Tafuta

Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, muda muafaka wa: sala, toba na wongofu wa ndani unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, muda muafaka wa: sala, toba na wongofu wa ndani unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. 

Jumatano ya Majivu, Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima Cha Siku 40

Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma. Ni kipindi kinachotualika kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo, kwa kufunga na kutenda matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni kipindi cha toba na kujipatanisha na Mungu, Kanisa, ndugu katika familia, marafiki zaidi sana ni kujipatanisha mtu na nafsi yake.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Siku ya Jumatano ya Majivu, siku ya kwanza ya kipidi cha Kwaresima katika mwaka C. Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma. Ni kipindi kinachotualika kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo, kwa kufunga na kutenda matendo ya huruma, kama vile kuwasaidia wahitaji hasa maskini, kuwatembelea wagonjwa na hata wafungwa. Ni kipindi cha toba, kipindi cha kujipatanisha na Mungu, kujipatanisha na Kanisa, ndugu katika familia, marafiki zaidi sana ni kujipatanisha mtu na nafsi yake. Kwaresima ni safari ya maishaya kiroho ambayo kilele chake ni adhimisho la fumbo la ukombozi wetu - mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo tunaloliadhimisha katika juma kuu, kuanzia alhamisi kuu, ijumaa kuu na jumamosi kuu, kilele chake ni domenika ya Pasaka. Kusali, kujitoa sadaka kwa ukarimu kwa wahitaji na kufunga, ndizo nguzo kuu tatu za kipindi cha Kwaresima, kipindi cha toba. Siku ya kwanza ya kipindi hiki cha Kwarema huitwa Jumatano ya Majivu kutokana na tendo la kupakwa majivu katika paji la uso na wakati huo mhudumu wa tendo hili takatifu la kiroho akisema; Mwanadamu kumbuka, u mavumbi wewe na mavumbini utarudi.

Jumatano ya Majivu Mwanzo wa Safari ya Kwaresima.
Jumatano ya Majivu Mwanzo wa Safari ya Kwaresima.

Jina hili la Jumatano ya majivu, lilianza kutumika rasmi mwaka 1099 na Papa Urbano II. Mwanzoni iliitwa “Mwanzo wa Mfungo”. Majivu yanayotumika siku hii ya Jumatano ya majivu ni ya matawi ya mitende yaliyotumika Jumapili ya Matawi ya mwaka uliopita ambayo yanaashiria ushindi dhidi ya dhambi na mauti kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwanini kupakwa majivu? Majivu ni alama au ishara tu ya nje inayoashiria toba ya ndani ya mioyo yetu kama ilivyo rangi ya kijivu ambayo ni rangi ya toba na matumaini. Kupakwa majivu ni ishara ya toba yetu ya ndani ya nafsi zetu tunayoifanya ambayo inatutakasa na kutusafisha na uovu wote, kama Majivu yanavyotumika kusafisha vyombo. Kumbe kupakwa majivu ni kukubali kwetu kuwa tu wachafu, tu wadhambi, tunahitaji kusafishwa, tunahitaji kutakaswa. Majivu ni mbolea na mbolea hutumika kukuza mimea na kuifanya izae matunda mema, mengi na bora. Toba ya kweli tunayoifanya ndani mwetu ikiashiriwa na alama ya majivu hutusaidia kukua na kuzaa matunda mema ya kiroho. Majivu haya yanapakwa kwenye paji la uso, kama vile siku ya ubatizo tulipopakwa mafuta ya Krisma takatifu, tukaondolewa dhambi ya asili na adhabu zake zote, kwa ishara ya msalaba, alama ya ushindi tuliyokombolewa nayo. Kumbe majivu yanatukumbusha kufanya toba na kuungama dhambi tulizotenda baada ya ubatizo. Kupakwa majivu katika paji la uso ni kukiri hadharani bila kujificha kuwa tu wadhambi na tunahitaji huruma ya Mungu Baba, tunahitaji msamaha, tunahitaji kutakaswa na kufanywa upya watoto wa Mungu na wa Kanisa.

Asili ya kujipaka majivu kama alama ya toba: Tendo hili la kiroho la kupakwa majivu katika paji la uso ni ishara ya toba ya kweli, ishara ambayo imekuwa ikitumika kwa maelfu ya miaka iliyopita hata kabla ya kuja Kristo. Katika ulimwengu wa wayahudi majivu yalikuwa ni alama ya huzuni, masumbuko, uchungu au uduni (Ayubu 2:8, 30:19; Zab 102:10). Baadaye utamaduni huu wa kupakwa majivu ulitumiwa na wakristo wa kwanza kama alama ya toba. Mwaka 600 hivi, Gregory Mkuu aliifanya siku ya Jumatano ya majivu kuwa siku ya kwanza ya Kwaresma na kufanya kipindi hiki cha toba kuwa ni cha siku arobaini. Miaka ya 800 hivi, baadhi ya makanisa yaliadhimisha ibada ya Jumatano ya majivu kwa ajili ya wadhambi waliokubuhu katika dhambi na waliojulikana. Wadhambi hawa waliojulikana walipoamua kufanya toba na kubadili maisha yao walipakwa majivu. Hivi wakati huu si wote walipakwa majivu ila tu wale waliokuwa wadhambi waliojulikana wazi, kama vile makahaba, wauaji na waasi. Kuanzia karne ya 11, Kanisa kwa kutambua kuwa mbele za Mungu hakuna asiye na dhambi, liliamuru tendo hili liwe kwa waamini wote likiambatana na kufunga, kusali, kutoa sadaka na kufanya matendo ya huruma.

Katika Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Yoeli (2:12-18); Mungu anatuita tumrudie Yeye kwa mioyo yetu yote, na kwa kufunga na kwa kulia na kwa kuomboleza. Tunaambiwa tuirarue mioyo yetu, na siyo mavazi yetu. Katika siku za Agano la Kale, watu walikuwa na desturi ya kurarua mavazi yao kama ishara ya kufanya toba. Hata hivyo, walikuwepo wengine waliokuwa wakiyararua mavazi yao kama ishara ya nje tu, lakini ndani ya mioyo yao hawakuwa na nia ya kufanya toba ya kweli. Mioyo yao ya “jiwe” haikuweza kubadilika! Watu hawa hawakuwa wameyaacha mambo ya kiulimwengu na kuanza kuyaishi maisha mapya, maisha ya kumcha Mungu. Nabii Yoeli, anatuita kumrudia Mungu sio kama mtu mmoja mmoja, bali ni wito kwa watu wote; “Pigeni tarumbeta katika Sayuni, takaseni saumu, kusanyikeni kusanyiko kuu; kusanyikeni watu, litakaseni kusanyiko, kusanyikeni wazee kusanyeni watoto na hao wanyonyao maziwa” (Yoe 2:15). Mtume Paulo, katika somo la pili la Waraka wake wa pili kwa Wakorintho (2Kor 5:20-6:2); anatusihi tupatanishwe na Mungu kwa ajili ya Kristo. Mungu Baba alimtuma Mwanawe wa pekee, Yesu Kristo, aje kutukomboa kwa kuteswa na hata kufa msalabani. Mungu asiyejua dhambi alimfanya Yesu Kristo kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye (2Kor 5:21). Yesu Kristo hakujua dhambi, lakini alifanywa kuwa dhambi; vivyo hivyo sisi tusio haki tunafanywa kuwa haki katika Yeye. Sisi wadhambi tulistahili kifo hiki cha kutisha, kifo alichokufa Yesu kutokana na Upendo wa Mungu.

Kwaresima ni Kipindi cha Kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu
Kwaresima ni Kipindi cha Kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu

Katika Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 6:1-6;16-18); Yesu anatufundisha namna tunavyopaswa kukiishi kipindi hiki cha Kwaresima. Yesu anatuonya tusiwe wanafiki, tusifanye matendo mema ili tuonekane machoni pa watu wengine, kwani kwa kufanya hivyo tunakuwa tumepokea thawabu yetu kwa njia ya watu wanaotutazama, kutustaajabia, na kutusifia. Kumbe, matendo yetu mema yasilenge kujionesha kwa watu wengine, bali yawe ni mawasiliano binafsi kati yetu na Mungu yaani kujenga muungano na Mungu wetu aliyemtakatifu kwa sala, sadaka na kufunga. Matumaini ya mafungo yetu hayana budi kujengeka katika njaa na kiu ya muungano na Mungu wetu mtakatifu. Muungano huu unawezekana tukiwafungulia mlango wenzetu hasa wahitaji na kuwapatia yale tutakayojinyima. Ni katika mfungo ndipo tunaweza kuiga mfano wa Msamaria mwema, anayejitolea kumsaidia mhitaji bila kuangalia tofauti zao kama inavyokaziwa katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii. » Mfungo unaoambatana na huduma kwa wahitaji ni njia ya kushinda tofauti zetu na vishawishi vinavyoambatana na tofauti hizo. Kwa hiyo, tunaalikwa katika kila hali tuliyonayo tushiriki mfungo huu wa Kwaresima kwa malengo ya kuhuisha maisha yetu ya kiroho na kujiweka karibu zaidi na Mungu.

Hatua za kuchukua ili tuweze kufanya vema mapinduzi ya kiroho, toba na wongofu wa ndani. Tukubali kwamba sisi ni wadhambi. Tusipokubali kuwa tu wadhambi hatutaona hitaji la kufanya toba na kubadilika. Ndiyo maana kwaresima lazima ianze kwa tendo la kupakwa majivu hadharani ili kukubali na kukiri hadharani kuwa tu wadhambi na tunahitaji kufanya toba. Sala, kufunga na matendo ya huruma ni mambo matatu ambayo tunahimizwa kuyafanya katika kipindi hiki cha Kwaresma. Yesu anatuangalisha kuwa, ili tuweze kufaidika kutokana na sala, matendo yetu ya huruma, na kufunga kwetu, tuondokane na unafiki. Mnafiki ndiye mdhambi pekee ambaye Yesu alimkemea hadharani bila kusita; huu ndio ufarisayo. Tusianze kipindi hiki cha Kwaresima kwa mazoea. Tukiingie kipindi hiki kama vile ni cha kwanza na cha mwisho katika maisha yetu. Tuitumie kwaresma hii kana kwamba hakuna tena Kwaresma nyingine. Kwa hakika hakuna hata mmoja mwenye uhakika wa kuiona Kwaresma nyingine. Mtume Paulo anatukumbusha kwamba kipindi cha Kwaresma ndio wakati uliokubalika, siku ya wokovu ndiyo sasa. Tusisubiri wakati mwingine. Tukitumie vema kipindi hiki. Nawatakieni nyote mwanzo mwema wa kipindi cha Kwaresima.

Majivu 2022
28 February 2022, 17:41