Familia Takatifu Ya Yesu, Maria na Yosefu Wajibu wa Familia: Malezi
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na salama! Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, daima inabaki kuwa mfano bora wa kila familia ya Kikristo. Tunaposoma Injili ya Sherehe ya Familia Takatifu tunabaki na maswali mengi juu ya familia hii na hivyo kujiuliza ujumbe hasa wa Mwinjili Luka ni upi katika Sherehe za Familia Takatifu. Inawezekanaje Maria na Yosefu wanasafiri umbali wa siku moja bila kujali uwepo wa mtoto wao aliyekuwa na umri wa takribani miaka kumi na miwili tu. Na hata wanapomkuta hekaluni baada ya kumtafuta kwa siku tatu, tunaona majibu ya Yesu kwa wazazi wake siyo yenye kuonesha uadilifu, staha na heshima ya mtoto kwa wazazi wake. Hivyo iwe kwa upande wa wazazi au ule wa mtoto Yesu tunabaki na mshangao zaidi kuliko kuwa na majibu. Yesu anabaki Yerusalemu bila kuomba ruhusa au kuwajuza wazazi wake. Baada ya kurejea Nazareti tunaona Yesu anawatii wazazi wake, lakini bado tunakosa majibu kwa nini alikosa utii huo pale mwanzoni na kuamua kubaki nyuma Yerusalemu bila ruhusa au kuwataarifu wazazi wake. Wapo wanaokuja na msimamo kuwa kwa desturi msafara wa mahujaji uligawanyika katika makundi mawili yaani la akina mama na la akina baba, hivyo wazazi wa Yesu kila mmoja alifikiri na kudhani kuwa mtoto wao yupo katika kundi lingine. Lakini wataalamu wa Maandiko wanakanusha ukweli huu na kutualika kutafuta sababu hasa za mwinjili Luka kutupa simulizi la aina hii pamoja na mikasa yake.
Sehemu ya Injili ya leo tukiisoma kama jinsi ilivyo tunabaki na ugumu na kutoeleweka vema na badala yake nawaalika tutafakari kwa pamoja ujumbe wa kitaalimungu nyuma yake. Mwinjili Luka haandiki Injili yake au sehemu ya Injili ya leo siku ya pili yake baada ya tukio au kama mmoja aliyeshuhudia kubaki kwa Yesu Hekaluni. Mwinjili Luka anaandika miaka 50 baada ya ufufuko wake Yesu Kristo na hivyo Injili yake ni mwaliko daima wa kumwelewa vema na vizuri zaidi Kristo Mfufuko. Ni katekesi kwa jumuiya ile ya waamini wa mwanzo. Ni mafundisho ya imani kuliko kitabu cha historia ya kawaida ya matukio na miaka. Ni baada ya kifo na ufufuko wake Yesu Kristo, wafuasi wa Yesu Kristo waliweza kumwelewa Yesu Kristo kuliko ilivyokuwa kwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu. Ni nia yake kuwasaidia Wakristo wale wa mwanzo na hata leo kuelewa maana ya mateso na magumu yanayokosa majibu kwa mantiki na akili za kibinadamu. Ni katika mtoto wa miaka kumi na miwili, tayari Mwinjili Luka anatuonesha kuwa ni Mwana wa Mungu, Mkombozi na Mwalimu wetu, anayemtii Baba yake siku zote za maisha yake. Mtoto huyu ni Mwalimu anayetoa maana sahihi ya Maandiko Matakatifu.
Mwinjili Luka pale mwanzoni mwa sehemu ya Injili ya leo hawataji kwa majina wazazi wake Yesu Kristo. Kwa kadiri ya tamaduni za Kiyahudi pale neno wazazi linapotumika pasipo kutaja majina ni kuonesha wajibu wa kila mzazi, na ndio ule wa kurithisha imani, tunu njema za kiutu na mapokeo kwa watoto. Ni wajibu wa kila mzazi wa Kiyahudi kuona kuwa mtoto anakua katika imani ya kumjua Mungu mmoja na kumpenda Yeye peke yake siku zote za maisha yake. Ni sawa na kusema neno mzazi mara moja linaingia kichwani kwa kila Myahudi wajibu huo wa msingi. Baba ni sawa na kusema mapokeo ya kiimani na mama daima anawakilisha Taifa zima la Israeli. Kama taifa wana wajibu wa kuwarithisha imani na mapokeo yao kizazi hata baada ya kizazi. Zaidi tunaona Mwinjili Luka anatuonesha kuwa wazazi wa Yesu, walikuwa ni Wayahudi kweli kweli walioshika imani yao, na hivyo kila mwaka walienda Yerusalemu kwa hija na sikukuu za amri kadiri ya sheria. Sheria iliwataka hasa wanaume watu wazima kuanzia miaka kumi na mitatu kwenda Yerusalemu mara tatu kila mwaka kwa sikukuu za Pasaka ya Kiyahudi, Pentekoste ya Kiyahudi na Sikukuu ya vibanda. (Rejea Kutoka 23:17 na Kumb 16:16) Hata wale waliokuwa wanaishi mbali na nchi yao walifanya jitihada na kila liwezekanalo haidhuru mara moja katika maisha kufanya hija katika mji wa Daudi, yaani Yerusalemu. Nazareti kutoka Yerusalemu ni umbali wa siku tatu maana ilikuwa ni safari ya miguu au kutumia punda kwa baadhi waliokuwa na uwezo huo.
Yesu akiwa na umri wa miaka kumi na miwili haikuwa bado na ulazima wa kufanya hija kwani umri rasmi wa kuwa mtu mzima na kuzishika sheria ni miaka kumi na mitatu, ila kwa vile kama nilivyotangulia kusema hapo juu mwinjili Luka anatuonesha kuwa wazazi wake walikuwa washika sheria kweli kweli na hivyo wakaambatana naye kwenda Yerusalemu kwa sherehe za Pasaka ya Kiyahudi. Hekaluni kama mahali patakatifu penye utukufu na uwepo wa Mungu, walikuwepo pia wataalamu wa Maandiko Matakatifu, ndio marabi na waandishi. Hawa walisoma Maandiko Matakatifu na kuwaelezea maana yake kwa mahujaji waliofika pale, walizunguka hekaluni na kusali zaburi na hata kuwapa ushauri wa kiroho mahujaji. Na ndio Yesu anakuwa na hamu na shauku ya kuwasikiliza na kuwauliza maswali na kujibu kiasi cha kuwastaajabisha, kwani alikuwa bado mdogo kuwa na uelewa mkubwa wa Neno la Mungu. Na ndio maana Mwinjili Luka anataja hata na miaka yake, siyo tu kwa kutupa taarifa za kihistoria bali ujumbe wa kiteolojia. Kuwa huyu Mtoto ni Mwalimu wa Neno la Mungu. Mshangao wao si kwa sababu mtoto Yesu ana akili au anajua Neno la Mungu bali wanabaki vinywa wazi kuona anawapa maana tofauti na ile ya kimapokeo waliokuwa wanaitoa wao kwa watu. Mtoto huyu ni kinyume na hata uelewa waliokuwa nao wazazi wake, anawafundisha maana mpya ya kulitafsiri Neno la Mungu, anawapa tafsiri mpya ya Maandiko Matakatifu. Wanabaki na mshangao! Mshangao ni kipaji kutoka kwa Mungu, vinginevyo, watu watafanya mambo kwa mazoea.
Mwinjili Luka anaenda mbele zaidi kwa kutupatia maneno ya kwanza ya Yesu katika Injili yake. Ni maswali mawili kwa wazazi wake na ndio: Kwa nini mnanitafuta? Je, hamkujua kuwa ninapaswa kuwa nyumbani kwa Baba yangu? Mwinjili Luka anatueleza kuwa wazazi wake hawakuelewa maneno yake. Ni sawa na kusema kumwelewa Yesu Kristo ni baada ya tukio la Mateso, Kifo na Ufufuko wake, na ndipo haswa tunaweza kuelewa hata na Maandiko ya Agano la Kale. Ili kuelewa Maandiko Matakatifu hata leo lazima kusoma katika mwanga wa mateso, kifo na ufufuko wake Yesu Kristo. Mwinjili Luka anatueleza kuwa wazazi wake walimtafuta kwa siku tatu, mji wa Yerusalemu wa nyakati za Yesu haukuwa mkubwa hivi kusema unaweza kumtafuta mtoto kwa siku tatu. Yerusalemu ya zamani ni mwendo wa masaa machache tu kuumaliza mji wote na kuweza kumpata mtoto Yesu. Hivyo siku 3 ni ujumbe tena wa kitaalimungu anaotupatia Mwinjili Luka. Ni siku ya tatu baada ya kifo chake tunaona wanawake wanafika na kumtafuta kati ya wafu pale kaburini. Ni kukosea mahali pa kukutana na Yesu, yu hai na yupo kati ya hai, ni mzima ameyashinda mauti. Ni siku ile ya ufufuko wake anawaangazia wafuasi wake wa Emau mpaka mioyo yao inawaka njiani kwa jinsi alivyokuwa wanafundishwa Maandiko na wakamtambua katika kuumega mkate.
Tofauti na kile tulichoona awali sehemu ya mwisho ya Injili ya leo tunaona Yesu anarejea Nazareti na wazazi wake na sasa wanatajwa kwa majina yao. Hivyo ni ujumbe sio tena wa jumla jumla kwa kila mzazi bali unaoihusu familia hii ya Yesu, Maria na Yosefu. Kuheshimu wazazi sio tu pale wanapokuwa wazee na kuwasaidia bali pia ilimaanisha kupokea kiaminifu dini na imani ya wazazi, ni kuwa mwaminifu kwa Mungu. (Rejea Kumb 6:20-25) Ni sawa na kusema Yesu alizidi kukua akimtii Mungu na kulishika Neno na maagizo yake siku zote za maisha yake. Hivyo tunaweza kuhitimisha kwa kusema tangu mwanzoni mwinjili Luka anatualika kusoma Injili yake kwa kuongozwa na fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Kama vile tukio la mateso na kifo na ufufuko wake linatokea Yerusalemu, na tukio la leo pia linajiri Yerusalemu. Yesu kila mara anakwenda Yerusalemu kutimiza mapenzi ya Baba yake kama alivyofanya iwe katika Pasaka ya Wayahudi na Pasaka mpya ya kifo na ufufuko wake na mara zote mbili aliachwa peke yake. (Rejea Luka 24:7; 26:44) Swali la Yesu kwa wanawake waliofika kaburini kumtafuta, mnamtafuta nani ni lile lile analowauliza wazazi wake leo. Ni swali hilo hilo ananiuliza mimi na weye katika Dominika ya leo.
Hata baada ya kuwatokea baada ya kufufuka siku ya tatu tunaona wanawake na wanafunzi wake bado wanakuwa wagumu kumtambua na kumwelewa kama ilivyokuwa kwa Maria na Yosefu pale hekaluni. Kama alivyowafundisha siku ile ya ufufuko wake na kuwaacha na mshangao kama tunavyosoma (Luka 24:32,44); ndio hivyo hivyo wasikilizaji wake leo wanabaki na mshangao kwa tafsiri mpya ya Neno la Mungu. Kama Bikira Maria nasi mara nyingi katika maisha yetu kuna mengi tunashindwa kuyaelewa hivyo tunaalikwa kuyaweka moyoni kwa maana ya kuyatafakari kwa mwanga wa Yesu aliyeteseka, kufa na kufufuka. Nasi leo tunapotafakari ujumbe wa kiteolojia wa mwinjili Luka hatuna budi kutafakari tena na tena fumbo lile la mateso, kifo na ufufuko ili kuweza kuulewa ujumbe wa Mwenyezi Mungu katika maisha na hasa katika familia zetu. Nawatakia tafakari njema na Sherehe njema ya Familia Takatifu. Kama Familia Takatifu walivyokuwa katika kumpenda Mungu na jirani nasi tusali ili familia zetu zikue katika upendo huo kwa Mungu na kwa jirani. Mwisho mwema wa mwaka na mwanzo mwema wenye kila baraka zake Mtoto Yesu!