Maadhimisho Dominika III ya Neno la Mungu: Habari Njema ya Wokovu
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Katika maadhimisho ya Dominika ya tatu ya mwaka tunaalikwa kuadhimisha Dominika ya Neno la Mungu, Mungu anayekubali kujifunua na kuishi pamoja nasi kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Neno la Mungu linapaswa kuwa taa ya kutuongoza na kutuimarisha katika maisha yetu. Dominika ya Neno la Mungu, kama anavyotualika Baba Mtakatifu Francisko uadhimishwa kila Dominika ya tatu ya Mwaka wa Kanisa kadiri ya Waraka wake wa Kitume wa Aperuit Illis (Akawafungua macho yao) ya Septemba 30, mwaka 2019. Kwa hiyo anatutaka sote, yaani wachungaji na waamini walei, kuona umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya kila mwamini, na pili kuangalia mahusiano ya ndani kabisa ya Neno la Mungu na Maadhimisho yetu ya Kiliturujia na hata yale yanayokuwa siyo ya Kiliturujia. Tunatafakari Injili Takatifu ilivyoandikwa na Luka 1: 1-4, 4:14-21.
Injili ya Luka katika dibaji yake inamtambulisha wazi wazi kuwa mwandishi wake ni mwanahistoria, na hakuwa mmoja aliyemuona au kuishi pamoja na Yesu Kristo wakati wa maisha yake hapa duniani. Ni lengo na shabaha ya Mwinjili Luka kukusanya taarifa zote kwa umakini mkubwa juu ya maisha, lakini hasa mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mwinjili Luka tofauti na wainjili wengine hakubahatika kumwona Yesu kwa macho yake na pia hakuwa Myahudi badala yake ni mtu wa mataifa kutokea Antiokia huko Siria. Na ndio mwinjili Luka anapoandika Injili pamoja na Kitabu cha Matendo ya Mitume anatuonesha kinagaubaga jinsi Injili ilivyoenea kuanzia Yerusalemu mpaka Roma. Hata namna ya uandishi wa Luka unalenga zaidi watu wa mataifa mengine zaidi ya lile la Israeli. Mwinjili Luka anaepuka kutumia zaidi maneno yatokanayo na lugha ya Kiaramayo na badala yake anatumia zaidi Kigiriki, lugha iliyojulikana na kutumika na watu wa mataifa wa nyakati zile waliokuwa chini ya dola la Kirumi.
Mwinjili Luka anatumia mtindo wa uandishi wa nyakati zile, hivyo anaandika Injili yake kwa kuanza na utangulizi unaoonesha nia na shabaha ya uandishi wake. Anamwandikia Teofilo, ni jina la Kigiriki likimaanisha mpendwa au rafiki wa Mungu. Labda tuone japo kifupi ni nani huyu Teofilo na kwa nini anaandikiwa Injili pamoja na Kitabu cha Matendo ya Mitume. Kuna nadharia nyingi kuhusu Teofilo na wapo hata wanasubutu kusema hakuwa mtu aliyeishi katika historia na badala yake ni mtu wa kufikirika maana haiingii akilini Luka kutumia miaka minne akifanya utafiti na kumwandikia mtu mmoja tu Injili pamoja na Kitabu cha Matendo ya Mitume. Na wengine wanasema alikuwa kweli mtu aliyeishi na yawezekana alikuwa ni mwanasheria wakili aliyepaswa kujua vema Habari za Yesu wa Nazareti na hata maisha ya Mtume Paulo ili kuweza kumtetea mteja wake Mtume Paolo aliyekuwa akikabiliwa na mashitaka huko Roma. Ni vile mwanasheria anapaswa kuwa na ushahidi kutoka kwa watu walioshuhudia kwa macho yaliyojiri kabla, na ndicho afanyacho Mwinjili Luka kujaribu kukusanya ushahidi wote kwa wale walioyaona yote kwa macho.
Na hata kuna nadharia nyingine kuwa Teofilo alikuwa ni mtu tajiri aliyefadhili kazi nzima ya uandishi ya Luka. Kama ishara ya shukrani kwake kwa ufadhili huo Mwinjili Luka anaona kuna sababu za kumtaja kwa jina katika Maandiko yake. Kwa hakika leo hii wataalamu wengi wa Maandiko wanatuambia Teofilo ni mtu aliyewahi kuishi kweli katika historia na kwa hakika alikuwa na nafasi muhimu na kubwa kwa Luka mwinjili na hasa kwa Kanisa lile la mwanzo. Luka kama mwandishi msomi anatumia pia aina ya uandishi wa nyakati zake kutaja mtu kama egemeo na mwakilishi wa hadhira yake. Teofilo kama mpendwa wa Mungu ni wewe na mimi! Ni sisi tunaoishi katika mahali na nyakati zetu za leo, tunaosoma Injili ya Luka na Kitabu cha Matendo ya Mitume, ni sisi wafuasi na rafiki zake Yesu wa Nazareti, ambao kwa hakika tunaalikwa kuwa mashahidi wa Habari Njema, ambayo ni Neno la Mungu kwa maisha na matendo yetu.
Na ndio tunaweza kusema Injili ya Luka na Kitabu cha Matendo ya Mitume ni mkusanyiko mzuri kabisa wa Historia ya Ukristo inayoeleza wazi wazi yaliyojiri kwa kipindi chote cha miaka 33 ya Yesu wa Nazareti mpaka kipindi alichokamatwa na kufungwa Mtume Paulo huko Roma. Lakini Mwinjili Luka si tu aliandika kama sehemu ya utetezi na ushahidi kwa mashitaka yaliyomkabili Mtume Paulo ila pia alikuwa na nia kwa ajili ya kutunza kumbukumbu zote muhimu kwa ajili ya vizazi na vizazi na hasa kwa kukuza imani ya waamini, hasa waliokuwa tayari kumpokea Yesu Kristo kama mjumbe wa Habari Njema. Kuenea kwa Habari Njema ya Yesu Kristo kulianza kuleta maswali mengi tangu mwanzoni mwa Kanisa na ndio Mwinjili Luka anaandika na kutueleza sababu za yeye kuandika Injili hii. Ni nia yake kutupa Habari zinazomuhusu Yesu wa Nazareti kutoka kwa wale waliomuona na kushuhudia matendo na mafundisho yake. Hivyo habari hizo sio uzushi au za kutungwa na mwanadamu.
Ni Habari za uhakika na kweli tupu kama ambavyo anaandika pia baadaye Mwinjili Yohane katika Waraka wake wa Kwanza. (1Yohane 1:1-4) Yohane mwinjili anaeleza naye kwa kuwa alimuona na hata kumshika huyu aitwaye Yesu wa Nazareti. Na ndio wanapata ujasiri hata wa kuhatarisha maisha yao ili kushuhudia ukweli umuhusuyo Yesu wa Nazareti. Mwinjili Luka kwa hakika naye anaona kuna haja kubwa ya kuandika yote yaliyojiri hasa kwa ajili ya jumuiya yake. Mwinjili Luka anafanya utafiti wake kwa umakini mkubwa na anatueleza anapata habari zote kwa wale mashuhuda wa kwanza, kwa maana ya watu waliomuona Yesu kwa macho yao. Ni watu walioishi kwa karibu na huyu Yesu wa Nazareti. Hivyo shabaha yake ni kutupa msingi imara waamini kwa Habari zisizokuwa na shaka yeyote. Luka anatupa sababu za kuamini kwetu kama vile hata nyakati zetu kuna wengi wanaokuwa na mashaka juu ya Yesu wa Nazareti. Mwinjili Luka anatupa historia ya kweli yenye ujumbe pia muhimu kwa ajili ya imani yetu. Ni masimulizi ya Kihistoria anayoandika hasa kuimairisha imani kwetu sisi wafuasi na rafiki zake Yesu Kristo wa Nazareti.
Sehemu ya pili ya Injili ya leo tunaona Mwinjili Luka anatupa simulizi la kuanza rasmi kwa kazi yake ya utume Yesu wa Nazareti. Yesu anaanza wazi wazi kazi yake katika kijiji chake cha Nazareti siku ya Sabato. Kwa kawaida Wayahudi walikusanyika katika Masinagogi yao siku ya Sabato ili kusali na kusikiliza Neno la Mungu na maelezo yaliyofuata kufafanua Neno lililosomwa, na hasa walikuwa wanasoma kutoka Vitabu vile vya Sheria au Vitabu vya Musa (Torati) na somo la pili lilitoka kwa Manabii. Kusanyiko hilo la kiliturjia lilianza na kukiri imani na ndio Shemà Israeli, yaani, sikia Israeli na kufuatiwa na baraka 18 kutoka kwa Mungu na ndipo baadaye wakasikiliza masomo kama nilivyoonesha hapo juu. Yesu alichukua gombo na kulifungua ndio kusema Mwinjili Luka anatuonesha kuwa bila Yesu Kristo, Neno la Mungu linakuwa limefungwa, linabaki kuwa mbali nasi, linabaki kutoeleweka kwetu. Hivyo ili kupata kuelewa vema Maandiko Matakatifu hatuna budi kuyasoma kwa kumwangalia Yesu Kristo kama mlengwa mkuu wa Neno hilo.
Na ndio baada ya kulisoma, Mwinjili anatuonesha kuwa watu wote walimkazia macho Yesu wa Nazareti. Ni mwaliko kwetu kila tunaposoma Maandiko Matakatifu kumkazia macho Yesu Kristo kwani bila Yeye hatuwezi kuelewa ujumbe kusudiwa na Mungu kwetu wanadamu. Ni Mungu ananena nasi hivyo hatuna budi kumkazia macho mnenaji ili kupata ujumbe wake. Ni muhusika mkuu katika historia yetu wanadamu. Ni Mungu anayejifunua na kujidhihirisha kwetu kwa njia ya Neno lake, hivyo hatuna budi kufungua macho ya mioyo yetu. Yesu Kristo leo anachagua somo kutoka kitabu cha Nabii Isaya ili kujitambulisha Yeye mwenyewe kuwa ni mjumbe wa Mungu aliyejaa Roho Mtakatifu kuja kutuletea Habari Njema. Kama vile Nabii Isaya anaandika kitabu hiki miaka 400 kabla ya Yesu akionesha Mjumbe wa Mungu anayetumwa kuwafariji watu wake mara baada ya utumwa wa Babeli. Ni katika mazingira magumu mara baada ya utumwa kama tulivyosikia katika somo la kwanza la leo, matajiri waliwanyonya maskini, wenye mashamba hawakulipa ujira wa kufaa kwa watumishi wao, wenye nguvu waliwaonea wanyonge na dhaifu.
Ni katika mazingira ya namna hii Mungu anamtuma mjumbe wake kutangaza mwaka wa neema, mwaka wa upendeleo wa Mungu kwa watu walio wanyonge na maskini. Ni mwaka wa maadhimisho ya Jubilei, ni mwaka wa furaha na shangwe kwani Mungu anakuja na kukaa na watu wake. Na ndio Yesu leo anasema unabii ule umetimia kwake, ni Yeye aliyezungumziwa na Nabii Isaya miaka mingi iliyopita. Ni Yeye mjumbe wa Mungu aliyejaa Roho wa Mungu, aliyetengwa kwa ajili ya kutuletea Habari Njema ya Wokovu, kuja kutuletea upendeleo wa Mungu, Mwaka wa Neema, yaani Kairos.Yesu hajaribu kuelezea maana ya unabii huo wa Isaya badala yake anatuambia unabii huo umetimia katika nafsi ya huyu Yesu wa Nazareti. Nabii Isaya anatumia neno la Kiebrania “deror” kumaanisha hali ya kuwa huru, ni neno linalomaanisha hasa kuwa huru na vifungo vyote vinavyomzuia mtu kutembea kwa haraka au kushindwa kukimbia. Na ndio Neno la Yesu Kristo linatuacha huru kutoka vifungo vyote iwe vya kimwili na hata kiroho. Hakika tunajua tuna vifungo vingi vinavyotufunga na hivyo kushindwa kumpenda Mungu na jirani, ni kwa kupokea Neno la Yesu Kristo na kuliishi hapo tunakuwa huru na vifungo hivyo kama ubinafsi, tamaa ya mali na kutawala na mengi ya aina hiyo yanayokuwa kama minyororo inayotufunga na kushindwa kuishi maisha huru ya wana wa Mungu.
Ni kwa nguvu ya Neno la Mungu na Roho Mtakatifu pekee nasi tunakuwa huru kutoka vifungo mbalimbali katika maisha yetu. Leo tunapoalikwa kuadhimisha Dominika ya Neno la Mungu, hatuna budi kutambua kama anavyotuonesha Mwinjili Luka kuwa Injili ni habari yenye ukweli wa Kihistoria, ni Mungu anayekubali kuingia katika historia ya mwanadamu, kutembea pamoja nasi, ni kwa njia ya Neno la Mungu nasi tunajaliwa kutambua mapenzi na njia za Mungu katika maisha yetu. Hivyo ni kwa msaada wa Neno la Mungu, mimi na wewe tunaweza kutembea katika njia iliyo sawa, katika mwanga wa ukweli. Neno halina budi kujimwilisha katika maisha yetu. Ni kwa njia ya Neno la Mungu linalojimwilisha tunaweza kuwafanya wengine kukutana na Yesu Kristo, na ndio kukutana na Mungu. Kuamini pia Injili, kitenzi neno la Kigiriki linalotumika ni πιστευετε (Pisteuete) ni kuwa na hakika katika HABARI NJEMA, siyo habari ya kubahatisha ni hakika kuwa Mungu anatupenda na anataka kuwa na mahusiano ya upendo na kila mmoja wetu. Ni ahadi ya Mungu aliye daima mwaminifu na hivyo kamwe hatutahadaika na Habari hii njema. Tunaalikwa kuamini Neno lake kwani Yeye daima ni mwaminifu kwetu, hata mara moja hatakwenda wala kutenda kinyume na Neno lake, ni Neno la Mungu linamuakisi Mungu mwenyewe. Na ndio Mwinjili Luka anatuonesha kuwa Injili sio Habari za kufikirika au kutengenezwa na mwanadamu, bali ni Upendo wa Mungu katika historia. Nawatakia tafakari njema ya Habari Njema ya Wokovu na Dominika yenye kila neema na upendeleo wake Mwenyezi Mungu. Neno lake na likae nasi na kutuongoza daima katika kweli yote.