Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili IV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Krisdto Yesu anakataliwa na watu wa nyumbani kwake na wanataka kumwondolea mbali kutoka katika uso wa nchi. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili IV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Krisdto Yesu anakataliwa na watu wa nyumbani kwake na wanataka kumwondolea mbali kutoka katika uso wa nchi. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili IV ya Mwaka C: Wanamkataa Yesu Kristo, Wanataka Kumuua!

Mwinjili Luka anatuonesha kuwa tangu mwanzo, Yesu anaanza utume wake akitokea katika kijiji kisichokuwa na umuhimu sana na kati ya watu wasiomwamini. Yesu anaanza utume wake katika mazingira magumu na ya kukatisha tamaa, ya watu waliomkataa na hata kutaka kumuua kwa kumtupa chini kutoka ukingo wa kilima, hali ikiwa ni mwanzoni tu mwa utume na maisha yake.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Somo la Injili ya leo, ni mwendelezo wa sehemu ya Injili tuliyoisikia na kuitafakari Dominika iliyopita yaani, Injili Takatifu ilivyoandikwa na Luka 4:21-30. Ni simulizi la kile kilichojiri katika Sinagogi la Nazareti, pale ambapo Yesu alitangazwa Mwaka uliokubaliwa na Bwana, yaani, Mwaka wa neema, ndio Kairos. Na hata wasikilizaji wake wanakiri kusikia “maneno ya neema”, ndio maneno yenye kuleta heri na furaha maishani mwao, na hapo tunaona wakazi wale wa Nazareti wakistaajabia maneno ya Yesu na hata kumshuhudia, huo ndio mwitikio wao wa mwanzo tunaposoma Injili ya leo. Lakini tunapatwa na maswali bila majibu pale tunapoona wakazi wale wanabadilika kutoka katika hali ile ya kustaajabia, kumsifu na kumshuhudia na kuanza kujawa na ghadhabu kiasi cha kutaka kumtupa chini kutoka ukingo wa kilima. Na hata tunaposoma tena hatusikii neno lolote baya dhidi yao kutoka kinywa cha Yesu, sasa kwa nini ghadhabu na hasira kali dhidi ya Yesu?

“Tabibu, jiponye nafsi yako” pamoja na “Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe” ni moja ya misemo anayoitamka Yesu katika somo la Injili ya leo, lakini tunajiuliza kwa nini Yesu anatumia misemo hii? Mwinjili Marko anatuonesha kuwa Yesu hakutenda miujiza katika nchi au kijiji chake kutokana na kutokuamini kwao (Marko 6:5); lakini Mwinjili Luka kinyume chake anatuonesha kuwa watu wale waliamini juu ya uwezo wa Yesu wa kutenda miujiza, na kama ndivyo basi kwa nini Yesu hakutenda miujiza katika nchi na kijiji chake cha Nazareti? Wote walijaa ghadhabu waliosikia maneno ya Yesu na kuondoka na kutaka kumtupa chini, aliwezeja kusalimika katikati ya umati ule mkubwa? Kwa hakika hakupotea kutoka machoni mwao kwa njia ya muujiza kwani Mwinjili anatuambia hakutenda muujiza huko, kwa hiyo kitendo cha kujisalimisha pia hakikuwa cha muujiza bali cha kawaida.

Yesu anatenda utume wake sio kwa kutafuta jina na umaarufu, kwani huko ni kuenenda kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu. Yesu anatenda utume wake kwa kutualika nasi kuingia katika majadiliano ya upendo naye, ndio yale ya kuwa tayari kufungua macho ya mioyo yetu na kuonja huruma na upendo wake kwetu. Natanaeli mara baada ya kusikia habari za Yesu wa Nazareti, anahoji ni nini chema kinaweza kutoka katika kijiji kile. Mwinjili Luka anatuonesha kuwa tangu mwanzo, Yesu anaanza utume wake akitokea katika kijiji kisichokuwa na umuhimu sana na zaidi sana kati ya watu wasiomwamini. Yesu anaanza utume wake katika mazingira haya magumu na ya kukatisha tamaa, ya watu wasio na imani naye, waliomkataa na hata kutaka kumuua kwa kumtupa chini kutoka ukingo wa kilima, hali ikiwa ni mwanzoni tu mwa utume wake. Wainjili wote wanatuonesha jinsi Yesu anavyokataliwa kati ya watu wake, yaani wa kijijini kwake na hata ndugu zake wanavyoshindwa kumwamini. (Marko 3:21 na Yohane 7:5) Wainjili Mathayo na Marko wanatuonesha kuwa Yesu alikataliwa na watu wake mwishoni mwa utume wake Galilaya (Marko 6:1-6 na Matayo 13:53-58). Mwinjili Luka anatuonesha kuwa Yesu anakataliwa sio mwishoni bali mwanzoni mwa utume wake. Ndio Mwinjili Luka anatuonesha hilo sio kama kweli ya kihistoria kwa muda ya tukio tu bali kwa sababu za Kitaalimungu na Kichungaji.

Hiki kilichojiri na tunachokitafakari katika somo la Injili ya leo, ni ufupisho mzima wa utume wa Yesu wa Nazareti. Ni katika tukio hili tunaweza kuona utumewake wa wokovu kwa walio wanyonge, maskini, wenye kuonewa na kusetwa na jamii, yaani walio pembezoni mwa jamii zetu, linajidhihirisha katika mapokezi yale ya awali ya watu wale kujawa na mshangao na hata kumshuhudia kuwa amejaa maneno ya neema, lakini muda si muda wakashindwa kumuelewa na hivyo kujawa na ghadhabu na kutaka kumtupa chini na kumuua. Mwinjili Luka anatuonesha leo Yesu anapelekwa katika kingo ya kilimo, ndio kusema anatuonesha tangu mwanzoni jinsi atakavyopelekwa katika kilima kile cha Kalvario ili ahukumiwe kifo. “Tabibu, jiponye nafsi yako”, ndio kauli ile inayosikika kwa watu wale waliokuwa chini ya msalaba wa Yesu, wakimdhihaki na kumkejeli, kuwa aliponya wengine na sasa jiponye na iokoe nafsi yako. (Luka 23:35). Hivyo kwa kifupi tunaweza kuona Mwinjili Luka anataka kutuonesha kuwa tangu mwanzo Yesu ni Masiha, yule ambaye saa yake ndio ile ya kukataliwa, mateso na mwisho kuuawa pale juu Msalabani.

Kristo Yesu aliteswa, akafa na hatimaye kufufuka kwa wafu.
Kristo Yesu aliteswa, akafa na hatimaye kufufuka kwa wafu.

 

Katika ibada ya Neno la Mungu katika Sinagogi, ilikuwa ni desturi msomaji wa somo la pili alichagua somo kutoka Vitabu vya Manabii na kusoma haidhuru aya au mistari mitatu. Na iliwezekana kabisa Sinagogi la Nazareti hawakuwa na Vitabu vyote vya Manabii na hivyo mara nyingi walisoma Kitabu cha Nabii Isaya. Na kama walisoma Kitabu kile kila Sabato, basi wengi walikifahamu na hata kukikumbuka kwa moyo. Sehemu ya Kitabu kile anachosoma Yesu ni wazi ilifahamika na kujulikana karibu na wote. Yesu hakusoma mstari au aya iliyobaki kwani anasimama mara baada ya kusema maneno yale, kuwa nimekuja kuutangaza mwaka wa neema ya Bwana na kuacha maneno yaliyosalia. “Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao” (Isaya 61:2). “…na siku ya kisasi cha Mungu wetu” Ndio maneno haya wasikiliza wake walikuwa bado wanayategemea na kuyasubiri kutoka kinywani mwa Yesu, ni maneno waliyopenda kuyasikia sio tu wakazi wa kijiji kile cha Nazareti bali Taifa zima la Wayahudi. Walikuwa anaisubiri kwa hamu na shauku kubwa siku ile ya kisasi cha Mungu kwa watu wapagani, yaani, watu wa mataifa mengine ambao waliwatesa kwa kuwachukua mateka na watumwa.

Ni Yesu badala ya kutangaza saa ile ya kisasi anatangaza mwaka wa neema, wote wanapata kusamehewa na kupokea huruma ya Mungu, ni wema sio tu kwa watu wa taifa lile bali kwa watu wote bila ubaguzi wowote ule. Na ndio hapo wakaanza kujihoji na kujiuliza kuwa anajifanya kuwa nani kwenda kinyume na tamaduni zenye mitazamo yao, ndio ile ya kisasi. “Huyu siye mwana wa Yusufu?” Sio kwamba lilikuwa swali wakitilia mashaka kuwa sio mwana wa Yusufu, lakini ndio sawa na kusema ni nani huyu anayekuja na mtazamo mpya ulio kinyume na ule sio tu wa kijiji chetu bali taifa zima la Israeli. Na hata baada ya wao kutokumuelewa Yesu, Yesu hakubali mafundisho yake, bali alizidi kuwaalika wasikilizaji wake kubadili vichwa vyao, kubadili namna zao za kufikiri na kutenda. Na ndio Yesu anatumia misemo ile miwili maarufu, yaani, “tabibu, jiponye nafsi yako” na ule wa “Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe”. Ni hapa tunaona watu wake wanapatwa na ghadhabu, kwani tayari walishasikia Yesu akitenda miujiza huko Kapernaumu na hivyo nao walitaka atende miujiza hiyo tena kwa wingi na ukubwa katika nchi yake mwenyewe na kati ya jamaa na ndugu zake.

Yesu anatumia misemo hiyo miwili ili kuwaonesha kinagaubaga kuwa mioyo yao ilikuwa mbali, wanashindwa kubadili vichwa vyao ili wapate kuwa na muono mpya, namna mpya ya kufikiri na basi walishupaa katika akili ya zamani, namna inayotuweka mbali na kweli za Injili. Na ndio namna tunazozishuhudia leo katika ulimwengu wetu, watu wengi kutaka na kusubiri miujiza ili waamini, ili waweze kuwa Wanakanisa basi kwao la kwanza ni miujiza kadiri ya mapenzi na matakwa yao na sio kadiri ya mapenzi ya Mungu. Imani yetu haipaswi kujikita katika miujiza bali katika huyu Yesu Kristo, huyu Yesu wa Nazareti anatualika kumkazia macho yeye ili kuweza kujua mapenzi ya Mungu katika maisha yetu ya ufuasi. Kumkazia macho Yeye ili atujalie na neema za kupokea mapenzi ya Mungu katika maisha yetu ya siku kwa siku.  Yesu anazidi kuwaonesha kuwa huruma na upendo wa Mungu ni kwa watu wote na ndio anawakumbusha hilo kutoka Maandiko Matakatifu; Eliya hakutumwa kwa mjane mmojawapo wa Israeli bali kwa mjane wa Sarepta katika nchi ya Sidoni, katika nchi ya Kipagani. Na Nabii Elisha anatumwa kwa Naamani ailiyekuwa mkoma wa nchi ya Shamu, pia nchi ya Kipagani.

Watu wake wanashangazwa na uamuzi wake wa kwenda kuishi na kufanya utume wake katika kijiji kile kilichojaa wapagani, yaani Kapernaumu, ni mahali ambapo watu wake hawakuwa waaminifu sana kwa Sheria ya Musa. Hivyo somo la Injili ya leo linatuonesha utume na misheni ya Yesu tangu awali ni ule unaojumuisha watu wa mataifa yote bila ubaguzi, sio misheni kwa ajili ya watu wake tu, wa nyumba yake na kijiji chake tu, lakini zaidi sana hata kwa wale ambao wanakuwa mbali kabisa, wale waliosetwa na kutengwa na jamii. Na ndio Kanisa la Kisinodi linaalikwa kujitafakari nini maana ya kuwa Kanisa, nini maana ya kuwa wafuasi na rafiki zake Yesu Kristo Mfufuka. Kuwa Kanisa kweli ni kutokumuacha au kumtenga mtu yeyote pembeni, ni Kanisa linalotembea pamoja na mantiki ya Bwana na Mwalimu wetu, Yesu Kristo.

“Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.” Kupita katikati yao haimaanishi kuwa kitendo kile kilifanyika kimuujiza, la hasha ila badala yake Mwinjili Luka anataka kuonesha wasikiliza wake wa Kanisa lile lililokuwa linapitia mateso na madhulumu mengi, ili huu uwe ujumbe wa faraja kwao, Ni ujumbe wa faraja kuwa hata Yesu Kristo alikataliwa na watu wake, wa kijijini kwake na hata ndugu zake, hivyo nao hawana budi kumkazia macho yule anayetuita na kuishi kama jumuiya moja ya Wabatizwa. Mungu daima analipitisha salama Kanisa lake hata kati ya watesi na wadhulumu wake, sio tu wa karne zile za mwanzo wa Kanisa bali hata katika nyakati zetu. Kila mmoja wetu tunaalikwa kuwa na imani thabiti na ya kweli ambayo kwayo itatuwezesha kupita katikati ya nyakati ngumu na hata za kukatisha tamaa. Niwatakie Dominika njema na tafakuri njema ya Neno la Mungu.

26 January 2022, 15:21