Tafuta

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana ni mwanzo wa safari ya ukombozi kwa njia ya imani katika Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana ni mwanzo wa safari ya ukombozi kwa njia ya imani katika Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai.  

Ubatizo wa Bwana Ni Mwanzo wa Safari ya Ukombozi Kwa Njia ya Imani

Kristo Yesu anakubali kubatizwa ili kuonesha utayari wake wa kuchukuliana na udhaifu wa mwanadamu ili amkomboe. Anataka aongozane naye polepole kuiinua hali yake duni aifikishe katika hadhi ya kimungu. Ubatizo wa Bwana ni sherehe inayotukumbusha Ubatizo wetu yaani mwanzo wa safari ya ukombozi kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Muhimu kutunza ahadi za Ubatizo.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Dominika hii tunaadhimisha Ubatizo wa Bwana. Yesu kabla ya kuanza rasmi utume wake anajiunga na umati uliokuwa ukimsikiliza Yohane Mbatizaji na yeye anapokea ubatizo wa toba kama wao. Yesu hana dhambi, anakubali kubatizwa ili kuonesha utayari wake wa kuchukuliana na udhaifu wa mwanadamu ili amkomboe. Anakubali kujichanganya na mwanadamu katika hali halisi ya maisha yake na yote anayoyapitia ili aongozane naye polepole kuiinua hali yake duni aifikishe katika hadhi ya kimungu. Ubatizo wa Bwana ni sherehe inayotukumbusha na sisi ubatizo wetu yaani mwanzo wa safari ya ukombozi kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Masomo kwa ufupi: Masomo ya Misa tunayoyasikia katika dominika hii, yanauweka ubatizo wa Yesu katika wigo mpana wa historia ya wokovu wa mwanadamu. Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya (Is 42, 1-4. 6-7), linafahamika kama utenzi wa kwanza kuhusu mtumishi wa Bwana. Tunafahamu kuwa Nabii Isaya ana tenzi nne anazomzungumzia Mtumishi wa Bwana. Katika utenzi huu wa kwanza, ni Mungu mwenyewe anayemsifia huyo mtumishi wake. Anamsifia kwa sababu amependezwa naye, anamsifia kwa sababu ni mvumilivu katika magumu, anamsifia kwa sababu ni mtumishi anayejua kuchukuliana na watu dhaifu – anasema mwanzi uliopondeka hatauvunja wala utambi utokao moshi hatauzima. Mwisho Mungu mwenyewe anasema atamtoa huyo mtumishi wake ali awe agano la watu na nuru ya mataifa.

Sasa, siku Yesu anapobatizwa kama tunavyosoma katika somo la Injili, (Lk 3, 15-16, 21-22), Mungu anatamka maneno yale yale ambayo Isaya aliyatabiri miaka mingi sana iliyopita. Sauti inatoka mbinguni “wewe ndiwe mwanangu mpendwa wangu, nimependezwa nawe.” Ubatizo wa Yesu unakuwa ni tukio la kumfunua Kristo kuwa ndiye Mtumishi wa Bwana aliyeahidiwa kuja kulifungua agano jipya na kuwaleta katika nuru ya wokovu watu wa mataifa yote. Yesu anapobatizwa anauanzisha ubatizo mpya. Wote wanaobatizwa kwa jina lake hawaupokei tena ubatizo wa Yohane Mbatizaji; Ubatizo wa toba bali wanaupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu na wanaingizwa katika Agano jipya alilokuja kulianzisha. Somo la pili kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume (Mate 10, 34-38) linakuja kutufunulia zaidi katika hili. Tunachokiona katika somo hili ni kuwa mtu aitwaye Kornelio, mtu asiye myahudi, anapopokea ubatizo anajazwa na Roho Mtakatifu. Na kama ishara ya nje ya kujazwa na Roho Mtakatifu, anaanza kunena kwa lugha. Petro anapoona anakiri kuwa kweli Mungu hana upendeleo. Yeye si Mungu wa wayahudi tu. Ni Mungu wa watu wote. Kwa njia ya ubatizo anawaita watu wote waingie na kuwa taifa lake. Wote kabisa bila kujali taifa, rangi wala hali za maisha. Ubatizo ndio mlango wa kuingia na kupata wokovu. Ubatizo ni muhimu kwa wokovu. Ndio maana Kristo mwenyewe alipokuwa anawaaga wanafunzi wake kurudi kwa Baba aliwaagiza waende ulimwenguni kote wakawafanye mataifa kuwa wanafunzi wake kwa kuwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, sherehe ya Ubatizo wa Bwana inatualika na sisi tuutafakari ubatizo wetu. Siku ile tulipobatizwa kuna kitu kikubwa sana kilitendeka ndani mwetu. Kitu hicho ni kuwa Mungu aliweka ndani mwetu alama isiyofutika, akatufananisha na mwanae Kristo akitufanya warithi sawa na yeye wa uzima wa milele, yaani kwa kufananishwa na Kristo tunajaliwa na sisi kuyashiriki maisha ya kimungu ndani ya Kristo. Na kielelezo cha yote haya ni kuwa tangu ubatizo wetu sisi tunaitwa wakristo kwa maana tunalitwaa jina la Kristo. Kuutafakari ubatizo wetu siku hii ya leo ni kuutafakari ukristo wetu, hadhi ambayo ubatizo unatupatia. Katika Amri Kumi za Mungu, amri inayotuongoza katika kuilinda hadhi anayotupa Mungu ni amri ya pili. Amri hii inasema “usilitaje bure Jina la Bwana Mungu wako.” Mungu anachokikataza katika amri hii sio tu kulitamka bure Jina takatifu, sio tu kutoa viapo vya uongo kwa Jina la Mungu na wala sio tu kuliingiza Jina la Mungu ili kujipatia maslahi binafsi. Amri hii inakataza kulitwaa bure jina la Mungu. Mungu alipokuwa anafunga Agano na Waisraeli katika mlima Sinai aliwaambia kuwa kwa Agano hilo, Yeye atakuwa Mungu wao na wao watakuwa watu wake. Wataitwa watu wa Mungu, taifa teule na hivi wataitwa kwa Jina la Mungu, watalitwaa Jina la Mungu. Ni katika amri hii Mungu anawaambia hadhi hii ya kuitwa kwa Jina Takatifu la Mungu wasiitwae bure; waipe uzito unaostahili katika maisha yao.

Kwa Ubatizo wetu tunaingia na sisi katika Agano kama walivyoingia Waisraeli mlimani Sinai. Sisi tunaingia naye Agano Jipya kwa njia ya Kristo mwanae. Amri hii ya pili inatukumbusha na kututaka sisi pia kuwa Jina Takatifu tunalopata kwa ubatizo tusilitwae bure, tulipe uzito unaostahili katika maisha yetu. Tusiingie kwa mzaha katika mahusiano haya na Mungu na tena tusiyachukulie kwa mzaha tukishaingia; ukristo wetu tusiuchukulie juu juu kufika hatua ya kujenga uhusiano wa juu juu na Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu anayependa vitu “feki”: kuwa na kiongozi feki, kuwa na mme feki, kuwa na mke feki, kuwa na rafiki feki n.k. sote tunahitaji watu wanaoaminika. Tujikite basi kumtolea Mungu uhalisia wetu. Tusiuishi ukristo wetu “mguu nje, mguu ndani;” leo mkristo, kesho muislamu, keshokutwa mganga wa kienyeji; leo mkatoliki, kesho mlokole, keshokutwa msabato; leo nashika dini, mkristo moto moto,  kesho ni mkristo jina, keshokutwa mpinga dini na adui nambari moja wa Kanisa. Kuutafakari ubatizo wetu leo kutuamshe na kutuongezea nguvu ya kuuishi vema ukristo wetu na kujikita kwa nguvu zetu zote, kwa uwezo wetu wote katika nia njema ya kuitunza hadhi ile Mungu mwenyewe anayotupatia kwa njia ya ubatizo wetu.

Ubatizo wa Bwana
07 January 2022, 17:32