Tafuta

Mama Kanisa tarehe Mosi Januari ya kila mwaka anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria sanjari na Siku ya Kuombea Amani Duniani Mama Kanisa tarehe Mosi Januari ya kila mwaka anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria sanjari na Siku ya Kuombea Amani Duniani 

Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Theotokos, Januari Mosi!

Bikira Maria ni Mama kweli wa Yesu, kwa kuwa hali ya ubinadamu wa Yesu ilichangiwa na Bikira Maria kwa ukamilifu wote. Pili, Bikira Maria ni kweli Mama wa Mungu, kwa kuwa alichukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na kuzaa nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Aliyezaliwa kwa Baba, tangu milele yote.. Ni Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga...!Imani!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu katika maadhimisho ya kilitrujia, siku ya tarehe moja ya mwaka mpya. Dhamira kuu ya kilitrujia ni kuadhimisha na kusherehekea sikukuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Lakini pia, Januari Mosi, ni siku ya nane katika Oktava ya Noeli, hivyo ni siku ya kutahiriwa na kupewa jina kwa mtoto Yesu – kufuatana na mapokeo ya sheria ya Musa ya kutahiriwa mtoto wa kiume na kupewa jina siku ya nane baada ya kuzaliwa kwake. Zaidi ya hayo, Januari 1 ni siku ya kuombea “Amani” duniani. Januari Mosi, ni siku ya kuuaga mwaka ulioisha na kuukaribisha mwaka mpya. Ni siku ya kufanya tathimini ya maisha yetu -kiroho, kimwili, kifamilia, kijamii na kimahusiano na kuweka mipango mikakati kwa mwaka unaoanza. Januari Mosi, pia ni siku shukrani kwa Mungu kwa mema aliyotujalia mwaka uliopita.

Siku ya kwanza ya mwaka mpya ni siku ya kumsherehekea Bikira Maria Mama wa Mungu na kujiweka chini ya ulinzi wake kwa mwaka mpya unaoanza. Itakumbukwa kwa dhambi ya asili – dhambi ya Adamu na Eva, mwanadamu alipoteza urafiki na Mungu na kujitenga naye (Mwanzo 3:23). Mungu kwa upendo na huruma yake kwa njia na namna mbalimbali, alianza taratibu kutufunulia mpango wake wa kumuumba upya mwanadamu. Kuzaliwa kwa Bikira Maria bila dhambi ya asili ulikuwa mpango wa Mungu katika harakati za kumkomboa mwanadamu (Isa. 7:14, 9). Kwa fumbo la umwilisho Bikira Maria amekuwa mama wa Mungu kwa kumzaa mwana wa Mungu – anasisitiza Mtume Paulo “Mungu alimtuma Mwanaye ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao walikuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana” (Gal 4:4-5)”.

Ukweli huu sio mgumu kuuelewa hata kama ni fumbo la kiimani. Katika lugha ya kawaida tunasema mama ya padre au sista, rais au mbunge, haimaanishi kuwa aliuzaa upadre, usista, uraisi au ubunge isipokuwa, mtoto wake wa kuzaa ana hadhi ya upadre au ubunge. Kwa hiyo Bikira Maria alimzaa Kristo Yesu ambaye ni Mungu kweli na mtu kweli ni Mama ya Mungu – “Theotokos” kwa lugha ya kigiriki kama mtaguso wa Efeso ulivyoweka wazi: Bikira Maria ni Mama kweli wa Yesu, kwa kuwa hali ya ubinadamu wa Yesu ilichangiwa na Mama Bikira Maria kwa ukamilifu wote. Pili, Bikira Maria ni kweli Mama wa Mungu, kwa kuwa alichukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na kuzaa nafsi ya Pili ya Mungu – Mungu Mwana, Mkombozi wetu Yesu Kristo kama tunavyosali katika Kanuni ya Imani; “Nasadiki kwa Bwana Mmoja Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba, tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli.”  

Sisi nasi kwa ubatizo tumefanywa watoto wa Mungu (1Yoh 3:1). Sisi ni ndugu zake Kristo naye haoni “aibu kutuita sisi ndugu zake” (Heb 2:11), washiriki wa uzima wa Mungu na furaha yake mbinguni (Gal 4:7). Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, tutashiriki pamoja na Kristo kile ambacho Mungu amemtayarishia (Rom 8:17). Kumbe Bikira Maria ni mama yetu. Tujiweke chini ya ulinzi wa Mama Bikira Maria kwani akiwa chini ya msalaba Yesu alitukabidhi kwake akisema - “Mama tazama huyu ndiye mwanao” (Lk 22:40). Siku ya kwanza ya mwaka mpya ni siku ya shukrani. Ni siku ya kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kumaliza mwaka salama na kuanza tena mwaka mpya. Kimwili ametutendea mengi: ametupatia chakula, mavazi na malazi, ametujalia uzima, afya njema na nguvu ya kufanya kazi. Kiroho: ametusamehe dhambi na makossa yetu pale tulipoungama, tukapokelewa katika pendo lake. Hivyo hatuna budi kumshukuru kwa sala, nyimbo na tenzi za rohoni. Kama wanavyosema wahenga, kushukuru ni kuomba tena. Tunampomshukuru Mungu kwa mema aliyotulia, tunamuomba neema za kuuishi vyema mwaka mpya uanoanza. Ni siku pia ya kuomba msamaha na kufanya toba kwa yote mabaya tuliyoyatenda mwaka jana. Zaidi sana ni siku ya kuweka nia thabiti ya kutorudia matapishi ya dhambi na kuzikufuru sakramenti.

Siku ya kwanza ya mwaka mpya ni Siku ya kutakiana heri na kuomba neema na baraka. Somo la kwanza kutoka Kitabu cha Hesabu (Hes. 6:22-27), ni sala ya baraka kuu ya Mungu kuwabariki wana wa Israeli kupitia mkono wa Aaroni na wanawe makuhani kwa kulitamka jina la Bwana mara tatu na kuwabariki watu kwa maombi mawili; “Bwana akubariki na kukulinda, Bwana akuangazie nuru za uso wake na kukufadhili; Bwana akuinulie uso wake na kukupa amani.” Katika siku hii ya kwanza ya mwaka mpya, Mama Kanisa katika liturujia amewaka utaratibu kwa makuhani – mapadre -  kutoa “Baraka kuu” na kuwabariki waamini kwa kutumia maneno ambayo Mungu aliagizi yatumike kuwabariki watu. Baraka hii inawapa waamini ulinzi dhidi ya balaa, majanga, magonjwa na hatari nyingine kwa mwaka mzima. Baraka hii iwape waamini nguvu ya kukabiliana na matatizo na magumu katika maisha ili wasikate tamaa. Kama ilivyokuwa katika kanuni ya baraka kwa waisraeli, Mungu anaahidi kuwaangazia nuru ya uso wake wale wote wanaopokea baraka zake kwa moyo wa shukrani.

Siku ya kwanza ya mwaka mpya ni siku ya kuombea Amani Duniani. Amani ni zawadi ya Kristo kwa ulimwengu; alijifanya mwanadamu kurudisha amani tuliyoipoteza kwa dhambi. Mtoto Yesu ni mfalme wa amani - Mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto na jina alilopewa ni mfalme wa amani (Is 9:6). Yesu alipozaliwa malaika waliimba; Amani kwa watu {anaowaridhia}anaowapenda Mungu (Lk 2:14). Ufalme wa Mungu siyo swala la kula na kunywa bali ni swala la utakatifu, amani na furaha ambayo ni roho tu anayeitoa (Rom 14:17). Maneno ya Yesu baada ya kufufuka kila alipowatokea wanafunanzi wake daima yalikuwa “Amani iwe kwenu”! (Yoh 20:19-26). Na mwishoni mwa maisha yake hapa duniani alisema; “Amani nawaachia, amani yangu nawapa” (Yoh 14:27). Kumbe amani ni gharama ya mateso ya Yesu; “Adhabu aliyoipata ilituletea amani” (Is 53:5). Basi nasi tuwe na umoja, tuishi kwa amani na Mungu wa upendo na amani atakuwa nasi (2Kor 13:11). Tunaalikwa tuwe wajumbe wa amani popote pale tunapokuwa na kuishi. Daima tupambane na maadui wa amani. Tuwe na amani kati yetu na Mungu: Tupatanishwe na Mungu, tukimpenda na kuzishika amri zake. Tuwe na amani kati yetu na jirani zetu huku tukitendeana mema. Tuwe na amani kati ya mtu na nafsi yake mwenyewe kwani bila amani mioyoni mwetu hapatakuwa na amani ya nje. Tuwe na amani na viumbe vyote na mazingira kwa kuyatunza ili yatutunze.

Katika somo la pili la Waraka wake kwa Wagalatia (Gal 4:4-7), Mtume Paulo anasema; Baada ya Mungu kumtuma Mwanae, “Aliyezaliwa na Mwanamke”, - akawa mmoja kati yetu kwa kila kitu isipokuwa dhambi ili kutupatanisha na baba na kutufanya kuwa wanawe kwa kutujalia amani. Kumbe amani ya kweli ni ile inayotokana na msamaha. Wale waliosamehewa dhambi wana amani na ni kweli watoto wa Mungu na hivyo tunaweza kumwita Mungu “Abba, Baba”. Hivyo hatuko tena watumwa bali ni “wana” na tunaweza kumwita Mungu “BABA”. Basi ikiwa tu watoto wa Mungu, ikiwa tumempokea Roho Mtakatifu wa Mungu, sisi ni ndugu – kaka na dada, ni wana na warithi wa uzima pamoja na Kristo, tu Hekalu la Mungu kwa njia ya Roho Mtakafu. Katika siku ya kwanza ya mwaka mpya, Januari Mosi, tunakumbuka kutahiriwa na kupewa jina kwa Yesu. Tufahamu kuwa japokuwa tumetakaswa kwa njia ya ubatizo, baado tunamwelekeo asili wa kuvutwa na dhambi.

Hivyo tunapaswa kuendelea kuifanyia tohara mioyo yetu - kuondoa utu wa kale wa dhambi na kumvaa Kristo kama anavyosisitiza Mtume Paulo - tutahiri mioyo yetu, kwa kushiriki mafumbo matakatifu na kukua katika fadhira za kikristo havyo hatutaweza kufuga chuki, ugomvi, hasira, na kuwanyanyasa wengine wala kulipa kisasi kwa waliotukosea. Tutaaminiana, tutapendana, tutasaidiana katika shida, ttabu na raha na tutaishi kwa amani. Basi, siku hii ya kwanza katika mwaka tujiweke chini ya ulinzi wa Bikira Maria Mama wa Mungu. Tumkimbilie daima katika shida ili atuombee kwa mwanae. Naye atatuambia; “Lolote atakalowaambieni, fanyeni” (Yn 2:5). Nasi tukifanya atakayotuambia Yesu, daima tutaona mafanikio katika maisha yetu mwaka mzima.

B. Maria Mama wa Mungu
29 December 2021, 14:42