Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili Pili ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Ishara ya Harusi ya Kana ya Galilaya. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili Pili ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Ishara ya Harusi ya Kana ya Galilaya. 

Harusi ya Kana ya Galilaya: Ufunuo Wa Utukufu wa Kristo Yesu: Divai

Ishara ya Harusi ya Kana ya Galilaya ni kielelezo cha upendo na uaminifu wa Mungu kwa watu wake. Divai ni ishara ya furaha na upendo, lakini wakati mwingine, mwanadamu anatindikiwa na divai, kumbe, katika muktadha huu, waamini wakimbilie katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, atakayewaonesha wa uwepo wa Mungu katika safari ya maisha yao ishara ya furaha na upendo.

Na Padre Gaston George Mkude

Amani na Salama! Simulizi la ishara ya harusi ya Kana si geni masikioni mwa wengi wetu, na mara nyingi kama anavyoandika Mwinjili Yohane kuwa ni mwanzo wa ishara, lakini kwa bahati mbaya sana, tunabaki kuona ni muujiza tu kama miujiza mingine aliyofanya Yesu. Naomba niwaalike katika tafakuri yetu ya leo kutokuishia tu katika muujiza wa Yesu kubadili maji na kuwa divai, na badala yake kuingia ndani na kupata maana ya ishara hii. Mwinjili Yohane katika Injili yake anaorodhesha ishara saba au miujiza anayofanya Yesu Kristo na wa kwanza ndio huu wa Kana ya Galilaya. Hata hivyo ni vema tangu mwanzo tukatambua kuwa Mwinjili Yohane tofauti na Wainjili wengine hatumii neno muujiza na badala yake anatumia ishara. Ishara inabeba ujumbe ndani mwake na hivyo kutualika nasi kuchota ujumbe kusudiwa katika matendo hayo makuu yta Mungu. Tunapoangalia ishara hii ya Kana, tunabaki pia na maswali mengi ya kujiuliza. Kama waalikwa na wenye harusi tayari walishakunywa divai ya kutosha, kwa nini Yesu Kristo anafanya tena muujiza wa kuwaongezea divai? 

Hata kulikuwa na haja gani ya ishara, wakati waalikwa na wenyeji wangeweza kufanya mchango na kwenda kwa wauzao divai ili kuongeza kiasi walichotindikiwa kwa sherehe ya harusi?   Wafuasi wa kwanza wa Yesu wa Nazareti, kabla ya kumfuata walikuwa wanafunzi wa Yohane Mbatizaji, ambaye alikuwa anafunga bila kula chakula au kunywa kinywaji, sasa Je, isingekuwa kwao makwazo? Tunajiuliza, kwa nini Mwinjili Yohane anatumia tukio hili kama mwanzo wa ishara alizofanya Yesu wa Nazareti? Ni mwanzo wa ishara na hata Yesu akiufunua utukufu wake kwa tukio la kugeuza maji na kuwa divai. Labda ingefaa atumie miujiza mikubwa na ya kugusa wengi, kama ile ya kumponya mtu aliyezaliwa kipofu au kufufuliwa kwa Lazaro, kama vielelezo vizuri zaidi vya kuudhihirisha utukufu wake. Tunasikia juu ya waalikwa na mkuu wa meza na watumishi lakini hatusikii juu ya maharusi wenyewe, yaani bwana na bibi harusi, na hata hatusikii neno lolote kutoka kinywani mwa bwana harusi na badala yake kutoka kwa mkuu wa meza.

Kwa nini Mwinjili Yohane anatutajia wengine na hata madarasi ya maji anatupa mpaka ukubwa wake lakini hasemi lolote kuhusu wahusika wakuu wa kusanyiko hilo yaani maharusi wenyewe? Kama anatupa idadi ya madarasi yale na ukubwa wake kwa nini hasemi neno lolote kuhusu wanaharusi? Ndio kusema Mwinjili Yohane kwa kusema ni ishara, anatualika kuwa makini na macho kabisa katika kupata ujumbe kusudiwa wa simulizi la tukio hili. Hata mama wa Yesu hamtaji kwa jina kama ambavyo hatafanya hata pale chini ya Msalaba (Yohane 19:25-27). Na lahiti tungekuwa na Injili moja tu ya Yohane, basi tusingejua kirahisi jina la Mama wa Yesu maana hamtaji kwa jina hata mara moja. Mwinjili Yohane anazungumzia pia juu ya Saa ya Yesu ambayo nayo labda kwa msomaji wa Maandiko Matakatifu anabaki na maswali nini maana yake. Na Mwinjili ataizungumzia juu ya saa ya Yesu tena na tena katika Injili yake. (Yohane 7:30; 12:23,27; 17:1) Na hata jibu analompa mama yake linaashirikia kutokuwa tayari kufanya lolote na bado akafanya muujiza huo. Maswali haya na hata mengi mengineyo tunayokuwa nayo baada ya kusoma sehemu hii ya Injili, tunaweza kusema Mwinjili Yohane lengo na shabaha yake sio kutupa simulizi tu la muujiza bali ni tukio lenye mafundisho mengi nyuma yake.

Injili ya Yohane naomba nikiri ni sawa na bahari yenye kina kirefu, hivyo ili kupata ujumbe hatuna budi kupiga mbizi na kutweka hadi kilindini, ili tuweze kuupata ujumbe kusudiwa au la sivyo tunabaki kuwa juujuu na kukosa maana kusudiwa na mwandishi. Ili kufika kilindini hatuna budi kuwa na nyenzo stahiki za kutusaidia kupiga mbizi na kufika katika kina kirefu. Kana ni kijiji kidogo katika mji wa Galilaya ambako ndiko kunafanyika harusi. Tunasikia juu ya waalikwa ila waweze kushiriki furaha ya wanaharusi ila cha kushangaza wanapungukiwa divai, na hata madarasi ya maji yalikuwa tupu bila maji mpaka itakapoamriwa na Yesu yajazwe maji. Ni mazingira ya mahangaiko makubwa ya kutindikiwa. Hii ni hali tunayoiona kwa haraka lakini yafaa tujiulize kuna ujumbe gani haswa ndani yake? Ili kuweza kupiga ile mbizi na kuzama kilindini hatuna budi kutumia msaada wa Maandiko Matakatifu na hasa Agano la kale ili kupata ujumbe katika ishara hii ya kwanza ya Kana.

Harusi: Jina Israeli kwa Kiyahudi ni la jinsia ya kike, sitaki kuingia sana ndani katika hili ila yafaa ikumbukwe katika baadhi ya lugha tunaona majina na vitu mbali mbali vinakuwa na jinsia. Ni kama hatutegemei mtu kuwa na mtoto wa kiume na kumbatiza Maria, hivyohivyo wa kike kumwita Yosefu. Sasa hata vitu pia vinakuwa na majina yenye kubeba jinsia aidha ya kike au ya kiume au isiyokuwa ya kike au kiume inayosimama katikati isiyo na jinsia. Uhusiano wa taifa la Israeli na Mungu daima unaelezwa katika mahusiano ya mume na mke. Mungu daima anabaki kuwa mchumba mwaminifu kwa watu wake au Taifa lile teule, lakini taifa lile mara nyingi linapoteza uaminifu na kuwa kama kahaba na kuanza kuabudu miungu mingine ya uongo na hivyo kuenenda kama kahaba au malaya. Ni kwa kinywa cha manabii wake, Mwenyezi Mungu daima anawahakikishia upendo wake wa daima. Kama bwana harusi amfurahiavyo biharusi ndivyo Bwana anavyofurahia taifa lile. (Rejea Isaya 62:5, Hosea 2:16-18) Ni Mungu anatoa ahadi ya kuwa mwaminifu daima kwa biharusi wake na ndilo taifa lile teule la Israeli.

Daima manabii wanatumia lugha ya picha zenye kuonesha mahusiano ya ndani na karibu kabisa na ya upendo na uaminifu kutoka kwa Mungu mwenyewe kwa watu wake.  Mungu anayewakikishia upendo wa daima hata pale milima na vilima vitakapoyeyuka Yeye anabaki daima mwaminifu. (Isaya 54:10) Tunaona wakati wa Yesu, Israeli kama taifa lilijiona lipo mbali na Mungu wao aliyewakomboa kutoka utumwani kule Misri na kuwapigania kutoka kwa maadui wao. Yote tunajaribu kuona nini hasa ujumbe wa ishara ya leo. Divai: Katika Agano la Kale, divai au mvinyo ni ishara ya furaha na upendo. (Muhubiri 10:19). Mvinyo hufurahisha roho. (Hekima ya Yoshua bin Sira 40:20); Sherehe bila mvinyo ni sawa na maziko, bila muziki, bila furaha, na hivyo maisha kukosa maana. (Yoshua bin Sira 31:27; Zaburi 104:15, Isaya 24:11). Kama tunapata nafasi tunaweza kusoma na kuona nafasi na umuhimu wa mvinyo katika Maandiko na hasa Agano la Kale. Wakati wa Yesu, Taifa la Israeli lilikuwa linasubiri kwa shauku kubwa ujio wa ufalme wa Mungu. Ufalme ambao manabii waliulezea ni sawa na sherehe kubwa ya harusi ambako kuna vinywaji na vyakula vya kila aina. (Isaya 25:6) Watu wanabaki katika huzuni kama wanakuwa katika sherehe bila mvinyo.

Ni nini kimepelekea Taifa kuwa katika huzuni kubwa, jibu lake ni rahisi, ni kukosekana kwa mahusiano mazuri na Mungu. Ni sawa na bibi harusi bila bwana harusi. Ni lile tabasamu na usalama anaoupata biharusi kwa kuwa karibu na bwana wake. Taifa la Israeli limekuwa mbali na Mungu na hivyo kukosa kuwa Taifa lenye furaha na amani na utulivu. Ni sawa na kuwa mtumwa kwa kuwa mbali na Bwana Mungu.  Ni mtumwa anayetumikishwa na kutii kwa lazima amri na maagizo ya bwana wake. Siyo kama mahusiano ya bwana harusi na bi harusi yanayojengeka katika upendo, uaminifu, furaha na amani ya kweli. Hata dini imebaki kuwa ni ile ya kutii na kuzishika amri, ni dini ya vitisho na kubebeshana mizigo mizito ya amri na sheria na maagizo. Kwa kuwa na lundo la sheria na amri nyingi, na hivyo basi kila mara watu walibaki na dhamiri zilizowasuta kwa kukosa kuzishika kiaminifu amri zile lukuki.  Hivyo walihitajika kuwa na maji ya kujitakasa kila mara, maana mara nyingi wamejikuta najisi kwa kwenda kinyume na sheria na maagizo. Na ndio tunaona katika sehemu ya Injili ya leo yale madarasi yalikosa maji, dini ile mzigo haikuwaletea tena watu furaha na utulivu wa nafsi na hivyo wanahitaji maji kutoka Yesu Kristo anayowaagiza watumishi wale kujaza na hapo kuyafanya kuwa divai.

Harusi ya Kana bila divai inawakilisha hali waliyokuwa nayo Taifa la Israeli kwa kuwa mbali na Mungu wao, kwa kukosa kwao uaminifu katika maagano yao.  Hivyo walikosa kuwa na mahusiano ya upendo kati yao na Mungu kama ya bwana harusi na bibi harusi na kubaki na mahusiano ya sheria na maagizo yaliyowaacha kuwa na mahangaiko kama nchi ile iliyoachwa na kuwa ukiwa. Mama wa Yesu inaweza kuwa ni Maria ila zaidi sana inawakilisha imani na uaminifu aliokuwa nao Maria na ndio anatufundisha nasi kumsikiliza Yesu Kristo.  Ni Maria anayetambua tangu mwanzo kuwa kimbilio letu kila tunapotindikiwa ni Yesu Kristo mwenyewe. Ni katika kumkimbilia na kumweleza shida na mahangahiko yetu, ukiwa wetu na kupungukiwa kwetu. Maria anabaki kuwa kielelezo cha mfuasi mwaminifu kama ambavyo Taifa la Mungu yaani Kanisa tunaalikwa kuiga mfano wa Maria katika safari yetu ya kuelekea uzima wa milele. Mwinjili Yohane anatumia ishara hii kama ya kwanza kama mwaliko wa mahusiano yetu na Yesu Kristo siku zote yanavyopaswa kuwa.  Kanisa anaalikwa kubaki daima kuwa mchumba mwaminifu, bi harusi mwaminifu siku zote na ni katika kubaki na bwana harusi yaani Yesu Kristo mwenyewe hapo tutakuwa na hakika na kubaki wenye furaha na amani ya kweli.

Ni katika saa yake pale Msalabani anajitoa yeye mwenyewe kuwa chakula na kinywaji chetu cha daima. Ni mwaliko wa upendo wa daima wa uwepo wa Mungu mwenyewe kati ya watu wake. (Yohane 19:34; 13:1; 4:14.) Somo la Injili ya leo, linatuonesha umuhimu wa uwepo wa Mungu iwe katika maisha binafsi ya kila mmoja wetu, lakini zaidi sana katika maisha ya familia. Yesu anafika na kuzaliwa sio tu kubaki na familia ile ya Nazareti bali na kila familia ulimwenguni kote. Na ndio yatupasa kutambua tukibaki daima naye na kusikiliza Neno lake basi familia zetu kamwe hatutatindikiwa na divai, yaani, maisha yenye upendo na furaha na amani. Leo tunashuhudia ndoa na familia nyingi zikiingia katika shida na mitafaruki na hata kutendeana ukatili mkubwa kabisa, chanzo ni kukosa kuwa na Yesu ndani mwetu, ni kushindwa kumwalika na kusafiri pamoja na Yesu katika maisha yetu. Mungu hakumuumba tu mwanadamu yule wa kwanza na kumuacha mwenyewe, bali aliunda familia ile ya kwanza, hivyo tangu mwanzo Mungu anataka kutembea na kuwa karibu na familia ya mwanadamu.

Na ndio Yesu anayekuja ulimwengu pia anazaliwa katika familia, narudia si tu ile ya Nazareti bali na familia pana ya kila mwanadamu. Na ndio kusema Mungu anataka daima atembee na abaki nasi katika safari ya maisha yetu ya hapa duniani. Na ndio tunaona ishara ile ya kwanza ya Yesu inafanyika katika muktadha wa familia, familia haiwezi kukamilika bila uwepo wa Mungu, bila uwepo wa Yesu Kristo! Shime vijana wanaotarajia kuingia katika maisha ya ndoa, shime kwa wanandoa kila mara hatuna budi kumwalika Yesu Kristo katika familia zetu ili daima tubaki na divai, ndio maisha ya furaha na amani ya kweli. Nawatakia Dominika na tafakari njema!

13 January 2022, 10:47