Dominika ya III ya Neno la Mungu: Maadhimisho ya Neno la Mungu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
UTANGULIZI: Ni dominika ya tatu ya Mwaka, dominika ambayo sasa inaitwa Dominika ya Neno la Mungu. Tangu mwaka 2020 Kanisa limeitenga dominika ya tatu ya Mwaka kuwa ni dominika ya kuliadhimisha Neno la Mungu: kulitukuza, kulisherehekea na kulitangaza. Hii ni kuzidi kulisimika Neno la Mungu katika mioyo ya waamini na kuonesha umuhimu wake katika maisha yao na katika maisha mazima ya Kanisa. Kwa upande wetu, Kanisa la Tanzania na Afrika kwa ujumla, tumekuwa tayari na utamadunisho wa Neno katika maadhimisho ya Misa, katika Jumuiya Ndogondogo za Kikristo na usimikaji wa Biblia katika familia. Dominika hii inakuja kutukumbusha kuziamsha tamaduni zetu hizo njema za kuliadhimisha Neno la Bwana.
MASOMO KWA UFUPI: Masomo ya dominika hii yanatuonesha namna Biblia yenyewe inavyoelezea umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya waamini. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Nehemia (Neh 8: 2-4, 5-6. 8-10) linaonesha namna Torati ilivyokuwa ikiadhimishwa. Torati ni Neno la Mungu katika vitabu vitano vinavyofahamika kama vitabu vya Musa. Siku hiyo ya kuliadhimisha Neno, kuhani Ezra aliileta Torati mbele ya kusanyiko la watu , akaisoma na kifafanua mbele ya kusanyiko. Torati hii ilipokuwa inasomwa, watu waliipokea kama kumpokea Mungu mwenyewe. Neno la Bwana walilipokea kama uwepo halisi wa Mungu. Liliwachoma mioyo wakalia na kuomba toba. Siku ya adhimisho la Neno ilikuwa ni siku Takatifu.
Wimbo wa katikati kutoka Zaburi ya 19 nao unaleta ushuhuda mwingine kuhusu Neno la Mungu. Zaburi hii ni wimbo wa sifa kwa Torati. Unailitukuza Neno la Bwana kuwa ni roho na uzima. Ndiyo maana Neno hilo linaposomwa, Neno hilo linapoadhimishwa, mzaburi anasema huburudha nafsi na humtia mjinga hekima. Ni Roho wa Bwana aliye katika Maandiko Matakatifu ndiye aitendaye kazi hiyo. Ni kwa Roho huyo, Neno la Bwana linatumika kuonya, kufundisha na kuhimiza maadili mema kama anavyofanya Mtume Paulo katika barua zake. Leo tunasoma barua yake ya kwanza kwa Wakorinto (1Kor 12:12-30) ambapo kwa nguvu ya Neno la Bwana anaasa waepuge utengano kati yao na waulinde umoja kwa kuwa wakristo ni kama viungo mbalimbali vya mwili mmoja wa Kristo.
Somo la Injili ni kutoka kwa Mwinjili Luka (Lk 1:1-4, 14-21). Hii ni Injili itakayotuongoza katika masomo ya dominika kwa mwaka huu mzima. Leo katika kuadhimisha dominika ya Neno la Mungu, somo hili linatupatia mambo makuu mawili. Jambo la kwanza ni kutuonesha kuwa Biblia Takatifu, Maandiko Matakatifu ni Neno la Mungu katika maneno ya mwanadamu. Maana yake ni kuwa Neno hili la Mungu liliandikwa na wanadamu chini ya uvuvio wa Mungu mwenyewe. Luka anasema mwanzoni mwa Injili kuwa yeye ametafuta ufahamu wa yote yaliyotokea, ni wazi kuhusu Kristo, na ameamua kumuandikia Teofilo ili apate kujua kwa uhakika mambo ambayo alikuwa tayari amekwishafundishwa. Sasa Teofilo maana yake ni mpendwa wa Mungu. Hakuna uhakika kama Luka alimaanisha kumuandikia mtu binafsi aliyeitwa Teofilo, au kwa jina hilo alimaanisha anawaandikia wapendwa wote wa Mungu. Msingi wa kifungu hicho ni kutuonesha kuwa alichoandika ni ushuhuda wake kama Mungu alivyomvuvia. Uvuvuio huu maana yake ni kuwa mwandishi wa vitabu vya Biblia aliandika kile tu ambacho Mungu alitaka kiandikwe kwa ajili ya manufaa ya ukombozi wa mwanadamu.
Jambo la pili ambalo Injili ya leo inatuonesha ni kuwa Yesu Kristo ndio utimilifu wa Neno la Mungu. Yeye alipoingia katika Sinagogi siku ya sabato alitwaa chuo cha Nabii Isaya akasoma. Kisha kumaliza akawaambia “leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu.” Hakumaanisha maneno yale tu aliyoyasoma, alimaanisha ufunuo wote wa Neno la Mungu tangu Agano la Kale hadi Agano Jipya unapata utimilifu katika Yeye. Yeye ndiye ufunguo wa kuyaelewa Maandiko Matakatifu. Ni kutokea kwake ndio tunaalikwa kuyatafsiri Maandiko yote ya Agano la Kale na ya Agano Jipya. Bila ufunuo wa Kristo hatuwezi kufikia ufahamu kamili wa Neno la Mungu.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tunayo mengi ya kutafakari na kujikumbusha kuhusu Biblia katika dominika hii ya Neno la Mungu. Neno la Mungu ni hazina, ni utajiri ambao kwa hakika hatujaweza bado kuutumia ipasavyo. Adhimisho la dominika hii lituvute, likuze hamu na lichochee ndani yetu kiu ya kuzama katika Neno la Mungu ili kuyashibisha maisha yetu na kuishibisha imani yetu na utajiri usiopimika wa Neno la Mungu. Wengi wetu huwa tunajiuliza, nitaweza vipi kuisoma na kuielewa Biblia? Vipo vifungu ninavisoma na kuvielewa lakini vipo vingine ambavyo ni vigumu kuvielewa, na huenda hivyo ndio vilivyo vingi. Wengine huona kama kilichoandikwa katika Biblia ni masimulizi yaliyopitwa na wakati, masimulizi ambayo kama ya kihistoria tu na ambayo hayagusi maisha ya sasa ya mwanadamu. Katika mazingira kama haya, sehemu ya kwanza kabisa ya kuanzia ni ile ambayo wakristo wa mwanzo kabisa walianzia.
Sio wote waliokuwa na elimu ya ufahamu kuweza kuichambua Biblia, wao walipoichukua Biblia hawakuisoma kama mtu anayetaka kukuza ufahamu wa jambo fulani, waliisoma kama mtu ambaye anataka Biblia ndiyo iyasome maisha yake. Waliiona Biblia kama kioo kinachomulika kuona undani wa maisha yao. Kwa sababu hiyo ilitosha tu kuchukua mistari michache katika Biblia, au maneno machache katika kifungu wanachokisoma na kuyarudia tena na tena ili kupata mwanga wa kuona Neno la Mungu linaniambia nini leo na sasa hivi. Kwa jinsi hii wao hawakuwa na lengo la kwanza la kuisoma Biblia bali kuisali Biblia. Zoezi hili ndilo lililozaa zoezi la kiroho linalojulikana kama “lectio divina”. Ni katika kuisali Biblia, watakatifu wengi wamepata mang’amuzi makubwa sana kuhusu maisha yao na hata kuandika tafakari nyingi za maisha ya kiroho ambazo zimewasaidia wengi. Ni katika kuisali Biblia Neno la Mungu limebadili maisha ya watu wengi katika historia na linaendelea kubadili maisha ya wengi hadi leo. Ninakualika nawe ndugu msikilizaji na msomaji wa Neno la Mungu kuanza kuchota katika hazina hii ya “Lectio Divina” yaani “Masomo ya maisha ya kiroho” utajiri wa nguvu ya Mungu iliyo katika Neno lake.