Tafuta

Mashemasi ni Wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa lakini zaidi mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini, utume unaotekelezwa kwa niaba ya Mama Kanisa. Mashemasi ni Wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa lakini zaidi mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini, utume unaotekelezwa kwa niaba ya Mama Kanisa. 

Jimbo Katoliki la Morogoro Lapata Mashemasi Wapya 7 kwa Mpigo

Mama Kanisa anafundisha kwamba, Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu. Mashemasi ni wahudumu wa Neno la Mungu kwa kutangaza, kuhubiri na kulishuhudia; kwa kusimamia na kubariki ndoa; kwa kuongoza mazishi na hasa zaidi kwa kujitoa kwa ajili ya kushuhudia Injili ya huduma ya huruma na upendo kwa niaba ya Mama Kanisa!

Na Padre Agapito Batholomeo Mhando, - Vatican.

Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu yaani: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja; Upadre na Ushemasi. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa ya kudumu na hivyo kufananishwa na Kristo Yesu aliyejifanya “Shemasi”, yaani Mtumishi wa wote! Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre katika maadhimisho ya Mafumbo ya Mungu na kwa namna ya pekee, Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Mama Kanisa anafundisha kwamba, Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu. Mashemasi ni wahudumu wa Neno la Mungu kwa kutangaza, kuhubiri na kulishuhudia; kwa kusimamia na kubariki ndoa; kwa kuongoza mazishi na hasa zaidi kwa kujitoa kwa ajili ya kushuhudia Injili ya huduma ya huruma na upendo kwa niaba ya Mama Kanisa!

Ni katika muktadha huu, Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania, tarehe 12 Januari 2022 ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi wa Mpito kwa Majandokasisi Saba wa Jimbo Katoliki la Morogoro. Ameawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa na hasa wito wa Daraja Takatifu, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwajalia neema zake, ili akamilishe kile alichokianza ndani mwao, ili waweze kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza ndugu zao katika Kristo Yesu huku wakiwa ni Mapadre. Na kwa njia hii, Mwenyezi Mungu anatukuzwa na binadamu anatakatifuzwa. Mashemasi wapya wametakiwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kutenda kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Mama Kanisa na wala si vinginevyo.

Mashemasi kamwe wasipate kishawishi cha kutaka kuwaungamisha waamini au kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwani hii si sehemu ya huduma yao kwa watu wa Mungu. Mashemasi watambue na kuheshimu mipaka ya utume wao; wajenge na kudumisha fadhila ya unyenyekevu na kuendelea kujikita katika utakatifu wa maisha. Kristo Yesu ni kielelezo cha mchungaji mwema, aliyejitaabisha kuzunguka katika miji na vijiji, akifundisha na kuhubiri Habari Njema; akiponya magonjwa na udhaifu wa kila aina, akaonesha huruma na upendo mkuu kwa binadamu wote, awe ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wao. Rej. 9: 35-38. Kwa kifupi kabisa, Kristo Yesu anajitanabaisha kuwa ni: Kiongozi, Mwalimu na Mponyaji. Ni jukumu la Wakleri kuhakikisha kwamba, wanaendeleza utume huu kwa wema, ukamilifu, uaminifu na uadilifu, ili Habari Njema ya Wokovu iweze kuwafikia watu wengi zaidi.

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. anasema, leo hii, watu wa Mungu wanakabiliwa na changamoto pevu kiasi cha kukosa dira na mwelekeo wa maisha. Kumbe, wajibu na jukumu la Mashemasi wapya ni kuitenda kazi njema kwa uaminifu na uadilifu mkubwa. Wawe ni dira mwanga kwa watu wa Mataifa, ili watu wa Mungu waweze kuvuka salama kutoka huku Bondeni kwenye machozi. Sheria, taratibu na kanuni hazina budi kufuatwa kikamilifu katika hali ya maisha yao kiroho na kimwili. Kwa njia ya katekesi makini na endelevu, iwasaidie waamini kutambua vyema mambo msingi ya imani yao, tayari kuilinda na kuitetea; kuitangaza na kuishuhudia kama kilelezo cha imani tendaji ndani ya Kanisa Katoliki. Mashemasi wawe na ari na moyo wa kuwafundisha watu, lakini hasa zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu.

Wawashauri na kuwaongoza waamini pale wanapoteleza na kuanguka. Wawe mahiri katika kufundisha Neno la Mungu ili watu waweze kumfahamu, kumpenda, kumtumikia na hatimaye, waweze kufika kwake mbinguni. Mashemasi wawe ni vyombo vya Injili ya huruma na mapendo. Watambue kwamba, leo hii, waamini wengi kutokana na shida, mahangaiko na changamoto nyingi wanatafuta njia ya mkato, wanatafuta miujiza na matokeo yake, wengi wamedanganyika na kuteteleka katika imani na hatimaye, wakakengeuka. Mashemasi wasaidie kutoa katekesi makini na endelevu ili kuwaelimisha watu wa Mungu na hatimaye, waweze kumfikisha Kristo Yesu kwa ustaarabu. Mashemasi wawe ni vyombo vya faraja, lakini wawe makini katika kufikiri, kuamua na kutenda, wasije wakaingizwa mkenge na hatimaye, wakajikuta wanakosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha na wito wao.

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. mwishoni mwa mahubiri yake, amewataka Mashemasi katika huduma, watoe kipaumbele cha kwanza kwa watoto yatima na maskini ambao ni amana, utajiri na walengwa wakuu wa Kanisa. Kumbe, Mashemasi wawe ni wajumbe wa Neno la Mungu, wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa na vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma na mapendo kwa watu wa Mungu. Kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, Mwenyezi Mungu atukuzwe na mwanadamu apate kutakatifuzwa. Yafuatayo ni majina ya Mashemasi wapya kutoka Jimbo Katoliki la Morogoro:

1. Shemasi David Ndibalema, Parokia ya Chalinze.

2. Shemasi Deodatus Mteme, Parokia ya Vidunda.

3. Shemasi Elia Mwaila, Parokia ya Itaragwe.

4. Shmemasi Innocent Byemerwa, Parokia ya Chuo Kikuu cha Sokoine.

5. Shemasi Otto Isdory Otto, Parokia ya Chuo Kikuu cha Sokoine.

6. Shemasi Pantaleo Makosa, Parokia ya Dakawa.

7. Shemasi Rogatus Mazigo, Parokia ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Patris Morogoro.

Mashemasi
13 January 2022, 15:50