Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika VIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Maisha ni kufa na kuishi ndani ya Kristo Yesu. Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika VIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Maisha ni kufa na kuishi ndani ya Kristo Yesu. 

Dominika ya VIII ya Kipindi Cha Mwaka C: Maisha Ni Kufa na Kuishi

Dominika hii inatuandaa kuingia katika kipindi cha kwaresma, kipindi cha kutafakari upendo na wema wa Mwenyezi Mungu, kipindi cha kuongeza nguvu katika sala, kufunga, kujirudi, kufanya toba, kuungama na kufanya mabadiliko ya maisha ya kiroho kwa ajili ya maandilizi ya sikukuu ya Pasaka. Ni kipindi cha kufa kuhusu dhambi na kuishi kitakatifu ili kuungana na Mungu mbinguni.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 8 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Dominika hii inatuandaa kuingia katika kipindi cha kwaresma, kipindi cha kutafakari upendo na wema wa Mwenyezi Mungu, kipindi cha kuongeza nguvu katika sala, kufunga, kujirudi, kufanya toba, kuungama na kufanya mabadiliko ya maisha ya kiroho kwa ajili ya maandilizi ya sikukuu ya Pasaka. Ni kipindi cha kufa kuhusu dhambi na kuishi kitakatifu hapa duniani ili mwisho wa maisha ya hapa duninia kwa njia ya kifo tukaishi milele yote mbinguni na Mungu Baba pamoja na watakatifu wake wote. Somo la kwanza ni la kitabu cha Hekima ya Yoshua Bin Sira (YbS 27: 4-7). Kitabu hiki kiliandikwa miaka 200 kabla ya kuzaliwa Yesu na kinabeba ushauri wa thamani kubwa sana katika nyanja mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Somo la dominika hii ya 8 ya mwaka C, linatuonyesha umuhimu wa majadiliano katika maisha yetu ya kila siku. Majadiliano huleta muafaka, hutatua matatizo au migogoro kati ya pande mbili zinazolumbana kwa njia ya amani. Ni katika majadiliano mtu hutoa yaliyo ndani ya nafsi yake na kuyaweka wazi na bayana. Kiuhalisia kinachotoka ndani ya moyo wa mtu katika kinywa ndicho kinachoonesha na kudhihirisha tabia yake. Ndivyo anavyotuambia Kristo katika injili kuwa mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu.

Kwa kuwa kinywa cha mtu hunena yale yaujazayo moyo wake, kwa hiyo ili tufahamu yaliyo ndani ya nafsi ya mtu, Yoshua bin Sira anatuasa na kutushauri kumpa kwanza nafasi ya kuongea na kujieleza, tumsikilize ndipo tumhukumu kwa haki kwa yaliyotoka kinywani mwake. Hali kadhalika kabla ya kupokea au kuunga mkono jambo, hoja au mtu lazima tusikilize kwanza anayosema ili tuweze kutambua uzuri na ubaya wake hapo tutakuwa sawa kuliongelea na kulipigania inapobidi. Haya yote yanawezekana kama kuna majadiliano na masikilizano. Mtume Paulo katika somo la pili (1Kor 15: 54-58); anatueleza kuwa hali ya mwili wetu wa sasa ni ya kufa na kuoza. Mungu anataka tuwe katika hali hii kwa muda, ikiwa ni mapito kuendea hali ya kutokufa, hali ya uzima wa milele. Kwa kifo na ufufuko wake, Yesu ametutayarishia hali hiyo ya kutokufa. Kwa hiyo Maisha ni kufa na kuishi. Tunaishi ili tufe na tunakufa ili tuishi milele. Huu ni ukweli na uhalisia wa maisha yetu kwamba tunaishi na tutakufa na baada ya kufa tutaendelea kuishi. Lakini ili tuweze kuendelea kuishi katika hali ya utakatifu ni lazima tuwe tayari kufa kuhusu dhambi na kuishi maisha ya kitakatifu ili tuwe na muungano zaidi na Mungu wetu aliye mtakatifu.

Jengeni uhusiano kati ya kinywa na akili wakati wa kuzungumza.
Jengeni uhusiano kati ya kinywa na akili wakati wa kuzungumza.

Kimsingi kifo ni ukweli ulio mgumu kuupokea na kuukubali maana hakizoeleki. Licha ya kuwa kila siku watu wanakufa nasi tunashuhudia, lakini kifo kinabaki kuwa tishio na hofu kubwa kwa mwanadamu. Watu wengi hawapendi kujua wala kusikia habari za kifo, kwa kuwa hawana matumaini na imani juu ya ukweli wa maisha yajayo maisha ya ufufuko. “Ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini” (1Thes. 4:13-17). Hii inatokana na kutokuamini uwepo wa Mungu na hivyo kutokuona thamani ya maisha ya sasa wala yajayo. Lakini hata kwa wanaoamini uwepo wa Mungu na wenye matumaini na imani juu ya maisha yajayo, nao wanakiogopa kifo. Hii ni kwasababu hatukeshi, hatujiandai kumpokea mjumbe wa Mungu – kifo - atakapokuja kutuchukua na hatujui ni lini atakuja. Hali yetu ya kuishi katika dhambi, kuwa mbali Mungu, kukosa muunganiko na Mungu wetu aliye mtakatifu ndiyo inayotufanya tuwe na hofu, mashaka na woga wa kufa.

Kifo ni matokeo ya dhambi ya asili, dhambi ya wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva ya kutotii amri na maagizo ya Mungu (Mw. 3:19). Ni ukweli kuwa kila nafsi itaonja mauti. Mtakatifu Francisko wa Assisi anasema; “Usifiwe, ee Bwana wangu, kwa ajili ya huyu dada yetu kifo cha mwili, ambapo hakuna mwanadamu yeyote, aweza kumkwepa. Ole wao watakao kufa katika dhambi ya mauti! Heri wale watakaokutwa katika mapenzi yako, kwani, kifo cha pili hakitawadhuru” (KKK 1014). Mtakatifu Yahane Paulo II, alisema; “Ninapata amani tele ninapofikiria kuhusu wakati, ambapo Bwana ataniita kutoka maisha kwenda maisha.” Maana yake, anapata furaha na amani tele anapofikiria siku yake ya kufa, ambapo Mungu atamwita kutoka maisha haya ya duniani kuelekea Mbinguni kwenye maisha ya umilele. Mtakatifu Thereza wa Avila alisema; “Nataka kumwona Mungu, nakumwona Mungu, lazima nife.” Kumbe, kifo ni sehemu ya mpangilio wa maisha yetu. Hatuwezi kikiepa. Hata hivyo hatupaswi kuwa na mashaka, tujiandae kufa vyema kwa kutambua, kujutia, kukiri na kutubu dhambi zetu, tujipatanishe na Mungu, tukubali kufa kuhusu dhambi ili tuishi katika Kristo na hivyo tutakuwa na ujasiri wa kutamka maneno ya mtume Paulo akisema; “Mimi kuishi kwangu ni Kristo na kufa ni faida” hana mashaka kabisa juu ya ujio wa kifo. Nasi pia hatupaswi kuogopa, kwani kwa kifo cha Kristo Msalabani kifo chetu kimepata maana mpya, ambapo kwayo maisha mapya yanazaliwa, maisha ya milele mbinguni.

Jamii inawahitaji waalimu bora, ili wawe mwanga na chumvi ya ulimwengu.
Jamii inawahitaji waalimu bora, ili wawe mwanga na chumvi ya ulimwengu.

Katika injili ya Luka (Lk 6: 39-45); tunakutana na misemo ya hekima na busara za Yesu juu ya viongozi au walimu wanavyopaswa kuwa. Katika hali ya kawaida mwalimu anapaswa kuwa na uwezo wa kuona, kutambua, kuhukumu na kutenda vyema ili awe mfano mwema kwa wanafunzi wake. Kama mwalimu ni kipofu, yaani hawezi kuona, kusoma na kutambua alama za nyakati ili atoe maelekezo yanayostahili ni hatari kwa kuwa anaweza kuwapoteza wanafunzi wake. Yesu anasisitiza umuhimu wa kuona, kusikiliza, kutambua na kuongoza kuliko kwema na sahihi. Pia anatuonya tusiwe wepesi katika kuwahumu wengine, maana hata sisi nasi tuna maboriti katika macho yetu, yaani tuna makosa, hatuko wakamilifu, tu wadhaifu, tu wadhambi mbele za Mungu na tunahitaji msamaha. Kilicho cha maana ni kuonyana na kusaidiana katika kuepuka nafasi za dhambi. Hivyo tuepuke maisha ya unafiki, tuwe wakweli na wema mbele za watu na mbele za Mungu.

Tunapojiandaa kuanza kipindi kitakatifu cha kwaresma tukumbuke kuwa hapa duniani tu wapitaji. “Sisi ni Raia wa Mbinguni” (Fil. 3:20). Huko ndiko tulikotoka, kwa maana tulitoka kwa Mungu na “Mungu wetu yuko mbinguni” (Zab.115:3a), kama tulitoka kwa Mungu aliye mbinguni, basi kumbe nasi tunapaswa kurudi mbinguni. Huku duniani tuliko ni ugenini tu, kama tunavyosali katika sala ya salamu Malkia, “Mama mwenye huruma, uzima tulizo na matumaini yetu salamu, tunakusihi ugenini hapa sisi wana wa Eva.” Maandiko Matakatifu yanasema; “wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani, kama wangalikuwa wanaifikiria nchi waliyotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko” (Ebr. 11:15). Tukumbuke daima kuwa maisha ni kufa na kuishi, tumwombe Mungu atufundishe kuzihesabu siku za maisha yetu hapa duniani na kujua kuwa ni chache ili zinapoisha tuwe tayari tumejiandaa kurudi kwetu Mbinguni kwa kufanya toba ya kweli.

Dominika 8 ya Mwaka C
23 February 2022, 14:40