2021.02.12 Querida Amazonia 2021.02.12 Querida Amazonia 

Miaka 2 ya Querida Amazonia,Celam inajibidisha kutimiza ndoto nne!

Wosia wa Kitume wa Papa Francisko wa“Querida Amazonia”uliochapishwa tarehe 2 Februari 2020 umetimiza miaka miwili.Kwa mujibu wa Barua ya Rais wa CELAM,Askofu Mkuu Miguel Cabrejos Vidarte, OFM,anaandika kwamba tukio hili ni sababu ya furaha na matumaini kwa ajili ya Kanisa la Amerika Kusini na Visiwa vya Carribien hasa kwa kujiwekea ahadi ya kutimiza ndoto nne za Papa: Kijamii,Kiutamaduni,kiikolojia na kikanisa.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika fursa ya kumbukizi la mwaka wa pili tangu kutangazwa kwa Wosia wa Kitume “Querida Amazonia” uliochapishwa mnamo tarehe 2 Februari  2020, baada ya Sinodi ya Amazonia, Baraza la mabara ya Maaskofu wa Amerika Kusini na Visiwa vya Carribien (CELAM) wameandika Ujumbe uliotiwa saini na Rais wake Askofu Mkuu Miguel Cabrejos Vidarte, OFM, wa Jimbo Kuu Katoliki la Trujillo, kwamba tukio hili ni sababu ya furaha na matumaini kwa ajili ya Kanisa la Amerika Kusini na Visiwa vya Carribien. Katika Ujumbe huo Askofu Mkuu Cabrejos Vidarte anabainisha juu ya juhudi za kufanya ndoto nne zake za kuitengeneza Amazonia zilizo hamasishwa na Baba Mtakatifu ambazo ni: “Ndoto ya kijamii, ya Kiutamaduni, kiikolojia na hatimaye ndoto ya kikanisa”.

Kipaumbele ni kuzungukia kiini cha Yesu Kristo

Pamoja na Baraza la Kikanisa la Amazonia (CEAMA) na Mtandao wa Kikanisa wa Panamazonia (Repam), CELAM imekumbatia ndoto hizi katika mchakato wake wa hivi karibuni wa kupyaisha na kuunda kwa upya ili  kuchukua wajibu kama jiwe la pembeni, liwe msingi mkuu wake wa kupewa kipaumbele, kwa kuzungukia kiini cha Yesu Kristo na kama kielelezo cha juhudi zao kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu na ikolojia fungamani na kuwa na Kanisa la Sinodi na la kimisionari linalotoka nje.

Muhimili huo wa Kanisa unamwilishwa na Mafundisho ya Kipapa

Rais wa Celam katika brua hiyo anaonesha kwamba muungano na utendaji wa Vituo vinne vya Kichungaji vya Muhimili huo wa Kanisa, vilivyojitokeza katika nuru ya upyaisho, vinamwilishwa na Mafundisho ya Kipapa ambayo wamepokea kwa njia ya Wosia wa ‘Querida Amazonia’ na kutafuta kuwa na jibu la dhati katika kilio cha kinabii kwa maskini na Mama Dunia, kwa njia ya utamadunisho wa Injili katika maeneo, kulida haki za watu na utamaduni asilia,  ambamo amesisitiza kuwa wana mengi ya kujifunza. Ujumbe wa Askofu Mkuu, unahitimishwa kwa kumwomba Bikira Maria, Mama wa Amazzonia, kwa ajili ya watu asilia na wale wote ambao wanaishi kanda ya Amazonia na akiomba msaada wa lazima kwa ajili ya kuwa waaminifu wa Ndoto nne za Papa Francisko ili Amazonia iweze kubaki bila mabaya, na ahadi ya wakati ujao kwa ajili ya kizazi kilichopo na kijacho.

 

15 February 2022, 15:21