Tafakari ya Neno la Mungu Sherehe ya Epifania, Tokeo la Bwana: Waamini waongozwe na nyota ya imani ili kwenda kumwona na kumsujudia Kristo Yesu: Kuhani mkuu, Mfalme na Mkombozi. Tafakari ya Neno la Mungu Sherehe ya Epifania, Tokeo la Bwana: Waamini waongozwe na nyota ya imani ili kwenda kumwona na kumsujudia Kristo Yesu: Kuhani mkuu, Mfalme na Mkombozi. 

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Imani Iwaongozwe Waamini Kumwona Kristo Yesu

Mamajusi walipomwona na kumtambua Kristo Yesu, Mwana wa Mungu walipiga magoti wakamsujudia, wakafugua zawadi zao, wakampa: Dhahabu ikiwa ni ishara ya ufalme wake, Ubani alama ya Ukuhani na Umugu wake, na Manemane - mafuta ya kupaka maiti kwa ajili ya maziko, ishara kuwa Yesu atajitoa sadaka, kuteswa na kufa kwa ajili ya dhambi zetu ili tupate kukombolewa. Imani.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Tokeo la Bwana - Epifania. Sherehe hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 06 Januari, lakini kwa sababu za kichungaji yaweza kuadhimishwa jumapili ya karibu ili waamini wengi waweze kushiriki na kutambua maana yake. Neno Epifania asili yake ni lugha ya Kigiriki, likimaanisha kutokea, kujionesha au kujifunua. Katika Sherehe linatumika kumaanisha kujifunua kwa Mungu mbele ya watu wa mataifa – wapagani- watu wasio wayahudi wakiwakilishwa na mamajusio - wataalamu wa elimu ya nyota waliotafuta ukweli wa mambo kupitia elimu ya nyota. Hawa walipoiona nyota ya pekee angani, walikumbuka utabiri wa Nabii Mika kwamba; Masiha atakapozaliwa itatokea nyota ya pekee mashariki - nao wakaifuata mpaka alikozaliwa mtoto Yesu. Nao walipomwona, walimtambua na kumkiri kuwa ndiye Mfalme, Kuhani na Mkombozi wa mataifa yote. Sala ya mwanzo katika sherehe hii ni mhutasari wa kile tunachokisherehekea kama anavyosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini akisema; Ee Mungu, uliyewafumbulia mataifa siku ya leo Mwanao wa pekee wakiongozwa na nyota, utujalie kwa wema sisi tuliokwisha kukutambua kwa imani, tuongozwe mpaka tuuone uso wako mtukufu.

Katika somo la kwanza Nabii Isaya (Isa 60:1-6), anatabiri kujifunua kwa Mungu kwa mataifa yote kupitia taifa lake teule la Israeli akisema kwamba; utukufu wa Bwana utakuja na kuiangaza Yerusalemu wakati huo kutakuwa na giza katika mataifa mengine ili watu waione hii nuru na kuja kuishujudia. Mataifa, wafalme na watu toka pande zote za dunia watakuja na kukusanyika ili waangazwe na hii nuru nao watamsujudia Bwana kama kiitikio cha wimbo wa katikati kinavyoimba; “Mataifa yote ya ulimwengu watakusujudia ee Bwana” (Zab. 72:11). Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Waefeso (Efe 3:2-3, 5-6), anadhibitisha utabiri wa Nabii Isaya kuwa; ahadi ya kuletewa mkombozi Yesu Kristo, haikuwa kwa ajili ya Waisraeli tu, bali ni kwa ajili ya mataifa yote. Paulo anasema kwamba yeye alifunuliwa na kujulishwa siri hii kwamba; “Mataifa ni warithi pamoja nasi (wayahudi) wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja wa ahadi yake Mungu iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili”.

Injili ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 2:1-12), ina wahusika mbalimbali ambao wanatuwakilisha kila mmoja wetu kwa nafasi yake anavyoishi. Wahusika wa kwanza ni Herode kibaraka wa Warumi – wakoloni wa enzi hizo na maaskari wake. Huyu ni mtu katili, mbinafsi na aliyelinda cheo chake kwa gharama yoyote, hata ikibidi kutoa uhai wa wengine. Aliposikia amezaliwa mfalme wa wayahudi “alihuzunika yeye pamoja na Yerusalemu pia”, na baaada ya kuona mamajusi hawakurudi kwake kumpasha habari yu wapi mtoto aliyezaliwa, alikasirika na akaanza mpango wa kumuangamiza Mtoto Yesu kwa kuamrisha wauawe watoto wote wa kiume waliozaliwa kipindi hicho. Matokeo ya chuki na hasira hiyo ni mauaji ya watoto watakatifu mashahidi ambao Kanisa linawakumbuka kila 28 desemba kila mwaka. Katika masomo ya siku hiyo utabiri wa nabii Yeremia unaosema; “Bwana asema hivi sauti imesikika Rama, kilio na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, asikubali kufarijiwa kwa kuwa hawako” ulitimia (Yer 31:15-16).

Tunaweza kushangaa ukatili huu wa Herode. Lakini, tujiulize, Je, sisi nasi hatujawahi kuhatarisha, kutishia, au hata kutoa uhai wa wengine tena wasio na hatia kama watoto ili kulinda nafasi au heshima zetu? Hatujawahi kuwatakia wengine mabaya ili washindwe na sisi tuchukue nafasi zao? Ni mara ngapi tumesababisha madhara kwa wengine kutokana na nafasi tulizonazo? Ukiwa ofisini, unatumiaje cheo chako? Kama mwalimu, karani, mwandishi wa habari, mwanjeshi, daktari au yeyote yule unatumiaje taaluma, weledi, ugwiji na ujuzi wako? Je, unautumia kuangamiza maisha na kutoa uhai kwa wasio na hatia, hasa wany’onge ili kulinda nafasi yako au heshima yako. Mara ngapi tumeshiriki katika mauaji ya watoto madhalani kwa utoaji mimba, au kutumia dawa za kuzuia mimba, kuwachukua, kuwauza au kuwafanyisha wengine biashara haramu za ngono, au hata kazi yoyote halali kwa mda mrefu lakini mshahara kiduchu ili asiwe na pa kwenda abaki kwako? Mara ngapi tunazima nguvu ya Kristo na Kanisa lake pale ambapo anasa, starehe, kiu ya mali, cheo na sifa vinatufanya tusishiriki Ibada siku za Jumapili, tusilishike Neno la Mungu, tusishiriki jumuiya, au tusipokee sakramenti? Mara ngapi tumemtumikia shetani kwa mambo ya ushirikina na uchawi kwa kuwatoa wapendwa wetu kafara? Je, hatujawahi kuwa kama maaskari wa Herode, ambao wanatii amri na kufanya mauaji ya kinyama? Basi na tupige magoti kwa moyo wa majuto, tutubu dhambi hii, tumlilie Mungu, tumuombe msamaha, naye ni mwingi wa huruma atatusamehe.

Wahusika wa pili ni Makuhani na Waandishi, hawa wanajua mengi juu ya Kristo, ila Kristo kwao si chochote, hana maana kwa maisha yao. Wanafahamu tu kuwa atazaliwa Betlehemu yatosha. Je, sisi nasi tuliobatizwa na kupata mafundisho ya imani yetu na kuyafahamu, ukristo wetu haujabaki wa jina tu? Je, imani yetu si moto wala si baridi? Je, hatuzidharau sakramenti hasa kitubio na Ekaristi Takatifu kwa dhamani ya starehe, anasa na tafrija za dunia hii? Basi na tupige magoti kwa moyo wa majuto, tutubu dhambi hii, tumlilie Mungu, tumuombe msamaha, naye ni mwingi wa huruma atatusamehe. Wahusika wa tatu ni Mamajusi. Biblia haitaji majina yao wala nchi walikotoka. Lakini wataalamu wa historia ya maandiko matakatifu wanataja majina yao na nchi walizotoka; Melkiori kutoka Uturuki, Baltazari kutoka Mongolia na Gaspari kutoka Ethiopia; kila mmoja peke yake akitokea katika nchi yake, walikutana njiani wakaamua kwa nia moja kuifuata ile nyota ili kumtafuta Masiha. Hatari, uchovu na urefu wa njia havikuwakatisha tamaa, mpaka wakafike alikokuwa mtoto Yesu.

Mamajusi walipomwona na kumtambua Mwana wa Mungu walipiga magoti wakamsujudia, wakafugua zawadi zao, wakampa: Dhahabu ikiwa ni ishara ya ufalme wake, Ubani alama ya Ukuhani na Umugu wake, na Manemane - mafuta ya kupaka maiti kwa ajili ya maziko, ishara kuwa Yesu atajitoa sadaka, kuteswa na kufa kwa ajili ya dhambi zetu ili tupate kukombolewa. Hata wanawake walibeba manemane wakienda kaburini kumpaka Yesu kama asemavyo mwinjili Marko, “Maria Magdalena, Salome na Maria mama yake Yakobo walinunua manukato ya manemane ili wakaupake mwili wa Yesu” (Mk.16:1). Kumbe tunu au zawadi ambazo mamajusi walizomtolea mtoto Yesu zilikuwa ni ishara ya kuanza kutimia kwa utabiri wa manabii wa yeye kumkomboa mwanadamu ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu katika sherehe hii padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali; Ee Bwana, tunakuomba utazame kwa wema dhabihu za Kanisa lako. Siyo dhahabu, ubani na manemane vinavyotolewa sasa, ila yule ambaye kwa dhabihu hizi tunamtangaza, tunamtoa sadaka na kumpokea, yaani Yesu Kristo.

Mamajusi ni mfano wa kuigwa wa namna ya kumtafuta, kumfuasa, kumwabudu na kumshuhudia Yesu Kristo katika maisha yetu. Mamajusi ni Ishara ya Wakristo waliompokea Kristo na kumfanya sehemu ya maisha yao. Hawa ndio wanaotualika katika wongofu, sala na malipizi kwa ajili ya nafsi zetu na ulimwengu. Tumtafute Kristo kama Mamajusi walivyofanya. Wao ni ishara kwa kila mtu anayemtafuta Mungu kwa moyo wote. Maisha yote ya mkristo ni safari ya kumtafuta Mungu. Njia ya safari hii ina milima na mabonde, inachosha na mitego ya adui ni mingi. Lakini tukiwa na imani na udumifu kama mamajusi, tusipokata tamaa tutafika. Tusitetereke na shida au ugumu wa safari ya maisha, wala tusipoteza imani. Lengo letu daima liwe ni kumwona mfalme baada ya maisha haya. Tufuate mfano wa mamajusi ambao walikabiliana na magumu, walisafiri umbali mrefu hadi wakamwona mtoto Yesu. Safari yao inawakilisha safari ya maisha yetu ya kumfuasa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunapokutana na Kristo katika neno lake, na katika Ekaristi Takatifu, ni lazima tuongoke, turudi nyumbani kwa njia nyingine kama mamajusi - tuwe watu wapya - tukiwa tumeuvua utu wa zamani – dhambi -  na kuuvaa utu mpya – neema ya utakaso. Hiyo ndiyo zawadi yetu ya pekee na ya dhamani kwa Mtoto Yesu.

Mamajusi waliongozwa na ishara ya nyota kumtafuta mtoto Yesu. Nyakati zetu, Kanisa ndilo ni Ishara ya uwepo wa Kristo ulimwenguni. Kanisa ni kama nyota inayowaongoza watu kwa Kristo. Ni wajibu wa kila mkristo kuwa nyota ya kuwaelekeza wengine katika maisha ya upendo, haki, na amani - kwa maneno na matendo yetu watu wamtambue Kristo. Tuige mfano wa Mtakatifu Yosefu ambaye alikuwa mtu wa haki, mpole na mkimya, wala hasikiki akilalamika wa kunung’unika bali katika upole wake na ukimya wake anasikiliza sauti ya malaika na kutekeleza kile alichoambiwa tangu siku ya kwanza alipoambiwa asiogope kumchukua Bikira Maria kama mke wake, alipoambia amchukue mtoto na mama akimbilie Misri na alipoambiwa amchukue na kurudi tena Yerusalemu na njiani anaagizwa asiende Yerusalemu bali Nazarethi. Tuombe neema na baraka zake ili nasi tuweze kuisikia na kuifuata sauti ya Mungu ili ituangaze katika nuru ya kweli kama tunavyosali katika sala baada ya komunio tukisema; Ee Bwana, tunaomba ututangulie daima na popote kwa nuru yako ya mbinguni; na hili fumbo ulilolitaka kutushirikisha, tulitambue waziwazi na kulikubali kwa upendo. Tumsifu Yesu Kristo.

Epifania
03 January 2022, 16:16