Askofu Mkuu Centellas,wa Bolivia anasema acheni uadui na kutenda pamo kwa ajili ya Nchi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kuishi kwa upendo unaotoka kwa Mungu anayesaida kutafuta daima msamaha na mapatano kati ya wote kwa kutenda wema hasa kwa walio mbali zaidi na kuwapenda maadui. Ndiyo mada ya Mahubiri ya Askofu Mkuu Ricardo Centellas, wa jimbo Kuu katoliki la Sucre nchini Bolivia, katika Misa ya Dominika tarehe 30 Januari 2022 kwenye Kanisa Kuu, akitafakari masomo ya kibibla ya siku na ambayo yalikuwa yakiangazia safari ya waamini wote wa kikristo. Askofu Mkuu akitafakari kifungu cha mwisho cha somo la kwanza (Yer 1,4-5.17-19) kisemacho: “Watakufanyia vita lakini hawatakushinda kwa sababu mimi niko pamoja nawe ili kukuokoa” alisema hii ni kuonesha kuwa kuishi kaika jitihada za kikristo ni mchakato wa safari ngumu sana lakini kwamba hawaswi waamini kukata tamaa, bali kwenda mbele na maisha ambayo Mungu anawajalia kwa kuishi misingi ya kibinadamu na ya kikristo ambayo Mungu anawaonesha kwa njia ya maisha ya Yesu.
Upendo uzidishe mipaka ya kuwapenda maadui
Katika kufafanua somo la Pili kutoka Barua ya Kwanza ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorinto (1Kor 12,31-13,13) Askofu Mkuu alisema kwamba, Paulo anakumbusha wakristo wote maana ya upendo wa kikristo kwa upendo wa Mungu. Yesu alifundisha kupendana kama Yeye alivyo penda watu wake na vilevile kujikita kutafakari kwa kina na kukua katika uzoefu wa upendo huku wakijaribu kupenda hata maadui zao. Kupenda ni kutenda wema, hasa kwa walio wadogo na si kwa yule aliye kwenye kundi binafsi, yule ambaye mkristo anampenda au mshabiki wa chama au mpira, kwa maana Yesu anawataka waamini wake wote kutenda wema hasa kwa walio pembezoni, waliobaguliwa, wenye kuhitaji msaada na zaidi waliosahauliwa kabisa, alisisitiza Askofu Mkuu Centellas
Ikiwa waamini wanataka kuishi imani binafsi, hawatakiwi kuwa na maadui
Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu Centellas alisema kwamba ikiwa waamini wanataka kuishi imani binafsi, hawatakiwi kuwa na maadui, kwa maana wote ni watu tofauti na kuna mitindo tofauti ya kukabiliana na maisha, lakini wao sio wapinzani. Na ikiwa wanataka kubadilisha lolote nchini Boliva lazima waache kuwa na tabia ya upinzani ili kufanya kazi pamoja kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao na maendelo ya kila familia; kwa sababu hawapati faida yoyote kuwa wapinzani na kukinzana kati yao, bali wanapoteza na kwa maana hiyo inakwenda kinyume na upendo wa Kikristo.
Njia ya upendo ni kujifunza kuishi kwa kusamehe na kushinda shauku za kibinadamu
Askofu Mkuu wa Bolivia aliwashauri waamini wote kwa njia hiyo kujifunza kuishi kwa kusamehana na kushinda au shauku ambazo ni za kibinadamu tu kwa maana ya kufanya hivyo wanaweze kweli kuishi upendo kama Mungu anavyopendekeza kwao na kukubali upendo ambao unaruhusu msamaha na maridhiano. Na ndiyo maana alisisitiza kwamba, Mama Kanisa anapendekeza upatanisho wa nchi ya Bolivia kwa sababu ikiwa wanaishi na kukubaliana na mwingine kama ndugu tu ndipo wanaweza kuendelea na kuwa na jamiii ambayo ina uvumilivu mwingi zaidi, na heshima ya mmoja na mwingine. Ikiwa hawana uwezo wa kujipatanisha wao wenyewe watavamiana na kujikuta daima ni wapinzani kati yao na kuzidisha uadui na makabiliano mabaya kati yao.