Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 5 ya Mwaka C wa Kanisa: Wito wa kwanza ni utakatifu wa maisha ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 5 ya Mwaka C wa Kanisa: Wito wa kwanza ni utakatifu wa maisha ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. 

Wito wa Kwanza Ni Utakatifu Ili Kumtangaza na Kumshuhudia Kristo Yesu

Kristo Yesu anatoa wito, mwanadamu anautikia wito na anaingia katika maisha ya Kristo akijifunza namna Kristo alivyoishi na yeye anamfuasa, yaani anayaishi maisha yake katika familia, katika kazi n.k, akichochewa na maisha ya Kristo na neema ambayo inaambatana na maisha hayo. Katika masomo ya leo tunaletewa wito wa watu wawili mashuhuri, Nabii Isaya na Mtume Petro.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Ni Dominika ya tano ya Mwaka C wa Kanisa. Dominika hii inatuonesha kuwa ukristo wetu, maisha yetu ya kushika dini ya kikristo, kimsingi, ni maisha ya kumfuasa Kristo. Kristo anatoa wito, mwanadamu anautikia wito na akishauitikia wito huo anaingia katika maisha ya Kristo mwenyewe  akijifunza siku kwa siku namna Kristo alivyoishi na yeye anamfuasa, yaani anayaishi maisha yake katika familia, katika kazi n.k, akichochewa na maisha ya Kristo na neema ambayo inaambatana na maisha hayo. Katika masomo ya leo tunaletewa wito wa watu wawili mashuhuri, nabii Isaya na Mtume Petro. Tuyaangalie sasa kwa ukaribu masomo yanayozungumzia miito hiyo miwili na kuona mafundisho tunayoweza kuyachota kuhusu maisha yetu ya ukristo. Masomo kwa ufupi: Wito wa nabii Isaya unaelezwa katika somo la kwanza ambalo linatoka katika kitabu cha Nabii huyo huyo (Is 6:1-2, 3-8). Isaya anapata maono; si ndoto bali ni maono kama ya mtu aliyetokewa. Anaona utukufu wa Mungu: Mungu aliyekaa katika kiti cha enzi kama mfalme na hapo hapo pindo la vazi lake limelijaza hekalu. Hapo Hekaluni malaika wanaimba mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu. Kuirudia sifa hiyo mara tatu humaanisha ukamilifu, ndiye mtakatifu wa hali ya juu kupita zote na ndiye utakatifu wenyewe. Tena wanamwita Bwana Mungu wa majeshi kukiri nguvu zake. Kumwita Mungu Bwana Mungu wa majeshi ni sawa na kusema Mungu Mwenyezi.

Sasa Isaya anapoyaona hayo yote anaogopa, anasema “Ole wangu!”Aanaogopa kwa sababu katika mapokeo ya kiyahudi huwezi kumuona Mungu hafalu ukabaki hai. Walibaki hai waliopata upendeleo wa pekee kama Musa. Isaya kuuona utukufu wa Mungu namna hiyo ilikuwa ni sawa na kumuona Mungu mwenyewe. Aliogpa pia kwa sababu alijitambua kuwa hastahili, si mtakatifu. Anasema mimi ni mtu mwenye midomo michafu - anataja mdomo akimaanisha mwili mzima, kwamba yeye ni mdhambi. Na anaongeza kuwa anaishi kati ya watu wenye midomo michafu, kumanisha kuwa anaishi kati ya watu wadhambi na yeye mwenyewe anashiriki katika dhambi ya watu anaoishi nao. Hapo Malaika mmoja akaja kumtakasa kwa kugusa midomo yake kwa kaa la moto. Baada ya ufunuo wote huo na baada ya utakaso, Isaya anasikia sauti ya Mungu ikiuliza nimtume nani? Ona sasa uhuru ambao Mungu anampatia Isaya. Hamwiti moja kwa moja, wala hamlazimishi. Yeye anamwonesha hitaji na anabaki kusubiri utashi wake binafsi wa kuupokea wito au kuukataa. Uhuru wa Mungu huusubiri uhuru wa mwanadamu. Isaya anapozingatia yote aliyotendewa na Mungu, anakuwa wa kwanza kusema “Mimi hapa, nitume mimi.”

Mwenyezi Mungu anaheshimu uhuru wa waja wake
Mwenyezi Mungu anaheshimu uhuru wa waja wake

Katika Injili tunapata simulizi la wito wa Mtakatifu Petro. Tunasoma katika injili ya Luka (Lk 5:1-11) kifungu ambacho Yesu anakwenda kuhubiri maeneo ya kandokando mwa ziwa. Hapo anamkuta Simoni, kabla hajampa jina la Petro, akiwa pamoja na wavuvi wenzake. Anapomaliza kuhubiri anamwambia Simoni na wavuvi wenzake watupe nyavu hadi chini ya ziwa, kilindini, wavue samaki. Wanafanya hivyo na wanapata samaki wengi ajabu. Petro anapoona hivyo anatambua kabisa kuwa huo ni muujiza. Anaona ni muujiza kwa sababu usiku kucha wamehangaika kwa kufuata ujuzi na maarifa yote ya uvuvi lakini hawakupata kitu. Petro anatambua huyo aliyewaambia si mtu wa kawaida. Kama ilivyokuwa kwa nabii Isaya, Petro naye anapouona muujiza, anapotambua kuwa yuko mbele ya mtu mwenye uwezo na anapouhusisha uwezo huo na Mungu  anamwambia Yesu “ondoka kwangu kwa maana mimi ni mtu mwenye dhambi.” Petro anashikwa na woga ule ule kama wa nabii Isaya. Woga wa ubinadamu mbele ya ukuu wa Mungu. Hapo Yesu anamwambia “usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.” Petro anakuwa mfuasi wa Yesu.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kupitia miito hii miwili: wito wa nabii Isaya na wito wa Mtume Petro, tunaisikia tena sauti ya Kanisa ikituambia hakuna asiyefaa mbele ya Mungu. Mungu anaita wote na anaita ili aokoe. Mara nyingi tunaposikia neno “wito” moja kwa moja huwa tunalihusisha na aina fulani ya maisha au watu. Tunauhusisha na upadre, tunauhusisha na utawa, ukatekista au kazi nyingine maalumu iliyo na mahitaji yasiyo ya kawaida. Wito tunaouangalia leo ni ule wa kumfuasa Kristo. Na huu ni wito unaotuunganisha sisi sote wakristo. Uwe mwamini mlei, uwe mtawa, uwe Padre, sote tunao wito huu mmoja wa kumfuasa Kristo na kuyaishi maisha ya Kristo katika maisha yetu ya kawaida. Katika wito huu wa kumfuasa Kristo, Mungu anaita kwa njia nyingi. Njia aliyoitumia kwa Isaya na kwa Petro ni ile ya kuufunua utukufu wake kwao. Hii ni ile hali ambayo mtu anaona anavutiwa kupiga hatua moja mbele na kumkaribia Mungu. Mtu anaanza kuvutiwa na watu wanaoenda Kanisani kila Dominika anavutiwa na wale walio mstari wa mbele katika vyama vya kitume, anavutiwa na wale wanaotolea muda wao na hata vitu vyao kwa huduma ya kanisa au ya wahitaji. Mwingine anaanza kuvutiwa kufanya maungamo ya mara kwa mara, kupokea sakramenti, kurekebisha vikwazo vya Kisakramenti n.k. Vichocheo kama hivi ni sauti ya Kristo anayeita “nimtume nani?”. Isaya anatuonesha kuwa Mungu humpa mtu vichocheo hivyo na kumuacha huru kuitikia. Na  ni Isaya huyo huyo anatuonesha mfano wa kuitika, “Mimi hapa, nitume mimi.”

Mwenyezi Mungu anaita, natakasa na kuwatuma wajumbe wa Injili ya matumaini.
Mwenyezi Mungu anaita, natakasa na kuwatuma wajumbe wa Injili ya matumaini.

Hatua ya pili ni ile tunayoweza kuiita wasiwasi wa mwanadamu kabla ya kuitika “Mimi hapa, nitume mimi.” Ni wasiwasi kama ule aliokuwa nao Petro. Yeye mbele ya ufunuo wa Kristo alijiona kama ni mtu ambaye amejikuta kimakosa katika sehemu takatifu. Anamwamia Yesu “ondoka kwangu, maana mimi ni mtu mwenye dhambi.” Yesu ni kama anambwambia “hapana, subiri kwanza, hauko hapa kimakosa, nitakufanya kuwa mvuvi wa watu.” Ndio kusema, msukumo unaoupata ndani, msukumo wa kuwa mtu mwema, msukumo wa kuwa mchamungu, msukumo wa kupiga hatua katika maisha ya sala, maisha ya Sakramenti usiuone kama ni kitu kisichowezekana kwa sababu ya udhaifu wa matendo yako. Hakuna asiyefaa mbele ya Mungu, isipokuwa yule tu ambaye haamini kuwa Mungu anaweza kumsaidia kubadilika. Miito hii miwili, wito wa Isaya na wito wa Petro, ni mwaliko basi wa kuisikia sauti ya Mungu ikituita na sisi kumfuasa Kristo na tena ni mwaliko wa kuishinda hofu na wasiwasi unaoweza kuwa unasababishwa na udhaifu wetu wa kibinadamu. Tuyakumbuke maneno ya Kristo mwenyewe; “wenye afya hawamwitaji daktari, sikuja kuwaita watu wema bali wenye dhambi ili wapate kutubu.”

Liturujia D 5
04 February 2022, 08:32