Sherehe ya Familia Takatifu: Maadui Wakuu wa Familia Ulimwenguni
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
UTANGULIZI: Dominika ndani ya oktava ya Noeli, Kanisa huadhimisha sherehe ya Familia Takatifu. Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu inawekwa kwetu kama kioo na kielelezo cha familia zetu ili kwa mfano wake, kwa maombezi yake na kwa neema zake sisi nasi tuweze kuufikia utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha katika familia zetu. MASOMO KWA UFUPI: Somo la kwanza linatoka kitabu cha nabii Samweli (1 Sam 1,20-22. 24-28). Somo hili linakuja kutukumbusha kwa mara nyingine tena kuwa watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu. Njia ambayo Biblia inatumia kutuonesha kuwa mtoto anakuja katika familia kama zawadi ni kutupa masimulizi ya akina mama wema machoni pa Mungu lakini wakiwa tasa na hawana watoto katika ndoa zao. Ndivyo inavyokuwa kwa Hana mama wa Samweli. Mtoto Samweli anapatikana kama tunda la sala ya muda mrefu sana ambayo mama yake alisali akimwomba Mungu. Anachokifanya Hana baada ya kupata mtoto ni kuwa anapofikisha umri wa kuachishwa maziwa anampeleka hekaluni na kumtolea kwa Bwana.
Ili kusisitiza ujumbe huu kuwa watoto ni zawati kutoka kwa Mungu, Kanisa linazielekea tena leo familia na ndoa ambazo zinapitia hali kama ya Hana, mama wa Samweli na akina mama wengine watakatifu wanaotajwa katika Biblia wakiwa hawana mtoto. Familia ambayo haijapata zawadi hii si familia iliyo na mapungufu wala si familia nusu. Ni familia kamili na tena inazidi kuitwa kumwamini Mungu na kuendelea kujiweka chini ya mapenzi yake. Kwa wazazi, mwaliko ni kulitambua fumbo kuu la Mungu lililo ndani ya watoto. Watot kama zawadi ya Mungu, wanabeba ndani yao fumbo kubwa ambalo ni Mungu mwenyewe analijua. Ni muhimu kumbe kwa wazazi kujitahidi kwanza kabisa kuwapokea watoto na kisha kuwalea kadiri ya mpango wa Mungu ili kuzidi kuikuza na kuifunua zawadi hii kwa manufaa ya familia na jamii yote ya watu wa Mungu.
Somo la pili kutoka katika Waraka wa kwanza wa Yohane kwa watu wote (1 Yoh 3, 1-2. 21-24) na somo la Injili kama ilivyoandikwa na Luka (Lk. 2, 41-52) yote yanatupatia fundisho moja. Fundisho hilo ni kuwa sisi sote tuna familia zetu, familia tulimozaliwa lakini pia tuna familia nyingine kubwa zaidi ambayo ni familia ya Mungu. Na sote ni wanafamilia wa familia hiyo. Sisi sote tu waana wa Mungu. Kwa kwa njia ya ubatizo tunafananishwa na Kristo mwanae wa pekee na hivyo tunafanywa kuwa warithi wa ufalme wa Mungu sawa na Kristo mwenyewe. Kwa jinsi hiyo, kama tulivyo na wajibu kwa familia zetu za hapa duniani, tunao pia wajibu kwa familia kubwa ya Mungu. Tena kama tulivyozoea kusema kuwa ‘damu ni nzito kuliko maji’, kuonesha uthabiti wa muunganiko wetu wa undugu wa damu injili ya leo inatualika tupige hatua zaidi na tuone kuwa ‘maji ya ubatizo ni mazito kuliko damu’. Kwa sababu hii Yesu mwenyewe analazimika kuacha familia yake iendelee na safari ya kurudi nyumbani ilhali yeye akibaki hekaluni kuyatimiza mapenzi ya Baba yake aliye mbinguni.
TAFAKARI YA JUMAPILI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican news, sherehe ya leo Familia Takatifu inatukumbusha umuhimu wa familia katika sisi kuishi vema hapa duniani na katika kuufikia utakatifu huko mbinguni. Huu ni umuhimu ambao Mungu mwenyewe ameuweka katika familia. Ndiyo maana mambo ambayo mtu anayapitia katika makuzi yake ndani ya familia yanaambatana naye katika karibu maisha yake yote; yawe ni mambo mema au mapungufu. Katika kumleta Kristo duniani, Mungu hakutaka Kristo aje kama shujaa anayetokea hewani kuja kumkomboa mwanadamu. Alimfanya azaliwe katika familia. Na tena hakuchagua familia isiyo na changamoto. Alichagua hiyo hiyo iliyo na changamoto ili kutuonesha namna ya kuzikabili kwa umoja, upendo na uvumilivu changoto katika familia zetu na kupitia changamoto hizo tuzidi kujifunza maisha ya fadhila na kutegemeana na kutegemezana.
Katika kuuenzi umuhimu wa familia katika maisha mazima ya mwanadamu, kuna umuhimu pia wa kuilinda dhidi ya maadui wake. Ndiyo maana nawaalika katika tafakari hii tuwaaangalie maadui wanaoishambulia familia leo. Tutawataja wawili. Adui wa kwanza tunaweza kumwita siasa mamboleo, au ukoloni wa kiitikadi. Katika miaka ya hivi karibuni, kote ulimwenguni kumekuwa na mwamko mkubwa wa kisiasa. Hii imepelekea siasa kuzidi kujipenyeza katika nyanja mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Hata pale ambapo awali paliachwa kwa ajili ya utashi binafsi wa dhamiri au imani kwa Mungu. Na kadiri ya muundo wake, viongozi na watawala wa kisiasa wamekuwa na sauti na hata maamuzi juu ya mambo hayo. Sasa katika uhai wa familia hii ni hatari sana na huu ndio ukoloni wa kiitikadi. Na ni hatari kwa sababu nafasi ya maamuzi binafsi kadiri ya utashi wa dhamiri au dini vinawekwa pembeni na badala yake linakuwa ni swala la kuamuriwa kwa kura. Na likishafikia hapo basi kuashiria pia uwepo wa upigaji wa kampeni na kutafuta ushawishi na matokeo yake ni kupata ushindi badala ya kuufikia ukweli. Kwa njia hii, siasa imepitisha mambo mengi ambayo ndani yake yanalenga kuuangamiza kabisa muhimili wa familia.
Adui wa pili ni utamaduni wa kuabudu uhuru kupita kiasi. Jambo jema kabisa na la msingi katika kulinda utu wa mwanadamu ni kulinda uhuru wake na haki zake. Dunia ya sasa imegeuza jambo hili kuwa ni nyenzo ya kuhalalisha hata yale yasiyo halali. Na madhara yake yanalipwa na familia. Hii ni kwa sababu nyuma ya pazia la uhuru na haki za binadamu wamejificha maadui wake. Hawa ni wale wanaowasukuma watu, kwa kivuli cha uhuru na haki za binadamu, kusambaza utamaduni wa kifo badala ya uhai: utoaji mimba, eutanasia, talaka, ndoa za jinsia moja n.k vyote hivyo vinasukumwa na uhuru na haki za binadamu. Uhuru badala ya kumsaidia mwanadamu kumuabudu na kumcha Mungu sasa wenyewe ndio unawekwa mbele ili uabudiwe. Na kwa kweli uhuru unaosambaza utamaduni wa kifo badala ya uhai si uhuru na haki isiyotetea uhai wa mwanadamu sio haki bali ni utumwa, tena ule utumwa mbaya zaidi. Madhara ya haya yote, kama tulivyokwisha sema hapo awali, yanalipwa na familia kwa maaana utamaduni wa kifo eneo lake la kwanza kushambulia ni familia.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tafakari hii itusaidie kuamka. Tumrudie Mwenyezi Mungu na tuwe na hofu naye. Thamani ile ambayo Mungu mwenyewe ameipa familia isichokonelewe. Tuiangalie Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu na tupate ndani yake matumaini ya kujitahidi kuwashidna maadui wa familia ili familia zetu ziendelee kuutunza utakatifu. Zituwezeshe kuishi vema hapa duniani ili tuweze kufika mbinguni.