Sherehe Za Noeli Misa ya Mchana: Neno Akatwaa Mwili Na Kukaa Kwetu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu katika sherehe ya kuzaliwa Bwana. Katika adhimisho la sherehe ya Noeli, Mama Kanisa ameweka Misa tatu; Misa ya usiku, Misa ya alfajiri na Misa ya mchana. Kila misa ina sala na masomo yake. Tafakari hii ni ya masomo kwa ajili ya Misa ya mchana. Noeli ni sherehe ya Umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili, kuwa binadamu na kukaa kwetu. Ni sherehe ya kuzaliwa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, Mfalme wa Amani kama tunavyoimba katika wimbo wa mwanzo; Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake, naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu (Isa.9:6) na katika sala mwanzo tunasali; Ee Mungu, ulimweka mwanadamu katika cheo cha ajabu, na tena ukamtengeneza upya kwa namna ya ajabu zaidi. Tunakuomba utujalie kushiriki umungu wake, yeye aliyekubali kushiriki ubinadamu wetu. Fumbo la umwilisho ni ishara wazi ya upendo wa Mungu mmoja katika Nafsi zake Tatu kwa mwanadamu. Tukio la kuzaliwa Bwana Yesu Kristo katika kipindi cha Noeli linaanzisha safari rasmi ya utimilifu wa ukombozi wetu sisi wanadamu kiroho na kimaisha kiujumla. Hivyo duniani kote ni furaha, shangwe, nderemo, vifijo na vigelegele vinasikika, kwa sababu amezaliwa mwokozi wetu; ndiye Kristo, Bwana wetu, mfalme wa amani na haki.
Wimbo wa mwanzo unaweka wazi sababu ya sisi kufurahi siku hii. “Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake, naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu” (Isa. 9:6). Kwa dhambi ya Adamu na Eva, utu wetu uliharibika. Dhambi iliingia duniani ikaleta doa katika utu wetu. Dhambi hii ilitutenga na Mungu. Ndivyo maandiko matakatifu yanavyotuambia; “Basi Mwenyezi Mungu akamfukuza Adamu nje ya bustani ya Edeni na kuweka mlizi upande wa mashariki wa bustani ya Edeni na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kulinda njia iendayo kwenye mti wa uzima wa milele” (Mwa.3:23-24). Lakini Mungu ni mwenye huruma. Licha ya uasi huo Mungu ameendelea kumwita mwanadamu arudi kwake. Aliwateua Waisraeli ili kuanzia kwao mataifa yote yapate kukombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Historia nzima ya waisraeli ilikuwa ni juhudi zake Mungu za kumrudisha binadamu kwake. Walipokosea aliwatumia manabii kuwarejeza kwake. Licha ya juhudi zote hizo binadamu alidumu katika uasi wake. Mwishowe Mungu akaamua kumtuma mwanae wa pekee. Siku za Krismasi ni siku za furaha tunapoadhimisha kuzaliwa kwake Kristo Mwokozi wetu. Katika sherehere za Krismasi tunaadhimisha fumbo la Umwilisho yaani Mungu kutwaa mwili. Kwa fumbo hili Mungu anakuwa mtu na anamfanya mtu kuwa kama yeye; ubinadamu na umungu vinakutana; dunia na mbingu zinaungana. Tunamshukuru Mungu kwa kuthamini hivyo ubinadamu wetu na tumuombe jinsi yeye alivyoshiriki ubinadamu wetu atusaidie na sisi tushiriki Umungu wake.
Katika somo la kwanza la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 52:7-10); Mungu anaahidi kuwa wayahudi watarudi tena Yerusalemu kutoka Babeli. Utumwa wao ni mfano wa hali ya dhambi, na ukombozi wao ni mfano wa ukombozi wa mataifa yote kutoka dhambini. Waisraeli wanapewa ujumbe huu wakiwa wanateseka utumwani Babeli. Ni ujumbe wa matumaini kuwa amani imefika, vita sasa vimekwisha, utumwa umekwisha. Isaya anawaalika watu wafurahi akiwaambia; “Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa”. Kwanini wafurahi wakati wako utumwani? Kwa sababu mda sasa umewadia wa Mungu kutimiza ahadi yake ya kuwakomboa na ncha zote za dunia zitauona wokovu wa Mungu wao. Ujumbe huu ni utabiri wa ukombozi wa binadamu wote kutoka utumwa wa dhambi ambao nasi tunafurahia kuupata kwa kusherehekea kuzaliwa kwake Yesu Kristo, Emanueli-Mungu pamoja nasi. Somo la pili la Waraka kwa Waebrania (Ebr. 1:1-6); linadhibitisha kuwa utabiri wa kale umetimia katika Yesu Kristo. Katika yeye utukufu wa Mungu umefunuliwa na ni katika yeye tu Mungu anaongea nasi katika nyakati hizi zetu kama tunavyosoma; “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwanaye, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu […]Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu.” Kumbe mtoto Yesu ni chapa ya Mungu ambaye tangu kuanguka kwetu dhambini anatutafuta kutukomboa. Manabii walitabiri zamani na sasa waliyotabiri yanakamilishwa ndani yake.
Katika Injili, Yohane (Yn. 1:1-18) anaelezea asili ya Yesu kuwa ni Mungu mwenyewe, naye ni Mungu kwa asili. Kuwa ndiye aliyekuja kulishinda giza na kutujalia nuru, kutufanya sisi tuweze kuona Mwanga wa Mungu na kuufuata kikamilifu. Yohane anashuhudia kuwa neema zilikuja kwa mkono wa Kristo, naye ndiye aliyemfunua Mungu kwetu. Yesu amekuja ili tusamehewe dhambi zetu. Amekuja ili kutufuta machozi yetu. Amekuja ili kutusafisha mioyo yetu, kutununua toka utumwa wa shetani kwa gharama ya uhai wake. Kuzaliwa kwake sio tu tukio la kihistoria, bali tukio halisi katika maisha yetu. Kristo yupo nasi katika maisha yetu: Yesu amekuja kujiunga nasi katika magumu ya maisha na katika udhaifu wetu. Yesu ni Emanueli “Mungu pamoja nasi, kwa hiyo, hatuko peke yetu katika maisha na mahangaiko yetu. Noeli ni sherehe ya kuanza upya. Tuanze upya katika maisha yetu, kama tulikuwa na mahusianao mabaya, hatuelewani, tuanze upya. Kama tulikuwa na tabia mbaya, tuanze upya. Tuthamini utu wetu na miili yetu: Kama Mungu amethamini utu wetu na kutwaa mwili kama sisi lazima sisi pia tujithamini na tuuthamini ubinadamu wetu na kuiheshimu miili yetu. Tusiudhalilishe ubinadamu wetu au kuwadhalilisha wengine. Mtu ana thamani, ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na Mungu amejiunga naye katika ubinadamu wake. Kwa hiyo, tuondoe yale yote yanayodhalilisha utu wa mwanadamu. Tuthamini miili yetu kwa kuitunza vizuri kwa heshima.
Katika shamrashamra, nderemo na vifijo vya kumshangia mkombozi aliyezaliwa, tusijiingize katika dhambi na kupoteza baraka na neema tulizojichotea katika kipindi cha majilio na hivyo kupoteza maana ya kusherekea Noeli. Mtu atakayeendelea kuishi katika giza ni sawa na hao anawasema Yohone kuwa: “Mwanga umekuja ulimwenguni lakini watu wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu. Kila mtu atendaye maovu anachukia mwanga, wala haji kwenye mwanga, maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe. Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu” (Yon.3:19-21). Tuipokee basi Nuru iliyokuja ulimwenguni, ituangazie tusiifanye Noeli kuwa msimu wa kutenda maovu. Tukumbuke kwa majuma manne tulijiandaa kusherekea Noeli kwa kufanya toba na malipizi kwa dhambi zetu. Tusisahau maazimio tuliyoweka. Kama tunavyosali katika sala baada ya komunyo tukisema; Ee Mungu mwenye huruma, tunaomba huyo Mwokozi wa dunia aliyezaliwa leo akatufanya watoto wako, atujalie pia uzima wa milele. Tumuenzi Masiha aliyezaliwa kati yetu kwa kutenda mema na kuepa dhambi na Mungu atatujaza baraka na neema zake. Mwisho tusali na kumwomba Mungu pamoja na Mtakatifu Francisko wa Assisi tukisema; “Ee Bwana unifanye kuwa chombo cha amani yako. Nieneze mapendo wanapochukiana, nilete msamaha wanapokosana, nipatanishe wanapogombana, nitumainishe wanapokata tamaa, niwashe taa penye giza, nilete furaha panapo kaa huzuni. Ee Bwana Mungu unijalie kufariji kuliko kufalijiwa, kufahamu kuliko kufahamika, kupenda kuliko kupendwa. Anayetoa atapokea, anaye samehe atasamehewa, anayekufa kwa ajili ya Kristo atazaliwa kwenye uzima wa milele”. Herini kwa sikukuu ya kuzaliwa Mwokozi wetu Yesu Kristo.