Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Majilio: Furahini katika Bwana, kwa sababu wokovu wenu umekaribia. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Majilio: Furahini katika Bwana, kwa sababu wokovu wenu umekaribia. 

Dominika ya Tatu ya Kipindi Cha Majilio: Wokovu Umekaribia Furahini

Tunaalikwa kufurahi kwa sababu tumekaribia mwishoni mwa Kipindi cha Majilio, kipindi cha maandalizi, kipindi cha kusubiria ujio wa Masiha. Hivyo sherehe ya Noeli i karibu, inabisha hodi katika malango ya mioyo yetu. Ndiyo maana dominika hii huitwa kwa Kilatini Dominica Gaudete yaani Dominika ya furaha. Waamini wanaalikwa kufurahi kwa sababu wokovu wao umekaribia sana!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio mwaka C wa Kanisa. Furahini nyote Bwana yu karibu ni mwaliko wa masomo ya Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio. Tunaalikwa kufurahi kwa sababu tumekaribia mwishoni mwa Kipindi cha Majilio, kipindi cha maandalizi, kipindi cha kusubiria ujio wa Masiha. Hivyo sherehe ya Noeli i karibu, inabisha hodi katika malango ya mioyo yetu. Ndiyo maana dominika hii huitwa kwa Kilatini Dominica Gaudete yaani Dominika ya furaha. Katika somo la kwanza Nabii Zefania (Zef 3:14-18), anawaalika Waisraeli wafurahi na kushangilia kwa sababu Mungu mfalme wao karibu atawaondoa na kuwaangamiza maadui wao. Historia inasimulia kuwa baada ya kuingia na kutawala nchi ya ahadi (Kanaani), katika kipindi cha utawala wa mfalme Manase (mwaka 689 hadi 642 KK) na Mfalme Amoni (Mwaka 642 hadi 640 KK), wafalme hao walirudia ibada kwa miungu ya mataifa mengine kwa nguvu sana. Mfalme Manase alidiriki hata kujenga madhabahu ndani ya hekalu la Yerusalemu kwa heshima ya Baali ambayo ni miungu ya kipagani ya Wakanaani na mbaya zaidi aliabudu jua, mwezi na nyota, na hata kumtoa mwanae sadaka kwa miungu hiyo na kufanya mengi yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na machukizo ya mataifa aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli (2Fal. 21:2-18).

Naye Mfalme Amoni aliendeleza utovu wa nidhamu wa baba yake, kwani alimwacha Bwana Mungu wa baba zake, wala hakushika njia ya Bwana (2Fal. 21:19-26). Kutokana na dhambi zao, Mwenyezi Mungu aliamua kuwaadhibu kwa kuyaruhusu mataifa mengine yawachukue waisraeli kama watumwa na kuwafanyisha kazi nyingi. Hata hivyo, kutokana na huruma yake kuu kwa watu wake, Mungu anamtuma nabii Sefania kuwapa wana wa Israeli ujumbe wa furaha, kuwa wokovu wao upo karibu, wazidi kumtumainia Mungu, shujaa pekee awezaye kuwaokoa. Hivyo wanaalikwa kuimba, kupiga kelele za shangwe, kufurahi na kushangilia kwa moyo wote. Sababu ya shangwera hizi ni kuwa Bwana ameziondoa hukumu juu yao, amemtupa nje adui yao, naye Bwana Mungu mfalme wao, Yu katikati yao, hivyo hawapaswi kuogopa wala kuwa na wasiwasi tena. “Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako, Shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atatulia katika upendo wake. Atakufurahia kwa kuimba” (Zef. 3:14-18). Mwaliko huu ni wetu sisi nyakati zetu. Nasi tunaalikwa kufurahi kwani ujio wa Kristo u-karibu.

Mtume Paulo katika Somo la pili la Waraka wake kwa Wafilipi (4:4-7), Vilevile, anawaalika wakristo wafilipi wawe na furaha daima, huku wakiendelea kumsubiri Bwana ambaye ndiye utimilifu wa furaha yao. Wafilipi wanapaswa kuwa wavumilivu, wapole, wema, watulivu na wenye kudumu katika imani. Tena, anawaasa wasijisumbue na mambo yoyote ambayo hayatawafikisha mbinguni, bali wadumu katika kusali, kuomba na kumshukuru Mungu kwa yote anayowajalia. Haja na mahitaji yao yote yafikishwe kwa Mungu mwenye kuwapenda na kuwasaidia wote wamkimbiliao kwa unyofu. Ujumbe huu wa Paulo usema; “Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema, furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu”.  Huu ni ujumbe wa nyakati zote. Nasi hatuna budi kufurahi, kwa kuwa Bwana yu-karibu. Noeli i-karibu. Furaha tunayopaswa kuwa nayo kwa mwaliko wa Paulo wa kufurahi inapaswa kuwa kubwa zaidi ya ile ya Waisraeli waliyoalikwa na Zefania. Hii ni kwasababu sisi tumekwisha samehewa dhambi zetu na Mungu. Nabii Zefania aliwaambia Wayahudi kwamba dhambi zao zitasamehewa. Sisi tumekwisha samehewa. Mtu anayedaiwa na asiye na uwezo wa kulipa fidia, anakuwa na furaha kubwa anapoambiwa kwamba deni lako limefutwa/kusamehewa. Ndivyo tunavyopaswa kufurahi na sisi.

Luka katika Injili (3:10-18), anamwonesha Yohane Mbatizaji akiwafundisha watu wawe na mwenendo mwema. Anakiri kuwa Kristo mwenye uwezo zaidi, atakuja kuwahukumu watu wote kadiri ya matendo yao. Matendo mema ndiyo njia ya uadilifu. Yohane Mbatizaji anatuasa kuwa; mwenye kanzu mbili anapaswa kumpa asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Zaidi sana Yohane anayakemea na kuyaonya makundi mbalimbali ya uongozi katika jamii; watoza ushuru na askari, wanasheria; kuwa yasiwe kikwazo cha amani kwa watu na kwa jamii nzima. Kwa watoza ushuru wasitoze kitu zaidi kuliko walivyoamriwa na askari wasidhulumu mtu, wala kushitaki kwa uongo; tena watoshewe na mishahara yao. Yohane pia anatoa mazingira ya hukumu ya mwisho kuwa matendo ya mwanadamu yatafananishwa na ngano bora na makapi. Wote wenye kuziandaa roho zao vizuri kwa matendo mema wataingia katika uzima wa milele bali wasiojiandaa vyema yaani wenye dhambi, ndiyo makapi ambayo yatateketezwa kwa moto usiozimika, yaani kutokuonana na Mungu milele yote. Mwaliko wa furaha unaotolewa na masomo ya domenika hii ni furaha katika Bwana. Tusiitafute furaha katika vitu kwani matokeo yake ni kuitafuta furaha katika dhambi, jambo ambalo halimfikishi mtu katika furaha kamili ya kuonana na Mungu bali huleta mahangaiko moyoni. Kumbe kadiri tunavyozidi kujiandaa kwa ujio wa Masiha ambaye atazistawisha na kuzichunga roho zetu, tuyaandae makao yake kwa kuzisafisha roho zetu. Tufanye upatanisho na kutoa msamaha kwa wale wote waliotukosea. Mwokozi tunayemngojea ndiye asili na utimilifu wa furaha. Sisi wabatizwa na wafuasi wa Kristo tuwe chanzo cha furaha kwa wengine.

Majilio J3
09 December 2021, 17:27