu anayejificha katika nyakati kama hizo. Yeye ni Mungu aliye na maskani yake kati ya watu, na kama alivyofundisha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, wakati watu wa Mungu wanateseka, Mungu anateseka pamoja nao. Mahangaiko na maumivu ya watu wa Mungu ni mahangaiko na maumivu ya Mungu pia. Na huenda mahangaiko makubwa ya Mungu ni pale anapomwona mwanadamu anazidi kujitenga naye; mwanadamu anaukimbia mwanga anapendelea giza na huko gizani anajiingiza katika mahangaiko na anakuwa chanzo cha mahangaiko kwa mwanadamu mwingine. Zitakoma vipi vita ikiwa utengenezaji wa silaha za kumuua mwanadamu ni biashara? Utaisha vipi umaskini wakati wizi na ubadhilifu vinakuwa ndio kipimo cha uongozi au wakati maslahi ya wengi yanahodhiwa na wachache kutokana na siasa duni na uongozi usiojali misingi na thamani ya utu, yataisha vipi magomvi na uhasama ikiwa kila mmoja anaendeleza ubinafsi na kujiona kuwa bora kuliko mwingine. Mwanadamu anateseka na Mungu anateseka pia. Yeye amekuja kuleta mwanga wa kumuangazia mwanadamu. Anasubiri mwanadamu aache kupendelea giza augeukie mwanga ili aupate uzima.