Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo katika maisha ya Wakristo wanaoshiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii ili kutangaza Injili na kushiriki ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo katika maisha ya Wakristo wanaoshiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii ili kutangaza Injili na kushiriki ujenzi wa Ufalme wa Mungu. 

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Ubatizo: Maji na Roho Mtakatifu

Sikukuu hii ya Ubatizo wa Bwana inatukumbusha uhusiano uliopo kati ya dhambi ya asili ambayo kwayo tulipoteza neema ya utakaso ndani mwetu - na Sakramenti ya ubatizo ambayo kwayo tunarudishiwa neema ya utakaso ndani mwetu kwa kuzaliwa mara ya pili, kwa njia ya maji na Roho Mtakatifu (Yn 3:5). Sakramenti ya ubatizo inatuondolewa dhambi ya asili na dhambi nyingine.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu katika Sherehe ya Ubatizo wa Bwana Mwaka C wa Kiliturujia katika Kanisa kama tunavyoimba katika wimbo wa mwanzo; “Bwana alipokwisha kubatizwa, mbingu zikamfunukia, Roho akashuka kwa mfano wa hua, na kukaa juu yake; na tazama, sauti ya Baba ikasema: Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” Ni siku ya kukumbuka ubatizo wetu ulio kiini cha Ukristo wetu ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu Baba, tunapozaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu na kufanywa kuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa, na kuwa washiriki katika ufalme, ukuhani na unabii wa Kristo kama anavyosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini katika sala ya mwanzo; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ulimtangaza rasmi Kristo kuwa ndiye Mwanao mpenzi hapo alipobatizwa katika mto Yordani na kushukiwa na Roho Mtakatifu. Utujalie sisi ulitufanya wanao tulipozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu tudumu siku zote katika upendo wako.” Itakumbukwa kuwa adhimisho la sherehe ya Tokeo la Bwana – Epifania - linahitimisha kipindi cha cha noeli. Kumbe Sikukuu ya ubatizo wa Bwana inaadhimishwa katika dominika ya kwanza ya Mwaka katika kipindi cha kawaida. Kipindi cha kwaresma kitafuata baada ya wiki tano hadi tisa za kipindi cha kawaida kinachofuata baada ya kipindi cha Noeli.

Sehemu hii ya kwanza ya kipindi cha kawaida cha mwaka wa kanisa kinaishia jumatano ya majivu tunapoanza kipindi kwa Kwaresima. Kipindi cha pili cha kawaida cha mwaka wa kanisa kinaanza baada ya sherehe ya pentekoste inayohitimisha kipindi cha Pasaka. Sikukuu hii ya Ubatizo wa Bwana inatukumbusha uhusiano uliopo kati ya dhambi ya asili – kosa la Adamu na Eva ambayo kwayo tulipoteza neema ya utakaso ndani mwetu -  na Sakramenti ya ubatizo ambayo kwayo tunarudishiwa neema ya utakaso ndani mwetu kwa kuzaliwa mara ya pili, kwa njia ya maji na Roho Mtakatifu (Yn 3:5). Kumbe Sakramenti ya ubatizo inatuondolewa dhambi ya asili na dhambi nyingine pamoja na adhabu zake zote na tunafanya upya watoto wa Mungu na wa Kanisa. Somo la kwanza la Nabii Isaya (Isa 42:1-4, 6 -7), ni utabiri wa wasifu wa mtumishi wa Mungu. Mtumishi huyu ni mteule wa Mungu, ambaye nafsi yake imependezwa naye. Mtumishi huyu atayafunua macho ya vipofu na atawatoa gerezani wale waliyofungwa. Ni utabiri wa matumaini kwa jamii ya wanadamu iliyo katika kifungo cha dhambi, inayoishi gizani dhambi. Wanadamu hao ni wale waliyopoteza neema ya utakaso kwa dhambi ile ya kwanza, dhambi ya asili.  Hawa ni watu waliyojitenga na Mungu.

Mtumishi huyu ndiye Mwana pekee wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu ambaye tunasherehekea ubatizo wake. Nabii Isaya alitabiri ujio wake, na Mungu anamtambulisha baada ya kubatizwa kwake kwa sauti iliyotoka katika wingu ikisema; Huyu na Mwanangu mpedwa, ninayependezwa naye, msikilieni yeye. Katika somo la pili la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 10:34-38), Mtume Petro anakiri upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote akisema: “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. Alimtuma Kristo kuwaponya watu wote walioonewa na Ibilisi kwa kumtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu baada ya ubatizo wa Yohane”. Kanisa la mwanzo lilihoji na kulumbana juu ya Ubatizo wa wapagani. Chini ya uvuvio wa Roho Mtakatifu Petro anasema wokovu ni kwa wote. Sisi sote ni sawa mbele ya Mungu kwani. Tumeumbwa kwa Sura na Mfano wa Mungu. Sote ni Hekalu la Roho Mtakatifu. Tumekombolea kwa Damu Azizi ya Kristo. Kristo alienda huku na huko akihubiri Habari Njema ya Ufalme wa Mungu, akitenda maajabu, akiponya wote bila kubagua, na Mungu alikuwa naye.

Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 3:15-16, 21-22), inatueleza habari za ubatizo wa toba uliotolewa na Yohane Mbatizaji mtoni Yordani. “Mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto” – anasisitiza Yohane. Mwinjili Luka anasimulia kuwa; Baada ya watu wote kubatizwa, wa mwisho kubatizwa ni Yesu. Hii ni kutuonyesha kuwa alifunga ubatizo wa toba naye akazichukua dhambi za watu wote waliotubu na kupokea ubatizo huo. Baada ya kubatizwa kwake, Yesu alisali na kuomba hata mbingu zikafunuka, Roho Mtakatifu akamshukia juu yake kwa mfano wa hua na sauti ya Mungu kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu, nimependezwa nawe.” Kwa tukio hili, Mungu alijinua na kujidhihirisha katika nafsi zake tatu – Mungu Baba kwa sauti yake, Mungu Roho Mtakatifu katika mfano wa hua, na Mungu Mwana katika nafsi ya Kristo. Ubatizo ni wa muhimu na wa lazima kwa sababu ni agizo la Yesu mwenyewe: “Enendeni duniani kote mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu na kuwafundisha yote niliyowaamuru ninyi, natazama mimi nipo nanyi mpaka mwisho wa dahari” (Mt. 28:19-20).

Ubatizo wa Yesu ulifungua mbingu, Roho Mtakatifu akashuka na Mungu kuongea nasi. Ubatizo ni mlango wa kuingilia mbinguni – “Kamwe usipozaliwa kwa mara ya pili kwa Maji na Roho Mtakatifu hutaingia kamwe katika uzima wa milele” - Yesu anamwambia Nikodemo (Yoh 3:3).  Kama ilivyotokea kwa Yesu siku ya ubatizo, sisi nasi wakati wa Ubatizo wetu tulimpokea Roho Mtakatifu na sauti iliyomshuhudia Yesu ikisema; huyu ni mwanangu mpendwa, nipendezwaye naye, ilitushuhudia hata sisi. Mungu alipendezwa nasi, kwasababu tuliamua kumkana na kumkataa shetani na fahari zake zote na tukaamua kujiunga katika familia ya watoto wa Mungu na ukoo wa kifalme, taifa teule la Mungu na kuwa hekalu la Roho Mtakatifu. Kwa ubatizo tunashuhudia na kukiri hadharani ufuasi wetu kwa Kristo. Kwa ubatizo tunapokolewa ndani ya Mwili wa Kristo ambao ndilo Kanisa (1Kor 12:13). Kwa ubatizo tunakubali kufa kuhusu dhambi, kuzikwa na kufufuka ndani ya Kristo (Rum 6:4-11 Kol. 2:12). Mbingu ilishafunguliwa kwa ajili yetu sisi kwa mateso, kifo na ufufuko wake Kristo ili sisi tuweze kumfikia Baba yetu wa Mbinguni.

Tusijifungie mbingu sisi wenyewe kwa dhambi zetu. Tupiganie kumpendeza Mungu daima kwa kuziishi ahadi zetu za ubatizo tukiongozwa na amri zake Mungu na za Kanisa. Pale tunaposhindwa kuishi atakavyo Mungu, tuchukue hatua tufanye toba ya kweli naye Mungu atatusamehe na kutujaza neema zake. Basi tunapoadhimisha sikukuu hii ya ubatizo wa Bwana, tunakumbushwa kuziishi vema ahadi za ubatizo wetu na wajibu tulionao kwa jirani zetu, kuulinda, kuutetea, kuuthamini, na kuutunza uhai na utu wetu tukiwa wakristo taifa teule la Mungu, watu tuliochaguliwa kuwa urithi wake Mungu. Imani yetu kwa Kristo iwe ya daima, wakati wa raha, taabu, dhiki, kiu, magonjwa, shida, taabu na katika afya njema. Kwa kuishi hivi Mungu ataendelea kupendezwa nasi, na sala tunayosali baada ya komunyo tukisema: “Ee Bwana, sisi uliotushibisha mapaji matakatifu tunakuomba sana rehema yako, tupate kumsikiliza kwa imani Mwanao wa pekee, tuweze kweli kuitwa na kuwa wanao,” itakuwa na maana na matunda yake tutayaona.

Ubatizo wa Bwana
05 January 2022, 16:08