Tafuta

Harusi ya Kana ya Galilaya imesheheni ujumbe mpana: Uhusiano kati ya Mungu na waja wake, Ujio wa Masiha chemchemi ya furaha na nafasi ya Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa. Harusi ya Kana ya Galilaya imesheheni ujumbe mpana: Uhusiano kati ya Mungu na waja wake, Ujio wa Masiha chemchemi ya furaha na nafasi ya Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa. 

Harusi ya Kana ya Galilaya: Ujio wa Yesu Masiha, Utakaso na Furaha

Liturujia ya neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa imesheheni utajiri wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Pili ujio wa Kristo Yesu, chemchemi ya utakaso na furaha ya kweli katika maisha. Mwinjili Yohane anamweka mbele ya macho ya Kanisa Bikira Maria anayeguswa na mahitaji ya wanafamilia hawa na hivyo kuomba huruma na upendo wa Yesu!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Dominika ya pili ya Mwaka. Katika dominika hii tunasoma Injili ya Yohane, kifungu kinachofahamika kama Harusi ya Kana. Yesu anageuza maji kuwa divai na kwa kufanya hivyo sherehe ya harusi inaendelea na watu wanaendelea kufurahi. Katika tafakari ya leo tunakwenda kuangalia kifungu hiki na lugha hii ya harusi inayotumika inatuambia nini sisi leo? Tuanze kwa kuyapitia kwa kifupi masomo yote matatu ya Dominika hii. Masomo kwa ufupi: Katika somo la kwanza (Isaya 62:1-5) Nabii Isaya anatoa unabii wa mambo mazuri ambayo Mungu anatangaza juu ya Yerusalemu. Anataja utukufu atakaoupa mji huo, anaahidi kuuangazia kwa mwanga wa haki yake na mambo mengine mengi mazuri. Mwishoni kama kilele cha ahadi hizo, Mungu anaelezea mahusiano yake na Yerusalemu kama harusi. Tunasikia maneno “kama kijana amwoavyo mwanamwali na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.” Lugha hii ya harusi imetumiwa na manabii wengi kuelezea uhusiano mpya ambao Mungu anaahidi kuingia na watu wake kwa njia ya masiha. Mara nyingi manabii wameelezea pia ujio wa masiha huyo kama ujio wa sherehe ya harusi, sherehe itakayowajaza watu furaha, haki na amani.

Somo la Injili ya dominika hii (Yn 2:1-11) ni somo la Harusi ya Kana ya Galilaya. Tunapolisoma somo hili katika mwanga wa manabii na namna walivyoitumia dhana ya harusi tunaona kuwa kitendo cha Yesu kugeuza maji kuwa divai nzuri na kwa jinsi hiyo kuruhusu sherehe ya harusi iendelee, ni kitendo kinachotangaza kuwa kipindi cha masiha kimefika. Na yeye huyo aliyetoa divai bora kuliko ile ya awali ndiye Masiha mwenyewe. Tunapoingia ndani ya somo hili la Injili na kuchambua uandishi wa Yohane tunaona alama nyingine ambayo inalenga kuonesha kuwa harusi hii ya Kana ni tangazo la ujio wa Masiha. Nayo ni ile ya mabalasi sita ya maji. Mabalasi ni kama matanki. Haya kwa kawaida yaliwekwa nje ya Hekalu na Wayahudi walifanya ibada ya kutawadha mikono na miguu kabla ya kuingia Hekaluni. Hii ilikuwa ni alama ya utakaso ambayo dini ya kiyahudi ilielekeza. Katika Injili hii, mabalasi hayo yako tupu. Hayana maji.

Tafsiri yake ni kuwa kile kilichotegemewa kutoa utakaso kimepoteza sifa hiyo. Yesu anaamuru yajazwe maji, yaani yarudishiwe uwezo wa kuwapa watu utakaso na anaenda zaidi ya hapo. Maji yanayowekwa yanageuka kuwa divai. Maana yake ni kuwa utakaso huu anaouamuru Yesu, utakaso unaotokana na Yesu (na si dini ya Kiyahudi ya Agano la Kale) una nguvu kuliko ule wa awali  Somo hili pia linatuonesha nafasi ya Mama Bikira Maria. Nafasi anayochukua ni ile ya kuwa daraja kati ya Yesu na watumishi. Alipogundua divai imeisha alikwenda kwa Yesu akamwambia “hawana divai” kisha akarudi kwa watumishi akawaambia “atakachowaambia, fanyeni”. Hayo ndiyo maneno pekee ambayo Maria anayatamka katika Injili yote ya Yohane. Sehemu yote inayobaki anashiriki lakini hasemi neno.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii yanatupatia mafundisho mengi ya kutafakari katika maisha yetu. Lipo fundisho la kutumainia ahadi na wema wa Mungu katika maisha yetu, lipo fundisho la kumpokea na kumwamini Kristo kama masiha anayeleta ladha mpya katika maisha yetu na hatuwezi pia kuweka kando dhana ya maisha ya ndoa. Maisha ambayo wakati mwingine ile furaha yake inakosekana kama furaha ya harusi ya Kana wakati divai ilipoisha. Hapo wanandoa na wanafamilia kwa ujumla wanaalikwa kumrudia Kristo anayeweza kurejesha divai bora, yaani furaha na amani katika maisha ya ndoa na familia. Tena katika Rozari Takatifu, Mafumbo ya Mwanga, tendo la pili tunafakari tukio hili la Yesu kugeuza maji kuwa divai, tukimwomba Mungu atujalie kuukoleza ulimwengu kwa chachu ya Injili, Injili ambayo ni Habari Njema ya Yesu Kristo mwenyewe.

Pamoja na mafundisho hayo, na mengine mengi ambayo tunaweza kuzidi kuchota kutoka somo hili la Injili, ni vema tukaliona somo hili pia kuwa linaelezea muujiza ambao Yesu aliufanya hapo harusini Kana. Katika Injili ya Yohane, ipo miujiza saba tu, na huu ndio wa kwanza. Muujiza huu wa kwanza unatendeka namna gani? Unaanza pale ambapo Maria anawaambia watumishi “atakachowaambia, fanyeni.” Na Yesu anawaambia “jalizeni mabalasi maji”. Wanapomaliza kujaza, maji tayari yanakuwa yamegeuka kuwa divai. Mwinjili Yohane anatusaidia kuelewa muujiza ni nini na unatendekaje. Anatuonesha kuwa muujiza unatendeka pale ambapo mwanadamu anakuwa tayari kufanya kile anachokisema Kristo. Na ndivyo hivyo miujiza yote iliyomo katika Injili ya Yohane inavyofanyika. Tukiiangalia michache tu: kumponya mtoto wa akida (Yoh 4:49) Yesu alimwambia “rudi nyumbani utamkuta mwanao yu hai”. Akida akarudi akakuta mwanae ameponywa. Kwa mgonjwa aliyepooza (Yoh 5:8) alimwambia “simama, jitwike godoro lako uende”, mgonjwa alipotii muujiza ukatendeka: akasimama, akajitwika godoro lake akaenda. Kuwalisha watu elfu tano (Yoh 6:7) Yesu aliwaambia wafuasi wawaketishe watu na wampe wale samaki wawili na mikate mitano.

Kumbe, Yohane anatukumbusha sisi ambao mara nyingi tunapenda imani yetu kwa Mungu isindikizwe na miujiza katika maisha yetu kuwa muujiza unaanza pale ninapojiweka tayari mimi kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Mungu hafanyi muujiza kutoka nje yangu, Mungu anafanya muujiza kupitia imani yangu na utayari wangu wa kuyatii mapenzi yake. Na tukiliangalia vizuri neno hilo alilosema Bikira Maria kuwa “lolote atakalowaambia, fanyeni” tunaona kuwa linafanana kabisa na lile jibu alilompa malaika Gabrieli; “mimi ni mtumishi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kumbe Maria mwenyewe anatufundisha kuwa jambo la kwanza ni kuyapokea mapenzi ya Mungu katika maisha. Na kimsingi huu ndio muujiza wenyewe. Yaani mwanadamu kufikia hatua akauachilia utashi wake akaukabidhi kwa Mungu na kuwa tayari kupokea chochote ambacho Mungu mwenyewe ataona kinampendeza kumfanya akipitie. Mtakatifu Padre Pio mara nyingi alikuwa akiwaambia Wakristo waliofika kusali pamoja naye kuwa kabla ya kumuomba Mungu atende muujiza katika maisha yako, mwombe kwanza neema ya kuyapokea mapenzi yake. Na kama mapenzi yake ni kukutendea muujiza unaomuomba basi hatasita kukutendea.

Liturujia D2 Mwaka C
14 January 2022, 15:33