Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya VI ya Mwaka C wa Kanisa: Heri na Ole za Mlimani: Umuhimu wa ufukara katika maisha na utume wa kumfuasa Kristo Yesu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya VI ya Mwaka C wa Kanisa: Heri na Ole za Mlimani: Umuhimu wa ufukara katika maisha na utume wa kumfuasa Kristo Yesu. 

Mafundisho Makuu ya Kristo Yesu: Heri na Ole za Mlimani! Ufukara

Mwinjili Luka anaona ili kuwa mfuasi ni lazima kuacha na kujikatalia yote ili kuweza kuwa mfuasi wa Yesu Kristo, na hii ni sifa muhimu na ya lazima kwa kila mfuasi. Na ndio tunaona jinsi Mwinjili Luka anavyokazia sana juu ya dhana zima ya kuwa maskini kuwa ni kitu cha heri na baraka kinyume na mtazamo wa Waisraeli ambao waliona umaskini ni sawa na laana kutoka kwa Mungu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Dominika iliyopita tulisikia juu ya wito na utume wa wale wanafunzi wa kwanza wa Yesu mara baada ya muujiza wa uvuaji wa samaki wengi. Tofauti na Injili ya Mathayo na Marko, Mwinjili Luka anatueleza juu ya wito wa wafuasi wale wa kwanza mara baada ya miujiza ya Kafarnaumu na muujiza wa uvuaji wa samaki wengi, wakati Mwinjili Yohane anatuonesha muujiza huu baada ya ufufuko wa Yesu Kristo. (Yohane 21:1-11). Kwa Mwinjili Luka ili kuwa mfuasi ni lazima kuacha yote na kujikatalia yote ili kuweza kuwa mfuasi wa Yesu Kristo, na hii ni sifa muhimu na ya lazima kwa kila mfuasi. Na ndio tunaona jinsi Mwinjili Luka anavyokazia sana juu ya dhana zima ya kuwa maskini. Mathalani Mwinjili Luka anasema, heri kwa walio maskini na ole wao walio matajiri, wakati Mwinjili Mathayo anasema heri walio maskini wa roho. Katika Injili ya Luka tunaona kuwa maskini ni kitu cha heri na baraka kinyume na mtazamo wa watu wa Israeli ambao waliona umaskini ni sawa na laana kutoka kwa Mungu mwenyewe. Mwinjili Luka tangu awali anatuonesha kuwa wazazi wa Yesu walikuwa maskini, na hivyo kutolea sadaka ya njiwa badala ya mwanakondoo.

Ni kwa familia maskini waliweza kutoa njiwa kadiri ya sheria za Walawi badala ya mwanakondoo. Si hapo tu, bali hii dhana ya umaskini tunaona inajirudiarudia mara nyingi katika Injili ya Luka (motif).  Mpe kila mtu anayekuja kwako kukopa na kuomba msaada na bila kudai kulipwa; Ufanyapo sherehe basi usialike wale wanaoweza kukualika nawe badala yake kualika maskini na viwete na walemavu ambao hawataweza kukulipa au kukuliaka. Mfano wa karamu ile kuu, mkuu wa karamu anatuma watumishi wake waende njia panda na kualika viwete, vipofu na walemavu na maskini; Mfano wa tajiri na Lazaro. Hizi ni baadhi za sehemu ya Injili ya Luka zenye dhana ya umaskini. Ni Mwinjili Luka anaonesha waziwazi juu ya Huruma ya Yesu kwa watu wote, kuwa ujio wake ni kwa ajili ya kila mwanadamu ili sote tupate uzima wa milele. Na ndio mtindo wa uandishi wa Mwinjili Luka unafanana na ule wa manabii hasa juu ya maskini na waliosetwa katika jamii, ni mtindo tofauti na ule wa Mwinjili Mathayo unaofanana na vitabu vya Hekima.

Ufukara kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu
Ufukara kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu

Lk 6:17, 20-26: Mtindo huu wa heri na ole ulitumiwa sana pia na marabi katika mafundisho yao hata nyakati za Yesu. Tumesikia hata Nabii Yeremia anatumia pia mtindo huu wa uandishi katika somo letu la kwanza la leo. Na aina hii ya uandishi tunaikuta pia hata katika Agano Jipya. Tunaweza kutoa mifano kadhaa ila yatosha kurejea mifano michache tu, Heri aaminiye (Luka 1:45); Heri tumbo lililokuzaa (Mt 12:49). Aina hii ya uandishi ya heri ulio mashuhuri katika Agano Jipya ni zile heri katika Injili ya Matayo na Luka. (Mathayo 5:1-12, Luka 6:20-26) Na ndio aina ya uandishi iliyotumika katika kufikisha ujumbe hasa juu ya mahusiano ya mwanadamu na Mungu, mintarafu maadili na uaminifu kwa Mungu. Nini mtu anapaswa kufanya ili kupata heri na kinyume chake ni ole, yaani mmoja anayaangamiza maisha yake mwenyewe. Ole sio laana kutoka kwa Mungu, bali ni angalisho la upendo wa Mungu kwetu wanadamu, hivyo neno Ole ni onyo la upendo kwetu na kamwe lisieleweke kama laana na adhabu kutoka kwa Mungu kwa mwanadamu.

Katika Injili ya Mathayo tunaona Yesu anatangaza heri nane akiwa ameketi juu mlimani (Mt 5:1); Wakati katika Injili ya Luka akiwa sehemu tambarare na heri zipo 4 sambamba na ole pia 4. Mwinjili Luka kinyume na Matayo anatuonesha kuwa Yesu alizitamka hizi heri sehemu ya tambarare, ndio sehemu ya kukutana na watu wa aina zote, ni katika maisha yetu ya kawaida ya kila siku tunaalikwa kuishi mpango huu wa maisha ya heri. Ni Neno na mpango wa Mungu katika maisha ya kawaida ya kila mmoja wetu. Tumeona pia katika somo la Dominika ya tano ya Mwaka C wa Kanisa Mwinjili Luka alituonesha Yesu akienda ufukweni na huko akiwahubiria na kutenda muujiza na hata kuwaita mitume wale wa kwanza, hivyo Yesu anakuja na kukutana nasi katika maisha yetu ya kawaida kabisa ya siku kwa siku. Mwinjili Mathayo anazungumiza juu ya maskini wa roho, wenye njaa na kiu ya haki hivyo kuchukua zaidi upande wa kiroho, wakati mwinjili Luka kinyume chake anaonesha heri katika maisha ya kijamii ya kila siku. Ndio umaskini, kuwa na njaa na kulia wakati kinyume chake ni ole ya kuwa tajiri, walioshiba na wanaocheka sasa. Hivyo katika Injili ya Luka kila kitu ni uhalisia wa maisha ya kila siku ya kila mmoja wetu.

Mwinjili Luka hamaanishi hapa umaskini au njaa au kiu kwa yenyewe ndio unaoleta heri katika maisha yetu, bali ni kutambua kuwa si mali au vitu vinavyoweza kumaliza kiu na njaa ya mwanadamu bali ni katika kumtegemea Mungu, ni katika kumtafuta Mungu katika yote. Sehemu ya Injili ya leo tunaona Yesu anawahutubia wafuasi wake. Hivyo ni ujumbe unaotuhusu mimi na wewe tulio wanafunzi na wafuasi wake Yesu Kristo. Ni mwongozo wa msingi kwa maisha ya kila muumini.  Ni hotuba kwa jumuiya na hasa maisha ya kila mmoja wetu. Heri ninyi maskini, labda inaleta maswali na mashaka mengi katika heri hii. Ni furaha gani tunapata kwa kuwa maskini? Je ni heri kweli kwa kuwa maskini na labda hohehahe katika maisha? Ni swali la msingi. Na je tukiangalia hawa wanafunzi wa kwanza wa Yesu wa Nazareti akina Petro, Andrea na Yohane na hata mitume wengine walikuwa kweli maskini? Kwa harakaharaka bila kusaka ushahidi mkubwa tunaona katika Maandiko kuwa walikuwa ni watu wa hali ya kawaida yenye nafuu kuliko wengi wa nyakati zile. Tunaona baadhi yao walikuwa wavuvi na walimiliki mitumbwi na hata nyumba, hivyo sio watu tunaoweza kusema kuwa ni choka mbaya kwa lugha ya mtaani.

Mashauri ya Injili ni kielelezo cha hali ya juu cha ufuasi wa Kristo Yesu
Mashauri ya Injili ni kielelezo cha hali ya juu cha ufuasi wa Kristo Yesu

Ni kwa kusoma Injili ya Dominika iliyopita hapo tunaweza kupata ujumbe wa Injili ya Dominika ya leo. Ni kwa kupokea wito wa Yesu wa Nazareti kuwa wavuvi wa watu wanaacha yote na kumfuata Yesu Kristo. Hata tunaona Lawi naye anaacha kazi na shughuli yake ya kuwa mtoza ushuru na kuanza kumfuasa Yesu Kristo. Ni katika Injili ya Luka tunaona wazo hili la kuacha yote ili kumfuasa Yesu Kristo linajirudiarudia kila mara. Yesu alimwalika pia yule tajiri kuuza yote ili kumfuasa. (Luka 18:22) Ili kuwa wafuasi wa Yesu Kristo sote tunaalikwa kuuza yote tuliyo nayo na kumfuasa. (Luka 14:33) Kuuza na kuacha yote maana yake nini? Ni kutupa kila kitu tulichonacho katika maisha yetu labda hata yale tuliyoyapata kwa kutoka jasho na akili nyingi? Ni kubaki ombaomba na hata bila kuwa na mahitaji ya msingi katika maisha yetu?  Yesu Kristo kamwe hakupinga utajiri, bali ile hali ya kutegemea na kujishikamanisha na mali au utajiri, ile hatari ya kuweka hazina ya mioyo yetu katika mali na utajiri ndio haswa tunaalikwa kuiepuka na kuwa macho nao.

Ni kuwa na moyo katika vitu na mali na utajiri unaokemewa na Yesu Kristo. Kuona mali au utajiri au vitu kuwa ni miungu yetu. (Luka 18:24-25) Ni kumweka Mungu nafasi ya pili kwani nafasi ya kwanza katika mioyo ndio imejaa mahangaiko ya mali na vitu na utajiri. Maskini kwa maana ya Injili ya leo ni yule anayeangazwa na Neno la Mungu na hivyo kuweza kuvipa vitu thamani na mahali stahiki. Anayepokea mali kwa moyo wa shukrani kwani ni zawadi kutoka kwa Mungu, hivyo anajua kuwa si mali yake bali ni ya Mungu naye anakuwa ni mwangalizi tu wa mali za Mungu na kuzitumia kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu. Yote ni zawadi na hivyo hatuna budi kutumia pia kama zawadi katika kumpenda Mungu na jirani. Kila mara tunaalikwa kutambua kuwa sisi ni walinzi, ni bawabu wa mali na karama zote tunazojaliwa na Mungu Mwenyezi katika maisha yetu.

Maskini ni yule asiyeweka moyo wake katika mali na vitu, anayekubali kuwa mlinzi tu wa mali na kamwe hatumii mali zake kwa ubinafsi, ni yule anayefanya kama Baba yetu wa mbinguni, pamoja na kumiliki yote lakini anatoa yote kama zawadi kwetu. Ni mtu mwenye moyo wa upendo na kutumia mali hizo kwa upendo. Na ndio mwaliko wa Injili ya leo kuwa na ulimwengu mpya ambapo hakutakuwa hata mmoja wetu atakayekuwa muhitaji wa chochote kwani sote tunaalikwa kuishi kama ndugu. Ni ulimwengu wa kushirikishana mali, vitu, utajiri, elimu, ujuzi, hekima, busara, muda na kila aina ya neema tunazojaliwa na Mungu pamoja na wengine. Na ndio pia mwaliko wa Kanisa la Kisinodi, ndio Kanisa linalojali kwa kuona uso wa Mungu kwa wahitaji na wanaokuwa maskini zaidi yetu, iwe katika familia zetu, jumuiya zetu na jamii zetu kiujumla. Ndilo Kanisa linalojali kwa kuona na wengine wanashirikishwa mema tunayoyapata kutoka kwa Mungu (Theo-drama). Ni Mungu anayekuwa katikati yak ila tunalofanya. Ni kwa kukubali kubadili mtazamo na kuwa maskini kama inavyotualika Injili, vinginevyo tunabaki watumwa wa vitu na mali, ndio kubaki wabinafsi (Ego-drama). Hatuwezi kupata furaha ya kweli na heri ikiwa tunabaki na ubinafsi wa aina yeyote ile.

Kujishikamanisha na mali au vitu ni sawa na kuvigeuza na kuanza kuviabudu, na ndio kumwacha Mungu na kugeukia viumbe. Ndio kukubali badala ya kumwacha Mungu aongoze maisha yetu yaani, Theo-drama, kwa kumpa nafasi ya kwanza, tunakuwa watumwa wa nafsi na tamaa na matamanio yetu ya kila namna, ndio Ego-drama, ndio mimi nachukua nafasi ile ya Mungu katika maisha. Na ndio Yesu anaendelea kuwa yule anayekuwa tayari kushirikisha wengine mali na utajiri wake inawezekana hata akabaki wakati mwingine bila mahitaji yake ya msingi, anaweza kutindikiwa hata na mkate wake wa kila siku lakini Yesu anawahakikishia kuwa watashibishwa. Ni heri kuwa na njaa kwa kuwa mkate wangu nimemshirikisha mwingine mwenye njaa na uhitaji. Ni heri kulia sasa, kilio anachozungumzia Yesu ni ile hali ya ndani ya kuteseka unapoona mwingine anaishi katika shida na uhitaji mkubwa, ni kuwaka kwa mapendo ya ndani kwa ajili ya wengine. Upendo ni kumtakia mema mwingine kama mwingine; Na kamwe sio kwa kujitafuta mimi bali kwa ajili ya mwingine kama mwingine. Heri yao wanaoteswa, kutusiwa na hata kuchukiwa kwa ajili ya Injili na Yesu Kristo, hakika Yesu anazungumzia uhalisia wa maisha ya ufuasi kwani daima kuna upinzani kutoka kwa yule mwovu na ulimwengu wa kale.

Heri Maskini wa roho maana Ufalme wa Mungu ni wao
Heri Maskini wa roho maana Ufalme wa Mungu ni wao

Ni mara ngapi katika maisha yetu tunapata upinzani mkali kwa kuishi kweli za Injili, kuishi imani yetu katika mazingira ya kila siku. Yesu anasema wana heri hao wanaoteseka kwa ajili yake. Tunaweza kupata ukinzani na upinzani hata katika familia zetu, jumuiya zetu za Kikristo na hata kati yetu wenye dhamana ya kuhubiri Injili. Wapendwa katika tafakari yetu ya leo tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu atujalie nasi ujasiri wa kubadili maisha yetu na kuwa maskini kwa ajili ya Injili, kutumia mali na karama zetu kwa sifa na utukufu wa Mungu na kamwe si masilahi yetu binafsi. Maisha yetu yanapata umaana wake kwa kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi yake stahiki, ni kwa kutambua kuwa sisi ni viumbe na Mungu Mwenyezi ndiye Muumbaji wetu. Nawatakieni nyote Dominika na tafakuri njema.

08 February 2022, 14:23