Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Mwanzo wa Maisha Mapya Katika Kristo Yesu
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Somo la Injili ya Dominika ya Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo, Lk 3:15-16, 21-22, linaanza na maneno yanayoonesha kuwa watu walikuwa wanasubiri, na hivyo kujiwa na swali ni nini hasa walikuwa wanasubiri? Tunaweza kirahisi kusema mtumwa alisubiri uhuru wake, maskini alitarajia mabadiliko ya hali yake na kuwa njema zaidi, waliokosa haki walisubiri haki, walio wagonjwa walisubiri kupona, walioteseka na kudharauliwa walisubiri kurudishiwa tena utu wao, na kadhalika na kadhalika. Ni zaidi ya miaka mia tatu, mbingu zilifungwa kwa maana hakukuwa na sauti ya kinabii kutoka juu, Mwenyezi Mungu aliacha kutuma manabii kwa watu wake kwa sababu ya uasi na madhambi yao. Dini haikuwapa watu furaha na badala yake ikawa chanzo cha hofu na uoga na mahangahiko kwa watu. Ni katika muktadha huu watu wanasubiri na kungoja kwa hamu mabadiliko katika maisha yao na hasa katika mahusiano yao na Mungu. Taifa la Israeli lilikuwa kama kundi lisilo na mchungaji (Marko 6:34), watu walimsubiri na kumngoja Masiha na ndio wanashawishika kudhani kuwa ni Yohane Mbatizaji. Kinyume na lugha ya kutisha anayotumia Yohane Mbatizaji na hata walimu au marabi wa nyakati zile, Yesu Kristo kinyume chake alikaa na kula pamoja na wadhambi, aliwashika wakoma, alimtetea mwanamke aliyekutwa katika kuzini, hakuwafukuza wadhambi bali zaidi aliwaacha na kuwaruhusu kubusu miguu yake.
Ni kwa ujio wa Yesu zinakoma zama zile za kuona Mungu ni mkatili na mwenye kisasi kwa watu wake, ni moto ulao na kuangamiza, ni hakimu asiye na huruma kwa yeyote anayekwenda kinyume na amri na mapenzi yake. Yesu Kristo anafunua sura halisi ya Mungu. Mungu anatuma moto wake ulimwenguni sio kutuangamiza wana wake bali kuangamiza dhambi na yule mwovu anayeharibu mahusiano yetu na Mungu na jirani. Ni Mungu anakuja ili sote tupate uzima wa kweli, na ndio uzima wa milele. Katika Maandiko Matakatifu mara nyingi wanapotaja mahali fulani mathalani bahari, mlima, jangwa, Galilaya ya Mataifa, Samaria, Mto Yordani na kadhalika, waandishi si tu wanataja eneo au mahali husika Kijiografia, bali pia wanataka pia kuleta ujumbe wa Kitaalimungu. Wakati Mwinjili Luka hataji ni wapi hasa ulifanyika ubatizo wa Yesu Kristo, ila Yohane anataja kuwa ulifanyika Betania, ng’ambo ya Yordani. (Yoh. 1:28). Na sehemu hiyo pia inajulikana kama Betabàra, ambapo ndipo Yoshua aliwaongoza wana wa Isreali na kuingia katika nchi ile ya ahadi wakivuka mto Yordani. Hivyo, kuwa Ubatizo wa Yesu umefanyika sehemu hiyo ni kutaka kuonesha jinsi anavyoongoza ulimwengu kuvuka kutoka utumwa wa dhambi na kuanza maisha mapya katika ya kutembea katika mwanga na uhuru wa wana wa Mungu.
Betabàra pia kijiografia ni sehemu iliyo chini yaani ni mita 400 chini ya usawa wa bahari, na hivyo kuonesha kuwa Yesu Kristo ameshuka kutoka mbinguni il kumwokoa mwanadamu aliyechini kabisa katika maisha ya dhambi. Ni kuonesha upendo wa Mungu kwa watu wake, kuwa Mungu anajishusha chini kabisa tunavyoweza kufikiri na kudhani ili kumkomboa kila mwanadamu kutoka katika hali duni na ya dhambi ili tufanyike wana wa Mungu. Ubatizo wa Yesu haukuwa kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, bali ni upendo wa Mungu anayetaka kutembea na kuambatana nasi wadhambi na wakosefu, kumbe Yesu anataka kufanya safari ya Kisinodi pamoja na mwanadamu, pamoja na Kanisa lake. Ni Ubatizo unamuonesha Mungu anayeingia katika safari na historia ya ukombozi wa mwanadamu. Ni Mungu anayejishusha na kusafiri nasi. Safari ya ukombozi ni safari ya Kisinodi pamoja na Mungu mwenyewe kati yetu, pamoja na kila mmoja wetu.Wakati Yohane Mbatizaji alibatiza kwa maji, yaani kwa maondoleo ya dhambi na toba, Yesu Kristo anakuja kubatiza kwa Roho Mtakatifu, ni ubatizo unaotufanya zaidi ya maondoleo ya dhambi pia kufanyika wana wa Mungu na warithi pamoja na Yesu Kristo, ni kuzaliwa upya katika roho.
Ubatizo wa Yesu Kristo ni zawadi kwetu kwani ni Mungu anayetujalia maisha yake ya Kimungu, ndio neema ile ya utakaso, neema inayotufanya kushiriki uzima wa milele. Ubatizo ni zawadi ya upendo mkubwa usi ona kipimo Mungu kwa mwanadamu. Mwinjili Marko tofauti na Matayo na Luka yeye hatupi masimulizi juu ya kuzaliwa na utoto wake Yesu Kristo. Ni mara ya kwanza hapa anaeleza kuwa wakati zile alikuja Yesu kutoka Nazareti ya Galilaya. Mwinjili Marko hatutajii umri wake Yesu wala familia yake zaidi ya kutuonesha jinsi, lini na wapi alivyoanza kazi yake hadharani ya kuhubiri Habari Njema ya wokovu. Yesu anaanza utume wake pale Yordani. Mwinjili Luka hatuoneshi kinagaubaga hasa simulizi la Ubatizo wake Yesu Kristo, bali hasa nini kilichojiri baada ya Ubatizo huo. Ndio kufunguka kwa mbingu, kushuka kwa Roho Mtakatifu na sauti kutoka juu. Ni nia ya Mwinjili Luka kutuonesha kuwa Yesu Kristo naye alibatizwa kama watu wengine, na ndio Injili ya Luka ni Injili ya Huruma ya Mungu, tangu mwanzo Yesu Kristo anajipambanua pamoja na wadhambi, anatembea na kuambatana nao, anakaa na kula nao. Ni ishara ya kutembea nao ili kuwaonesha maisha mapya ya uhuru wa wana wa Mungu. Ni Yesu anakuwa pamoja nasi kutuonesha Njia ya kwenda kwa Baba. Maisha ya ufuasi ni safari ya Kisinodi pamoja na Mungu mwenyewe kati yetu.
Mwinjili Luka pia leo anakazia juu ya nafasi na umuhimu wa sala katika utume wa Yesu Kristo. Yesu Kristo sio tu kama mfano kwetu bali naye alihitaji kusali ili kujua mapenzi ya Baba yake katika utume wake wa kuukomboa ulimwengu. Yesu Kristo kadiri ya Mwinjili Luka anatuonesha anasali hata mwanzoni mwa utume wake na ndio Roho Mtakatifu anamshukia katika umbo lile la njiwa, anasali kabla ya kuwachagua wale wanafunzi wake wa karibu kabisa yaani mitume, anasali kabla ya mateso yake na hata akiwa pale juu Msalabani. Kusali ni kitendo cha mahusiano na Mungu, ni majadiliano na mazungumzo na Mungu, ni katika kusali tunaonesha upendo wetu wa dhati kwa Mungu. Yesu Kristo anayetoka katika kijiji cha Nazareti ya Kiyahudi, sehemu ambayo waliishi pia watu wa mataifa mengine au wapagani, hivyo haikuwa inahesabika kama sehemu ya heshima katika dini ya Kiyahudi, ndiko anakotoka Yesu. Na zaidi anashuka na kufika Yordani na kujiunga na watu waliofika pale kupokea Ubatizo wa toba. Yesu anajipambanua pamoja na wapagani na wadhambi, na labda hilo nalo linatuletea maswali mengi. Na ndio hapo tunakutana na Mungu anayetupenda na kushuka na kukaa kati yetu na kufanana nasi isipokuwa dhambi.
Ni Mungu amemtuma Mwanaye wa pekee kuja ulimwenguni, ili atukumboe kutoka utumwa wa dhambi na kuujenga ulimwengu mpya yaani ufalme wa Mungu hapa duniani. Na ndio waandishi wote watatu wa Injili ndugu yaani Matayo, Marko na Luka wanatuonesha ishara tatu katika Ubatizo wa Yesu Kristo, yaani, kufunguka kwa mbingu, njiwa na sauti kutoka juu. Wakati kwa wainjili Matayo na Luka watu wote waliokuwepo pale waliona na kutafakari juu ya mbingu zilizofunguka na kuona Roho akishuka kwa mfano wa njiwa na kusikia sauti, kwa Mwinjili Marko badala yake ni Yesu mwenyewe alipotoka katika maji akaona mbingu zikifunguka na kusikia sauti, na hivyo kuwa ndio wakati ambapo anapokea kwa namna ya pekee misheni yake. Mbingu kufunguka; Katika Maandiko Matakatifu, ishara hii ya kufunguka kwa mbingu inazungumziwa pia na Nabii Isaya. Wanawaisraeli walielewa vema lugha hii ya kufunguka kwa mbingu kwani daima Mwenyezi Mungu alikuwa anatuma wajumbe wake kuongea na watu wake. Ila ni karne kadhaa kabla ya ujio wa Yesu Kristo Wanawaisraeli walishuhudia kuwa mbingu zilifungwa kwani Mwenyezi Mungu hakuendelea tena kutuma wajumbe wake kwa sababu ya madhambi yao na kukosa uaminifu katika Agano lao na Mwenyezi Mungu. Ilikuwa ni sala ya baadhi ya Wayahudi wenye hofu ya Mungu kumuomba Mungu afunguke na kushuka kutoka juu. (Isaya 64:7-8; 63:19) Hivyo mbingu kufunguka ni ishara wazi kuwa ujio wa Yesu Kristo ni mwanzo mpya wa Mwenyezi Mungu kuwa ametuma tena mjumbe wake kati ya watu wake.
Ni upendo na uwepo wa Mungu tena kati ya watu wake na Taifa lake. Ishara ya Njiwa kama ujio wa Roho Mtakatifu. Daima Mwenyezi Mungu anapotuma mjumbe wake pia anamjalia nguvu za Roho wake wa Kimungu na kufanyakazi pamoja naye. Hivyo huyu Yesu ni mjumbe wa Mungu mwenye nguvu za Kimungu na uwepo wa Kimungu ndani mwake. Njiwa kama ishara katika Biblia tunakutana nayo mara nyingi, katika Agano la Kale na Jipya pia. (Mwanzo 1:2). Kabla ya uumbwaji wa ulimwengu wakati wa ile vurugu kuu, Roho wa Mungu mfano wa njiwa hakuwa sehemu ya ile vurugu ila alikuwa juu yake. Katika gharika ya Nuhu, pia njiwa alitumika kumpasha habari kuwa sasa gharika imeisha kwa kurudi na tawi la mzeituni katika safina. (Mwanzo 8:8-12) Hivyo Njiwa anashuka juu ya Yesu Kristo baada ya Ubatizo kuonesha kuwa ndio mjumbe wa amani duniani na nguvu ya Mungu ndani mwake. Njiwa kama ishara ya upole, wema na pia jinsi anavyoishi karibu na kiota chake. Ni katika nafsi ya Yesu Kristo, Roho wa Mungu anajikuta katika kiota na makazi yake matakatifu. Na mwisho ni sauti kutoka juu. Mwinjili Marko anaandika Injili baada ya ufufuko wake Yesu Kristo, na hivyo anajaribu kuwaonesha jumuiya ile ya mwanzo ya waamini kuwa huyu aliyesulubiwa na kuuawa pale juu Msalabani, alifufuka kwani ni Mwana wa Mungu.
Na ndio Mwinjili ananukuu maneno kutoka Agano la Kale yanayomtambulisha Yesu Kristo. Wewe ni Mwanangu ni maneno kutoka (Zaburi 2:7 ; Waebrania 1:5 ; Yohane 1:18). Katika utamaduni wa Kiyahudi kuwa mwana ina maana kubwa zaidi kwa si kuwa mtoto kibaiolojia kwa damu ila pia inamaanisha mfanano wa karibu. Anayetaka kumwona baba basi yatosha kumwona Mwana. Hivyo Yesu ni sura kamili au ufunuo kamili wa Mungu Baba. Ni ufunuo kamili wa sura kamili ya upendo wa Mungu kwetu. Yesu Kristo anatambulishwa si tu Mwana bali pia Mpendwa. Yesu Kristo ni kama Isaka aliyekuwa mwana mpendwa wa Abrahamu. Hivyo katika Biblia kuwa mwana mpendwa ni kuwa na mahusiano ya pekee zaidi na baba kuliko wana wengine. Na ndivyo alivyo huyu Yesu Kristo kuwa ni Mwana pekee wa Mungu Baba. (Mwanzo 22:2; 12:16) Yesu Kristo ndiye mtumishi mwaminifu wa Mungu anayetajwa katika somo la 1 la Nabii (Isaya 42:1), anayetumwa kuja kuleta haki ya kweli duniani. Jumuiya za Wakristo wa mwanzo waliona katika huyu mtumishi anayesemwa na Nabii kuwa ni Yesu Kristo mwenyewe, aliye mwanga wa mataifa, anayekuja kuwafungua macho vipofu, kuwakomboa wafungwa na watumwa wanaotembea katika giza la dhambi na uovu.
Na Mtume Petro anajaribu kuelezea Wakristo wale wa kwanza kuwa Mungu hana upendeleo, ujio wa Yesu ulimwenguni ni kwa ajili ya wanadamu wote. Yesu Kristo alikuja na kuwahubiria watu wote wokovu na kuwaponya wote waliokuwa chini ya nguvu za yule mwovu bila kuangalia makabila au utaifa wao. Yesu aliyejawa na Roho Mtakatifu. Wapendwa katika Dominika ya Ubatizo wa Bwana ni vema nasi tukakumbuka siku ya Ubatizo wetu na hasa ahadi zetu za kubaki waaminifu daima na kutembea katika mwanga na upendo wake Mwenyezi Mungu. Ni katika Ubatizo wetu katika Roho Mtakatifu sisi nasi tumefanyika kuwa wana na warithi pamoja na Mwana pekee wa Mungu, ni upendo wa ajabu tuliojaliwa na Muumba wetu hivyo hatuna budi nasi kuilinda na kuitunza heshima hiyo kubwa. Sisi ni wana wa Mungu kwa Ubatizo wetu! Ni kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo tunajaliwa kushiriki maisha ya Kimungu, maisha ya neema na utakatifu. Hivyo hatuna budi kuienzi zawadi hiyo kubwa kwa ushuhuda wa maisha yetu ya siku kwa siku. Dominika njema ya Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo.