Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Majilio. Bikira Maria anamtembelea Elizabeti: Toba, Wongofu wa Ndani: Upendo kwa Mungu na Jirani. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Majilio. Bikira Maria anamtembelea Elizabeti: Toba, Wongofu wa Ndani: Upendo kwa Mungu na Jirani. 

Jiandaeni Kuadhimisha Fumbo la Umwilisho: Utimilifu wa Unabii

Katika kipindi hiki cha Majilio, Kanisa linatupatia pia mifano ya watu mbalimbali kutoka katika Maandiko Matakatifu. Watu hao wanaletwa kwetu kulingana ili kutusaidia kulielewa zaidi fumbo hili tunaloliadhimisha. Ni kwa jinsi hiyo tumewatafakari Manabii na ujumbe wao, tumemtafakari Yohane Mbatizaji na Mtakatifu Yosefu. Dominika hii inatupa mfano wa Mama Bikira Maria na Elizabeti.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Dominika ya Nne ya Majilio. Safari yetu ya majuma manne ya Majilio inafika katika juma la mwisho, juma ambalo linatuingiza katika maadhimisho ya Noeli. Katika sehemu hii ya mwisho ya Majilio, dhamira kuu si tena kujiandaa kwa ujio wa pili wa Kristo, dhamira iliyotuongoza katika majuma mawili ya kwanza ya majilio, dhamira kuu sasa ni kujiandaa kuadhimisha ujio wake wa kwanza, yaani kutwaa mwili na kuzaliwa kama mwanadamu. MASOMO KWA UFUPI: Somo la kwanza, kutoka Kitabu cha Nabii Mika (Mika 5, 1-4a), linatuonesha kuwa kuzaliwa kwa Kristo kunakuja kama utimilifu wa unabii. Yesu anazaliwa si kama anavyozaliwa mwanadamu mwingine. Anazaliwa ili kuja kuutekeleza mpango wa Mungu unaohusu wanadamu wote na ulimwengu mzima. Akakuja kukomboa. Mpango huu wa kuukomboa ulimwengu, Mungu alikuwa amekwisha utangaza kwa njia ya manabii. Na kwa kweli sio Mika pekee aliyetoa unabii huu. Manabii wote walikuwa na kazi hiyo, kuutangaza ujio wa masiha na kuiandaa mioyo ya watu kwa ujio huo. Liturjia ya dominika hii inatuletea unabii wa Mika kwa sababu ndio unaotaja mji atakaozaliwa Masiha. Unataja Betlehemu, mji uliokuwa mdogo kabisa. Kilikuwa ni kijiji, tena cha pembezoni. Huko ndiko atakakotoka Masiha na Mkombozi wa ulimwengu.

Katika Somo la Pili, Somo la Waraka kwa Waebrania (Ebr. 10,5-10) tunayasikia maneno haya: “ndipo niliposema, tazama nimekuja niyafanye mapenzi yako Mungu.” Haya ni maneno ya Zaburi 40 ambayo Waraka huu wa Waebrania unayatumia kumuelezea Yesu. Ni maneno yanayotoa muhtasari wa maisha yote ya Yesu. Waraka huu unatuambia kuwa maisha yote ya Yesu unaweza kuyapa muhtsari katika maneno hayo, kuwa yeye ndiye anayekuja kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Na kwa njia hiyo anamkomboa mwanadamu na kuukomboa ulimwengu mzima. Kwa namna moja anatuonesha kuwa hata leo, ukombozi wa mwanadamu katika hali zake zote unaanza pale ambapo mwanadamu anajiweka tayari kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Ni pale mwanadamu anapofika mahala na kusema “mimi niko hapa duniani kwa sababu yako Mungu, maisha yangu yote yamo ndani ya mipango yako na mimi si kitu bila wewe.” Ni ujumbe mzito ambao somo hili linatupatia kuwa Noeli hii tunayojiandaa kuiadhimisha, sio suala la sherehe tu na kufurahi, ni suala pia la kumuona Yesu kama yule anayekuja kutuonesha namna ifaayo ya kuishi hapa duniani. Anakuja kutufundisha utii kwa Mwenyezi Mungu Katika kipindi hiki cha Majilio, Kanisa linatupatia pia mifano ya watu mbalimbali kutoka katika Maandiko Matakatifu. Watu hao wanaletwa kwetu ili kutusaidia kulielewa zaidi fumbo hili tunaloliadhimisha. Ni kwa jinsi hiyo tumewatafakari Manabii na ujumbe wao, tumemtafakari Yohane Mbatizaji na Mtakatifu Yosefu. Dominika hii inatupa mfano wa Mama Bikira Maria. Kwa jinsi hii tunasoma Injili ya Luka (Lk 1: 39-45) Simulizi la Bikira Maria kwenda kumtembelea Elizabeti.

TAFAKARI YA JUMAPILI: Tafakari ya Dominika ya Nne ya Kipindi cha Majilio inajikita katika somo la Injili: tukio la Bikira Maria kwenda kumtembelea Elizabeti. Kutoka katika Injili hii hii ya Luka tunapata kujua kuwa Elizabeti na Zakaria mumewe walikuwa ni wazee sana na hawakuwa na mtoto kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa. Kwa familia, tayari hili ni tatizo. Malaika anamtokea Zakaria akiwa hekaluni na anamwambia kuwa Elizabeti mkewe atamzalia mwana. Zakaria anashindwa kuamini. Kama alama ya kutokuamini kwake anapigwa na ububu asiweze kuongea tena. Hili pia lilikuwa ni tatizo. Tena ni tatizo juu ya tatizo katika familia hiyo ambayo sasa katika uzee ilikuwa inamtarajia mtoto. Bikira Maria anapopashwa habari na malaika Gabrieli, anajulishwa pia kuwa Elizabeti ndugu yake naye ni mjamzito. Ndipo anafunga safari kwenda kumtembelea. Elizabeti anapomwona Bikira Maria anashituka: anasema “imenitokeaje jambo hili hata mama wa Bwana wangu aje kunitazama?” Neno Bwana lilitumika kumaanisha Mungu. Na hivi Elizabeti anatambua kuwa Maria anambeba Mungu ndani ya tumbo lake. Injili haituelezi Elizabeti alijuaje: nawezekana alifunuliwa na Mungu mwenyewe, inawezekana tukio la kupashwa habari Maria lilifahamika kati ya ndugu, injili inatuoesha tu mwitikio wake ulikuwaje. Elizabeti aliyejiona mnyonge na mdogo kwa changamoto mbalimbali zilizomkumba na zilizoikumba familia yake, anajikuta ametembelewa na Mama wa Mungu. Haamini kama Mungu angeweza kumwona katika udogo na unyonge wake huo. Na ni hapa ndipo mwinjili Luka anaelezea fumbo la ujio wa Yesu Kristo duniani.

Noeli tunayoingoja ni ujio wa Kristo -Mungu anayekuja kukutana na udogo, unyonge na udhaifu wa maisha ya mwanadamu. Pale ambapo mwanadamu anafikia hatua ya kusema; ‘Mungu hanioni, Mungu labda hajui hata kama ninaishi, haoni ninayoyapitia’. Na tena ‘hivi kati ya watu wote wanaomwomba na kumlilia Mungu, kati ya mambo mengi na makubwa anayofanya mimi nina nini hadi anisikilize? Noeli inakuja kutuonesha kuwa kwa namna kama ile Maria aliyokwenda kumtembelea Elizabeti ndivyo Kristo anavyokuja kutufikia. Kristo anakuja afike nyumbani kwako unapoishi, kazini kwako, katika biashara yako, katika utume wako na hasa zaidi katika moyo wako. Ni kwa njia hii Kristo anajitambulisha kuwa kweli Emanueli, yaani ni Mungu pamoja nasi. Si Mungu anayeketi mbinguni katika kiti cha enzi akiwaacha mbali wanadamu. Ni Mungu anayeshuka na kukaa na wanadamu ili awainue na auinue ubinadamu wote ufanane na umungu, kwa sababu uliumbwa na sura na mfano wake. Dominika hii ya mwisho ya Majilio iamshe basi ndani yetu moto wa matumaini. Tumfungulie Mungu milango ya mioyo yetu ili aje azaliwe ndani mwetu. Tuukumbuke tena mwaliko wa Yohane Mbatizaji: tuitengeneze njia ya ujio wa Kristo kwa toba, maungamo na wongofu wa kiroho ili tujiweke tayari kuadhimisha Noeli ya Bwana.

Liturujia Majilio J4

 

17 December 2021, 13:59