Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio: Tema kuu: Furahini katika Bwana! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio: Tema kuu: Furahini katika Bwana! 

Dominika ya Tatu ya Kipindi Cha Majilio: Haki Katika Huduma Ya Upendo

Tufurahi kwani Bwana yu karibu! Ujio wake unatupa maisha mapya ya kuwa wana wa Mungu, na katika hilo tunapata furaha ya kweli. Ni kwa kuishi maisha ya uana wa Mungu tunakuwa huru na wenye furaha ya kweli. Tafakari yetu leo, inatusaidia kuona ni kwa jinsi gani tunaweza kufikia hiyo furaha ya kweli katika maisha yetu kama wafuasi wake Yesu Kristo. Nasema "Gaudete! Furahini!

Na Padre Gaston Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Furahini katika Bwana siku zote! Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio pia hujulikana kama “Dominika ya Furaha”, inaitwa kwa Kilatini: “Gaudete” maana yake ni Furahini. Na ndio antifona ya mwanzo katika Liturujia ya Misa ya leo kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi, inatualika kufurahi katika Bwana siku zote.  Tufurahi kwani Bwana yu karibu! Ujio wake unatupa maisha mapya ya kuwa wana wa Mungu, na katika hilo tunapata furaha ya kweli. Ni kwa kuishi maisha ya uana wa Mungu tunakuwa huru na wenye furaha ya kweli. Tafakari yetu leo, inatusaidia kuona ni kwa jinsi gani tunaweza kufikia hiyo furaha ya kweli katika maisha yetu kama wafuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo. Si nia wala lengo langu kuanza mijadala ya kifalsafa na migumu juu ya maana ya furaha ya kweli au nini maana ya furaha. Itoshe kama Yohana Mbatizaji jinsi alivyoweka kwa maneno mepesi na rahisi kueleweka kwa hadhira yake walipofika kwake ili wabatizwe Ubatizo ule wa toba. Ni hamu yetu katika Dominika ya leo kuuliza swali lile lile walilouliza wale watu waliokwenda kwa Yohane Mbatizaji. Katika sehemu ya Injili ya leo tunaona makundi matatu, yaani makutano, watoza ushuru na maaskari. Tufanye nini nasi, ni swali lisilo na hila kwa yule anayetaka kuoneshwa au kufundishwa nini cha kufanya baada ya kutambua makosa au madhambi yake.

Ni swali nyofu lisilo na kujikweza au kujihesabia haki.  Linapaswa kuwa ni swali la kila mmoja wetu tunapojiandaa kwa ujio wake Mwokozi wetu. Nini napaswa kufanya au ni jinsi gani napaswa kuishi maisha yangu ya siku kwa siku katika hali zote na popote na yeyote. Nini wajibu wangu kwa Mungu na kwa jirani? Kwa namna ya maisha ya Yohane Mbatizaji aliyejitenga na malimwengu na kwenda kuishi jangwani, maisha ya umonaki na upweke labda tungelitegemea mwaliko wa watu watoke pia katika maisha ya yao ya kawaida na kuishi kama yeye kule jangwani. Ni kishawishi wakati fulani kutaka kila mmoja aishi kama mimi au aina ya maisha niliyochagua mimi ili kupata furaha ya kweli. Ni kishawishi kikubwa hata kwa wahubiri kudhani furaha ya kweli inaanza katika kusali, kufunga, kushika taratibu za kidini na mambo kama hayo. Au pengine kwa kuwa Padre au mmonaki au mtawa au kuwa na maisha ya pekee, ndio hakika ya kupata furaha ya kweli. Kwa kweli hapana, kadiri ya Yohane Mbatizaji tunaona kila mmoja katika maisha yake yake kuna jambo la kuzingatia ili kuipata hiyo furaha ya kweli.

Yohane Mbatizaji anatualika nasi kuanza katika maisha yetu ya kawaida kabisa ya siku kwa siku. Mabadiliko ya wongofu wa kweli yanaanza na upendo kwa jirani. Dominika iliyopita mwaliko wa Yohane Mbatizaji ulikuwa ni kubadili vichwa vyetu, kwa maana namna zetu za kufikiri mintarafu mahusiano yetu na Mungu, na leo anatualika pia kubadili vichwa vyetu kwa kuangalia mahusiano yetu na jirani, ndio upendo, haki na umoja wa kindugu kati yetu kwa kujaliana na kutendeana iliyo ya haki. Tunakusanyika kila Dominika kushukuru, kusifu, kutukuza na kuomba hivyo basi sala yetu haina budi kutusaidia katika kufanya mabadiliko ya kweli katika maisha yetu ya siku kwa siku. Haitoshi kuwa wakristo wa Dominika tu au wa sala tu bila kuweka imani yetu katika maisha yetu ya siku kwa siku, yaani katika matendo. Hii ni hatari kubwa kwetu kuona inatosha ninakwenda kanisani au jumuiyani au nasali kila siku na familia yangu. Leo tunaalikwa kutafakari mahusiano yetu na wenzetu iwe nyumbani katika familia, na majirani na ndugu na jamaa na marafiki na hata sehemu zetu za kazi na popote pale namna tunavyohusiana na wengine. Kusali ni kuingia katika mahusiano ya upendo kwa Mungu kwa nafasi ya kwanza na hapo tunakuwa na macho ya imani ya kuweza kuona sura na mfano wa Mungu kwa wengine.

Sala ni mlango unaopaswa kutuingiza katika muono mpya, ni kutufungua macho ya rohoni ili tuweze kumpenda kweli Mungu na jirani. Mwenye kanzu mbili ampe moja asiye nayo na mwenye chakula ampe mwenye njaa, ni jibu lake Yohana Mbatizaji kwa makutano na pia ni muhutasari wa maisha ya upendo kwa kila mwenye uhitaji anayefika mbele yetu. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema, hakuna mtu maskini hivi kiasi cha kusema hana kitu cha kutoa na vile hakuna mtu tajiri kiasi kwamba hana uhitaji wa kitu cha kupokea. Kwa maneno marahisi kila mmoja wetu ana utajiri wake na kila mmoja wetu ana umaskini wake. Hivyo kila mmoja wetu anaalikwa kutoa na kupokea. Na kwa kuishi ukweli huu tunaweza kuifikia furaha ya kweli, kuna furaha katika kupenda! Noeli ni moja ya sherehe ambayo inajitanabaisha na utamaduni wa kupeana zawadi, ni Mungu Baba kwa nafasi ya kwanza anayemtoa Mwanae wa pekee kuwa zawadi kwa ulimwengu mzima, lakini nasi tunaalikwa kwa maisha yetu kuwa zawadi kwa wengine wanaotuzunguka. Maisha ya kila Mbatizwa hayana budi kuwa zawadi kwa wale anaokutana nao, maisha ya Mkristo yanapaswa kuwa baraka katika ulimwengu wetu.

Kundi la pili ni watoza ushuru, hawa ni kundi ambalo kwa bahati mbaya, siyo tu kati ya Wanawaisraeli bali katika jamii nyingi duniani ni watu wanaochukiwa. Na wanachukiwa sio kwa sababu tu wanakusanya ushuru ila pia wamekuwa na sifa mbaya ya kutokuwa na haki katika kazi yao. Hata katika Taifa letu tuna kelele nyingi kuhusiana na kodi na tozo mbali mbali, kwani mara nyingi haziakisi haki na uhalisia wa maisha ya kawaida ya mwananchi. Nao pia wanaona haja na wajibu wa kwenda mbele ya Yohane Mbatizaji na kumuhoji nini wafanye. Watoza ushuru nao wanaona kuna kitu kinapungua katika maisha yao. Yohane Mbatizaji hawaambii hawa waachane na kazi yao ya kukusanya ushuri au kodi na tozo, ila badala yake watende haki, watoze iliyo haki na si kuwanyonya au kuwakandamizi watu. Na ndio mwaliko wa Yohane Mbatizaji kwetu sote kila mmoja katika sehemu yake ya kazi kuwa wajumbe wa haki, kuwa watenda haki na kuacha kukandamiza au kuwaumiza walio wanyonge. Kila mmoja wetu anaalikwa kuwa mtu wa haki, iwe katika familia, kwenye jumuiya zetu mbali mbali na popote pale.

Kundi la mwisho, ndilo la maaskari nao wanamuuliza Yohane Mbatizaji wafanye nini. Yohane Mbatizaji hawaambii nao waache kazi yao au wabadili shughuli ya kufanya, ila kinyume chake anawaalika kutokuonea watu na watosheke na ujira wao. Maaskari wa nyakati zile walikuwa wanalipwa ujira mdogo labda karibu sawa tu na wa nyakati zetu katika nchi yetu. Na hivi walikuwa katika kishawishi kikubwa cha kuonea watu ili wapate rushwa. Ni mara ngapi hata katika Taifa letu tunaona maaskari wakionea wananchi wasio na hatia, kelele za kubambikizia watu kesi na mashitaka ya uongo ya kupikwa tu, au wale rafiki zetu wa usalama barabarani, tuna mengi tunaweza kusema juu yao ila mwaliko wa Yohane  Mbatizaji ni ule ule kuwa watu wa haki kwa jirani. Na huu ni mwaliko kwetu sote kila mmoja katika sehemu yake ya kazi. Tendeni na iweni watu wa haki, toshekeni na mishahara yenu! Tunaweza kuorodhesha kila aina ya kazi au shughuli au aina ya maisha ya kila mmoja wetu. Na kila mmoja wetu aingie katika maisha yake na kujihoji nini napaswa kufanya ili kujiandaa vema na ujio wa Mwokozi Yesu anayeleta furaha ya kweli. Furaha ya kweli inapatikana tu kwa kuwa watu huru maana yake kuenenda kama wana wa Mungu, kuishi kitakatifu na ndio kumpenda Mungu na jirani, kuishi kwa kuongozwa na kweli za Injili.

Kila mmoja wetu kuna kitu cha kufanyia kazi katika maisha yake, kwani tukijiangalia ndani tunagundua kuna mahali hapako sawa na hivyo panatudai kubadilishwa. Kila mmoja wetu ndani mwake ana mabonde ya kujazwa na vilima vya kushushwa, ndio kusema kila mmoja wetu anaalikwa kufanyia kazi maisha yake ili yaweze kuendana na Injili yake Bwana wetu Yesu Kristo. Kila mmoja wetu kadiri ya Injili ya leo, tuna nafasi kama makutano, watoza ushuru na askari katika nafasi mbalimbali za maisha yetu ya siku kwa siku. Kuna kishawishi kudhani mimi sio mtoza ushuru au askari au labda wale makutano, lakini kiukweli sisi pia tu makutano, watoza ushuru na maaskari, tujihoji vema na tukubali kufanya mageuzi ya kiroho kwa kubadili maisha yetu. Ni wito wa kuingia ndani kabisa ya mioyo yetu tunapojiandaa kusherehekea sikukuu za Noeli, ili tuweze kubadili maisha yetu na kuwa tayari daima kwa ujio wake Bwana na Mkombozi wetu Yesu Kristo.

Sehemu ya pili ya Injili ya leo tunaona Yohane Mbatizaji anarudia kutumia lugha kali na ya vitisho hasa kwa wadhambi wasiokuwa tayari kufanya toba. Yafaa kujuliza nini maana yake maneno haya.  Tunapoangalia aya ile ya 18, tunaona kwa maneno haya Yohane aliwahubiri watu Habari Njema. Neno la kigiriki linalotumika ni παρακαλεω (Parakaleo) maana yake maneno ya faraja, na ndio Mwinjili Luka ujumbe huu ni Habari Njema (ευγγελιον), ni Habari ya matumaini. Ni Habari Njema kwani ujio wa Masiha ulimwenguni ni kutuokoa, kutufanya kuwa wana wa Mungu na rafiki zake Mungu na si kutuangamiza, na mabadiliko yanayolengwa ni kutualika kuishi maisha mapya na maisha ya kweli na yenye kuleta furaha ya kweli. Yohane Mbatizaji anawaandaa kwa Ubatizo wa kweli wa Roho na moto, Ubatizo wa Yesu Kristo, ni Ubatizo unaotufanya kuwa wana wa Mungu, warithi pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo. Ubatizo wa Yohane Mbatizaji ulikuwa ni mwaliko wa watu kubadili namna zao za maisha, ni Ubatizo wa maji kama ishara ya kuoshwa na kutakaswa kwao kwa nje, ni sawa na mtu anayeenda mtoni au baharini kuoga kwa kuosha mwili wake, bali kwa Ubatizo wa Yesu Kristo tunafanyika viumbe wapya kwa njia ya Roho Mtakatifu, ni kubadilika kwa hadhi yetu. 

Na ndio Ubatizo katika moto, yaani ujio wa Roho Mtakatifu kwa kila mbatizwa, ni kufanyika watu wapya kwa nguvu za huyo Roho wa Mungu. Ni kuingia katika mahusiano mapya na Muumba wetu, kuwa wana wake Mungu. Ni kwa ujio wa Roho wa Mungu ndani mwetu tunasamehewa dhambi zetu na kutakatifuzwa, na hivyo kushiriki maisha ya Mungu mwenyewe, ndio maisha ya neema na utakatifu. Wapendwa Majilio ni kipindi cha neema, ni Kairos, ndio wakati wa Mungu uliokubalika, ni wakati mzuri wa kubadili vichwa na maisha yetu ili tuenende maisha ya wana wa Mungu kwa kuishika ile amri ya mapendo kwa Mungu na kwa jirani. Tunaweza kufanya mambo mengi mema na mazuri lakini tuongozwe daima na Upendo kwa Mungu na kwa jirani. Nawatakia Maandalizi mema ya Sherehe ya Noeli na Dominika njema yenye furaha ya kweli.

09 December 2021, 16:57