Sherehe ya Familia Takatifu: Familia Msingi Wa Malezi na Utu!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, katika sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Utaratibu wa kuwataja wanafamilia hii ni kinyume kabisa na mazoea yetu ambapo kawaida tunatamka majina tukianzia - Baba, mama na watoto. Kwa hii familia tunaanza na jina la mtoto, mama na baba - Yesu, Maria na Yosefu. Hii ni kwa sababu; Yesu ni Mungu katika nafsi ya pili - Mungu-mwana, lazima apewe nafasi ya kwanza. Maria ni mama wa Mungu ambaye kwake Mungu katika nafsi ya pili - Mungu-Mwana alichukua mwili katika fumbo la umwilisho akawa mwanadamu akakaa nasi. Hivyo Bikira Maria kwa upendeleo huu wa kumzaa mwana wa Mungu, anachukua nafasi ya pili. Yosefu ni baba mlishi wa Yesu, kwa hiyo anachukua hiyo nafasi ya tatu. Itakumbukwa kuwa kiini na mwanzo wa sherehe hii ni kunako mwaka 1921 ambapo Baba Mtakatifu Benedikto XV, alitangaza kuwa jumapili katika oktava ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, au tarehe 30 desemba itakuwa ni sherehe ya Familia Takatifu. Katika sherehe ya Kristo Mfalme mwaka 1981, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika barua ya kitume “Familiaris consortio” akieleza wajibu wa familia ya Kikristo kwa Kanisa na ulimwengu - akisisitiza umuhimu wa familia katika malezi ya watoto na ujenzi wa Kanisa na taifa anasema; Familia ni kitalu cha kanisa na jamii kwa ujumla. Ili jamii na Kanisa lifanikiwe ni lazima kuwe na msingi mzuri katika familia ambayo ndio inaathiri tabia, mwenendo na maisha ya wanajamii. Hivyo basi; Familia ni Kanisa la nyumbani. Familia ni shule ya sala. Familia ni shule ya upendo. Familia ni shule ya amani na mshikamano. Familia ni makao ya furaha na kitalu cha uhai.
Familia Takatifu ni ile ya kumpendeza Bwana, ni familia inayodumu katika pendo la Mungu, imejaa amani tele na baraka za mwenyezi Mungu. Familia ya Yesu, Maria na Yosefu inawekwa mbele yetu kuwa mfano wa familia zetu ambao kwao unatuonyesha namna zinavyoweza kuiishi vyema furaha ya upendo katika familia na tiba kwa zile zilizojeruhika kwa kukosa upendo kama anavyosisitiza Papa Francisko katika Amoris laetitia. Ndiyo maana, katika hitimisho la barua yake, Mtakatifu Yohani Paulo II aliziweka familia zote chini ya ulinzi na usimamizi wa Yesu, Maria na Yosefu. Lengo kuu la kuadhimisha sherehe hii ni kuziombea familia zote zikue na kuishi kwa mshikamano zikimpendeza Mungu, zikidumu katika pendo lake, ziweze kujaa amani tele na baraka za mwenyezi Mungu ziwe ndani mwao daima, zaidi sana kujifunza na kuiga mfano bora wa hii familia kama tunavyoomba katika sala ya mwanzo; Ee Mungu, umependa kutuonyesha mifano bora ya Familia Takatifu. Utujulie kwa wema tuweze kufuata mifano ya hiyo Familia Takatifu katika fadhila za nyumbani na kuungana kwa mapendo. Tunaomba fadhila ya upendo ambayo ni kiini cha furaha ya familia kama maneno ya mwanzo katika barua ya kichungaji ya Papa Francisko juu ya maisha ya familia yanavyoashiria; “Amoris letitia” furaha ya upendo. Kwamba katika magumu yote; upendo unaleta furaha.
Tunapoongelea familia hapa ni vyema tukafahamu maana halisi kadiri ya mpango wa Mungu kuwa; Familia ni muungano wa Mume na mke, unaofungamishwa na upendo na tunda litokanalo na Upendo wao ni watoto ambao ni zawadi toka kwa Mungu na ndiyo inayowafanya waitwe wazazi; Baba na mama. Familia ni mpango wa Mungu (Mw. 1:26-28; 2:24). Tangu mwanzo aliwaumba mume na mke, Adamu na Eva akawashirikisha uwezo wake wa uumbaji ili tunu ya uhai iendelee kuwepo duniani. Kumbe familia ni wito wa kuishi pamoja kwa wanandoa, kuendeleza kazi ya uumbaji na kuwezesha mwendelezo wa tunu ya uhai kwa kuzaa watoto, kuwalea na kuwaridhisha tunu zilizo njema. Familia ni kitovu cha uumbaji, shule ya kutambua mapenzi ya Mungu. Katika familia Injili inapaswa kusomwa na kutafakariwa, liturujia inapata msingi kwa njia ya sala, nyimbo na sakramenti. Masomo ambayo mama kanisa anatupatia katika sherehe hii yanatuongoza kutambua umuhimu wa siku hii katika maisha ya familia na ndoa. Somo la kwanza kutoka kwa Yoshua Bin Sira (YbS 3:2-6, 12-14), linasema “Bwana amempa baba utukufu mintarafu wana na kuithibitisha haki ya mama mintarafu watoto.” Familia ya Kikristo inatakiwa ijengwe kwa mahusiano mazuri kati ya wanafamilia yaani wazazi na watoto wawe na wajibu na ari ya kudumisha amani na mapendo wakistawisha tunu za kikristo, kimaaadili na kiutamaduni. Familia ya Nazareti ni mfano mzuri wa kuigwa.
Katika Somo la pili la Waraka wake kwa Wakolosai (Kol 3:12-21), Mtume Paulo anatuasa kwamba kwa kuwa tumekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, tujivike moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, tukichukuliana na kusameheana zaidi ya hayo yote tujivike upendo ndio kifungo cha ukamilifu. Hizi ndizo zilikuwa tunu za familia takatifu. Familia ni mahala pa msingi pa kuujenga utu wa mtu kwa ajili ya kanisa na jamii na hivi ndio chanzo au chimbuko la “Uhai na Mapendo." Katika Injili ya Luka (Lk 2:22-40) tunasoma hivi; “Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii - na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea kukua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu”. Injili hii inatukumbusha wajibu wa wazazi katika kuwafundisha na kuwarithisha watoto mila na tamaduni zilizo njema na zaidi sana imani na upendo kwa Mungu na mwanadamu. Sherehe ya Familia Takatifu ni siku ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya familia zetu: wazazi, walezi, watoto na ndugu na jamaa aliotujalia katika familia zetu. Familia imeundwa na ina msingi wake katika Mungu. Kwanza katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na pia katika kuwaumba Adamu na Eva na kuwaweka katika familia (Mwa.1:27). Ili kuonyesha umuhimu wa familia katika maisha ya binadamu Kristo amekuja na kuishi katika familia ya Nazareti ya Yesu, Maria na Yosefu. Tunamshukuru Mungu kwa kutupatia familia hii ya Nazareti ambayo ni mfano wa kuigwa na familia zetu katika raha na shida.
Sherehe ya familia takatifu ni siku ya kuwashukuru na kuwapongeza wazazi na Walezi: usione vyaelea, vyaundwa. Kila binadamu ametoka katika familia na kwa namna moja au nyingine tumekuwa tulivyo kwa msaada wa familia zetu au za wengine. Hivyo hatuna budi kuwakumbuka wazazi watu na kuwashukuru. Lakini zaidi sana kuwaombea walio wazee Mungu awaimarishe katika uzee wao na pia sisi tuwasaidie katika uzee wao ili tujipatie neema na baraka mbele za Mungu. Kwa wale waliotutangulia mbele za haki tuwaombee ili Mungu awapokee katika uzima wa milele. Sherehe ya familia takatifu ni siku ya kumshukuru mwenzi wako wa ndoa: Mkumbuke mme wako, mkumbuke mke wako na kumshukuru kwa upendo anaokuonyesha, kwa kukuvumilia na kukusamehe ulipomkosea. Tunawapongeza walioweza kuishi vizuri katika ndoa. Maisha ya ndoa si mchezo yanahitaji uvumilivu. Tuwaombea walio katika ndoa neema na baraka za Mungu wazidi kufurahia upendo wa ndoa katika maisha yao.
Sherehe ya familia takatifu ni siku ya kuwashukuru na kuwapongeza watoto: watoto wanayo nafasi kubwa sana katika ustawi wa familia. Watoto ni kiungo kikubwa sana cha baba na mama na ni sababu ya furaha katika familia. Hivyo, wanafamilia mshukuruni Mungu kwa zawadi ya watoto aliowajalia kwa kuwalea vyema na kuwaridhisha tunu zilizo njema. Muwaombee na kuwakinga dhidi ya yule mwovu ili wapate mafanikio katika maisha yao. Kama ilivyokuwa kwa Yesu kuna Maherode wengi wanaotafuta kuwauwa watoto wetu: vyombo vya mawasiliano, mitazamo potofu ya maisha hasa kuhusu ujinsia, madawa ya kulevya na pombe. Kama Yosefu na Maria lazima tuwakinge watoto wetu na maadui hawa. Mfuatilie mtoto na kumwelekeza usimwache akatangatanga kama kondoo wasio na mchungaji – anasisitiza Yoshua Bin Sira (Sira 30: 1-3; 7-13). Jihadhari sana na kuwapatia uhuru unaopita kiasi. Wafundisheni watoto wenu kutambua mema na mabaya. Waelekezeni kusema ndiyo kwa mema na hapana kwa mabaya. Wafundisheni watoto wenu kusema inatosha.
Ni kweli kuna changamoto nyingi katika familia - kukosa upendo, kukosa uaminifu, magonjwa, kukosa watoto, vyombo vya mawasiliano, usasa na mambo yake. Yote haya huleta matatizo katika familia ikiwa ni pamoja na kuvunjika na kusambaratika kwa familia, watoto kukosa upendo wa wazazi, kuongezeka kwa watoto wa mitaani, umaskini unaongezeka, vijana wanaogopa kuingia katika maisha ya ndoa, familia za mzazi mmoja. Ili kuepekana na haya kwa ambao bado hawajaingia katika maisha ya ndoa na familia ni vyema kufanya maandalizi ya kina ya kabla ya ndoa ikiwa ni pamoja na kumwomba Mungu Roho Mtakatifu akupe mchumba mwema. Kwa walio ndani ya ndoa, ziheshimuni ndoa zenu mkijua kabisa ni tunu bora mno aliyowajalia mwenyezi Mungu, ishini kwa upendo. Jivikeni rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, uaminifu na roho ya kujisadaka, kutoa maisha yako kwa ajili ya familia, kuyasadaka mawazo yako, vionjo vyako, matamanio yako, haki zako, majukumu yako na mengine kwa ajili ya familia, kuweza kusema inatosha. Uwe na muda na wanafamilia na mwenzako wa ndoa.
Wanandoa, ishini kwa ushirikiano. Kila mtu atimize majukumu yake katika familia. Jihadharini sana na itikadi za kikoloni zinazokuja siku hizi kuhusu “uhuru na ukombozi wa mwanamke.” Kila mmoja anastahili heshima, haki na kuthaminiwa. Lakini mwanamke asitafute kuwa mwanamme na mwanamme asitafute kuwa mwanamke. Ujinsia huu si muundo wa binadamu ni wa asili na unaendana na ubaiolojia na maumbile ya kila mmoja kadiri ya mpango wa Mungu aliyetuumba. Kutoelewa ujinsia huu umesababisha kuibuka ndoa za jinsia moja ambazo zinaharibu maana na tunu ya familia zetu. Zaidi sana tuzifanye nyumba zetu na familia zetu kuwa nyumba za sala. Tumwombe Mungu azibariki familia zetu ziwe mahali pema pa kuishi, chimbuko la Kanisa na chimbuko la Taifa lenye ustawi.