Dominika ya VII ya Mwaka C: Jifunzeni Kusamehe Ili Kushinda Uovu na Visasi
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
UTANGULIZI: Ni dominika ya saba ya Mwaka C wa Kanisa. Dominika hii inatupatia mwaliko wa kuwa watu wa msamaha, watu wasioona kuwa kisasi ni njia ya kusuluhisha makosa au njia ya kutuliza hasira dhidi ya uovu. Ni dominika inayotualika kuunda familia, jumuiya, kanisa na jamii ambayo iko tayari kuushinda uovu kwa kujiunda upya na kuuishi upendo wa Kristo kwa kusameheana. MASOMO KWA UFUPI: Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha kwanza cha Samweli na linatupatia simulizi la tukio moja kuwahusu Sauli na Daudi. Sauli alikuwa ndio mfalme wa kwanza wa Israeli. Ni mfalme ambaye baadaye Mungu alimkataa kwa sababu ya makosa yake ya kutokutii. Badala yake, Mungu akamchagua Daudi awe mfalme. Sasa katika kipindi hicho ambacho Daudi amepakwa mafuta awe mfalme na hapo hapo bado yupo mfalme Sauli unatokea uhasama kati yao.
Sauli anakusudia kumuua Daudi na analiweka waziwazi azimio hilo, suala ambalo linamfanya Daudi akimbie akajifiche ili asiuwawe na Sauli. Sasa somo hili la leo linatuonesha kuwa Daudi akiwa huko mafichoni, kwa bahati anaingia katika pango ambalo Sauli alikuwa amelala akipumzika. Alikuwa ameenda huko nyikani kumtafuta Daudi. Msaidizi wa Daudi anamwambia “Mungu amemleta adui yako mikononi mwako, niruhusu nimwangamize.” Daudi anasema usimwangamize, ni mpakwa mafuta wa Bwana. Daudi hafikirii katika dhana ya kisasi, dhana ya “akuanzae mmalize”, dhana ya kutafuta amani kwa kumwondolea uhai adui. Daudi anasukumwa na hofu ya Mungu na anakuwa tayari kuujibu uovu kwa wema.
Katika somo la Injili (Lk 6:27-38) Yesu anathibitisha fundisho kuhusu msamaha. Fundisho hili Yesu analitoa kwa kueleza mifano halisi ya mazingira ya kutoa msamaha. Anasema mpende adui, mtendee mema anayekuchukia, mbariki anayekulaani, muombee anayekuonea, akupigaye kofi shavu moja mgeuzie na la pili, anaykunyang’anya koti mpe na shati. Tukiiangalia vema, hii yote ni mifano inayosisitiza jambo moja kubwa katika mafundisho ya Yesu: uovu hautokomezwi kwa njia ya uovu. Uovu unatokomezwa kwa upendo. Fundisho hili sio jepesi, ni zito. Lakini tukikaa vizuri na kujiuliza endapo angesema kama labda ulimwengu unavyotaka: adui yako muangamize, anayekuchukia na wewe mchukie tena usimsogelee, anayekulaani na wewe mlaani, anayekuonea mtendee ubaya hadi akuogope, anayekupiga kofi shavu moja mrudishie kwa kumpiga kofi n.k – mahusiano yetu, familia zetu na jamii nzima kwa ujumla vingekuwa na sura gani? Uovu ungezidi kushamiri na wema usingepata nafasi hata kidogo.
Yesu hatoi fundisho hilo ili kuendekeza uovu au ili kuruhusu watu fulani wafanye wanavyotaka kwa sababu wengine lazima wawasamehe. Yesu anaalika kila mmoja kwanza atwae jukumu ambapo atakuwa tayari kumtendea mwingine kile ambacho angependa atendewe yeye mwenyewe. Ni kutoka hapo ndipo anaalika kuishi maisha ya fadhila kwa kuwatendea mema watu wote bila mipaka wala bila kutegemea kulipwa mema kutoka kwao. Anayetenda mema akitegemewa kulipwa mema haiishi fadhila kwa maana Yesu anasema hata wadhalimu huwatendea mema wadhalimu wenzao. Mwisho, kutoka katika fundisho hilo ambalo linaonekana ni la kiungwana na la kibinadamu kabisa, Yesu anaongeza kipengele ambacho kwacho binadamu anachota kutoka namna ambavyo Mungu anatutendea sisi. Anasema iweni na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma kwenu, Msihukumu nanyi hamtahukumiwa naye kwa maana kipimo mnachopimia watu ndicho Yeye pia atawapimia.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kusikiliza masomo ya dominika hii na baada ya kupata ufafanuzi wake, ninawaalika tutafakari kipengele kimoja kati ya vingi ambavyo masomo yenyewe yametupatia kuhusu msamaha. Kipengele hicho ni mwaliko wa Yesu usemao “Msihukumu nanyi hamtahukumiwa.” Neno hili “kuhukumu” maana yake ya kawaida ni ile ile tunayoifahamu. Ni kutoa maamuzi au kutoa shauri juu ya jambo lenye utata kama afanyavyo hakimu mahakamani. Katika muktadha wa kifungu cha injili ya leo, neno hili “kuhukumu” linachukua maana nyingine. Katika kifungu hiki cha Injili kinachozungumzia msamaha, upendo kwa adui na kumgeuzia shavu la pili mtu akupigaye kofi shavu moja, kuhukumu ni pale ambapo mtu anafunga kabisa milango ya mahusiano na mtu mwingine kwa sababu ya uadui. Ni pale ambapo mmoja anafikia maamuzi na kusema, kwa mfano, fulani siko tayari kupatana naye au siko tayari kuzungumza naye tena.
Kama ni ndugu, unasikia mmoja anasema fulani kuanzia sasa undugu umeisha na si ndugu yangu tena. Mwingine anafika hadi kusema nikifa asikanyage katika mazishi yangu. Maamuzi kama haya ni maamuzi yanayofunga kabisa milango si tu ya kupatana bali pia ya kurekebisha kosa na kutoa nafasi ya kuumaliza uovu. Tena yanatoa hukumu ya moja kwa moja bila kutambua kuwa binadamu hata kama ni mkosaji mkubwa namna gani anao uwezo wa kubadilika. Leo katika kifungu hiki, Kristo anatuambia tusifikie mahali hapo. Tusihukumu. Mungu mwenyewe kwa makosa tunayomfanyia hatupatii hukumu ya namna hiyo. Yeye hadi dakika ya mwisho ya maisha yetu anaendelea kutungoja tugeuke na anaendelea kutumaini kuwa tutageuka tutubu ili tuupokee msamaha wake. Sisi ni akina nani hadi tuwahukumu hivyo wenzetu. Huyo tunayemfuata na huyo ambaye tunaitwa kwa jina lake, ametufundisha kwa vitendo kuwa kamwe uovu hauwezi kushindwa kwa uovu. Yeye ameushinda uovu kwa wema na anatualika na sisi kufanya vivyo hivyo. “Basi, iweni na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.”