Tafuta

Tarehe 2 Februari Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Watawa Duniani Tarehe 2 Februari Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Watawa Duniani 

Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, Siku ya Watawa Ulimwenguni

Tarehe 2 Februari 2022 Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, Sanjari na Siku ya Watawa Duniani. Mzee Simeoni na Ana wakiwa wameongozwa na Roho Mtakatifu wanamtambua Kristo Yesu kuwa ni Masiha wa Bwana. Mzee Simeoni akamshukuru Mungu kwa utenzi wa sifa, aliyewawezesha kuuona wokovu, nuru na utukufu kwa watu wake Israeli. Watawa!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika sikukuu ya kutolewa Bwana wetu Yesu Kristo Hekaluni, siku 40 baada ya kuzaliwa kwake kama ilivyokuwa desturi ya Musa. Sherehe hii ilianza kusherehekewa Yerusalemu miaka 400 baada ya kuzaliwa Kristo. Katika sherehe hii waamini walifanya maandamano ya kuingia Kanisani wakiwa wamebeba mishumaa kama ishara ya Kristo kuwa mwanga kwa mataifa. Hii pia ni Siku ya Watawa Duniani. Somo la kwanza la kitabu cha Malaki (Mal. 3: 1- 4), ni malalamika ya Nabii kwa Makuhani na watu walioishi maisha ya dhambi. Malaki anaseama; Ibada zao ni kama mlio wa madebe mbele ya Mungu, maana hazina uchaji wowote. Hii ni kwasababu Makuhani waliendesha ibada kwa namna isiyo ya heshima, bila kufuata taratibu na sheria za Musa na watu nao sababu ya uchoyo hawakuwa tayari kutegemeza Hekalu na wahudumu wake kwa zaka na sadaka. Hivyo Mungu anatangaza kwamba: atamtuma Mjumbe wake kumwandalia njia, kwani yeye mwenyewe ameamua kuja Hekaluni mwake. Atafanya hivyo katika nafsi ya Masiha ajaye. Atawatakasa makuhani na watu wa Israeli kutoka dhambi zao na kuwafundisha kutolea dhabihu zenye mastahili machoni pa Mungu.

Ibada na matoleo hayo ya dhabihu hayatafanyika tu Yerusalemu bali katika ulimwengu wote. Utabiri huu ni kweli umetimia kama tunavyosali katika sala ya Ekaristi ya III tukisema; “Maana, kwa njia ya Mwanao, Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa uwezo tendaji wa Roho Mtakatifu, unavitia uzima vitu vyote na kuvitakatifuza, wala huachi kuwakusanya watu kwako, ili, toka maawio ya jua hata machweo yake, dhabihu safi itolewe kwa jina lako” (Mal 1:11). Ujumbe wa Nabii Malaki unakamilishwa kwa kutolewa Yesu hekaluni. Mwinjili Luka (Lk. 2: 22- 40), anasimulia jinsi mpango huo wa Mungu ulivyokamilika. Itakumbukwa kuwa kulikuwa na madhebu ya aina tatu aliyofanyiwa mtoto wa kiume baada ya kuzaliwa, mosi; siku ya nane baada ya kuzaliwa mtoto wa kiume alitahiriwa na kupewa jina; Pili, Kadiri ya Sheria ya Musa, mwanamke aliyejifungua hakuruhusiwa kuingia Hekaluni kwa ibada wala kutoa sadaka kwa siku 40 ikiwa mtoto ni wa kiume na siku 80 ikiwa mtoto ni wa kike.

Watawa wanao mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa
Watawa wanao mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa

Baada ya siku 40 - ikiwa alizaa mtoto wa kiume - mwanamke alilazimika kujionesha na kujitambulisha Hekaluni kutolea dhabihu ya mwana kondoo wa mwaka mmoja au njiwa wawili ili apate kutakaswa na kuruhusiwa sasa kuingia hekaluni kusali na kutolea sadaka mbele za Mungu na tatu ni kumkomboa mtoto, maana watoto wote wa kwanza wa kiume walihesabiwa kuwa ni mali ya Mungu kwa ajili ya kutumikie hekaluni.Ikiwa wazazi wanataka mtoto wao wa kwanza wa kiume awe mali yao, walipaswa kumpeleka hekaluni na kufanyiwa madhehebu ya kumkomboa na kulipa shekeli 5 (aina ya sarafu ya fedha) (Walawi 12:1-8; Hes 18:16). Sheria hii ilikuwa ni ya kuwafanya Waisraeli kukumbuka kwamba walikuwa watumwa Misri na walikombolewa kutoka utumwani kwa malipo ya kifo cha wazaliwa wa Kwanza wa Wamisri, hivyo kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atakuwa mali ya Mungu (Kut 13:12-14). Kwa kuwa Yesu ni mzaliwa wa kwanza wa kiume hivyo alistahili kuwa ni Mali ya Mungu.

Siku ya 40 baada ya kuzaliwa kwa Yesu, Maria na Yosefu walienda Hekaluni kadiri ya Sheria hiyo ya Musa ilivyowadai. Luka katika injili yake anaunganisha madhehebu ya kutakaswa kwa mama na kukombolewa kwa mtoto lakini bila kusema waziwazi kuwa Yesu alifanyiwa madhehebu hayo. Mkazo wake uko katika kutakaswa ambapo anatufundisha mambo mawili – kuwa familia ya Yesu, Maria na Yosefu ilishika vyema sheria za dini na kuwa ni familia masikini. Hii iko wazi, maana familia tajiri ilitakiwa kutoa kondoo wa mwaka mmoja wakati wa madhehebu ya kutakaswa kwa mama aliyejifungua mtoto wa kiume wa kwanza na familia maskini walipaswa kutoa sadaka ya njiwa wawili. Na ndicho walichokitoa Maria na Yosefu. Hili lilikuwa tukio la kawaida la kila mwisraeli. Kumbe, machoni pa watu, hakuna cha ajabu ambacho kingeweza kuwatofautisha Yesu, Maria na Yosefu kati ya familia nyingi zilizofika kwa lengo lile lile la kuwatolea watoto wao kwa Bwana. Lakini, kadiri ya mpango wa Mungu, fumbo kubwa lilijidhihirisha na kupata ukamilifu wake Maria na Yosefu walipomtolea mtoto Yesu Hekaluni.

Watawa ni mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu
Watawa ni mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu

Tofauti ni kuwa Yesu anajitoa mwenyewe Hekaluni kwa Mungu na anajiachilia au kujiweka kikamilifu chini ya mamlaka ya Mungu ili kukamilisha mpango wa Mungu ambao kwa huo alichukuliwa mimba tumboni mwa mama Bikira Maria. Mpango huu ni ukombozi wa Mwanadamu kwa kujitoa Yeye mwenyewe sadaka na kuyatimiza mapenzi ya Mungu Baba – “Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, kafara na sadaka za dhambi hakuzitaka, ndipo nikasema, tazama nimekuja, niyafanye mapenzi yako Ee Mungu” (Waebr 10: 5-7). Kumbe, katika tukio hili Mwenyezi Mungu anakamilisha kile alichoahidi kwa kinywa cha Nabii Malaki kuwa kuja mwenyewe Hekaluni, katika nafsi ya Mwanae na na kujitoa mwenyewe kuwa dhabihu iliyo hai na Takatifu, na inayompendeza. Ni katika ujio wake atawatakasa makuhani na watu wote, tena atawafundisha namna iliyobora ya kuadhimisha ibada katika Hekalu la Mungu. Katika tukio hili, Roho wa Mungu anawaongoza Simeoni na Anna kumtambua Yesu kama Masiha na mkombozi. Simeoni hakuwa kuhani, bali mzee, mlei mchaMungu aliyesali daima juu ya ujio wa Masiha kuwakomboa Waisraeli.

Kati ya familia nyingi zilizowaleta watoto wao hekaluni kuwatolea kwa Bwana, Simeoni akiongozwa na Roho wa Mungu aliweza kumtambua Mtoto Yesu kuwa ndiye Masiha wa Bwana aliyetabiriwa na aliyekuwa akimsubiri kwa hamu. Moyo wake ukajawa na furaha, akaimba wimbo wa kumsifu Mungu: “Sasa Bwana waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani, kwa maana kwa macho yangu nimeuona wokovu wako, uliouweka machoni pa watu wote, nuru ya kuwa mwangaza kwa mataifa, na kuwa utukufu kwa watu wako Israeli (Lk 2:29-32). Mwinjili Luka anasema: “Babaye na Mamaye walikuwa wakiyastaajabia yaliyonenwa juu yake” (Lk 2:33). Akasisitiza mzee simeoni - “Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka kwa wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa”. Kisha akamwambia Bikira Maria; “Nawe mwenyewe upanga utakuingia moyoni mwako, ili ukafunuliwe mawazo ya mioyo mingi” (Lk 2:33-35).  Simeoni anatufundisha kuwa faraja yetu ya uhakika, ya kudumu, isiyoweza kuibwa, mchwa hawezi kuiharibu ndiye Yesu Kristo tunayempkea katika Neno la Mungu na katika Sakramenti hasa Ekaristi Takatifu na Kitubio. Kama ni hivyo basi tujipeleke kwa Yesu bila kujibakisha, hata kama katika Yesu tunakutana na mateso mengi na ya kuumiza. Tukivumilia yote hayo faraja yetu ni kubwa Mbinguni kama kwa Bikira Maria aliyevumilia mateso mengi kama mzee Simeoni alivyotabiri. Kumbe basi sikukuu hii inatukumbusha kuwa Kristo Yesu ni Nuru yetu, ni mwanga kwa kila mmoja wetu (Yn 1:9). Imani yetu kwake ni kama taa ituongozayo katika njia ya Uzima. Sherehe hii inatufundisha pia tujitoa na kujiachilia mikononi mwa Mungu.

Bwana Hekaluni

 

01 February 2022, 08:26