Harusi ya Kana ya Galilaya: Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Mungu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 2 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Katika mzunguko wa mwaka wa Kiliturujia, mwaka A tunatafakari Injili ya Mathayo, mwaka B injili ya Marko na mwaka C Injili ya Luka. Lakini, dominika ya pili tunasoma Injili ya Yohane, kwa sababu ni yeye peke yake anayesimulia Yesu kujifunua umungu wake kwa muujiza wa kugeuza maji kuwa divai katika Harusi ya Kana. Mapokeo yanasimulia kuwa waamini wa Kanisa la mwanzo, waliadhimisha matukio manne kwa pamoja katika sherehe ya Tokeo la Bwana – Epifania – Mungu kujifunua kwa njia mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo: Kuzaliwa kwake Bethlehemu, kujitokeza na kujifunua kwake kwa watu wa mataifa yote kwa njia ya Mamajusi, Ubatizo wake mtoni Yordani na kugeuza maji kuwa divai katika harusi ya Kana - muujiza wake wa kwanza kuufanya. Baadae kila tukio lilipewa siku na tarehe yake maalumu ya kuadhimishwa. Kuzaliwa kwake 25 Desemba, Epifania - Yesu kujionesha kwa Mamajusi 6 Januari na ubatizo wake jumapili baada ya Epifania, ambapo kimsingi ni dominika ya kwanza ya mwaka kipindi cha kawaida. Tukio la kugeuza maji kuwa divai katika harusi ya Kana halikupewa siku yake maalumu. Ni katika dominika ya pili ya mwaka baada ya ubatizo wa Bwana – tunaouadhimisha domenika ya kwanza, Injili inayosomwa ni ya muujiza wa Kwanza wa Yesu: Kugeuza maji kuwa divai katika Arusi ya Kana ya Galilaya ya Nazareti.
Katika somo la kwanza la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa 62:1-5), kwa kutumia lugha ya kimahusiano ya wanandoa - mahusiano kati ya mume na mke kuelezea mahusiano kati yake na mwanadamu yalivyo, Mungu anawaahidi waisraeli kuwaondolea fedheha na dharau waliyoibeba kwa kudharauliwa na kufananishwa na mke mtalikiwa, aliyeachika na mkiwa. Jinsi mahusiano ya Bwana na bibi arusi katika ndoa yanavyopaswa kuwa ndivyo mahusiano kati ya Mungu na taifa lake yanavyokuwa. Kama uaminifu ulivyo wa muhimu katika mahusiano ya wanandoa, ndivyo ulivyo kati ya mahusiano ya Mungu na mwanadamu. Kama mwanaume asivyotulia mkewe akiwa katika shida na mahangaiko, ndivyo Mungu asivyoweza kunyamaza wala kutulia, mpaka pale haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo kwa Taifa teule la Israeli, hata mataifa waione haki yake, na wafalme wote wauone utukufu wake. Israeli ataitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana Mungu mwenyewe. Jina hilo ni taji ya uzuri.
Nasi tunapokiuka viapo na maagano ya Ubatizo wetu, kwa kuabudu miungu mingine - fedha, mali, cheo, anasa na starehe, tunakuwa makahaba wa kiimani kwa tamaa za kimwili - masuria, vimada na nyumba ndogo, tunaachwa na Mungu. Nabii Isaya anatufariji kwa ujumbe wa matumaini, kwa waliokata tamaa kwa dhambi na kujiona kuwa Mungu hawezi kuwasamehe tena katika uasi wao. Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake. Daima anatukumbusha ahadi zake na mwaliko wake wa kuishi kitakatifu. Anatuambia rudini kwangu. Nitawapa Jina Jipya. Sitawahesabia tena dhambi zenu bali nitawatakasa na kuwafanya watu wangu nami nitakuwa Mungu wenu. Nitawaondolea fedheha ya dhambi na uasi na kuwavika kilemba cha Ufalme na Wokovu kwani mtatawala pamoja na Kristo. Tunaalikwa kumrudia Mungu ili tupewe jina jipya linalopendeza la kuitwa wana wa Mungu, Taifa teule.
Katika somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor12:4-11); Paulo anatufafanulia juu ya zawadi na karama mbalimbali ambazo Roho wa Mungu anatugawia. Karama mbalimbali tulizonazo zina chanzo kimoja – zatoka kwa Roho Mtakatifu. Kila mmoja anajaliza karama na vipawa vyake tofauti na mwingine na hivyo tunakuwa tofuati tofauti. Tofauti hizi zilizopo kati ya mtu na mtu kadiri ya karama tunazojaliwa ni ili kuwe na tofauti za huduma na tofauti za kutenda kazi, lakini lengo ni moja tu - kufaidiana. Kumbe kila mmoja anawajibika kutumia vyema karama na vipawa alivyojaliwa sio kwa manufaa yake tu bali kwa manufaa yake na ya jumuiya ili kila mmoja aweze kunufaika na kuishi kwa furaha, amani na upendo. Ukijaliwa vipawa, karama na baraka nyingi ujue kabisa sio kwa ajili yako tu bali Mungu amekubariki na kukufanya mhudumu wa wengine. Hivyo wajibu wako ni kuhakikisha unazitumia vyema kwa ajili ya manufaa ya jumuiya na watu wake. Ni kwa ajili ya hivyo siku ya hukumu ya mwisho kila mmoja atawajibika jinsi alivyovitumia.
Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn 2:1-12); ni ufunuo wa Umungu wa Yesu Kristo kwa kugeuza maji kuwa divai katika Arusi ya Kana. Kwa mila na desturi ya Wayahudi, katika sherehe ya Arusi jukumu la kuandaa vinywaji (divai) lilikuwa ni la Bwana arusi akisaidiwa na marafiki zake. Katika arusi aliyoihudhuria Yesu vinywaji/divai iliyoandaliwa haikuwatosha – iliisha mapema kabla ya sherehe kufungwa. Bikira Maria, alimweleza mwanye Yesu adha iliyojitokeza. Yesu anachukua jukumu la bwana arusi la kuandaa divai. Kwa kufanya hivyo, anakuwa yeye Bwana arusi na kuwaandalia watu karamu. Hapa unaanza kutimia utabiri wa manabii kuwa Mungu atawafanyia watu karamu; “Katika mlima huu, Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta” (Is.25:6-10). Kama ilivyokuwa katika Agano la kale la mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu kuelezewa kama mahusiano kati ya mume na mke, ndivyo ilivyo katika Agano Jipya. Yesu ni Bwana arusi na Kanisa ni Bi Arusi wake; “Je walioalikwa harusini waweza kufunga wakati Bwana arusi akiwa bado pamoja nao?” – alihoji Yesu. Yeye ndiye Bwana Arusi aliyekuja kumtafuta Israeli – mwanadamu - aliyeachika kwa dhambi ya kuigeukia miungu mingine ili amrudishe kwake. Baada ya kuachika, Israeli – mwandamu- aliishiwa divai, ishara ya huzuni, mateso na mahangaiko. Yeye anamletea divai – furaha na amani - ndiyo neema ya utakaso.
Nasi kila tunapotenda dhambi tunaachwa na Mungu, tunakuwa kama mwanamke aliyeachika kwa kukosa uamifu kwa mume wake. Njia ni moja ya kumfanya Mungu aturudie, atupende na kutujalia neema na baraka zake – kutubu dhambi zetu. Yesu katika sakramenti ya kitubio anatupatanisha na Mungu na kurejeza upya uhusiano kati yetu na Mungu Baba na kutuandalia divai na urojorojo wake ili tunywe kwa furaha na amani. Katika maisha tunapopoteza ladha ya imani tumwombe atuongezee divai, kwa njia ya sala na Sakramenti hasa Kitubio na Ekaristi. Katika Injili ya Yohane, Maria anajitokeza mara mbili tu - katika Harusi ya Kana (Yn 2:1), na chini ya msalaba pale Kalvario - “Mama, tazama mwanao…Tazama mama yako” (Yn 19:25-26). Katika Harusi ya Kana alimwambia Yesu; “hawana divai” kisha akawaambia watu; “Lolote atakalowaambia fanyeni.” Tujifunze kutoka kwake kumtegemea na kumkimbilia Mungu katika magumu yoyote. Tujifunze kwake fadhila ya kimama ya kuona shida za wengine na kuwasaidia. Tumkimbilie Mama Maria tunapotindikiwa na neema na imani ili amnog’oneze mwanae “hawana divai”. Tuwe watu wa sala. Tusikilize ushauri wa Bikira Maria - “Lolote atakalowambieni fanyeni”. Tukitaka kufaulu na kukaa na divai njema wakati wote, tutimize mapenzi ya Mungu nasi tutaishi kwa furaha na amani tele.