Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Kristo ambaye ndiye utimilifu wa unabii wenyewe anakataliwa na watu wa nyumbani kwake. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Kristo ambaye ndiye utimilifu wa unabii wenyewe anakataliwa na watu wa nyumbani kwake. 

Dominika ya IV ya Mwaka C: Kristo Yesu Utimilifu wa Unabii Wote: Mateso

Kristo Yesu ni utimilifu wa unabii wote na hatima yake ni kifo Msalabani. Nabii anapokataliwa ni kwa sababu watu hawako tayari kuupokea ujumbe na ushuhuda wa maisha yake. Kumbe jambo la kwanza la kutafakari kuhusu kukataliwa kwa nabii katika mazingira yetu ya leo ni lile la kuangalia utayari wetu wa kuupokea ujumbe wa kinabii, utayari wetu wa kuupokea ujumbe wa Mungu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Dominika ya IV ya Mwaka C wa Kanisa. Neno la Mungu dominika hii linatupatia tafakari juu ya wito wa unabii. Tunaona katika dominika hii, Kristo ambaye ndiye utimilifu wa unabii wenyewe anakataliwa na watu wa nyumbani kwake. Naye mwenyewe anasema “hakuna Nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe.” Tuitafakari basi leo hii dhana ya nabii kukataliwa inatuachia nini katika maisha yetu ya Kikristo nyakati hizi. Masomo kwa ufupi: Tuyaangalie kwanza kwa kifupi masomo yote matatu ya dominika hii. Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha nabii Yeremia (Yer 1:4-5, 17-19 na linahusu wito wa Nabii huyo huyo Yeremia. Katika orodha ya manabii wote wa Agano la Kale, Yeremia ni kielelezo cha nabii aliyekataliwa. Alipitia magumu mengi sana katika utume wake wa unabii hadi kunusurika kuuawa.

Katika masimulizi ya wito wake, tunayoyasikkia katika somo la kwanza, tunaona kuwa magumu aliyoyapata Yeremia yalitokana na aina ya utume wenyewe ambao Mungu alimwitia. Yeye ameitwa ili aende kinyume na wafalme wa Yuda na wakuu wake, makuhani wake na watu wa nchi yake. Ameitwa awe kinyume nao na aseme yote ambayo Mungu anamwambia ili aijenge nchi ambayo imesimikwa katika Mungu mwenyewe. Ni wazi katika wakati ambapo Yeremia anaitwa, nchi ilikuwa imemwacha Mungu na Yeye mwenyewe aliamua kuisimamisha misingi ya uchaji kupitia mtumishi wake Yeremia. Yesu naye anakataliwa kama Yeremia. Katika somo la Injili (Lk 4:21-30), Yesu yuko nyumbani kwake. Siku ya Sabato anaenda katika Sinagogi, anachukua kitabu cha Nabii Isaya na anasoma kifungu kile cha “Roho wa Bwana yu juu yangu”.

Roho wa Bwana yu juu yangu amenituma kuwahubiria watu Habario Njema ya Wokovu.
Roho wa Bwana yu juu yangu amenituma kuwahubiria watu Habario Njema ya Wokovu.

Anakifunga kitabu, anaanza kuyafafanua Maandiko akiwaonesha kuwa Yeye ndiye utimilifu wa unabii huo wa Isaya. Wapo waliodharau wakajikwaa katika kutokuamini kwa sababu tu walimfahamu: “huyu siye mwana wa Yusufu?” Kingine kilichotokea ni kile kinachotokea hata nyakati zetu hizi. Mji au kijiji kinapokuwa na kiongozi mkubwa au mtu maarufu anayetokea huko, watu wanategemea afanye mambo mazuri huko au awarahisishie mambo.Hivyo wanamwambia na Yesu “tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe.” Yesu anawajibu anawaambia habari ya Neno la Mungu haiendi hivyo. Neno la Mungu haliendi kwa ukanda, kwa ukabila wala kwa undugu. Akawakumbusha kipindi cha Eliya kuwa walikuwapo wajane wengi waisraeli wakati ule wa njaa.

Eliya hakutumwa kwa Waisraeli wenzake isipokuwa kwa mjane wa Serepta katika nchi ya Sidoni na huyo ndiye akamfanyia muujiza wa chakula. Akawakumbusha pia habari ya wakoma kipindi cha nabii Elisha. Elisha hakutakasa wakoma waisraeli isipokuwa Naamani, mtu wa Shamu. Neno la Mungu linatenda kazi katika moyo ulio tayari kulipokea na wala si vinginevyo.  Kushindwa kuupokea ukweli huo, wakajaa gadhabu, wakamtoa Yesu wamtupe chini ya bonde. Tukirudi sasa katika somo la pili (1Kor 12:31-13:13) Mtume Paulo katika barua yake ya kwanza kwa wakorinto anatukumbusha juu ya upendo. Anautaja upendo kuwa ndiyo karama iliyo kuu kupita karama zote na kualika kuishi na kutenda katika upendo.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo haya ya dominika hii kuhusu kukataliwa kwa nabii yanatuambia nini sisi leo? Tukiangalia kwa undani dhana hii, nabii wa kweli hakataliwi kwa sababu tu ni nabii. Nabii anapokataliwa ni kwa sababu watu hawako tayari kuupokea ujumbe wake au ushuhuda wa maisha yake. Kumbe jambo la kwanza la kutafakari kuhusu kukataliwa kwa nabii katika mazingira yetu ya leo ni lile la kuangalia utayari wetu wa kuupokea ujumbe wa kinabii, utayari wetu wa kuupokea ujumbe wa Mungu. Maandiko Matakatatifu yanatuambia Neno la Mungu ni kama upanga wenye makali kuwili. Tena ni kama umande, pale linapotua na kupokelewa ni lazima lilete mabadiliko. Sasa sisi wakati mwingine hayo mabadiliko ndiyo hatuyataki. Kwa hali hiyo tunajikuta tunataka tulisikie Neno ambalo linatufariji, neno linalotubembeleza, neno linalotuambia hakuna shida hata pale ambapo kuna shida.

Kristo Yesu ni utimilifu wa Unabii wote.
Kristo Yesu ni utimilifu wa Unabii wote.

Sasa hatari iliyopo ni kujikuta unajiundia ukristo unaoendana na matakwa ya hali yako. Na kwa sababu hiyo kila neno au ujumbe unaokuja “kutikisa” aina yangu hiyo ya ukristo, kwangu haupokelewi; “ninafunga vioo”. Huko ndugu yangu ni kuukataa unabii na ndiko kumkataa nabii kama alivyokataliwa Yeremia na kama anavyokataliwa Yesu. Ndugu yangu, usiogope unapoona Neno la Mungu ni gumu kuliishi, ogopa unapoona ni rahisi sana; usiogope unapoona Neno la Mungu linayachokonoa maisha yako, ogopa kama Neno la Mungu haliyachokonoi maisha yako, ogopa kama Neno la Mungu halikutikisi na kukufanya ujiulize kila wakati “sasa nifanye nini”, usiogope kwamba Neno la Mungu linakudai ufanye vitu vingi, linakudai uzidi kupiga hatua kila siku, ogopa kama Neno la Mungu halikudai ufanye chochote, ogopa kama Neno la Mungu halikuambii bado hujafika unahitaji kuzidi kupiga hatu. Ogopa. Ukristo laini haupo, isingekuwa hivyo Yesu asingechagua njia ya Msalaba, njia ya mateso makali na kifo cha aibu ili tu wewe uwe mkristo.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika hatua nyingine ya kuutafakari ujumbe huu wa leo, tuangalie pia mahusiano yetu na wale manabii wa ukweli ambao Mungu anawaleta katika maisha yetu. Hawa ni wale watu waaminifu, wakweli, wachapa kazi n.k tunaokutana nao katika hatua mbalimbali za maisha: katika familia zetu, kama marafiki au katika maeneo ya kazi. Tunawachukuliaje? Uwepo wao kati yetu ni kichocheo cha sisi kuishi maisha ya fadhila kama wao au ni kikwazo kwetu kiasi cha kuwafanya walengwa wa kebehi au hata walengwa wa njama za kuwaangamiza. Kuwachukia watu wema Mungu anaotutumia katika maisha yetu ni kuwakataa wajumbe wake manabii.   Tuhitimishe tafakari yetu hii fupi kwa maneno ya Musa baada ya kumwomba Mungu ashushe roho ya kinabii kwa wazee 70 aliowachagua: “Ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii, na kama Bwana angewatia roho yake” (Hesabu 11:29).

Liturujia D4 Mwaka

 

 

 

 

28 January 2022, 08:24