Askofu Severine Niwemugizi Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu: Makuu ya Mungu
Na Askofu Flavian Matindi KASSALA, Jimbo Katoliki la Geita, Tanzania.
Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki Geita, ambaye pia ni Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika makala hii, anapenda kumpongeza na kumshukuru Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara aliyezaliwa tarehe 3 Juni 1956 huko Katoke. Tarehe 16 Desemba 1984 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 8 Novemba 1996 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge na kuwekwa wakfu na Askofu mkuu Anthony Peter Mayalla kuwa Askofu tarehe 16 Februari 1997. Tarehe 22 Februari 2022, Sikukuu ya Ukulu wa Mtume Petro anaadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu. Askofu Flavian Matindi Kassala anapembua kwa umakini mkubwa uongozi wa Askofu Niwe kama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kati ya Mwaka 2000 hadi mwaka 2006 na siasa za wakati ule. Awamu ya Pili kati ya Mwaka 2012 hadi mwaka 2015. Askofu Flavian Matindi Kassala anasema, shangwe na nderemo zilizosikika tarehe 16 Februari 1997 zinavuma tena kwa namna ya pekee hapo tarehe 22 Februari 2022, ikiwa ni mara ya 25 tangu pale Mama Kanisa alipopiga kengele za shangwe kumpokea mwanaye, Padre Sererine Niwemugizi kama mojawapo wa Makhalifa wa Mitume.
Miaka hii 25 ya utumishi wa kiaskofu inafumbatwa na majitoleo mengi na utendaji wa Askofu Severine Niwemugizi katika eneo la Jimbo la Rulenge-Ngara, Kanisa la Tanzania na ulimwengu kwa ujumla katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifu watu wa Mungu ndani nje ya Tanzania. Baba Niwemugizi: Askofu wa Rulenge na Rulenge-Ngara. Kama Askofu wa Jimbo la Rulenge, wakati huo, Askofu Severin ni mrithi wa aliyejulikana kama Baba wa Mkamilishano, Baba Askofu Christopher Mwoleka. Baba Askofu Severin anaweka historia Jimboni Rulenge pale ambapo mwaka 2008 aliamua kubadilishwa kwa jina na Jimbo toka Jimbo la Rulenge na kuwa Jimbo la Rulenge-Ngara. Mabadiliko haya yalihusisha hasa sababu za kichungaji. Hayakuwa maamuzi mepesi, lakini ulikuwa ni uamuzi ambao ulilenga katika kutanua mtandao wa huduma za Kanisa Kijimbo na Imani kwa Ujumla katika eneo la lililokuwa Jimbo la Rulenge. Pamoja na kubadilisha jina la Jimbo, pia makazi ya Askofu Jimbo yalihamishwa kutoka eneo la Rulenge na kupelekwa mjini Ngara. Pia Kanisa Kuu la Jimbo na Kiti cha Kiaskofu vilihamia katika eneo hilo la Ngara.
Hata hivyo ikumbukwe kuwa eneo la Jimbo halikubadilika kutokana na mabadiliko haya. Moja wapo ya mafanikio makubwa ya kuhamishwa kwa Makao Makuu ya Jimbo ilikuwa ni pamoja na urahisi wa kufikika kwa huduma zilizodai kufanyika katika ofisi za kiaskofu, kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo. Mahali yalipo makao makuu ya Jimbo kwa sasa yanatoa pia nafuu kubwa kwa mawasiliano na sehemu nyingine za taifa na dunia kwa ujumla, ikizingatiwa kuwa kuwepo kwa Makao Makuu Rulenge, wakati huo, kulizuia kufikika kwa kutumia huduma mawasiliano kama vile simu pengine hata Internet. Uwepo wa Askofu katika eneo la Ngara inafungua pia mahusiano ya karibu na mamlaka mengine tendaji ya kitaifa na kimataifa, kwani ofisi za kiserikali kwa ngazi ya wilaya zinapatika mjini Ngara.
‘Baba Niwe’: Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Jina ‘Baba Niwe’ nimekuwa nikilisikia sana katika mahusuano yetu ya urika tunapokuwa katika shughuli mbalimbali za ki-Baraza. Ni jina ambalo litumikapo hunipatia vionjo vya upendo, unyenyekevu na upendo kitumishi kwa ndugu zake. Kitaifa, Askofu Niwemugizi ameliongoza Baraza la Maaskofu la Tanzania, TEC, kama Rais wake kwa kipindi cha miaka sita (2000 hadi 2006). Kihistoria ninakumbuka kuwa ni kipindi cha sherehe za za Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Kumbe, alikuwa kinara wa kusimamia maadhimisho hayo ambayo yalikuwa ya namna yake katika Kanisa Katoliki ulimwenguni. Kama kiongozi wa Baraza wakati huo aliliongoza Kanisa la Tanzania kutafakari hitimisho la maadhimisho Barua ya Kichungaji “Mwenye Nguvu Amenitendea Makuu, na Jina Lake ni Takatifu” (Lk 1:49)’ barua ambayo iliwaalika Waamini na Taifa la Mungu kwa ujumla nchini Tanzania kuyaishi mafanikio na mafundisho makubwa yaliyopatikana katika adhimisho la Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.
Rais wa Baraza na Siasa wa Wakati: kipindi cha uongozi wa Askofu Severine kama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kilikuwa na changamoto zake kisiasa. Kilikuwa ni kipindi cha mabadiliko makubwa kiuchumi, ambapo Kanisa lilihitajika kusimamia haki, ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote. Hivyo, matarajio mengi wa waamini na wasiowaamini yaliwekwa katika Maaskofu, ambao yeye alikuwa Kiongozi na msemaji wao. Ni kipindi ambapo alishuhudia mabadiliko ya Marais wawili: Mhe. Ali Hasan Mwinyi akimalizia muda wake na Mhe. Benjamin Willim Mkapa akiingia katika awamu ya kwanza ya madaraka yake. Uongozi wake ulihakikisha mahusiano ya Kanisa na Serikali yanalindwa na kudumishwa hali kila upande ukilinda misingi yake. Ikubukwe kuwa Baba Niwemugizi naingia katika uongozi wa Baraza muda mfupi tu baada ya Baraza, kwa niaba ya Jamii, kuhoji hali fulani zenye utata katika mabadiliko makubwa yaliyokuwa yakitokea ndani ya nchi. Katika barua yao “WHAT WE SEE AND HEAR: The Opinion of the Tanzania Episcopal Conference on Certain National Issues.” (Ref. Raymond Saba (Ed), Compendium of Major Pastoral Letters, Guidelines and Statements of the Catholic Bishops in Tanzania: 1953-2018, 2018, pp. 325-330.)
Maaskofu walikuwa wamehoji kuhusu: hali wakulima, soko huria, mabadiliko katika mfumo wa elimu sanjari na kukosekana fursa za ajira kwa vijana. Barua hiyo iliyohoji pia kuhusu mfumo wa demokrasia nchini ilikuwa ni utekelezaji wake katika kipindi cha uongozi wa Baba Niwemugizi. HAIKUWA KAZI RAHISI. Hii ilikuwa ni “patashika nguo kuchanika.” Mhashamu Askofu Severine: Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Pamoja na kumaliza kipindi chake cha uongozi hapo 2006, Askofu Severine hakusita pale ndugu zake Maaskofu wa Tanzania walipomwomba kushiriki tena katika uongozi wa Baraza. Askofu Severine alilitumikia Baraza kwa nafasi hiyo toka mwaka 2012 hadi 2015. Ni katika kipindi hicho pia aliongozana na Maaskofu wenzake kwenda kwenye hija ya Kitume: “Ad Limina Apostolorum Visitatio” na kwa kifupi, “Ad Limina.” Wakiwa katika ziara hii, alibahatika kuwa ni kati ya Maaskofu wa wachache sana duniani kuzungumza ana kwa ana na Mtakatifu Yohane Paulo II katika siku za mwisho za uhai wake. Ni wazi bahati na baraka hiyo haikosi nafasi yake katika maadhimisho haya ya miaka 25 ya utumishi wa Kitume.
Baada ya utumishi huo wa nafasi ya uongozi katika Baraza, Baba Severine amekuwa mnyenyekevu katika nafasi mbalimbali alizotumwa na Kanisa la Tanzania katika Baraza la Maaskofu Katoliki. Kati ya nafasi alizotumikia hivi karibuni ni pamoja na kuongoza Kamati cha Mahesabu na Maadili ya Baraza. Kwa sasa Baba Askofu Severine ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Bugando (CUHAS), “Catholic University Of Health And Allied Sciences, CUHAS, Bugando, Mwanza. Tafakari hii fupi ya Baba Niwe ni sehemu ya pongezi kwa Baba Askofu Severine Niwemugizi katika kutimiza miaka hii 25 ya utumishi, ambayo ameendelea kuipokea kama zawadi toka kwa Muumba wake. Hali tukimpongeza ni nafasi yetu pia ya kutoa matashi mema kwa sehemu iliyo mbele yake ya utumishi. Tunamwombea baraka, amani na utulivu katika kuyapokea mapenzi ya Mungu yaliyopo mbele yake. Hali tukielekeza macho, masikio na miguu yetu huko Ngara hushuhudia hayo makuu ya Mungu,
Katika utumishi,
+ Flavian Matindi Kassala, Askofu wa Jimbo la Geita. (Jirani wa Rulenge-Ngara).