Tafuta

Viongozi wa Kijeshi chini ya uongozi mpya wa “Lieutenant Colonel” Paul-Henri Damiba tarehe 26 Januari 2022 wamekutana na viongozi wa kidini kuelezea msimamo wao. Viongozi wa Kijeshi chini ya uongozi mpya wa “Lieutenant Colonel” Paul-Henri Damiba tarehe 26 Januari 2022 wamekutana na viongozi wa kidini kuelezea msimamo wao. 

Mapinduzi ya Kijeshi Burkina Faso: Tamko la Maaskofu Katoliki B. Faso

Baraza la Maaskofu linafuatilia kwa umakini mkubwa mwenendo wa mapinduzi yaliyofanyika tarehe 24 Januari 2022 kinyume kabisa cha demokrasia na katiba ya nchi ambayo kimsingi ndiyo sheria mama. Viongozi wa kijeshi wanapaswa kujiandaa kikamilifu kukabiliana na changamoto kubwa zilizoko mbele yao: wimbi kubwa la wakimbizi, hali ngumu ya kiiuchumi na umoja wa Kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Viongozi wa Kijeshi chini ya “Lieutenant Colonel” Paul-Henri Damiba, waliompindua na kumwondoa madarakani Rais Faso Roch Kaboré wa Burkina Faso pamoja na wenzake, Jumatano tarehe 26 Januari 2022 wamekutana na kuzungumza na viongozi wa kidini nchini Burkina Faso. Lengo lilikuwa ni kuelezea mambo msingi yaliyopelekea hata Jeshi likaamua kufanya mapinduzi na kumwondoa Rais Faso Roch Kaboré kutoka madarakani. Viongozi wa kijeshi wanasema, tatizo kubwa ni usalama wa raia na mali zao, pamoja na kukosa rasilimali fedha na vifaa ili kupambana na wimbi kubwa la mashambulizi ya kigaidi yaliyokuwa yanatendeka nchini mwao. Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso na Niger katika tamko lao, linasema, Baraza la Maaskofu linafuatilia kwa umakini mkubwa mwenendo wa mapinduzi yaliyofanyika tarehe 24 Januari 2022 kinyume kabisa cha demokrasia na katiba ya nchi ambayo kimsingi ndiyo sheria mama. Viongozi wa kijeshi wanapaswa kujiandaa kikamilifu kukabiliana na changamoto kubwa zilizoko mbele yao ikiwa ni pamoja na wakimbizi na wahamiaji kutoka Burkina Faso ambao kwa sasa wanataka kujerea katika makazi yao ambayo tayari yanakaliwa na watu wengine, kinyume cha sheria.

Ujumbe wa Maaskofu Katoliki Burkina Faso: Umoja, Upatansho na maendeleo ya wengi
Ujumbe wa Maaskofu Katoliki Burkina Faso: Umoja, Upatansho na maendeleo ya wengi

Changamoto kubwa kwa wakati huu ni mchakato wa upatanisho wa kitaifa ili kujenga umoja na udugu wa kitaifa bila kusahau kuchechemea kwa uchumi. Changamoto zote hizi zinahitaji ushiriki mkamilifu wa wananchi wote wa Burkina Faso wanasema, Maaskofu Katoliki nchini Burkina Faso na Niger. Maadhimisho ya Siku ya 52 ya kuombea amani duniani kwa Mwaka 2019 yaliongozwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani.” Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu Francisko alikazia Injili ya amani; changamoto katika siasa safi; upendo na fadhila zinazoweza kudumisha siasa safi kwa ajili ya haki msingi za binadamu na amani duniani. Aligusia maovu ya wanasiasa na umuhimu wa siasa safi katika kudumisha ushiriki wa vijana pamoja na hali ya kuaminiana: umuhimu wa kukataa kishawishi cha vita na sera vitisho na umuhimu wa kudumisha amani duniani! Siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi yanayowashirikisha wadau mbalimbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani.

Kumbe, viongozi wa Burkina Faso waliojitwalia madaraka watambue kwamba, uongozi ni huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Burkina Faso. Huu ni wakati wa kujipanga kikamilifu ili kuhakikisha kwamba, viongozi walioingia madarakani wanajipanga vyema, ili kutekeleza matamanio halali ya watu wa Mungu kutoka Burkina Faso. Kwa viongozi waliopinduliwa kutoka madarakani, wahakikishiwe usalama wa maisha; walindwe na utu wao uheshimiwe. Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso katika kipindi hiki kigumu, wanawaombea viongozi walioko madarakani, hekima na busara, ili hatimaye, kipeo hiki kiweze kumalizika na hatimaye, watu wa Mungu Burkina Faso waweze kupata amani ya kudumu. Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso na Niger linapenda kuwaweka watu wa Mungu nchini Burkina Faso chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa Amani na ya Mtakatifu Yosefu Mlinzi na Mwombezi wa Kanisa, waweze kuwasindikiza watu wa Mungu nchini Burkina Faso katika kipindi hiki kigumu wanachotafuta haki, amani, upatanisho na umoja wa Kitaifa. Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso na Niger limetolewa na Askofu Laurent B. Dabire wa Jimbo Katoliki la Dori.

Viongozi wasikilize matamanio halali ya watu wa Mungu
Viongozi wasikilize matamanio halali ya watu wa Mungu

Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba, mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso ni matokeo ya wananchi kutoridhishwa na mwenendo wa hali ya usalama kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yaliyosababishwa na vikundi vya kigaidi nchini humo. Kuna zaidi ya watu 2, 000 ambao wamepoteza maisha kwa kushambuliwa na vikundi vya kigaidi. Wananchi zaidi ya milioni 1 na nusu wameyakimbia makazi yao. Wananchi wamekuwa wakishambulia kambi za kijeshi kuomba msaada wa chakula. Vitendo vya kigaidi vinahatarisha sana mustakabali wa umoja wa Kitaifa, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Burkina Faso. Demokrasia imefifia sana, kiasi cha kuwacha mwanya kwa wanajeshi kujitwalia madaraka. Inasikitisha kuona kwamba, utawala wa “Mababe wa Kijeshi Afrika ya Magharibi” unarejea kwa kasi kubwa.

Burkina Faso
28 January 2022, 14:53