Tafuta

Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake zinazofumbatwa katika hekima ya njia mbili: heri na ole. Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake zinazofumbatwa katika hekima ya njia mbili: heri na ole. 

Heri za Mlimani Ni Hekima ya Njia Mbili Katika Maisha ya Mkristo: Heri na Ole!

Mwinjili Luka hazungumzii umaskini wa roho, wala njaa ya kiroho n.k. Anazungumzia umaskini katika ujumla wake. Analenga kumgusa mfuasi wa Kristo katika mazingira yake ya kawaida kabisa ya maisha na kumwalika kuwa katika heka heka zake za maisha ikimbidi kuwa maskini ili tu ampate Kristo, yuko radhi abaki maskini ili asimpoteze Kristo, ili asipoteze imani kwa Kristo. HEKIMA!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Ni dominika ya Sita ya Mwaka C wa Kanisa. Masomo ya dominika hii yanayaweka maisha ya mwanadamu kati ya njia mbili: kati ya njia ya kibinadamu na njia ya kimungu, kati ya njia ya wenye haki na njia ya wasio haki, njia ya kidunia na njia ya kiroho. Tuyapitie kwanza masomo yenyewe kabla ya kuingia katika tafakari ya mafundisho yake katika maisha yetu. Masomo kwa ufupi: Katika somo la kwanza, Nabii Yeremia (Yer 17:5-8) anataja watu wa aina mbili. Wa kwanza ni yule anayemtagemea mwanadamu na wa pili ni yule anayemtegemea Mungu. Anasema, yule anayemtegemea mwanadamu na kumfanya mwanadamu kuwa kinga yake, amelaaniwa; yaani amejifunga, hayuko huru kushamiri na ategemee kuanguka tu. Anayemtegemea Mungu, yeye amebarikiwa. Anafananishwa na mti uliopandwa kando ya maji. Ni mtu ambaye yuko karibu na chemichemi hivyo lazima atashamiri. Yeremia anatoa maneno haya ya hekima kwa waisraeli ambao wakati huo walikuwa utumwani. Walikuwa wamechukuliwa mateka, wamefungwa kwa sababu hawakumtegemea Mungu na badala yake waliyategemea mataifa yenye nguvu wakati huo.

Kumbe, Nabii Yeremia anachowaambia, kwanza, ni kuwa “ninyi mmefikia hali hii ya ugumu wa maisha kwa sababu hamkumtegemea Mungu. Mliweka tumaini lenu kwa mwanadamu.” Jambo la pili analowaambia ni kuwa “huko mbeleni, kesho, Mungu atakapowarudisha katika nchi yenu, Mungu atakapowatoa utumwani, mjue sasa ni nani wa kumwamini na ni nani wa kumtegemea kati ya Mungu na mwanadamu.” Fundisho hilo hilo tunalipata katika Zaburi ya kwanza, Zaburi ambayo ni wimbo wa katikati wa dominika hii. Somo la Injili (Lk 6:17, 20-26) linatupatia mafundisho ya Yesu yanayojulikana kama Heri na Ole. Yesu anawakusanya Mitume na wafuasi wake wote na anaanza kuwafundisha. Kimsingi mafundisho haya ni yale yale ambayo Mwinjili Mathayo anayatoa katika Heri nane. Ni mwono mpya wa maisha ambayo mfuasi wa Kristo anaalikwa kuwa nao. Ni vigezo vipya, vigezo vinavyomwezesha mkristo kuishi duniani akiwa na maelekeo ya kufika uwinguni. Tofauti inayoonekana ni kuwa wakati mwinjili Mathayo anatoa mafundisho ya Heri nane katika mafundisho yaliyo kama katekesi, mwinjili Luka yeye anatoa mafundisho katika mpangilio wa hekima ya kale, hekima inayoitwa ya njia mbili, njia chanya ya kufuata na njia hasi ya kuepuka. Anaeleza heri nne na ole nne. Heri masikini, heri walio na njaa, heri waliao na heri watu wanochukiwa.

Kuna Umaskini wa hali na kipato.
Kuna Umaskini wa hali na kipato.

Katika Heri nne - Heri maskini, heri walio na njaa, heri waliao pamoja na heri watu wanochukiwa, anamsifu mfuasi ambaye kwa ajili ya mwana wa Adamu, yaani kwa ajili ya Kristo Yesu haoni haya kuwa masikini, kuwa na njaa, kulia au kuchukiwa. Hivyo ni vitu ambavyo havitangulizi katika maisha yeke. Na Mwinjili Luka hazungumzii umaskini wa roho, wala njaa ya kiroho n.k. Anazungumzia umaskini katika ujumla wake. Analenga kumgusa mfuasi wa Kristo katika mazingira yake ya kawaida kabisa ya maisha na kumwalika kuwa katika heka heka zake za maisha ikimbidi kuwa maskini ili tu ampate Kristo, yuko radhi abaki maskini ili asimpoteze Kristo, ili asipoteze imani kwa Kristo. Hali kadhalika yuko radhi kuwa na njaa, yuko radhi kulia na yuko radhi kuchukiwa ili tu asimpoteze Kristo katika maisha yake.Sambamba na hilo, katika zile ole nne – ole mlio na mali, ole ambao mmeshiba, ole mnaocheka na ole mnaoomboleza -  anamwonya mfuasi wake ambaye yeye yuko tayari kuchagua mali, kuchagua shibe, kuchagua kicheko na kuchagua kusifiwa na watu kwa gharama ya kumpoteza Kristo katika maisha yake. Yaani kama kuna kitu cha kupoteza kati ya mali na Kristo yeye yupo tayari kumpoteza Kristo abaki na mali; hali kadhalika shibe, kicheko na kusifiwa na watu; yeye hayuko tayari kupoteza vitu hivyo. Kwake ni bora apoteze imani, ni bora ampoteze Kristo ili tu apate mali, apate shibe, apate kicheko maishani na asifiwe na watu.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii yanatukumbusha kuwa maisha yetu yanakabiliwa daima na uchaguzi. Mungu ametuumba katika uhuru, ametuweka katika ulimwengu uliojaa wema wake lakini pia ulio na hila za yule mwovu. Yeye anapenda tuutumie uhuru wetu kuchagua mema. Masomo haya yanatutahadharisha, kuwa si kila kilicho mbele yako kinafaa, si kila kinachowezekana kufanyika ni halali na si kila kinachopendeza kinaleta manufaa. Tunakumbushwa leo kuchunguza mambo vizuri kabla ya kufanya maamuzi kwa sababu tunapofanya maamuzi sahihi tunapata baraka ya Mungu, tunapata Heri lakini endapo hatutafanya maamuzi sahihi tutaikosa baraka ya Mungu na tutaangamia. Tumeyaangalia kwa kirefu kidogo masomo mawili ya dominika ya leo, somo la kwanza la Nabii Yeremia na somo la Injili ya Luka.

Heri na Ole Ni Hekima ya Njia Mbili katika Ukristo
Heri na Ole Ni Hekima ya Njia Mbili katika Ukristo

Katika mafundisho hayo mazuri kuhusu njia mbili kama tulivyoona, linaongezeka somo la Waraka wa Paulo ambalo linazungumzia ufufuko wa Kristo. Unaweza kujiuliza ufufuko wa Kristo unahusika nini na fundisho hili la njia mbili? Ufufuko wa Kristo ni uhakika wa uwepo wa maisha ya umilele baada ya maisha ya hapa duniani. Ufufuko wa Kristo unatuonesha kuwa sisi tunaomwamini Kristo, maisha yetu hayakomei hapa duniani, tumeitwa kuirithi mbingu na kuishi pamoja naye mbinguni. Hii ni sababu kubwa sana ya kutusaidia namna ya kuishi hapa duniani na namna ya kuchagua. Kwa kutambua kuwa tumeitwa kuirithi mbingu, tunahimizwa kuishi hapa duniani tukichagua mambo yale ambayo si kikwazo na maisha ya umilele tunayoyaendea kwa maana kma inavyotukumbusha heri ile ya kwanza ufalme wa Mungu ni wa wale wanaochagua njia ya maisha ya Heri hapa duniani.

Liturujia D6
11 February 2022, 08:15