Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya V ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Dhambi, Toba, Wongofu na Utakatifu wa maisha. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya V ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Dhambi, Toba, Wongofu na Utakatifu wa maisha. 

Dominika ya V ya Mwaka C wa Kanisa: Wito, Dhambi na Utakatifu

Wito ni zawdi toka kwa Mungu. Mungu anapomchagua na kumwita mtu, haangalii ukamilifu wake bali moyo wake wa unyenyekevu na utayari wake wa kutambua hali yake ya dhambi, kutubu na kuwa tayari kufuata maongozi yake. Tunaalikwa kuwa wakweli kwa nafsi zetu, kuisikiliza sauti ya Mungu, kutambua udhaifu wetu, kuukiri na kusema kama Nabii Isaya; Mitume Paulo na Petro.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya 5 ya mwaka C wa Kanisa. Masomo ya dominika hii yanatualika kutafakari juu ya wito wa kumtumikia Mungu katika watu wake. Wito ni zawdi toka kwa Mungu. Mungu anapomchagua na kumwita mtu, haangalii ukamilifu wake bali moyo wake wa unyenyekevu na utayari wake wa kutambua hali yake ya dhambi, kutubu na kuwa tayari kufuata maongozi yake. Kwa hiyo tunaalikwa kuwa wakweli kwa nafsi zetu, kuisikiliza sauti ya Mungu, kutambua udhaifu wetu, kuukiri na kusema kama Nabii Isaya: “Mimi nina midomo michafu,” na kama Mtume Petro; “Mimi ni mtu mwenye dhambi,” na kama Mtume Paulo; “Sistahili kuitwa mtume kwa maana naliliudhi Kanisa” kisha kuomba neema za Mungu kwa moyo wa unyenyekevu ili atujaze neema na baraka zake. Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 6:1-2a, 3-8), ni Isaya kuchaguliwa na kuitwa na Mungu kuwa nabii kwa njia ya maono. Katika maono hayo, Isaya aliona utukufu wa Mungu katika Hekalu la Yerusalemu katika sehemu ya ndani kabisa iliyoitwa “chumba kitakatifu” - “Patakatifu pa Patakatifu” – palipokuwa na jiko lenye makaa ya moto ambapo Kuhani mkuu pekee aliruhusiwa kuingia, mara moja tu kwa mwaka katika sikukuu ya maondoleo ya dhambi kwa ajili ya kutotea dhabihu za kuteketeza na kuchoma ubani mpaka chumba kile kijae moshi, ishara ya sala za waamini kupaa mbele za Mungu na kupokelewa.

Katika hali hii Isaya aliwasikia Malaika wakimsifu Mungu kwa maneno ambayo ni kiunganishi kati ya Prefasio na Sala mageuzo (Sala ya Ekaristi katika Misa): “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa Majeshi, Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.” Mbele ya macho ya Mungu Mtukufu na Mtakatifu, Isaya alitambua hali yake ya udogo na ya kuwa ni mdhambi, asiyestahili kufanya kazi ya Mungu, hiyo akaogopa na kutetemeka na kusema; Ole wangu! “Mimi niliye na midomo michafu na ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu” na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi. Kisha Isaya alimwona malaika akichukua kaa la moto kutoka katika tanuru iliyoko altareni, nakugusa midomo yake kwa ule mkaa uwakao, kama ishara ya kumtakasa dhambi zake na kumweka wakfu kuwa mjumbe wa Mungu ndipo sasa Isaya akaitika wito wa Mungu na kusema; “Mimi hapa Bwana, unitume mimi” (Isa 6:9).

Wito unasimikwa katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha
Wito unasimikwa katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha

Somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 15:1-11), Mtume Paulo anatufundisha kuwa imani yetu juu ya ufufuko wa Kristo ina msingi thabiti kabisa - Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu. Paulo anatambua makossa yake aliyoyafanya ya kuliudhi Kanisa la Mungu kabla kuongoka kwake na kuwa mtume wa mataifa. Ni kwa neema ya Mungu amekuwa mtume na neema hiyo si bure, bali ni ya kufanya kazi ya utume na wala si yeye aliyeweza kuhubiri kwa juhudi zaidi ya wengine, bali ni neema ya Mungu iliyo pamoja naye. Paulo alipotumwa na Makuhani wa Yerusalemu kwenda Dameski kuwatesa na kuwatenda jeuri wafuasi wa Kristo alijiona kuwa anatenda kazi ya Mungu. Njia Yesu alipojifunua kwake alimuuliza: “Wewe ni nani Bwana.” Jibu; Mimi ni Yesu, unayenitesa” (Mdo 9:5). Paulo alitambua dhambi zake, akawa kipofu wa kimwili, ili aangaziwe utukufu wa kiroho na kuona vitu katika uangavu wake.

Mbele ya Anania, alielezwa anachopaswa kufanya, akakubali kubatizwa na kupata kuona tena. Akiongozwa na Roho Mtakatifu alienda jangwani, na huko kwa njia ya sala, alijifunza mpango wa Mungu katika maisha yake. Baadae alianza kuhubiri habari za Ufalme wa Mungu, akimtangaza Yesu Kristo huko Damaski, Yerusalemu, na mwisho katika himaya ya Kirumi. Kutokana na ari yake ulimwengu wa wakati ule ulionekana kuwa mdogo sana. Alifanya safari kadhaa za kimisionari akilenga kumtangaza Kristo na Ufalme wa Mungu. Kwa maisha yake yote Paulo aliyajenga maisha yake katika nguzo kuu mbili. Kwamba daima alijihesabia kutokuwa na mastahili ya kuwa mjumbe wa Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo: “Maana mimi ni mdogo kati ya mitume, nisiyestahili kuitwa mtume” (1Kor 15:9). Aliweka matumaini yake yote kwa Mungu; “Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa kama nilivyo na Neema yake kwangu haikuwa bure, bali ni neema ya Mungu pamoja nami” (1Kor 15:10).

Katika Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 5:1–1), Yesu anawaita Simoni/Petro, Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo kuwa wafuasi wake wakiwa wanavua samaki katika ziwa Genezareti, (lijulikanalo pia kama ziwa Galilaya au ziwa Tiberia). Kabla ya kuitwa kwa hawa mitume kuna mambo mawili yaliyofanyika. Kwanza Yesu kuwahubiria makutano akiwa ndani ya mtumbwi wa Petro. Alipomaliza aliwaagiza watupe nyavu zao ili wavue samaki, kazi waliyoifanya usiku kucha bila mafanikio. Lakini kwa neno la Yesu, walitii, watatupa nyavu, wakapata samaki wengi kiasi che nyavu zao kuanza kukatika na hivyo kuomba msaada kwa rafiki zao nao wakaja na mtumbwi wao wakaijaza mitumbwi yote miwili samaki hata ikataka kuzama. Kitendo hiki kinamfanya Petro kujaa hofu na masaka na kusema; “Ondoka kwangu Ee Bwana kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi.” Kama nabii Isaya na Paulo mtume, Petro naye anajiona hastahili kuwa mfuasi wa Kristo.

Maneno haya ya Petro yamejaa unyenyekevu unaojionesha katika kukiri na kuungama udhaifu wake. Nasi yatupasa kujifunza fadhila hii ya unyenyekevu ili ituwezeshe kukiri na kuungama makosa yetu mbele za Mungu na wenzetu. Fadhila hii ya unyenyekevu inatupa nafasi ya kufika mbinguni kwani inatustahilisha kuwa kama watoto wadogo. “Msipokuwa kama watoto wadogo, hamwezi kuingia katika ufalme wa mbinguni” (Mt 18:3; Lk 18:17). Mtu akikosa fadhili hii ya unyenyekevu, hawezi kamwe kukiri makosa yake na kujuta na kuomba msamaha, na hivyo anajifungia njia ya kwenda mbinguni kwa kujifanya hana dhambi. Tukisema kuwa hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe na wala ukweli haumo ndani yetu (1Yoh 1:8). Ili tuweze kujitambua na kujikubali kuwa sisi ni wenye dhambi lazima tuyalinganishe maisha yetu na maisha ya Kristo. Yeye awe mizani ya uadilifu wetu. Ukitaka kujua ukweli kuhusu maisha yako usijilinganishe na watu wengine; jilinganishe na Kristo maana “mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Kristo” (1Yoh 2:6).

Nabii Isaya na Mitime Paulo na Petro ni mifano bora ya toba na wongofu wa ndani
Nabii Isaya na Mitime Paulo na Petro ni mifano bora ya toba na wongofu wa ndani

Tukijilinganisha na watu wengine tutajiona tu wakamilifu, hatuna dhambi, wema na wenye haki.  Isaya hakutambua uovu wake wala wa watu wake mpaka alipouona utukufu wa Mungu. Paulo hakutambua uovu wake mapaka alipokutana na Krsito akiwa safarini kuelekea Damaski. Petro aliutambua udhambi wake pale tu alipoyaweka maisha yake mbele ya Kristo maana Krsito ndiye nuru ya uzima inayoangaza maisha yetu. Wakati mwingine tunawatumia watu wengine kuwa vipimo vya uadilifu wetu na kuhalalisha matendo maovu kwa kusema “hata wengine wanafanya hivyo. Maneno haya si suluhisho” maana “hata wao wana midomo michafu”. Sera za kiulimwengu haziwezi kuwa mizani ya maadili yetu kwa maana zima “midomo michafu.” Tukishafanikiwa kutambua kuwa tuko dhaifu, basi tukubali kuacha. “Wakaacha vyote wakamfuata.” Tunapompokea Kristo lazima kuwe na mabadiliko katika maisha yetu. Kama ni hasira – ukubali kuacha, ubaguzi - ukubali kuacha, wivu – ukubali kuacha, urafiki mbaya – ukubali kuacha, uongo na kusengenya wengine – ukubali kuacha, dharau kwa wengine – ukubali kuacha, nyumba ndogo – ukubali kuacha, ulevi – ukubali kuacha. Lakini kuacha dhambi unayoipenda si kazi rahisi. Ili kuitakasa midomo ya Isaya lilitakiwa kaa la moto lipitishwe katika midomo yake, kaa la moto ambalo hata Malaika aliogopa kulishika kwa mikono na hivyo alitumia koleo.

Lakini hili ndilo kaa lililohitajika ili kumtakasa Isaya. Kwetu sisi tunahitaji kukisogelea kiti cha maungamo kwa moyo wa unyenyekevu na majuto. Usiseme dhambi yangu ni ngumu siwezi kuachana nayo au siwezi kusamehewa. Jipe moyo kama Paulo Mtume na kusema; “kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo.” Si kwa ujanja wetu bali ni kwa nguvu za msalaba tunaweza kushinda dhambi. “Mtumaini Mungu kwa moyo wako wote wala usizitegemee nguvu zako mwenyewe” (Met h.3:5). Ni “walio wagonjwa ndio wanaomhitaji daktari na Yesu hakuja kwa watu walio wema bali kwa wadhambi ili wapate kutubu” (Mk 2:17). Nenda katika Sakramenti ya Kitubio “bila fedha na bila thamani” (Isa.55:2). Yesu anatualika; Njooni nyote wenye kusumbuka na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha (Mt 11:28).  Tumwombe Roho Mtakatifu atujalie fadhila ya unyenyekevu katika maisha yetu, ili itusaidie kukiri mbele za Mungu; “Mimi nina midomo michafu na ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu” nihurumie Ee Mungu. “Ondoka kwangu kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi”. Sauti ya Mungu itasikika kwetu ikitufariji na kusema; “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukiwavua watu”. Nasi tutaweza kusema kwa ujasiri; “Kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo,” na kuitikia Mungu anapotuita kwa kusema; “ndipo niliposema, mimi hapa nitume mimi.”

Dominika 5
03 February 2022, 17:22