Msumbuji:Kampeni ya kusaidia Cabo Delgado
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kampeni ya “Together for Cabo Delgado,”yaani “Pamoja kwa ajili ya Cabo Delgado”, iliyozinduliwa 2022 na Caritas jimbo la Pemba nchini Msumbiji, inajikita katika kutaka kusaidia malfu ya watu waliotawanyika, familia ambao zinahitaji msaada zaidi. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Caritas Msubiji, Santos Gotine, anasema wote walioathirika na matukio ya mashambulizi huko Cabo Delgado wanahitaji msaada kutoka kwa kila mmoja. Gotine aidha anatoa mwito kwa wenye mapenzi mema na jamii kwa ujumla ili kusaidia kampeni iliyoanzishwa na Caritas Pemba.
Msemaji mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini Msumbiji, Askofu João Carlos Hatoa Nunes, wa Jimbo la Chimoio, ametoa wito naye kwa wale wote ambao wanaweza kuguswa kwa kina ili waweze kusaidia dharura hiyo. Amesema kuwa kufariji mateso ya watu wa Cabo Delgado kunahitaji kujitoa na sadaka. Familia zinahisi mahitaji kutokana na kuishi katika maeneo ya migogoro mahali ambapo wanasema kuna kuhitaji msaada wa kibinadamu. Hata hivyo Caritas Musumbiji inawajibika kuratibu misaada yote inayotolewa ili kusaidia watu wa Cabo Delgado. Muhimili huo wa Kitaifa wa Caritas Msumbiji unafanya kazi pamoja na Caritas nyingine za majimbo ili kuweza kusaidia mateso ya Jimbo la Pemba.
Shirika la Kimataifa la Madaktari wasio na Mpaka (Médecins Sans Frontières MSF), Wiki iliyopita liliripoti kuwa vurugu za hivi karibuni za Cabo Delgado zilisambaratisha maneo ya watu ambao tayari walikuwa wameshapata pigo la migogoro kwa miaka miaka 5 iliyopita. Mbali na hayo yote lakini watu wengi wa Cabo Delgado kwa sasa ni waathirika wa ukosefu wa kufikiwa hata madawa na tiba. Katika wiki ya kwanza ya mwezi Februari, Shirika la Kimataifa la Madaktari wasio na Mpaka (MSF ) lilisema kuwa mamlaka mahalia, ilithibitisha kuwa zaidi ya mashambulizi 20 katika vijiji vinne nyumba 2,800 ziliharibiwa au kuchomwa kwa moto. Mgogoro kwa sasa unahusiana na kitovu cha Cabo Delgado, kwa namna ya pekee huko Meluco na Kusini mwa Wilaya ya Macomia.
Tangu mapema Januari 2022, zaidi ya watu 14,000 wamelazimika kuondoka kwenye makazi yao kutokana na kuongezeka kwa migogoro wa mashambulizi. Na sasa wanatafuta mahali salama na mahali pa kuishi. Hili ndilo wimbi kubwa la watu waliohama kushuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni. Wakati huo huo, Msumbiji kwa sasa iko katika hatari kubwa ya tabianchi kutokana na mzunguko wa kila mwaka wa dhoruba ya kitropiki ambayo tayari imesababisha vifo na uharibifu mkubwa wa nyumba na miundombinu. Watu wamekuwa na wakati kidogo wa kujiandaa na kupona katika dhoruba. Mnamo tarehe 24 Januari 2022, dhoruba ya kitropiki iitwayo Ana ilianguka katika wilaya ya Angoche, Mkoa wa Nampula na kuathiri kwa kiasi kikubwa majimbo ya Zambezia, Nampula, Tete, Niassa, Sofala, na Cabo Delgado.
Kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Kitaifa ya Kudhibiti Hatari za Majanga (INGD) ya Msumbiji, watu 38 walikufa na wengine zaidi ya 207 kujeruhiwa. Dhoruba ya Tropiki Ana iliathiri raia 180, 869 wa Msumbiji. Takriban nyumba 12,000, vituo vya afya 26, mifumo 25 ya usambazaji maji, nguzo 138 za umeme na baadhi ya kilomita 2 275 za barabara ziliharibiwa. Mbali na athari za Dhoruba ya Tropiki Ana, wasiwasi unaendelea kuhusu kimbunga kikali cha Batsirai, ambacho kiliingia kwenye mkondo wa Msumbiji mnamo tarehe 6 Februari 2022.