Dominika ya VIII ya Mwaka C wa Kanisa:“Toa kwanza boriti katika jicho lako mwenywe ndio utakapoona vema kukitoa kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.” Dominika ya VIII ya Mwaka C wa Kanisa:“Toa kwanza boriti katika jicho lako mwenywe ndio utakapoona vema kukitoa kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.” 

Dominika ya VIII ya Mwaka C: Toa Kwanza Boriti, Ili Uone Kibanzi Jichoni Mwa Jirani Yako.

Katika dominika VIII tunapokea fundisho la Bwana wetu Yesu Kristo akituambia “Toa kwanza boriti katika jicho lako mwenywe ndio utakapoona vema kukitoa kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.” Ni fundisho lililo wazi na la moja kwa moja! Huu ni mwaliko wa kukosoana kwa heshima, amani na upendo, ili kwa pamoja, tuweze kuwa ni mashuhuda wa upatanisho na kweli.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Ni dominika ya nane ya Mwaka C wa Kanisa. Katika dominika hii tunapokea fundisho la Bwana wetu Yesu Kristo akituambia “Toa kwanza boriti katika jicho lako mwenywe ndio utakapoona vema kukitoa kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.” Ni fundisho lililo wazi na la moja kwa moja, tunapenda lakini kuliangalia namna linavyofafanuliwa kwetu leo kupitia masomo mengine ya Misa ya dominika hii. MASOMO KWA UFUPI: Somo la kwanza ni kutoka kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira (Ybs 27:5-8). Kama jina lenyewe linavyodokeza, hiki ni kitabu ambacho kimo katika kundi la vitabu vya Agano la Kale vinavoitwa vitabu vya Hekima. Navyo ni kitabu cha Ayubu, cha Mithali, cha Mhubiri cha Hekima ya Sulemani na hiki cha Hekima ya Yoshua bin Sira. Kwa ujumla vitabu hivi vinalenga kufundisha ufunuo wa kimungu kupitia uzoefu wa maisha na mang’amuzi ya siku kwa siku ambayo watu wanayapata katika maisha. Sasa katika uzoefu huo ambao watu wameupata maishani, somo hili linatuonesha kuwa ukitaka kumjua mtu, mojawapo ya vigezo ni maneno yake. Mwandishi anasema usimsifu mtu kabla ya kumsikia anachoongea. Maneno kwa mtu ni kama matunda kwa mti.

Kipimo hiki kwa haraka haraka kinaweza kisiwe sahihi sana kwa sababu wapo pia watu waoongea wasichomaanisha. Waongo. Katika Zaburi ya 62: 4 mzaburi mwenyewe anasema maadui zake kwa kinywa hubariki lakini moyoni hulaani. Hekima hiyo inayowaongoza wanadamu inawaambia kuwa  maneno ya mtu ni zaidi ya kile anachokisema. Ni ujumla wa maisha yake mazima: namna yake ya kufikiri, mtazamo wake juu ya maisha, namna yake ya kukabiliana na hali mbalimbali za maisha, mwono alionao juu ya wenzake, misimamo yake si ya anachokisema bali anachokiishi n.k. Hayo ndiyo yanayomfunua mtu kuwa ni nani kati ya wengine. Mafundisho ya Yesu katika Injili (Lk 6:39-45)  yanafuata pia mfano wa mafundisho ya hekima. Mafundisho yanayotolewa kwa njia ya mithali, hadithi fupifupi na misemo inayobeba uzoefu wa maisha. Anatoa mifano mitatu: wa kwanza ni kuhusu kipofu, kwamba aliye kipofu awezaje kuongoza kipofu mwenzake kama si wote wawili kutumbukia shimoni? Mfano wa pili wa yule aliye na boriti katika jicho lake na anamwambia mwenzake aliye na kibanzi kwenye jicho “niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako”. Mfano wa tatu wa mti na matunda: kwamba hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya wala mti mbaya uzaao matunda mazuri.

Maneno kwa mtu ni kama matunda kwa mti.
Maneno kwa mtu ni kama matunda kwa mti.

Kipofu ni mtu anayehitaji msaada. Hawezi katika hali yake kumwongoza mwingine anayehitaji msaada. Kumbe kwanza anahitaji apate kiongozi, yeye afuate nyayo za kiongozi na ndipo anapoweza kumshika mkono kipofu mwingine amuongoze. Mfano huu unawaelekea kwanza mitume, watakaochukua nafasi ya kutangulia mbele ya wafuasi, lakini pia unawaelekea wafuasi wote wa Kriso kwamba wamweke daima mbele yao Kristo kama kiongozi na mwalimu na wote pamoja wafuate nyayo zake ili wasiingie shimoni. Katika safari hiyo ya kumfuasa Kristo, mfano wa pili unawaalika wafuasi kuchukuliana. Lipo hitaji la kurekebishana pale mmoja anapokosea na huu ni wajibu wa msingi. Kristo anataka yule anayechukua wajibu wa kumrekebisha mwingine amrekebishe akijua kuwa na yeye anayo mapungufu yake na inawezekana yakawa makubwa kuliko ya yule anayerekebishwa. Si mfano unaozuia maonyo au kukosoana. Ni mfano unaozuia kuwahukumu wengine, kujisafisha kwa njia ya kuwachafua wengine, kuwa wa kwanza kuyaona makosa ya wengine ilhali makosa yetu tunayafumbia macho. Mfano wa tatu, sambamba na miwili iliyotangulia, unalenga kuonesha utu wa ndani na utu wa nje wa mtu. Matendo ya mtu daima ni matokeo ya undani alionao katika utu wake, kutoka katika hazina njema ya utu wa ndani hufuata matendo mema na kutoka katika hazina mbaya ya utu wa ndani hufuata matendo mabaya.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, umefika wakati sasa tuangalie, haya masomo ya leo pamoja na mafundisho yake yote yenye hekima yanatupatia mwaliko gani sisi tunaoyasikiliza leo? Binafsi ninauona mwaliko huo katika ile kiu ambayo naamini watu wengi kama sio wote tunayo: kiu ya kuona mabadiliko mazuri katika mwenendo wa watu, kiu ya kuona ulimwengu unakuwa mahali bora zaidi pa kuishi, kuona amani inatawala, kuona upendo unashamiri, kuona ubinadamu katika maisha na mahusiano yetu yote. Masomo ya leo yanakuja kutuambia kuwa ili kufikia hali hiyo tunayoitamani sana, hatua ya kwanza ni wewe mwenyewe. Anza wewe kubadilika, anza wewe kuhusiana kibinadamu na wenzako, anza wewe kusambaza upendo na amani; anza wewe. Tunakumbushwa leo kuwa mabadiliko haya hayawezi kuja endapo kila mmoja atakuwa anamwangalia mwenzake na kutaka mwingine ndio aanze kubadilika. Hatutafika. Tutazidi kunyoosheana vidole, tutazidi kulaumiana, tutazidi kuanikana na tutabaki palepale na hata pengine kurudi nyuma.

Mama Theresa wa Calcutta: Familia ni kitovu cha mabadiliko
Mama Theresa wa Calcutta: Familia ni kitovu cha mabadiliko

Unaniijia kichwani usemi maarufu wa Mtakatifu Mama Theresa wa Calcuta, Yeye aliwahi kusema “kama unataka kuubali ulimwengu, anza kwa kuipenda familia yako.” Katika usemi huo, Mama Theresa wa Calcuta ametoa muhtasari mzuri kabisa wa hiki tunachokitafakari leo. Anatukumbusha upendo huanzia nyumbani. Na kama kila mmoja atajitahidi kuuishi upendo huo katika mazingira yake, katika yale yaliyo ndani ya uwezo wa himaya yake, ulimwengu wote utajaa upendo. Tuupokee basi mwaliko huu na tuanze ndani mwetu wenyewe. Tuanze kuyapa uzito maneno yetu. Tuwe ni watu wa maneno yetu. Tuwe na ujasiri kama anavyosema Yesu wa kuondoa kwanza boriti katika jicho letu, kuyaangalia yale tuliyonayo ambayo  yanawakwaza wengine kabla ya kupiga tarumbeta kuhusu namna wengine wanavyotukwaza sisi au kuikwaza jamii. Sote tunasafiri katika mtumbwi mmoja -  amezoe kusema Papa Francisko, na mwalimu wetu ni mmoja tu Kristo. Yeye aendelee kuwa dira yetu na nguvu ya kutusaidia kufikia mabadiliko ya ndani ili kwa mabadiliko yetu, ulimwengu wote ubadilike na uwe mahala bora zaidi pa kutusaidia sote kuufikia utakatifu.

Liturujia D 8 Mwaka C
25 February 2022, 08:21